Serikali ya Tanzania yatuma salam za
pongezi kwa Papa Francis
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania, Ijumaa 15 Machi, 2013 amemtumia salamu za
Pongezi Baba Mtakatifu Francis kwa kuchaguliwa kwake kuwa Khalifa wa Mtakatifu
Petro na kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki.
“Kuchaguliwa kwako ni ushuhuda tosha wa imani na heshima kubwa ambayo Kanisa
Katoliki inayo kwako, historia yako na upendo wako wa kujali na kuwapenda
wanyonge, unyenyekevu ni sababu tosha ya kuwapa Wakatoliki, wasio Wakatoliki na
wasio Wakristo pia kusherehekea uteuzi wako” Rais Kikwete amesema kwenye barua
yake ya Pongezi kwa Papa Francis .
Vatican na Tanzania imekua na uhusiano wa muda mrefu na hivyo Rais Kikwete
amemhakikishia Papa Francis kuwa uhusiano huo utadumu na anatarajia utaimarika
zaidi chini ya uongozi mpya wa Papa Francis.
Papa Francisko amtuma Kardinali Pengo
kuwaimarisha ndugu zake katika imani Visiwani Zanzibar
Kardinali
Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na
Madagascar ambaye pia ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania,
katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, hivi karibuni alipokutana na
Baba Mtakatifu Francisko, alimtuma kwenda Zanzibar ili kuwaimarisha ndugu zake
katika imani.
Kutokana na agizo hili, Kardinali Polycarp Pengo, anatarajiwa katika
maadhimisho ya Jumapili ya Matawi, kushiriki na waamini wa Jimbo Katoliki
Zanzibar kwa Ibada inayoliingiza Kanisa katika Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka,
yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Kristo.
Kardinali Polycarp Pengo anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema
kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, ili Mwenyezi Mungu aweze kumlinda na
kumwiimarisha katika utekelezaji wa malengo yake ya kitume. Papa Francisko
akiishaimarika katika imani, matumaini na mapendo, aweze pia kuwaimarisha ndugu
zake katika Kristo, hasa wale wanaoishi katika wasi wasi na hofu ya madhulumu
ya kidini. Wasikie na kuonja uwepo na sala za Baba Mtakatifu Francisko katika
hija ya maisha yao hapa duniani, kamwe wasidhani kwamba, wamesahaulika!
Mamia ya maelfu watarajiwa kuhudhuria
Ibada ya Papa Francis kuzindua utawala wake wa kitume, Jumanne: Hakuna
kiingilio wala tiketi.
Siku
ya Jumanne Machi 19, 2013, ambamo Mama Kanisa ana adhimisha Siku Kuu ya
Mtakatifu Yosefu Mchumba wa Bikira Maria, na Msimamizi wa Kanisa la Ulimwengu,
majira ya asubuhi ya saa tatu na nusu za asubuhi, (saa za Roma), Papa Francis,
ataongoza Ibada ya Misa Takatifu , kama alama rasmi ya kuzindua utume na
utawale wake wa Kipapa katika kiti cha Mtume Petro.
Mamia ya maelfu ya mahujaji na wageni wanatarajiwa kuujaza uwanja wa Kanisa Kuu
la Mtakatifu Petro, kwa ajili hiyo. waamini wote mnatagaziwa kwamba Ibada hii
ni wazi kwa wote na hakuna haja ya kuwa na tiketi kama kiingilio.
Ibada hii, itatangazwa moja kwa moja na vituo vingi vya redio, televisheni na
njia nyingine za mpya za mawasiliano, kama itakavyo sikika moja kwa moja pia
katika tovuti za Radio Vatican.
Katika Ibada hii, viongozi na Wajumbe rasmi wa viongozi wa kidini na kisiasa
watakuwepo.Vivyo hivyo Makardinali wote, Maaskofu Wakuu na Maaskofu kadhaa
kutoka pande mbalimbali za dunia, wameteuliwa kuja kuwakilisha makanisa mahalia
na kuionyesdha sura ya kanisa la Kanisa la Ulimwengu.
Na kwamba Patriaki wa Kiekuemeni wa Constantinople, Bartholomayo I, ambaye ni
huchukuliwa katika nafasi sawa na Papa katika Usharika wa Kanisa la Kiotodosi
la Mashariki,pia anatarajia kuandika historia ya mpya ya kushiriki ibada hii
kwa mara ya kwanza. Na Jumuiya ya Kianglikani duniani , inawakilishwa na Askofu
Mkuu wa York Uingereza , Dr. John Sentamu, anayemwakilishi kiongozi mkuu wa
Jumuiya hiyo, Askofu Mkuu wa Canterbury, kama itakavyo kuwa pia uwepo
wawakilishi wa imani na tamaduni zingine kubwa duniani.
