Translate

Wednesday, October 31, 2012

Tazara saccos kujenga Hosteli ya kisasa

Na Thompson Mpanji,Mbeya

CHAMA cha kuweka na kukopa cha Tazara Saccos Mkoani Mbeya kinatarajia kujenga hosteli kubwa ya kisasa ili kuachana na dhana ya kuwa tegemezi kutoka kwenye taasisi za kibenki na kuwa mradi huo mkubwa utaweza kusaidia chama kujitegemea chenyewe badala ya kutegemea zaidi kukopa katika benki hizo.



Hatua ya kuwa na ujenzi huo wa hosteli imekuja baada ya uongozi wa Tazara kwa kushirikiana na wanachama kuamua kwa pamoja kuwa na kitega uchumi chao wenyewe ambacho kitasababisha kuacha kukopa katika mabenki kwani hosteli hiyo itakapokuwa imekamilika hakutakuwa na sababu ya kukimbilia tena katika mabenki badala yake watatumia kitega uchumi chao kukuza mtaji wa chama.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama hicho wa kumi na tisa toka kuanzishwa kwake, Mwenyekiti wa Tazara Saccos Mkoani Mbeya Ambrose Shayo amesema kwamba kuanzia wameona kuwa mradi pekee ambao wanaweza kuanza nao ni hosteli kutokana na vyuo vingi kuanzishwa Mkoani hapa na ongozeko la wananchi kuwa kubwa.


Shayo amesema kuwa mradi huo utagarimu kiasi cha shilingi bilioni. 2 na kuwa fedha hizo zitapatikana kwa kila mwanachama kuchangia hisa zake ambazo ni shilingi 3,0000 ambazo watatoa kwa kila mwezi na kwamba mbali ya hisa za wachama pia chama kama kitakuwa kinanunua hisa za mil.8 kila ujenzi huo unatarajio kukamilika ndani ya miaka mitano ijayo sababu uwanja upo tayari ni kuanza tu mchakato wa kutafuta fedha mapema kutoka taasisi zingine kwa kutumia njia mbali mbali.

Aidha Mwenyekiti huyo amesema mwisho wa utekelezaji wa mpango huo ni kuweza kuwekeza na kuanza kujitegemea wenyewe badala ya kutegemea mabenki zaidi ambazo wamekuwa wakitumia kwa muda mrefu.
Mwiisho.

Ajinyonga kwa waya wa simu baada ya kumpiga mkewe

Na Thompson Mpanji,Mbeya

MKAZI wa Iziwa Mkoani Mbeya Mbwiga Mwalungwe(60), amefariki dunia baada ya kujinyonga nyumbani kwake kwa kutumia waya wa simu Oktoba 24 mwaka huu baada ya marehemu kumpiga mkewe.


Inadaiwa marehemu alimpiga mkewe aitwaye Taines Mbwiga(45) Oktoba 23 hali iliyompelekea kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Jijini hapa ambapo alipewa PF3 kwa ajili ya kutibiwa na kulazimu kulazwa hospitalini hapo.

Kutokana na tukio la baada ya mkewe kulazwa hospitalini, Jeshi la Polisi lilianza kufuatilia tukio hilo ndipo marehemu alipogundua kuwa anakabiliwa na mkono wa sheria aliamua kuchukua uamuzi mgumu kwa kuchukua waya wa simu majira ya saa 4 kamili asubuhi Oktoba 24, kisha kujinyonga nyumbani kwake.


Aidha polisi walifika eneo la tukio majira ya saa 6:00 mchana na kuuchukua mwili wa marehemu hadi hospitali ya rufaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kwamba hali ya mwanamke huyo inaendelea vema ambapo ameruhusiwa kutoka hospitalini Oktoba 2 na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali hiyo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi,kuhusiana na tukio hilo Balozi wa mtaa huo Chaina Juma amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba amewaachia jeshi la polisi kufanya uchunguzi ili kupata kiini hasa cha Mwalungwe kujiua kwa kujinyonga na kumuacha mkewe akiendelea kuugua hospitali.


