Na Thompson Mpanji,Mbeya
KANISA Katoliki Jimbo la Mbeya limelishangaa Shirika la Umeme la
Taifa (TANESCO)Mbeya kwa kuliamisha deni la umeme lenye thamani ya zaidi
ya Sh.Mil.20 na kulibambikia kanisa,kukataa umeme kwa takribani mwezi
mmoja sasa sanjari na kung’oa waya wa ‘service line’ na kusababisha
ukosefu wa umeme kwa takribani mwezi mmoja tangu mwezi Novemba,2012.
Aidha kanisa hilo limesema limeshindwa kuelewa nia ya uongozi wa
tanesco Mbeya kutokana na deni hilo huku wakiwa na majibu ya dharau,
limemuomba Waziri wa Nishati na Madini Prof.Sospeter Muhungo kuingilia
kati suala hilo na kulimaliza.
"Hatutaki kuingia zaidi kuhusina na suala hili…tunamsihi Waziri
Muhongo aingilie kati suala hili hatupendi kufika mbali …afuatilie
ataona mauza uza wanayoyafanya watumishi wake wa Tanesco ambao wanaona
kama shirika ni mali yao na kumpatia mtu deni mtu ambalo siyo haki yake
ni rahisi ,"alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya walei jimbo la
Mbeya,Magoma.
Mwenyekiti huyo alisema alipokea malalamiko kutoka kwa wapangaji wa
nyumba ambazo zinamilikiwa na kanisa Katoliki jimbo la Mbeya kuwa
wamekatiwa umeme kwa kudaiwa deni la Sh.Mil.4 na baada ya kufuatilia
walibadilishiwa na kuambiwa wanadaiwa Sh.Mil.16 na kwamba wamehamishiwa
deni hilo katika mita yao ili watoe msukumo kwa kanisa kulilipa deni
ambalo wamekuwa wakipiga chenga kulilipa.
Magoma alisema mazingira ya majibu hayo yanaonesha dhahiri kuwa
baadhi ya watumishi wa Tanesco hawajatenda haki kwa kuhamishia deni
katika akaunti ambayo haidaiwi,lakini bado amekuwa akijiuliza kama
kanisa linadaiwa Tanesco Mbeya imeshindwa nini kufuatilia badala ya
kwenda kuwabambikia deni la mamilioni watu ambao hawana uwezo wa
kulilipa deni hilo hata baada ya miaka 100 kama siyo kuwadhulumu haki ya
kupata umeme.
Bibi.Veronika Mwazembe Mkazi wa nyumba hizo kwa sasa Mtakatifu
mathias Mulumba alisema wanao ushahidi wa kulipa deni la mita
lililoachwa na watumiaji wengine iliyokuwa ikidaiwa tangu mwaka 2010 na
kuthibitishwa na ofisa wa Tanesco Mbeya aliyesaini ambapo wamelilipa
taratibu hadi kulimaliza.
Bibi.Mwazembe alisema baada ya kumaliza deni hilo mwaka 2011
walibadilishiwa mita ya luku na kuendelea kuitumia lakini katika hatua
ya kushangaza oktoba,2012 wamezuiwa kutumia huduma hiyo kwa madai ya
kudaiwa zaidi ya Sh.mil.16 jambo ambalo limewakatisha tamaa ya kuendelea
kunufaika na umeme wa shirika la Tanesco kwa madai hata kama lingekuwa
ni deni halali hawana uwezo wa kulilipa hata kwa miaka 100 ijayo.
Mkazi mwingine ambaye aliomba jina lake kuhifadhiwa kwa sababu
maalum alisema wateja wa Tanesco wanaokutwa wameiba umeme kwa
kujiunganishia isivyo halali wanachukuliwa hatua kali za kisheria hivyo
kwanini shirika hilo nalo lisifikishwe mahakamani kwa kuwalimbikizia
deni watu wasiohusika huku wakijuwa ni uonevu,unyanyasaji, kinyume na
haki za binadamu sanjari na makosa kisheria.
Alisema baada ya kufungiwa kutumia umeme walifika kutoa malalamiko
yao kwa Mhasibu wa Tanesco Mkoa aliyemtaja kwa jina moja la Mkotwe
ambaye alidai ofisa aliyekuwa akishughulikia suala hilo yupo Dar es
salaam kikazi kwa hiyo anawafungulia kwa muda kutumia umeme wakati
wakiendelea kumsubiri mhusika kuja kutatua madai hayo ya deni la
Sh.mil.4.
Alifafanua kuwa mwezi Novemba,2012 walipoenda kununua umeme wa Luku
waliambiwa wamefungiwa na baada ya kuwasiliana na wahusika wa huduma
kwa wateja wa Luku makao makuu Dar es salaama waliwaambia kuwa wanadaiwa
Sh.mil.10 katika mita moja na Sh.mil.6 katika mita nyingine jambo
ambalo liliwashtusha.