Kwa dunia ya Kisiasa , kati ya wanaotarajiwa kuwepo ni pamoja na Rais wa
Argentina Cristina Kirchner, pia Rais Dilma Rousseff Rais wa Brazil, na Rais
Enrique Peña Nieto, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, na Mwana Mfalme wa
Uingereza anayemwakilisha Malkia Elizabeth 11 . Rais Obama wa Marekani
anawakilishwa na Makamu wake Joe Biden, na Gavana Mkuu wa Canada, Daudi
Johnston.
Wengine watakao kuwepo katika uzinduzi huu, ni pamoja na Kansela wa Ujerumani
Angela Merkel, Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault na Waziri Mkuu-Waziri
Mariano Rajoy wa Hispania. Na Rais wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy, na
Rais wa Tume ya Ulaya, José Manuel Barroso, wote wameonyesha nia za kuhudhuria,
kwa kutaja wachache.
Papa Francis , anazindua kazi zake kama Askofu wa Roma na Mkuu wa Kanisa
Katoliki la ulimwengu baada ya kuchaguliwa na Makardinali siku ya Jumatano
illiyopita katika kura ya siri iliyopigwa kikao cha Conlave, nyakati za jioni.
Na Ibada hii ya Jumanne , ni alama ya mwanzo kabisa ya utawala wake kama
khalifa wa Mtume Petro.
Wasifu wa Baba Mtakatifu
Francis!
Baba Mtakatifu Francis
ni Myesuiti wa kwanza kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni Papa wa kwanza katika
historia ya Kanisa kutoka nje ya Bara la Ulaya na Papa wa kwanza katika
historia ya Kanisa kutoka katika nchi za Amerika ya Kusini, nchi ambazo kwa
sasa zina idadi kubwa ya waamini wa Kanisa Katoliki. Kwa mara ya kwanza Jina la
Mtakatifu Francis linatumiwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Lakini ikumbukwe kwamba, kuna watakatifu wanne wenye majina ya Francis. Hawa ni
akina Mtakatifu Francis wa Assisi, Msimamizi wa Italia; Mtakatifu Francis wa
Sale, Mwalimu wa Kanisa na Msimamizi wa Waandishi wa Habari; Mtakatifu Francis
Xsaveri, Myesuit na Msimamizi wa Wamissionari pamoja na Mtakatifu Francis wa
Paulo, Mkaa pweke na mwanzilishi wa Shirika la Ndugu wadogo wa Calabria.
Kardinali Jorge Mario Bergoglio, SJ, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos Aires,
Argentina, alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 mjini Buenos Aires. Yeye ni mtoto
wa Mzee Mario na Mama Regina Sivori, waliobahatika kupata watoto watano. Katika
ujana wake, alisoma na kufuzu kama mtaalam wa kemia, baadaye akaacha kazi hii
na kujiunga Seminarini huko Villa Devoto.
Tarehe 11 Machi 1958 alijiunga na malezi ya Kinovisi katika Shirika la Wayesuit
akaendelea pia na masomo dunia nchini Cile na kunako mwaka 1963 alirejea tena
Buenos Aires na kujipatia shahada ya uzamili kutoka katika Kitivo cha Falsafa,
Chuo Kikuu cha San Josè huko San Miguel.
Kati ya mwaka 1964 na mwaka 1965 alikuwa ni Jaalim wa Fasihi Andishi na
Saikolojia katika Chuo cha Bikira Maria wa Santa Fe. Kunako mwaka 1966
akafundisha masomo haya kwenye Chuo Kikuu cha Salvatore cha Buenos Aires.
Kuanzia mwaka 1967 hadi mwaka 1970, alijiendeleza kwa masomo ya Taalimungu
katika Chuo Kikuu cha San Josè kilichoko San Miguel na kujipatia shahada ya
uzamili.
Tarehe 13 Desemba 1969 akapewa daraja takatifu la Upadre. Kati ya mwaka 1970
hadi mwaka 1971 alikamilisha hatua ya tatu ya majiundo yake kama Myesuit huko
Hispania na tarehe 22 Aprili 1973 akaweka nadhiri za daima. Kati ya mwaka 1972
hadi mwaka 1973 alikuwa ni mlezi wa Wanovisi, Jaalim, Mshauri na Gombera wa
Chuo cha Massimo. Tarehe 31 Julai 1973 akateuliwa kuwa Mkuu wa Jimbo la
Argentina kwa upande wa Shirika, utume ambao aliutekeleza kwa muda wa miaka 6.