Mwisho.



Mtoto wa miaka nane ajinyonga

MTOTO  mdogo aliyefahamika kwa jina la Calvin Patrick mwenye umri wa miaka nane  mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Iwambi ,Mkazi wa Mtaa wa Ivwanga Kata ya Iwambi Mkoani Mbeya amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya viatu nje ya nyumba yao.
Tukio la kujinyonga kwa mtoto Patrick limetokea majira ya saa 5.00 octobar 27 mwaka huu asubuhi katika mtaa wa Ivwanga wakati wazazi wa mtoto huyo walipokuwa wametoka nyumbani hapo na ndipo mtoto huyo alipochukua jukumu hilo zito na la aina yake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa mtaa huo Chonde Calisto alisema wakati tukio hilo linatokea Baba mzazi wa mtoto huyo Patrick Mwakapalila alikuwa ametoka na kaka mkubwa wa marehemu aitwaye Joshua kuelekea mjini kutafuta mahitaji na kwamba baada ya tukio hilo baba mzazi wa mtoto huyo alipigiwa simu na kutakiwa kurudi haraka nyumbani.

Amesema kuwa baada ya tukio baba mzazi wa mtoto huyo alipigiwa simu ili arudi nyumbani kuona tatizo lililotokea kwa mtoto wake na kwamba baada ya kufika alikuta mwanae huyo mdogo akiwa nje ya nyumba yao akiwa ananing'inia juu akiwa amejinyonga kwa kamba ya viatu"alisema.

Hata hivyo mama mzazi wa mtoto huyo nae hakuwepo nyumbani hapo kwani alikuwa katika shughuli zake za kibiashara ambako anauza duka la mahitaji mbali mbali ya nyumbani eneo la Iwambi ambako jirani na nyumbani.

Chonde amesema mpaka sasa bado hakijafahamika chanzo cha kujinyonga kwa mtoto huyo na polisi walifika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu kwa uchunguzi zaidi ili ndugu waweze kukabidhiwa mara baada ya uchunguzi huo kukamilika .


Mwisho.

serikali haijaridhishwa na ujenzi wa barabara ya kuelekea Chunya

SERIKALI imetishia kuinyang’anya kampuni ya China Communication Construction Limited zabuni ya ujenzi wa barabara ya kutoka Mbeya mjini hadi Lwanjilo wilaya ya Mbeya Vijijini yenye urefu wa kilometa 36 baada ya kutoridhishwa na kasi ya utendaji kazi ya mkandarasi huyo.




Hatua hiyo ya Serikali imetokana na mkandarasi huyo kushindwa kufikia malengo ya ujenzi huo kwa kiwango cha lami katika muda uliopangwa huku akiwa tayari ameshakabidhiwa fedha za awali za mradi huo shilingi bilioni Nane za Tanzania.



Ujenzi huo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 55 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Wahisani wa maendeleo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Mbeya mjini hadi wilayani Chunya yenye urefu wa kilometa 72.



Sehemu ya pili ya ujenzi huo kutoka Lwanjilo hadi Chunya mjini utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 44 kupitia mkandarasi mwingine.



Mkandarasi huyo aliyeanza kazi hiyo Novemba mwaka jana amechukua nafasi ya mkandarasi wa awali kampuni ya Kundan Sing iliyokabidhiwa ujenzi huo mwaka 2010 kabla ua kushindwa kuendelea na kazi kutokana na Serikali kuchelewa kutoa fedha mradi huo.



Hata hivyo tangu alipokabidhiwa kazi hiyo, kasi ya utendaji wake imekuwa ikilalamikiwa na mamlaka husika kwa maelezo kuwa ameshindwa kuifanya kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa.



