Translate

Saturday, April 23, 2011

Friday, April 15, 2011

Mashirika ya caritas nchini yametakiwa kutokuwa mzigo majimboni

Na Thompson Mpanji,Mbeya
MASHIRIKA ya caritas nchini yametakiwa kujipanga vizuri katika utendaji wa kazi ,uwazi,uwajibikaji na ushirikishwaji ili yasionekne kuwa mzigo wa majimbo ya kanisa katoliki.
Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shirika la Caritas Mbeya,Bw.Edgar Mangasila ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano mtandao wa mashirika ya Caritas kanda ya kusini (SHICANET)  wa siku moja uliofanyika katika ukumbi wa kituo cha malezi kwa vijana,kanisa katoliki,jimbo la Mbeya jijini hapa.
Bw.Mangasila amesema ili  Mashirika la Caritas yaweze kufanya vizuri katika utoaji wa huduma katika jamii na kuonekana yanafanyakazi vizuri, watendajike wanapaswa kufanyakazi kwa ushirikiano,kujipanga vizuri,kufuata miiko na taratibu za kazi na matumizi ya fedha yanayozingatia uwazi pale taarifa inapohitajika.
“Wafanyakazi wa Caritas mjitahidi msiwe mzigo wa majimbo,fanyeni kazi kwa uwazi na uwajibikaji siyo ibakie dhamira  safi tu bali  kila mtu anapohitaji kujuwa kinachoendelea akione,na hili ndiyo moja ya tatizo zinazofanya caritas nyingi zisipige hatua,kuna mashirika mengi kama Miserior ambayo yanapenda kufanyakazi nasi,hivyo tuzitumie fursa hizi,”alisema.
Ametaja sababu nyingine inayopaswa kuizingatia ni kuboresha mazingira ya watendaji,kutafuta mbinu za kutafuta fedha,mahusiano mema ya wafanyakazi na jimbo pamoja na kutekeleza  kwa muda muafaka shughuli zinazopangwa.
Mratibu wa SHICANET,Bw.Lufunyo Mlyuka amesema mkutano huo ni utaratibu wa mtandao kuwaunganisha wanachama  watendaji wa Caritas kutoka  katika majimbo nane ambayo ni Caritas Mbeya,Njombe,Iringa,Songea,Tunduru Masasi,Mahenge,Mbinga na Sumbawanga lengo likiwa ni waratibu kubadilishana mawazo na uzoefu,kuangalia changamoto,mafanikio  na mpangokazi wa Shicanet ili uweze kuwafikia wakurugenzi wote wa caritas.
Mwisho.

Mlemavu asiyeona Chunya aibuka na kudai kutibu magonjwa sugu na ukimwi

Na Thompson Mpanji,Chunya

IDADI ya wataalamu wa tiba ya kikombe inazidi kuongezeka baada ya ‘Babu’Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapila wa Loliondo, wilayani Chunya Mlemavu wa asiyeona  ameibuka  na kudai kutibu magonjwa yote sugu ukiwemo Ukimwi  ambapo maelfu ya wananchi wanamiminika kupata tiba hiyo inayodaiwa kutibu kwa muda wa siku 43.

Hata hivyo taarifa za uhakika zilizolikia gazeti hili zinasema kuwa  msaidizi wa mlemavu huyo, aliyemsindikiza kwenda kuchimba dawa hiyo anadaiwa kutouona mti huo kwa mara ya pili   baada ya kumtoroka bosi wake na kwenda katika msitu kwa lengo la kuichukua dawa hiyo ili aifanyie biashara.

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi baadhi ya wananchi wa Kijiji ch Mbuyuni wamesema wameanza kupata huduma hiyo bure  tangu,aprili,7 mwaka huu  na kwamba kuanzia jana mtaalamu huyo ameanza kutoa tiba ya kikombe kwa familia nzima kuchangia kiasi cha sh.500.

Akisimulia kuibuka kwa mtaalamu huyo mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Mbuyuni,Nico Haule amesema mlemavu huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho amedai kuoteshwa mara kadhaa na babu yake marehemu lakini alikuwa akidharau hadi ilipofikia siku  hiyo alipomuomba kijana mmoja amsindikize kuelekea katika milima ya Iseche,Tarafa ya kwimba,wilayani humo.

Msaidizi wa mtaalamu huyo,kaburi Mwankumbi alisema kuwa  aliombwa na Mahela kumsindikiza katika msitu wa milima ya Iseche na Mkwajuni na baada ya kufika huko alishangaa kumwambia walipokuwa wakielekea syo ulipo mti huo na kuelekeza eneo jingine ambapo kipofu huyo alirudi kinyume nyume na kuukamata mti huo na kumwelekeza auchimbe na kurudi nao nyumbani.

“Tulichemsha mti huo na akanywa yeye na mimi na majirani sita akiwemo mdogo wake wa kike ambaye ni mja mzito siku ya pili watu baada ya kupata taarifa walifika wengi,nami nilipoona anatoa  tiba hiyo bure nikamkimbia ili nikauchimbe mti ule na kuwauzia watu lakini nilishangaa sikuuona kabisa na niliporudi kumwambia (Mahela)alicheka,”alisema Mwankumbi.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mbuyuni,Romwad Mwashiuya amethibitisha kuibuka kwa mkazi huyo wa Mbuyuni  aliyemtaja kwa jina la Simon Patson  Mahela ambaye ni  mlemavu wa macho na anaishi kwa msaada wa kuongozwa.