Kati ya Mwaka 1980 hadi mwaka 1986, alikuwa ni Gombera wa Chuo cha Massimo na
Paroko wa Parokia ya Patriaki San Josè, Jimboni San Miguel.
Kunako mwaka 1986 alikwenda nchini Ujerumani kumalizia masomo yake katika
Shahada ya Uzamivu na wakuu wake wa Shirika wakampatia jukumu la kuwa mkuu wa
malezi ya kiroho na muungamishi katika Chuo cha Salvatore.
Tarehe 20 Mei 1992 Papa Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo
kuu la Buenos Aires, akawekwa wakfu kama Askofu tarehe 27 Juni 1992. Tarehe 3
Juni 1997 akateuliwa kuwa Askofu mwandamizi wa Jimbo kuu la Buenos Aires na
tarehe 28 Februari 1998 akasimikwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Buenos
Aires baada ya kifo cha Kardinali Antonio Quarracino na hivyo kuwa pia ni Mkuu
wa Kanisa Katoliki Argentina.
Mwenyeheri Yohane Paulo II akamteuwa na kumsimika kuwa Kardinali kunako tarehe
21 februari 2001. Ameshiriki katika Sinodi ya Maaskofu iliyofanyika kunako
mwaka 2001. Akashiriki pia kwenye mkutano wa Makardinali wakati wa uchaguzi wa
Papa kati ya tarehe 18 na 19 Aprili 2005. Alikuwa ni mjumbe wa Halmashauri ya
Sinodi ya kumi na moja ya Maaskofu kuanzia tarehe 2 hadi 23 Oktoba 2005.
Mjini Vatican alikuwa ni mjumbe wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya
Sakramenti za Kanisa, Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri, Baraza la Kipapa
la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Tume ya Kipapa ya Amerika ya Kusini,
Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri na Mjumbe wa Sekretarieti ya Sinodi.
Nchini Argentina alikuwa ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Argentina.
Rais wa Tume ya Baraza la Maaskofu kwa ajili ya Chuo Kikuu cha Kipapa cha
Argentina. Alikuwa ni mratibu mkuu wa Mahakama ya Kanisa; Mratibu wa Mahakama
ya Jimbo kuu la Buonos Aires. Tangu mwaka 2005 hadi 2011 alikuwa ni Rais wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina.
Ni mwandishi wa Vitabu vifuatavyo:
1982: Meditaciones para religiosos
1986: Reflexiones sobre la vida apostólica
1992: Reflexiones de esperanza
1998: Diálogos entre Juan Pablo II y Fidel Castro
2003: Educar: exigencia y pasión
2004: Ponerse la patria al hombro
2005: La nación por construir
2006: Corrupción y pecado
2006: Sobre la acusación de sà mismo
2007: El verdadero poder es el servicio
Baba Mtakatifu Francis ni kiongozi
anayetaka kutoa huduma kwa Kanisa la Kristo!
Padre
Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Kanisa
limempokea kwa mikono miwili, Baba Mtakatifu Francis anayetoka Amerika ya
Kusini ambako kwa sasa Kanisa lina waamini wengi wenye fursa na changamoto
katika maisha na utume wa Kanisa.
Uchaguzi wa Jina la Francis una maana kubwa katika maisha na utume wa Papa
Francis, jina amblo kwa mara ya kwanza linatumika katika historia ya Kanisa kwa
ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni jina linalobainisha unyofu na ushuhuda
wa Kiinjili, mambo ambayo yamejionesha kwa Baba Mtakatifu alipotokeza hadharani
kwa mara ya kwanza kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican
hapo Jumatano tarehe 13 Machi 2013.
Ameonesha unyenyekevu wa hali ya juu kwa kuomba sala na baraka kutoka kwa
waamini na watu wenye mapenzi mema, kabla hata ya Yeye mwenyewe kuwapatia
baraka yake ya kitume! Ni mtu wa sala, kama ilivyojionesha pia wakati
akizungumza na waamini wa Jimbo kuu la Roma. Inapendeza kuona Familia ya Mungu
inasali kwa pamoja.
Baba Mtakatifu Francis ni Myesuit na Wayesuit wanajipambanua na Watawa wa
Mashirika mengine kwa njia ya huduma kwa Kanisa, kwa kuhakikisha kwamba,
wanatumia karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya Kanisa. Uongozi ni huduma na wala si uchu wa madaraka!