Akikagua ujenzi huo Oktoba 15, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Greyson Lwenge, amesema Serikali hairidhishwi na kasi ya utendaji kazi ya mkandarasi huyo na kutishia kumnyang’anya zabuni hiyo.



“Nimetembelea ujenzi huu kwa kilometa zote 36 kutoka Mbeya mjini hadi hapa Lwanjilo, ukweli sijaridhishwa na kazi inavyokwenda, mvua zinakaribia kunyesha na hakuna mafanikio yaliyofikiwa kama tulivyotarajiwa.”



“Serikali imeshatangaza kuwa barabara hii ni lazima ikamilike kwa wakati, hivyo kama tutaona mkandarasi huyu anaendelea kusuasua, hatutasita kumnyang’anya kazi na kumtafuta mkandarasi mwingine, tunataka kazi ifanyike hatutaki maneno.” alisema Injinia Lwenge.



Hadi sasa mkandarasi huyo amenza ujenzi wa barabara hiyo katika kijiji cha Lwanjilo katika urefu usiozidi kilometa tano hali inayoitia shaka Serikali kuwa huenda isikamilike kwa wakati katika kipindi cha miezi 36 tangu alipokabidhiwa zabuni hiyo Novemba mwaka jana.



Kutokana na hali hiyo Injinia Lwenge ameiagiza Wakala wa Barabara nchini, TANROADS mkoa wa Mbeya na Mhandisi wa mkoa kuhakikisha mkandarasi huyo anatekeleza kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba uliopo pamoja na kuhakikisha barabara hiyo haifungwi wakati wa mvua ili kuepusha usumbufu kwa wananchi.



Hata hivyo viongozi wa kampuni hiyo ya China Communication Construction Limited hawakuwa tayari kuzungumza na Waandishi wa habari kuhusu hali hiyo huku wakishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kuchelewa kuanza kwa ujenzi huo wakati wakizungumza na Injinia Lwenge.



Awali mmoja kati ya viongozi wa kampuni hiyo ambao pia hawakuwa tayari kutaja majina yao, alijifanya hajui kuzungumza lugha ya Kiingereza na kutumia mkalimani kumjibu Injinia Lwenge kabla ya Naibu Waziri huyo kubaini ujanja huo na kumlazimisha kuzungumza lugha hiyo na hatimaye kufanya hivyo kwa ufasaha mkubwa.



Barabara hiyo ni miongoni mwa barabara zilizomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, CCM, ya mwaka 2010 ambapo Rais Jakaya Kikwete, aliwaahidi wakazi wa vijiji vinavyopitiwa na barabara kuwa atahakikisha inatengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuwaondoakuwa atahakikisha inatengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuwaondolea kero ya usafiri hasa wakati wa mvua.



Ubovu wa barabara hiyo umesababisha wakazi wa kijiji cha Lwanjilo kutozwa kati ya shilingi 8,000 hadi 10,000 kwenda Mbeya mjini umbali wa kilometa 36 wakati nauli ya kutoka Mbeya mjini hadi wilayani Kyela umbali wa zaidi ya kilometa 110 ikiwa ni shilingi 3,000.



Mwisho

Padre Mawasawe-Mkuu wa shirika la waconsolata aliyekufa maji kuzikwa

Jimbo kuu la Dar es Salaam linapokea kwa majonzi na masikitiko makubwa habari za kifo cha Padre Salutaris Luca Massawe, Mkuu wa Shirika la Waconsolata Tanzania, kilichotokea hapo tarehe 25 Oktoba 2012 kwa kuzama baharini, eneo la Msalaba Mtakatifu, mjini Bagamoyo nyakati za Alasiri na mwili wake kupatikana asubuhi tarehe 26 Oktoba 2012.



Kanisa limempoteza kiongozi mahiri na mchapakazi aliyetekeleza kazi zake kwa ufanisi. Kabla ya kuchaguliwa na Wanashirika wenzake hapo tarehe 7 Septemba 2011 kuliongoza Shirika nchini Tanzania, alishiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.


