Translate

Tuesday, December 11, 2012

Mbunge wa Jimbo la Songwe akanusha kutoa mamilioni CCM ishinde

Na Thompson Mpanji,Chunya
 
MBUNGE wa Jimbo la Songwe(NEC),Mh.Philipo Mulugo amekanusha madai ya Chama cha Demokrasia na maendeleo(CHADEMA) Mbeya amemwaga mamilioni ya fedha kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinashinda katika uchaguzi mdogo wa Kijiji cha Saza na vitongoji vyake,wilayani Chunya sanjari na kuhakikisha Jeshi la polisi limewatia mbaroni viongozi wake wakiwemo na wagombea.
 
Baadhi ya wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani wamemtuhumu Mh.Mulugo kuhusika na maagizo ya kukamatwa kwa viongozi hao kuwaita maofisa usalama wa taifa waliomwagwa katika kampeni za uchaguzi huo kuanzia Desemba,3,2012 siku ya uzinduzi sanjari na nguvu kubwa iliyotumika ya magari zaidi ya matano ya polisi aina ya 110 defender na askari Polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) yaani fanya fujo uone wakivalia 'magwanda' ya kutisha na kofia ngumu (element),ngao,mabomu,silaha za moto na virungu, ambapo walifika ameneo hayo Desemba,8 majira ya saa 10 jioni.
 
Kufuatia madai hayo Mbunge Mulugo ambaye ni Naibu waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi amekanusha vikali na kuhoji "nani anayelalamika?,huku akijigamba kuwa yeye kama Mbunge wa eneo husika ni lazima ahakikishe chama chake CCM kinapata ushindi mnono kwa kufanya kampeni zinazofuata taratibu za uchaguzi, na kuendelea kuhoji kuwa wanosema amemwaga mamilioni wameyaona wapi?."
 
Katibu mwenezi wa Chadema Wilaya ya Mbeya,Mh.Lucas Mwampiki ambaye pia na Diwani wa kata ya Mwakibete jijini Mbeya amedai askari hao walimwagwa kutokana na shinikizo la Mbunge kuhakikisha CCM inashinda na kuhakikisha baadhi ya Viongozi na wanachama wanakamatwa ili kupunguza kasi ya wapinzani na waogope kwenda katika mikutano ya kampeni.
 
Amewataja Viongozi waliokamatwa na Jeshi la Polisi wilayani Chunya ni pamoja na Diwani viti maalum Kata ya Kanga,Katibu wa Chadema wilaya ya Chunya Bryson Mwansimba,wagombea wawili wa kitongoji cha saza kati ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kata ya kanga John Mponzayo,Katibu mwenezi wa Chadema Kata ya Kanga Suleimani Tanganyika,Katibu Mwenezi Kata,Amosi Tanganyika aliyekuwa anagombea Mwenyekiti wa kitongoji cha Saza kibaoni, wasanii waliofika na gari la matangazo na mpiga picha aliyefahamika kwa jina moja la Chris.
 
Mwampiki alisema walishamwandikia barua msimamizi wa uchaguzi mdogo wa Kata ya saza,Maurice Sapanjo ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya kutokubaliana kufanyika uchaguzi huo kutokana na madai matano ya ukiukwaji wa sheria za uchaguzi lakini amepuuza na uchaguzi unafanyika leo.
 
Ametaja baadhi ya mambo yaliyokiukwa ni pamoja na 1.kuandikisha watu wanaojuwa kusoma na kuandika 100 huku wote wanajuwa kusoma na kuandika,kutowahusisha viongozi au vyama kujuwa na kukagua vituo vya kupigia kura,3.kutowatambulisha wasimamizi wa vituo kwa wagombea au vyama vyao, kutopokea,kuwapa voapo wala kupokea orodha ya mawakala wa vyama pinzani,5.kutokujibu barua za malalamiko za wagombea au vyama kwa wakati.
 