Huu ndio mwelekeo unaoneshwa na Kanisa kwa wakati huu kwamba, watu wanaalikwa
kuhudumia na kwamba Baba Mtakatifu Francis ni mtu anayeonesha kwamba, kweli
anataka kulihudumia Kanisa, kwani uchaguzi wake umekuja wakati ambapo Papa
Benedikto wa kumi na sita, alipoamua kung'atuka madarakani, kielelezo cha hali
ya juu kabisa cha huduma kwa Mungu na jirani, kwa kutambua uwezo na umri wake.
Baba Mtakatifu Francis amezungumza tayari kwa njia ya simu na Papa mstaafu
Benedikto wa kumi na sita na kwamba, anaendelea kumwombea katika utume wake
kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Ataitwa "Baba Mtakatifu
mstaafu"
Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita baada ya kung'atuka rasmi madarakani hapo tarehe 28
Februari 2013, saa 2:00 Usiku ataanza kuitwa "Baba Mtakatifu
Mstaafu". Ufafanuzi huu umetolewa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu
wa Vatican baada ya wanasheria wa Kanisa kukaa na kulitafakari tukio hili la
kihistoria katika maisha na utume wa Kanisa.
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro tayari umesheheni waamini, mahujaji na
watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliofika kutoka
heshima zao za mwisho kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kama
Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Ratiba inaonesha kwamba, Alhamisi, tarehe 28 Februari 2013, Majira ya asubuhi,
Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na Makardinali ambao wamekwisha wasili hapa
mjini Roma kwa ajili ya mazungumzo ya faragha. Jioni ataagwa rasmi na Vikosi
vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican. Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa
Vatican ataongoza ujumbe wa viongozi waandamizi kutoka Vatican watakaomuaga
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kabla ya kuondoka rasmi mjini Vatican
kuelekea kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma.
Baba Mtakatifu anatarajiwa kufika jioni mjini Castel Gandolfo, na huko
atapokelewa na Kardinali Giuseppe Bertello, Gavana wa Mji wa Vatican pamoja na
Askofu mkuu Giuseppe Sciacca, katibu mkuu wa Gavana wa Vatican, Askofu Marcello
Semeraro wa Jimbo la Albano pamoja na viongozi wa Serikali. Atakapo wasili
Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, Baba Mtakatifu atatokeza dirishani kusalimiana
na wananchi pamoja na wageni watakaokuwa wamefika mjini Albano. Saa 2:00 Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, atakuwa anang'atuka rasmi kutoka
madarakani na tangu wakati huo Kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kitakuwa wazi.
Walinzi wa kutoka kutoka Uswiss ambao wamepewa dhamana maalum ya kumlinda
Khalifa wa Mtakatifu Petro, kadiri ya Mapokeo ya Kanisa, watakuwa wamemaliza
utume wao na kurudi makao makuu ya Vikosi hivi mjini Vatican. Vikosi vya ulinzi
na usalama kutoka Vatican vitaendelea kushughulikia masuala ya ulinzi na
usalama wa Papa mstaafu. Tangu wakati huo, Baba Mtakatifu hatavaa tena ile
"Pete ya Mvuvi" inayoonesha ukulu wake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro wala hata vaa tena vile viatu vyekundu alama ya ushuhuda wa imani hata
ikibidi kumwaga damu!
Padre Lombardi anasema kwamba, mwanzo mwa Mwezi Machi, Dekano wa Makardinali,
atatuma barua ya mwaliko kwa Makardinali wote ili kushiriki katika Mkutano wa
Dekania ya Makardinali utakaokuwa na dhamana ya kuanza mchakato wa uchaguzi wa
Papa Mpya. Mikutano ya Makardinali inatarajiwa pia kuanza Juma lijalo. Mikutano
hii itafanyika kwenye Ukumbi Mpya wa Sinodi.
Kutokana na sababu za kiufundi, Padre Lombardi anasema, Makardinali watahamia
kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican, siku moja kabla ya
uchaguzi wa Papa Mpya. Utaratibu wote utapangwa wakati wa mkutano wa
Makardinali. Kikanisa cha Sistina ambacho kina utajiri mkubwa wa Sanaa
kitafungwa rasmi kuanzia tarehe 28 Februari 2013 ili kutoa nafasi kwa ajili ya
maandalizi ya mchakato wa uchaguzi wa Papa Mpya.