Anakumbukwa sana kutokana na mchango wake wa ushauri katika maboresho ya Taasisi ya Tumaini Media, ambayo iko chini ya Jimbo kuu la Dar es Salaam, inayosimamia TV Tumaini, Radio Tumaini na Gazeti la Tumaini Letu. Alikwisha wahi kufanya utume wake katika Kituo cha Sala cha Waconsolata kilichoko Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.


Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam amesema kwamba, kifo cha Padre Salutaris Lucas Massawe kimeacha pengo kubwa, ambalo halitakuwa rahisi kuweza kuzibika.Waamini wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam wanatarajiwa kufanya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Padre Salutaris Massawe tarehe 29 Oktoba 2012 kabla ya kusafirishwa kwenda Jimboni Iringa kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika hapo siku ya Jumanne tarehe 30 Oktoba 2012, kwenye Makao Makuu ya Shirika la Wamissionari wa Consolata nchini Tanzania.

Aliyekuwa Mlezi wa Chadema,Thomas Nyimbo akionesha bango alilobuni wakati akigombea ubunge lililoandikwa "MTU kwanza Chama baadaye"



Sunday, October 28, 2012

CHADEMA yapata pigo,yadaiwa kuhusika kwa asilimia 50 mauaji ya Mwangosi

Na Thompson Mpanji,Mbeya




CHAMA cha Demokrasia na maendeleo nchini(CHADEMA) kimepata pigo kubwa kutokana na kujiondoa uanachama kwa aliyekuwa mmojawapo wa wafadhiri na walezi wakuu wa chama hicho huku akidai hakuna lolote jipya zaidi ya viongozi kuangalia kuchumia tumboni.



Aidha Mlezi huyo ambaye ni mwanasiasa machachari na mkongwe,muasisi wa TANU na Chama cha Mapinduzi na amewahi kuwa Mbunge wa Njombe kupitia CCM kwa miaka 10 ,Thomas Nyimbo licha ya kutangaza rasmi kujiondoa uanachama wa Chadema kwa madai ya kupumzika siasa za vyama na kwamba watu wanaopaswa kutuhumiwa na mauaji ya mtoto wake,rafiki yake Mwanahabari Daud Mwangosi ni Polisi kwa asilimia 50 na CHadema asilimia 50.



“Ninajihudhuru na mambo ya chama nimeona hakuna jipya katika vyama hivi siyo CCM wala Chadema zaidi ya kila mmoja kuangalia malahi binafsi na siyo wawafanyie nini watanzania…ukisema wewe ni CCM damu na Nyerere je?,Viongozi wa vyama hawaambiliki,hawasikii,unakwenda kufungua tawi la Nyororo nililolifunguwa mimi Nyimbo miezi miwili,mitatu iliyopita maana yake nini, ”alisema.



Aliongeza,”sintojishughulisha na siasa nina resign Party Politics nilizaliwa Kiongozi nitabaki kuwa kiongozi wa wananchi,kama kuna jambo nitajitokeza kama kiongozi wa wananchi kukemea kwa sababu tukiendeleza u-darling darling tutaipeleka nchi pabaya,kazi ya siasa nitaifanya nje ya vyama ambapo Mu kwanza chama baadaye…nitaifanya katika church forum nitatumia legal forum.”



Alisema utafiti wake alioufanya akiwepo katika vyama vya siasa tangu alipokuwa TANU na baadaye CCM, alipoanzisha Chama cha Pona, na kuhamia Chadema ni kwamba Viongozi walio wengi wamejawa tamaa ya kujitajirisha jambo ambalo halitasaidia chochote hata kama kutakuwepo na mabadaliko kama ya (Movement for change-M4C).



