ULE usemi usemao mfa maji haishi kutapatapa na dalili za mvua ni
mawingu umeanza kuonekana mapema katika jimbo la Songwe wilayani Chunya,
ambapo kunatarajiwa kufanyika uchaguzi mdogo wa Mwenyekiti wa Kijiji
cha saza na vitongoji viwili kutokana na wananchi kumtuhumu Mbunge wa
Jimbo hilo Philipo Mulugo kuagiza kuhakikisha Chama cha Mapinduzi (CCM)
kinashinda kwa gharama yeyote na kwa aina yeyote alimradi Jimbo hilo
lisiingie dosari ya kushikwa na vyama vya upinzani hali ambayo inaelezwa
na wachambuzi wa kisiasa kuwa ndiyo kwisha kisiasa.
Ujumbe mmoja kutoka kwa kada wa Chama cha mapinduzi (CCM)
uliofanikiwa kunaswa na gazeti hili unasema kuwa,"Nilijaribu kuongea na
usalama uchaguzi usimamishwe hadi mazungumzo ya mezani yatakapochukuwa
nafasi wakaelewa ila wansema kesho (Desemba,10) uchaguzi."
Wanaodaiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi wilayani Chunya ni pamoja
na Diwani viti maalum Kata ya Kanga,Katibu wa Chadema wilaya ya Chunya
Bryson Mwansimba,wagombea wawili wa kitongoji cha saza kati ambaye ni
Mwenyekiti wa Chadema Kata ya kanga John Mponzayo,Katibu mwenezi wa
Chadema Kata ya Kanga Suleimani Tanganyika,Katibu Mwenezi Kata,Amosi
Tanganyika aliyekuwa anagombea Mwenyekiti wa kitongoji cha Saza kibaoni,
wasanii waliofika na gari la matangazo na mpiga picha aliyefahamika kwa
jina moja la Chris.
Tafsiri hizo kwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa zimekuja kufuatia
kukamatwa kwa Viongozi,wanachama,wapenzi na watu wanaofanya kazi na
Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA),wilayani Chunya ambao
wanadaiwa kukamatwa kwa madai ya kusababisha uvunjifu wa amani na
utulivu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Mwenyekiti wa Kijiji cha
Saza na vitongoji viwili juzi.
Katika kampeni hizo zinazodaiwa kufungwa kwa amani na utulivu
Desemba,4 mwaka huu majira ya saa 11 jioni viongozi hao wanadaiwa
kukamatwa saa 9 usiku katika nyumba za kulala wageni na wengine
majumbani mwao ambapo gari tano za jeshi la polisi aina ya 110 Defender
zikiwa na askari zinadaiwa kuonekana kufanya doria mithili ya operesheni
ya kusaka majambazi lakini kumbe ilikuwa inafanyakazi kubwa ya
kuhakikisha Chama cha mapinduzi kinashinda.
"Haikuweza kufahamika mara moja kuwa kwanini kulikuwepo na askari
lukuki na gharama za mafuta na posho kwa magari na askari polisi
zinatokea wapi ingawa kulikuwepo na tetesi kuwa mamilioni kadhaa
yamemwagwa kuhakikisha lengo la kuilinda CCM linatimia,"kilisema moja ya
chanzo cha habari kutoka Saza, Chunya.
Kutokana na kuibuka kwa sintofahamu hiyo baadhi ya wachambuzi wa
masuala ya kisiasa wanasema kuwa kitendo kinachoendelea kufanyika Jimbo
la Songwe kulazimisha uchaguzi kufanyika Desemba,10,2012 licha ya
Chadema kumwandikia barua msimamizi wa uchaguzi huo Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Chunya,Maurice Sapanjo kutokubaliana na kuwepo
kwa uchaguzi huo kutokana na kukiukwa kwa sheria za uchaguzi bado
inaonesha dhahiri ni shinikizo kutoka kwa Mbunge huyo ambaye anadaiwa
kusikika akisema lazima CCM ipite kwa gharama yeyote.
