Na Thompson Mpanji,Mbeya
WATU watano wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wameuawa na
Polisi baada ya kutokea mapambano makali
ya kurushiana risasi na askari polisi.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya,kamishna msaidizi wa
polisi,Diwani Athumani amesema tukio hilo limetokea leo mei,3,2013 majira ya saa 6.00 mchana huko
maeneo ya Garijembe,Wilaya ya Mbeya vijijini katika barabara ya Mbeya-Tukuyu,mkoani Mbeya ambapo
kulitokea mashambulizi ya risasi kati
ya askari polisi na watuhumiwa wa ujambazi.
Kamanda Diwani alisema kabla ya kuanza kwa mashambulizi hayo
majambazi walishuka katika gari lenye nambari za usajili T.911 BUG aina ya
Toyota Spacio rangi ya fedha (silver) mara baada ya kusimamishwa na askari
polisi na kuanza kurusha risasi ovyo kwa askari.
Alisema kwa haraka askari walijibu mashambulizi na
kuwajeruhi majambazi hao sehemu mbalimbali za miili yao na kwamba silaha
walizotumia ni SMG 848628 ambapo kwenye magazine zilibakia risasi 16 pamoja na
silaha aina ya Mark III namba 94695J na risasi mbili sanjari na koa za shaba
zilizokutwa ndani ya gari.
Kamanda Diwani alisema watuhumiwa hao watano walikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya
Mbeya kwa ajili ya matibabu lakini
ilithibitishwa na daktari kuwa wamefariki dunia.
Aidha alisema Jeshi
la Polisi lilipokea taarifa za
kiinterejensia kuwa wapo majambazi wanaojipanga kufanya uhalifu kwa
wafanyabiashara katika maeneo na miji
ya Ushirika na Tukuyu wilayani Rungwe pamoja na Uyole jijijini
Mbeya na kwamba taarifa zilionesha
kwamba watakuwa na gari dogo.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya ametoa wito kwa yeyote mwenye
taarifa zinazohusu uhalifu na wahalifu
azitoe katika mamlaka husika kwa wakati ili zifanyiwe kazi kwa haraka.
Hata hivyo Kamnada Diwani ameendelea kutoa onyo kwa watu
wanaoendelea kutegemea kufanya uhalifu kama njia
ya kujipatia kipato kuachana na shughuli hiyo kwani hawataweza kufanikiwa.
Mwisho.