Nyimbo alisema ni makosa kujenga dhana katika vichwa vya watanzania kuwa maendeleo na maisha bora kwa kila mtanzania yataletwa kwa njia ya mabadiliko M4C,haitasaidia kuondoa CCM kuleta Chadema,ondoa hiki weak kile na matokeo yake wanaweza kuwa kama senene na kuanza kujitafuna wenyewe.



Alisema pamoja na kujiondoa Chadema kama alivyowahi kujiondoa CCM na kuendelea kubaki na kadi za Umoja wa vijana wa TANU(TANU Youth league) na baadaye CCM ataendelea kubaki na kadi za chama kwa sababu ni mali yake na haki yake ya msingi na hatathubutu kukitukana chama chochote zaidi ya kukemea maovu yatakayobainika.



Alisema Chama cha Mapinduzi kinavurugu amani kutokana na kutowadhibiti watendaji wa vijiji na Kata wanaoendelea kuonekana miungu watu kwa kufikia hatua ya kuwavua nguo wanakijiji kwa kukosa mchango wa maendeleo na hivyo kuifanya CCM kuchukiwa kwa kitendo cha mtu mmoja,ihamke na isijiweke pembeni katika mamlaka iliyoomba kuwatumikia wananchi.



Alikadhalika alitolea mfano chama cha Chadema kuwa utaratibu wa kuitisha mikutano kwa ghafla bila kufuata mpangilio huku kukiwepo na matamshi kama “katika mkutano wa leo Tutapasua jipu”,tuandalieni ikulu 2015 nayo itaweza kuchochea uvunjifu wa amani kwa sababu inaajenga watu kuwa na uhakika wa kushinda na endapo hawatashinda wataleta vurugu.



Mwanasiasa huyo mkongwe alitolea mfano kwa Rais wa Zambia Chiluba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa chama cha MMD kutoka chama cha wafanyakazi wa Labour Movement kuwa alitumia Mobe justice ambapo wananci walimbeba kupeleka Ikulu lakini ndiyo hao hao waliompeleka Mahakamani baada ya kushindwa kutekeleza aliyoahidi.



“Juzi tumeshuhudia nguvu ya umma Sumbawanga iliyovyoleta athari kwa watu kuchoma moto matrekta bila sababu za msingi,nchi hii ina watanzania zaidi ya Mil.40 lakini wanasiasa hawafikii hata asilimia 10,kwa hiyo tuangalie maslahi ya watanzania na siyo ya watu wachache,ndani ya vyama siyo CCM wala Chadema ukiwashauri hiki wanafanya kile,”alisema.



Nyimbo alisema kwa muda wa miaka miwili tangu aingie chadema mwaka 2012 anaifahamu vizuri nao wanamfahamu vyema kama ilivyo kwa CCM na hatimaye kufikia hatua ya kujibizana na akina mkapa na Sumaye kwa ajili ya masuala ya umeme ambayo leo amempongeza Waziri wa Nishati na madini Prof.Mhongo amekuja kuyasema na kuyashughulikia.



“Wapo watu wanasema leo makanisa yanachomwa moto Rais hasemi mnataka aseme nini wakati IGP yupo na DI yupo?,kwa sababu Rais anaweza kuwa kuwa kipofu ama bubu lakini hao wanaweza kuiendesha nchi bila tatizo,angekuwa kila kitu anasema mngesema Rais Mlopokaji,mnaiuwa nchi vijana vyma vinatupeleka pabaya,tayari wamekufa watu 20 kwa ajili ya mikutano mseme sasa inatosha,”alisema.



Alifafanua kuwa kifo cha Mwangosi kisingetokea kama Viongozi wa Chadema wangefuata utaratibu wa kuandaa mikutano mapema na kuwasiliana na Viongozi wa Iringa na Nyororo.