Mteja huyo alisema walishangazwa na taarifa hiyo ambayo awali mwezi
oktoba ilionekana wanadaiwa Sh.Mil.4 ambazo ziliingizwa kimakosa na
kwamba katika hatua ya kushangaza inaonesha dhahiri kuwa Mhasibu wa
Tanesco mkoa alionesha deni la awali wateja wamelikubali na hivyo
kukatwa asilimia 100 yaani asilimia 50 kwa mita moja na asilimia 50 kwa
mita nyingine jambo lililowatia mashaka kuwa Mhasibu huyo anahusika na
kuwahujumu.
Aidha alisema baada ya kuwasiliana na Mhasibu huyo aliwaambia baada
ya kufungua katika mfumo wa awali na kubadilisha masharti, wateja hao
wanatakiwa kulipia kiasi cha Sh.100,000 ama 500,000 kupunguza deni ili
wafunguliwe umeme na kuendelea kuutumia.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa kuna mchezo
mchafu unaochezwa na baadhi ya maofisa wa Tanesco kubambika madeni watu
wasiohusika ikiwa ni njia mojawapo ya kujipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu huku wakiwaacha walalahoi wakikosa matumaini na imani na
shirika lao la kitanzania.
Gazeti hili liliwasiliana na Ofisa anayehusika na udhibiti wa
madeni aliyejitambulisha kwa jina la Rehema ambaye alikiri kuwa deni
hilo siyo la wahusika wanaotumia luku lakini kutokana na kanisa katoliki
jimbo la Mbeya ambao wamenunua nyumba hizo kutoka kampuni ya Mbeya
Retco kupuuzia kulilipa deni hilo wamefikia uamuzi wa kulihamishia
katika mita ya luku inayotumiwa na wapangaji ambayo haikuwa na deni.
Ofisa huyo alisema wateja hao wanaolalamika wanapaswa kulishinikiza
kanisa kulilipia deni hilo ili nao waendelee kupata huduma hiyo
vinginevyo wataendelea kukosa huduma hiyo na kwamba hata kanisa
likibomoa nyumba hizo na kujenga nyumba nyingine deni hilo litaendelea
kuongezeka na watapaswa walilipe hata baada ya miaka 100.
Mmoja wa wafanyakazi wa Tanesco ambaye hakupenda kutajwa jina lake
kwa madai yeye siyo msemaji alisema wateja hao hawakutendewa haki kwa
sababu mmiliki wa deni hilo anafahamika ambaye ni Mbeya retco
aliyemuuzia kanisa katoliki hivyo ilikuwa ni jukumu la kuwatafuta na
kuwabana wahusika hao badala ya kuwaonea walala hoi hao.
Mfanyakazi mwingine alitoa ushauri kuwa wateja hao waonanne na
uongozi wa kanisa ambao walinunua majengo hayo na kuwaomba waende katika
shirika la Tanesco kwa kuandika barua kuwa hawakununua nyumba na madeni
hili deni hilo liingie katika akaunti ya Mbeya Retco badala ya
wapangaji hao.
Gazeti hili limepata nakala ya Ankara ya umeme iliyoandikwa" LUKU
Sms operator fungua luku meter no.01319959639 ameshalipa deni lote bado
kufuta riba chini kukiwa na sahihi yake julai,18,2011, na chini yake
kukiandikwa ujumbe mwingine uliosainiwa na ofisa mwingine ukisema ," SRA
mteja hana deni kiasi kilichobaki ni interest imeshaandikiwa bado
kufutwa."
Hata hivyo gazeti hili lilikwenda kwa undani zaidi kuangalia jina
la akaunti hiyo ambayo inatumika na wateja hao wanaodaiwa kubambikiwa ni
Mr.Prince M John P.O.BOX 109,Mbeya ambayo ilonesha kuwa na deni la
Sh.200,000 iliyopokelewa na kubakia Sh.1,566.05 katika nambari ya hesabu
Prop Ref:T87.09.09203,cust Ref:85006773.
Wananchi hao walisema kuwa matumaini ya kuendelea kupata huduma ya
umeme wa Tanesco yametoweka kabisa na kwamba wapo walala hoi kama wao
waliobambikiwa madeni kama hayo na kwamba endapo Waziri wa nishati na
madini atalivalia njuga suala hili kwa shirika la tanesco Mbeya na
kwingineko watanzania watarudi katika dhama za mkolono kutumia vijinga
vya moto na koroboi.
Meneja wa Shirika la Tanesco Mbeya,John Bandiye akizungumza na
mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu aliulizia nambari ya akaunti
ya mita na baada ya kupewa aliwaomba walalamikaji kufika ofisi ya
Tanesco ke kwa ajili ya kueleweshwa kuhusiana na tatizo hilo ambapo
baada ya kumjibu kuwa walishapewa kutoka kwa ofisa aliyekuwa
akilishughulikia suala hilo hakuweza kujibu tena hadi tunakwenda
mtamboni.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment