Translate

Tuesday, November 13, 2012

Wajasiliamali Mbeya wasema bidhaa za nje zinawatesa

Na Thompson Mpanji,Mbeya




BAADHI ya wajasiliamali wametoa wito kwa serikali kuwawezesha mitaji,mazingira ya kufanyia kazi sanjari na kuwaweka katika vikundi ili waweze kumudu na kuingia katika ushindani wa soko la ndani na nje kuliko ilivyo sasa ambapo bidhaa za nje zinawatesa katika soko la ndani kutokana na kuzalishwa kwa muda mfupi kwa wingi na kuuza bei ya chini.



Wakizungumza wakati wa maonesho ya wajasiliamali kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania na baadhi ya nchi za afrika mashariki,walisema kuwa kutokana na changamoto hiyo serikali haina budi kutumbukiza mkono wake kuwasaidia kwa hali na mali ili waweze kuendelea kujiajiri,kuwauzia watanzania wa chini,kati na juu bidhaa imara kwa bei nafuu sanjari na kupata tija na hatimaye kujiinua kiuchumi.



Mkurugenzi wa Witega Works and Fubrication iliyopo jijini Mbeya,William Gamba alisema kampuni yake inajishughulisha na utengenezaji wa zana za kilimo mathalani majembe ya kukokota kwa ng'ombe (plau) na majiko banifu lakini wamekuwa wakikumbana na ushindani mkubwa kutoka kwa wafanyabiashara kutoka nje kutokana na kuwa na mitaji midogo na vitendea kazi vya kukodi.



Alisema endapo serikali itamwezesha anao uwezo wa kutengeneza majembe ya kukokota kwa ng'ombe zaidi ya 200 kwa mwaka ambayo atawauzia wakulima kwa bei nafuu na hivyo kufikia adhama ya kauli mbiu ya taifa ya kilimo kwanza kwa vitendo na hivyo kuwakomboa wakulima hasa wa vijijini na wote wakafanikiwa kujiinua kiuchumia na kuongeza uzalishaji wa zana za kilimo na mazao.



Gamba alisema kutokana na utaalamu alioupata kutoka katika kiwanda cha utengenezaji wa zana za kilimo(ZZK) cha jijini Mbeya kilichokufa katika miaka ya 70 anao uwezo wa kutengeneza majembe ya mkono,koleo na fyekeo lakini mtaji mdogo ndiyo kikwazo.



Hata hivyo ameiomba serikali kuwaangalia kwa macho mawili waandaaji wa maonyesho mbalimbali ya wajasiliamali kwani ni kazi ngumu kuwakusanya pamoja hadi kufanikisha zoezi hilo linalohitaji wadhamani wa kutosha na fedha za kuendeshea shughuli hiyo.



Naye Mhasibu wa kampuni hiyo ambaye pia ni Mke wa Mkurugenzi huyo,Odilia Gamba ametoa wito kwa wanawake kuwasaidia waume zao katika shughuli mbalimbali za ujasiliamali ili kuinua kipato cha familia na kuendeleza miradi mbalimbali waliyoianzisha.



Maonyesho hayo ni ya tatu kuaandaliwa na Kampuni ya Mbeya Trade Fair and Enterteinment yalifunguliwa na Mkuu wa mkoa wa Mbeya,Abbas kandoro na kuwakilishwa na Mkuu wa wilaya ya Mbeya,Dkt.Norman Sigalla ambapo wageni wengine waliohudhuria maonyesho hayo ni Mkuu wa wilaya ya Ileje na kufungwa na Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya,Diwani Athuman.



Katika maonyesho hayo wakazi mbalimbali kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya walijitokeza kwa wingi kujionea na kununua bidhaa mbalimbali vikiwemo vyakula na vinywaji vya asili,nguo za asili,tiba asili,zana za kilimo na majiko banifu yanayosaidia kwa kiasi kikubwa utunzaji na uhifadhi wa mazingira.



Mwisho.

No comments:

Post a Comment