“Uongozi wa Chadema unaweza kutoka makao makuu na kuja mahali bila kibali wala taarifa kwa viongozi wa maeneo husika na kuanza kutafuta kibali kuitisha mikutano huo si utaratibu,unasababisha kuhatarisha amani na ndiyo yaliyotokea Nyororo,mimi nilishalifunguwa lile tawi alipouawa Mwangosi miezi miwili mitatu iliyopita ,sasa akina Dkt.Slaa walikuja kufungua nini tena,na kibaya zaidi hata sisi Vingozi wa Iringa hatukuwa na taarifa,nasema Chadema wanahusika kwa asilimia 50,kifo cha Mwangosi,”alisema.



Alielezea kuhusu tume ya nchi kuwa angeteuliwa yeye angekataa kwa sababu wamekwenda kuchunguza ama kuthibitisha namna Nchimbi,Jeshi na wengine walivyoshiriki kufanya mauaji.



Nyimbo alisema ili nchi iweze kuendelea na kupata viongozi bora siyo bora viongozi wanaowazia matumbo kama ilivyo kwa Viongozi walio wengi wa vyama ni lazima katiba mpya ipitishe mbomgea urais binafsi ili aweze kuja kupata fursa ya kuwachagua mawaziri wasiotokana na bunge,kuwepo na sera ya taifa ya maendeleo kama ilivyo Marekani,utaifa kwanza vyama baadaye.



“Mimi nilibuni bango langu la kuogombea ubunge ukiliangalia mimi ndiye mtu wa kwaza kunadi sera ya MTU KWANZA VYAMA BAADAYE na ndiyo maana ukiliangalia bango langu bendera ya Chadema imekuwa ndogo na bendera ya taifa imebeba nafasi kubwa na nilisema nimedhaminiwa na Chadema,pia tunaomba matamshi yaangaliwe kwani ni hatari kuvuka mto kama haujafika na kuangalia,”alihitimisha.



Mwisho.



















Saturday, October 27, 2012

Mujata yaiasa jamii kushirikiana na Polisi

Na Thompson Mpanji,Mbeya




CHAMA cha Muungano wa Jamii Tanzania (MUJATA) kimewataka wanajamii wote kwa ujumla kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kukomesha maovu yanayotokea kwenye jamii mbali mbali nchini.



Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mujata kanda,Shayo Soja katika kongamano la Chama hicho ambalo limehusisha viongozi mbalimbali na wajumbe kutoka mikoa mbalimbali ya nyanda za juu kusini ikiwepo Iringa,Njombe,Ruvuma,Katavi pamoja na Mbeya.



Akizindua kongamano hilo katika ukumbi wa Royal College of Tanzania tawi la Mbeya,kamanda wa polisi mkoani hapa Diwani Athuman amesema jeshi la polisi lipo kwa ajili ya kushirikiana na Mujata ili kuhakikisha kuwa maovu yote yanayotendeka katika jamii yanakomeshwa.



Diwani amewaomba Mujata kutoa ushirikiaano wa hali na mali kwa jeshi ili kuweza kutokomeza kabisa kila aina ya uovu na amewashukuru kwa kutoa taarifa kwa jeshi la polisi katika vitendo vya ukatili vilivyowahi kujitokeza hapo awali kwa kuzika watu wakiwa hai.



Alisema vitendo vya ukatili,unyanyasaji wa kijinsia pamoja na maovu yatendekayo kwenye jamii yatakomeshwa endapo jamii haitakuwa tayari kufumbia macho vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa polisi.



Wakati huo huo,Chama hicho kimefanya uchaguzi wa kuteuwa viongozi katika nafasi mbalimbali za Chama ikiwa ni pamoja na kumpata Mwenyekiti wa pamoja na makamu wake.



Uchaguzi huo ambao umesimamiwa na kamati ya uchaguzi ya Mujata ambapo Mwenyekiti aliyechaguliwa ni Soja pamoja na makamu wake Christina Joel hao wote kwa pamoja wamekishukuru chama kwa kuwaamini kwa mara nyingine.



Mwisho.