"Tulisikia juu juu maneno kuwa zimemwagwa Mil.10 kuhakikisha mafuta
kwa ajili ya magari na posho za kutosha kwa watakaoendesha zoezi la
kufanikisha ushindi wa kishindo kwa CCM,mimi pia nipo mafichoni kwa
sababu ni miongoni mwa watu waliowekwa katika orodha kuwa lazima
tukamatwe na kuswekwa mahabusu kwa sababu tunatishia kibarua chake cha
ubunge lakini unadhani nini kitafuata kama siyo kuzijaza hasira
ndugu,,jamaa na marafiki zetu tunaosaidiana kwa hali na mali,hiki ni
kifo cha CCM Jimbo la Songwe," kilisema chanzo kingine.
Aliongeza, "Unajuwa mbinu wanazotumia baadhi ya wagombea ubunge za
kupita bila kupingwa ni kuwaweka sawa baadhi ya viongozi wa upinzani ili
wasisimamishe wagombea na hivyo kuonekana wanapita bila kupingwa jambo
ambalo siyo kweli huku wakidai rafu hizo zitadhihirika 2015 itakapokuja
kuanguka CCm jimbo Songwe kifo cha mende."
Akizungumza na gazeti Katibu Mwenezi wa Chama cha Demokrasi na
maendeleo(CHADEMA),wilaya ya Mbeya Lucas Mwampiki hilo alisema
walishamwamndikia barua msimamizi wa uchaguzi mdogo wa Kata ya
saza,Maurice Sapanjo ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya
Chunya kutokubaliana kufanyika uchaguzi huo kutokana na madai matano ya
ukiukwaji wa sheria za uchaguzi lakini amepuuza.
Mwampiki ambaye ni Diwani wa Kata ya Mwakibete aliyataja makosa
hayo ni pamoja na 1.kuandikisha watu wanaojuwa kusoma na kuandika 100
huku wote wanajuwa kusoma na kuandika,kutowahusisha viongozi au vyama
kujuwa na kukagua vituo vya kupigia kura,3.kutowatambulisha wasimamizi
wa vituo kwa wagombea au vyama vyao, kutopokea,kuwapa voapo wala kupokea
orodha ya mawakala wa vyama pinzani,5.kutokujibu barua za malalamiko za
wagombea au vyama kwa wakati.
Katibu huyo alitaja rafu iliyochezwa na CCM katika vituo vya
kupigia kura ni kuongeza majina bandia ya wapiga kura ambapo katika
kituo cha Saza kati wapiga kura waliojiandikisha walikuwa 96 waliongeza
majina bandia 32 na kufanya idadi kufikia 128,kituo cha Bwana mzungu
walioandikisha kihalali walikuwa 86,majina bandia 38 na kufanya idadi
kuwa wapiga kura 124,kituo cha kibao 99 majina yaliyoongezwa 27 na kuwa
jumla ya watu 126,kituo cha bwawani 98 waliongeza majina bandia 47 kwa
hiyo watu waliowaongeza ni 144 ambapo ni vituo viwili vya Mwembeni na
makambini hawakupata idadi.
"Watu walioandikishwa na kuongeza 844 kura zao (CCM)zilikuwa
744,kura za Chadema 100 walivyopanga matokeo yaani huo ndiyo ushindi
waliojipangia.wananchi wamechoma moto na kuchana karatasi za kupigia
kura baada ya kutoridhika na rafu zinazochezwa,"alisema Katibu.
Alisema hiyo ni idadi iliyotengenezwa kwa ajili ya ushindi kwa
kuchukuwa katika kura za maoni ndani ya CCM na walichoshangazwa ni
kupelekwa magari aina ya defender tano, mbili zilirudi Mbeya mjini na
tatu zilirudi chunya,wamelazimisha leo (Desemba,10)ufanyike ni
wao,vyombo vya ulizi na usalama vinahusika,kijiji cha saza kina
malalamiko ya uuzwaji wa kifusi cha mchanga wa dhahabu kwa
Sh.Mil.392,shinikizo ni kwa viongozi wakuu wa serikali na mtoto mmoja wa
kigogo kwa gharama yeyote lazima ushindi.