Katibu huyo ametaja rafu iliyochezwa na CCM katika vituo vya kupigia kura ni kuongeza majina bandia ya wapiga kura ambapo katika kituo cha Saza kati wapiga kura waliojiandikisha walikuwa 96 waliongeza majina bandia 32 na kufanya idadi kufikia 128,kituo cha Bwana mzungu walioandikisha kihalali walikuwa 86,majina bandia 38 na kufanya idadi kuwa wapiga kura 124,kituo cha kibao 99 majina yaliyoongezwa 27 na kuwa jumla ya watu 126,kituo cha bwawani 98 waliongeza majina bandia 47 kwa hiyo watu waliowaongeza ni 144 ambapo ni vituo viwili vya Mwembeni na makambini hawakupata idadi.
 
Amesema CCM imeandaa matokeo na kufanya idadi ya watu walioandikishwa kihalali kufikia 844 badala ya 744 na matokeo wameyapanga kuwa CCM itaibuka kidedea kwa kupata kura za kishindo 744 dhidi ya Chadema watakaoanguka vibaya kwa kupata kura 100 na kwamba kijiji cha saza kina malalamiko ya uuzwaji wa kifusi cha mchanga wa dhahabu kwa zaidi ya Sh.Mil.392 walizonufaika viongozi wachache kwa hiyo ili kuepuka kashfa hiyo wameona njia pekee ni kucheza rafu.
 
.Hata hivyo Katibu huyo ameionya CCM kuwa Chadema haitarudi nyuma kudai haki za wanyonge,haitarudi nyuma kupigania haki za watanzania na matokeo yake wanawachochea zaidi kuelekeza nguvu zao Jimbo la Songwe,waache kutumia vyombo vya dola sanjari na kuvishauri vyombo vya dola kuacha kufanyakazi ya CCM waache mazoea,wasiwe chanzo cha kuvuruga amani.
 
Wakati huo huo,kumekuwepo na hofu ya uvunjifu wa amani na utulivu katika Kijiji ch Saza,Kata ya Saza,wilayani Chunya kutokana na madai ya Chama cha demokrasia na maendeleo( CHADEMA)kudaiwa kukodi makundi ya vijana,wanachama na wanaharakati kutoka mpakani mwa Zambaia na Tanzania Tunduma na Mwanjelwa ili kufanya vurugu na kuhakikisha uchaguzi mdogo usifanyike.
 
kutokana na hali hiyo hali ya ulinzi na usalama imezidi kuimarishwa kuliko ilivyo kawaida kuanzia maeneo ya mji mdogo wa Mbalizi kuelekea barabara ya Mkwajuni ndani ya jimbo la Songwe na barabara ya kupitia Isanga Mbeya mjini kuelekea makao makuu ya Wilaya kupitia Makongolosi hadi Saza ambapo askari wa kikosi cha kutuliza ghasia wametanda wakiwa na silaha za moto,mabomu,virungu huku wakiwa wamevalia rasmi na ngao kwa ajili ya kukabili hali yeyote itakayojitokeza ya uvunjifu wa amani.
 
Mmoja wa wanachama wa Chadema kutoka Mkwajuni aliyejitambulisha kwa jina moja la Mambwe,ambaye yupo katika maeneo ya Saza anasema kuwa kila kituo kuna askari wanne wa kikosi cha kutuliza ghasia wakiwa wamevalia sare zao rasmi,ngao,mabomu na virungu huku maofisa usalama wakiwa wametanda kila maeneo na kuongeza kuwa ni uchaguzi unaofanywa na wanaccm pekee.
 
Msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya,Maurice sapanjo alipopigiwa simu yake ilikuwa ikiita licha ya kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi ambao nao hakujibiwa.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Diwani Athumani amekanusha madai ya jeshi lake kutumika kwa maslahi ya chama chochote zaidi ya kuangalia hali ya ulinzi na usalama na kuchukuwa majukumu yake hasa pale inapoonekana uvunjifu wa amani na utulivu unatokea na usalama wa watu na mali zao upo hatarini.
 
Kamanda Diwani amesema ni uzushi wa watu wasiopenda amani na amefafanua kuwa jukumu la msingi la Polisi ni kuwalinda watu na mali zao na kwamba juzi mali ziliharibiwa Saza,watu waliumizwa na kufanyika uporaji kwa hiyo nafasi ya polisi katika mazingira hayo ni kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inaimarishwa na kurejesha amani na amesema anaamini kuwa mpenda amani hawezi kuwahofia askari.
 
Mwisho.

No comments:

Post a Comment