Kardinali Pengo atamka vurugu za Tanzania asema "Kamwe msitumie kinzani, vurugu na misigano ya kidini kujinufaisha kiuchumi, kisiasa, kijamii na kidini"

 Na Thompson Mpanji

MAASKOFU waliopo katika Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya inayoendelea mjini Vatican wamesema, kati ya mambo yanayoendelea kukwamisha mchakato wa majadiliano ya kidini ni pamoja na misimamo mikali ya kiimani.



Wamesema vyanzo hivyo vinasababisha watu kutoheshimu sheria za nchi kwa kutaka kujichukulia sheria mikononi mwao pamoja na malumbano ya kidini yanayolenga kuvunja misingi ya amani na mshikamano kati ya watu wa mataifa kwa malengo binafsi,kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini.



Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar alisema , choko choko, machafuko na uharibifu wa mali kwa misingi ya kidini, zimeendelea kujionesha kwa namna ya pekee nchini Nigeria na Tanzania



Alisema hii ni kutokana na sababu kwamba, watu wanashindwa kuelewa kwamba, kimsingi hakuna dini inayoshabikia mapigano wala machafuko ndani ya Jamii.



Kardinali Pengo alisema, kuna watu ambao wanapenda kutumia tofauti za kidini kama njia ya kujijenga kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini, kiasi hata cha kuhatarisha amani, usalama, utulivu na mshikamano wa kitaifa.



Alisema hali hiyo inatokana na watu kugubikwa na ubinafsi, uchu wa mali na kupenda mno madaraka ambapo hawataki kusikia ukweli mkamilifu kuhusu masuala ya kidini, kwao jambo la msingi ni kufaidika na migogoro na kinzani za kidini.



Kardinali Pengo ametoa wito kwa Waamini wa Dini ya Kiislam na Kikristo kuendeleza moyo wa majadiliano ya kidini, kwa kuheshimiana, kuthaminiana na kujadiliana masuala muhimu ya kidini kwa ajili ya mafao ya wengi na kamwe tofauti zao za kidini zisiwe ni chanzo cha kinzani, vurugu, umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia na uharibifu wa mali ya watu.



Hata hivyo ameishauri Serikali na vyombo vya dola kutekeleze wajibu wake kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unashika mkondo wake.



Amewaonya wanasiasa wanaotumia tofauti za kidini kama njia ya kujitafutia umaarufu, ili hatimaye, kujijenga kiuchumi, kisiasa na kijamii, kuacha mara moja kwani wanaweza kusababisha maafa makubwa kwa Jamii,"Kamwe hasiwepo mtu anayetumia dini kama ngao yao katika medani mbali mbali za maisha."



Aidha Kardinali Pengo amewaomba watanzania na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba, tofauti za kidini na kiimani zimekuwepo nchini humo miaka nenda rudi, lakini watu wakaheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana na anajiuliza, kumetokea nini hata leo hii dini iwe ni chanzo cha kinzani, vurugu na machafuko nchini Tanzania?.



Amefafanua kuwa wote wanaotaka kuchochea vurugu, vita na kinzani kwamba, amani ikitoweka, hakuna mtu atakayesamilika kwani matunda ya kuvunjika kwa misingi ya haki kamwe hayawezi kudumu hivyo ni jukumu la kila mtu kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani na kamwe tofauti za kidini zisiwe ni chanzo cha kinzani, vurugu na umwagaji damu.



Mwisho.





Thomas Nyimbo awashangaa watanzania kumshangaa waziri Mulugo




MWANASIASA mkongwe nchini,Thomas Nyimbo amesema yaliyotokea kwa Naibu Waziri wa Elimu na ufundi stadi,Philipo Mulugo katika mkutano nchini Afrika ya kusini siyo ya kushangaza katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani hiyo ndiyo taswari ya viongozi wetu.