"Nawaonya ccm hatutarudi nyuma kudai haki za wanyonge,haturudi
nyuma kupigania haki za watanzania ndiyo wanatuchochea zaidi,ccm waache
kutegemea vyombo vya dola na kama kweli wangekuwa wanataka haki mbona
katika majukwaa yao hawasemi haki wanang'angaania amani na utulivu
,wajuwe amani na utulivu haviwezi kuja bila kutimiza ama kutekeleza
haki,navishauri vyombo vya dola waache kufanyakazi ya CCM waache
kufanyakazi kwa mazoea,wasiwe chanzo cha kuvuruga amani,"alisema.
Wakati yakiwa yametendeka,Hali ya ulinzi na usalama imezidi
kuimarishwa kuliko ilivyo kawaida kuanzia maeneo ya mji mdogo wa Mbalizi
kuelekea barabara ya Mkwajuni ndani ya jimbo la Songwe na barabara ya
kupitia Isanga Mbeya mjini kuelekea makao makuu ya Wilaya kupitia
Makongolosi hadi Sawa ambapo askari wa kikosi cha kutuliza ghasia
wametanda wakiwa na silaha za moto,mabomu,virungu huku wakiwa wamevalia
rasmi na ngao kwa ajili ya kukabili hali yeyote itakayojitokeza ya
uvunjifu wa amani.
Kwa mujibu wa mshuhuda wamesema kuwa ulinzi huo umeimarishwa
kufuatia kuwepo kwa tetesi kuwa wanachama wa Chadema kutoka Tunduma na
Mwanjelwa jijini Mbeya wamepanga kuvamia jimboni Songwe kuhakikisha
wanafanya vurugu ili uchaguzi usifanyike.
Mmoja wa wanachama wa Chadema kutoka Mkwajuni aliyejitambulisha kwa
jina moja la Mambwe,ambaye yupo katika maeneo ya Saza anasema kuwa kila
kituo kuna askari wanne wa kikosi cha kutuliza ghasia wakiwa wamevalia
sare zao rasmi,ngao,mabomu na virungu huku maofisa usalama wakiwa
wametanda kila maeneo na kuongeza kuwa ni uchaguzi unaofanywa na wanaccm
pekee.
"Hali huku siyo shwari wanafanya uchaguzi wa CCM uliolazimishwa na
Msimamizi wa uchaguzi wa Wilaya Sapanjo,amepita kutangaza leo kuwa
lazima uchaguzi ufanyike na wanapita kuwalazimisha wanachama kwenda
kupiga kura,picha za wagombea wa chadema hakuna zimebaki za wagombea wa
CCM,nikwambie mizengwe ilianza tangu Desemba,3 walimwagwa maofisa
usalama na kufuatilia kila mkutano wa Chadema,,Polisi waliingia tangu
Desemba,8 majira ya saa 10 jioni na vitisho vyao utadhani kuna
vita,"alisema Mambwe.
Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya
wilaya ya chunya,Sapanjo alipopigiwa simu hakuweza kupokea licha ya
kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kuhusu madai ya ukiukwaji wa sheria
za uchaguzi katika uchaguzi huo mdogo wa Kijiji cha saza na vitongoji
vyake viwili hakuweza kujibu.
Mbunge wa jimbo la Songwe ambaye pia ni Naibu waziri wa Elimu na
mafunzo ya ufundi,Philipo Mulugo alipoulizwa kuhusiana na madai hayo
dhidi yake alijibu kwa kuhoji"nani anayelalamika?Mimi ni Mbunge wa eneo
husika ni lazima nihakikishe chama changu kinapata ushindi mnono kwa
kufanya kampeni zinazofuata taratibu za uchaguzi,sasa hao wanaosema
mamilioni wameyaona wapi?."
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Diwani Athumani amekanusha madai ya
jeshi lake kutumika kwa maslahi ya chama chochote zaidi ya kuangalia
hali ya ulinzi na usalama na kuchukuwa majukumu yake hasa pale
inapoonekana uvunjifu wa amani na utulivu unatokea na usalama wa watu na
mali zao upo hatarini.
"Ni uzushi,nikukumbushe tu kuwa jukumu la msingi la Polisi ni
kuwalinda watu na mali zao.juzi mali ziliharibiwa Saza,watu waliumizwa
na uporaji ukafanywa.unadhani ni ipi nafasi ya ya polisi katika
mazingira hayo? Naamini kuwa mpenda amani hawezi kuwahofia
askari,"alisema kamanda Diwani.
Mwisho.