Mwashiuya alisema,  baada ya uongozi kupata taarifa hiyo walifika nyumbani kwake na kuukuta umati wa watu zaidi ya 1000 wakiendelea kupata tiba hiyo na baada ya kumhoji aliwaelekeza na hatimaye  walichukuwa hatua za awali za kumuongezea vikombe kwani alikuwa akitumia kikombe kimoja kuwanyweshea watu wote,pamoja na kumpatia pipa la kuchemshia dawa sanjari na kuboresha hali ya vyoo.

Ofisa wa Afya,Bw.Nicholaus Likokolo alisema baada ya kufika katika eneo hilo wameshauri huduma za choo ziboreshwe na kwamba ingawa yupo nje kikazi lakini  amepata taarifa kuwa  mganga wa kituo cha Afya Mbuyuni amefika pia na kushauri kuchukuwa sample ya dawa na  kuipeleka kwa mganga mkuu wa wilaya ya chunya  ili  aweze kuifikisha kwa mkemia mkuu kwa uchunguzi zaidi.

Wakati huo huo,Katika mtaa wa mianzini,Kata ya mabatini,jijini Mbeya,babu mtoto jafari fikiri amesikika akiwatangazia wananchi wanaokwenda kunywa kikombe kwake kuwa mtu yeyyote atakayefika kwa nia ya kumjaribu ataona cha mkata kuni.

Taarifa hiyo amekuwa akiitoa mganga huyo kufuatia kuumbuka kwa mzee mmoja ambaye anadaiwa kufika kumjaribu na kuichafua huduma hiyo ambayo imekuwa kimbilio la wananchi walio wengi kutoka wilaya mbali mbali za mkoa wa Mbeya ambao wanashindwa kusafiri kufika katika kijiji cha samunge,wilayani Loliondo kwa mchungaji babu Ambilikile mwasapila.

Hata hivyo kuna taarifa ya kupata madhara  baadhi ya wananchi  waliokunywa  dawa hiyo  na kukiuka masharti ya kunywa pombe,kuvuta sigara,kutokunywa dawa ya aina yeyote  na kutofanya tendo la ndoa kwa muda wa siku nane baada ya kunywa vikombe viwili vya tiba hiyo.

Mwisho.

Kibaka aliyeiba Sh.10,000 yang'angania mkononi,apooza miguu na mkono

Na Thompson Mpanji,Mbozi

KIJANA mmoja mpiga debe wa magari yanayofanya safari zake Kamsamba-Mlowo wilayani Mbozi amekumbwa na mkasa wa aina yake baada ya  kudaiwa kuiba fedha  ambayo baadaye ilikutwa imenasa katika mkono wake wa kulia na miguu yote miwili kupooza huku akiwa amelazwa katika zahanati moja wilayani humo.

Tukio hilo la aina yake limetokea ,aprili,10 majira ya mchana baada ya kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Jacob Jengela kuokota fedha Sh.10,000 inayodaiwa kudondoshwa na  muhudumu wa kituo cha kuuza  mafuta kinachomilikiwa na mfanyabiashara aliyetajwa kwa jina moja la Chaula kilichopo maeneo ya Mlowo wilayani humo na kuikanyaga kwa mguu baada ya kuiona na baadaye kuificha mkononi ambapo mhudumu huyo baada ya kushtuka alipiga kelele ya kuibiwa na kijana huyo aliamua kutimua mbio lakini mbio zake ziliishia sakafuni baada ya kudondoka ghafla na kupooza.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa baada ya kijana huyo kuanguka chini huku akiwa anajizoa zoa na kuonekana anashindwa kunyanyuka wananchi wenye hasira kali walimvamia na kutaka kumchoma moto lakini askari polisi wa kituo kidogo cha Polisi cha mlowo walifanikiwa kumuokoa na kumkimbiza katika zahanati iliyotajwa kwa jina la Tumaini kwa ajili ya  uchunguzi na matibabu zaidi.

Aidha  inadaiwa kuwa chanzo cha kuanguka na kupooza miguu yote miwili na mkono wa kulia ulionasa noti hiyo  ya sh.10,000 iliyoendelea kung'ang'ania  ikiwa imenasa mkononi huku akiwa amelazwa  katika zahanati hiyo  hadi kipindi hiki kinaporuka hewani ni kutokana na imani inayohusishwa na masuala ya kishirikana kuwa fedha hiyo ilikuwa imetegwa.

Hata hivyo kipindi hiki baada ya kusasiliana na mmiliki wa kituo hicho aliyetajwa kwa jina moja la Chaula amesema anadhani kijana huyo alikuwa na matatizo ya maradhi ya muda mrefu kwani baada ya yeye kupokea taarifa hiyo alimuuliza mhuhudu ambaye alidai hakumbuki kama alidondosha fedha hiyo.

Mwisho.