Nyimbo ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Njombe,mwasisi wa TANU na Chama cha Mapinduzi (CCM) na mlezi wa CHADEMA ameyasema hayo leo katika mkutano wake na wanahabari katika Hoteli ya Mount Livingstone,jijini hapa na kuongeza kuwa tukio la Naibu waziri Mulugo kuzungumza mambo ambayo hayaendani na nafasi yake siyo jambo jipya kwake kutokana na nchi inavyoendeshwa.



Alisema hiyo ni taswira tosha kuwa asilimia kubwa ya Viongozi wa nchi wanaoteuliwa hawana sifa ya uongozi bali wanapewa nafasi hizo kama zawadi kutokana na kufanikisha jambo fulani hali itakayoendelea kuwatafuna watanzania kutokana na mfumo na utaratibu huo.



"Hili jambo ni jipya kwa watu wasiojuwa utaratibu na mfumo mzima wa nchi,kwagu mimi siyo jipya...nimeambiwa nilete dereva nami badala yake nampeleka 'Tandiboi' unategemea nini ndiyo manaa nchi haiendi,"alisema.



Aliongeza kwa kusema hakuna sababu ya kumlaumu Mulugo kwa kuonekana kushindwa kuzungumza lugha ya kiingereza vizuri sanjari na kutoijuwa historia ya Tanzania kwa sababu wapo wengine ambao wangeshindwa kabisa hata kuongea na kuishia mabubu.



"Wanamlaumu nini huyo Waziri hii ndiyo hali halisi,afadhari hata yeye aliyejitahidi hata kuzungumza na mmesikia,wapo wengine wanaweza kunyama kwa kushindwa kuzungumza na tusingejuwa,aibu hii tuendelee kubeba,kwa sababu watamlinda,"alisema.



Baadhi ya wananchi wa jimbo la Songwe ambao ndiye Mbunge wao walisema kuwa tukio hilo limepokelewa kwa maoni tofauti kutokana na kushindwa kuamini kile kilichomtokea Mbunge wao Mulugo.



"Tunamsubiri aje atuambie,ni nini kilichomsibu,ndiyo hali halisi ya uwezo wake ama alikumbwa na kitu ambacho hatujakijuwa ni nini...lakini ili ni mojawapo ya nyundo ya kummaliza kisiasa katika uchaguzi mkuu mwaka 2015,"alisema mmoja wa wananchi hao.



Mkazi wa Kijiji cha Mkwajuni wilayani Chunya (jina limehifadhiwa ) alisema yeye ni mwanachama wa CHADEMA lakini amempongeza Naibu waziri kwa kutoa nafasi na matumiani makubwa kwa upinzani kushindwa katika uchaguzi mkuu unaokuja kutokana na kuonesha uwezo wake mdogo wa ufahamu na hivyo kushindwa kuwaletea maendeleo.



"Kama Naibu waziri wa elimu katika wizara nyeti kama hiyo haelewi hata historia ya nchi yake ataifanyia nini Tanzania na hawezi kutusaidia hata wapiga kura wake katika maendeleo kwa sababu uwezo na upeo wake unaonekana ni mdogo,na kibaya zaidi amekuwa akionekana kutumia mabavu na vitisho vingine kuongoza,"alisema.



Alisema kuwa Mulugo alifikia hatua ya kupeleka viti vya walemavu zaidi ya 200 akisema amenunua yeye pamoja na msaada wa wa visima vya maji ya kunywa vilivyofadhiriwa na mfanyabishara maarufu nchini Sabodo akidai alitoa yeye jambo linaloonesha kuwa haijapangi katika kuzungumza.



"Amefikia hatua anawaagiza watendaji wa vijiji na Kata kuwa hataki vyama vya siasa katika jimbo lake,kweli anaelewa maana ya Demokrasia?,na kila anapopita anatoa vitisho hata kwa walimu,nchi haiwezi kuongozwa kwa mtindo wa mabavu akama anavyotaka yeye,alisema.



Mwisho.