Moses Ng’wat na
Thompson Mpanji, Mbeya.
WATU wawili , akiwemo mtoto
mdogo wamepoteza maisha na
wengine 10 kujeruhiwa vibaya katika ajali, mkoani Mbeya , baada ya Lori
la mizigo kuzigonga na kuzitumbukiza Mtaroni
Daladala mbili zilizokuwa zimeegeshwa kituoni.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 5:30 katika eneo la
Kalobe baada ya Lori la Mizigo lenye namba za usajili T 7821 BVD lililokuwa likielekea nchini Zambia kuzigonga
gari mbili za abiria (Daladala) zenye namba za usajili T 945 AFJ na T 150
AJL zilizokuwa zimeegeshwa katika kituo
cha Njia Panda eneo la Kalobe Jijini hapa.
Kwa mujibu wa Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Ruufaa ya Mbeya,
Thomas Isidory, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba walipokea maiti ya
mtu mmoja ambaye hata hivyo jina lake halikuweza kupatikana licha ya kukutwa na
tiketi yenye jina moja la Joshua, huku kifo cha mtoto huyo mdogo kilitokea
wakati akipatiwa matibabu katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
Alisema kwa upande wa majeruhi waliopokelewa Hospitalini
hapo, walikuwa 10, ambapo kati ya hao wawili hali zao zilikuwa
mbaya na wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi wenye kuhitaji uangalizi
maalumu (ICU).
Hata hivyo Isidory
alisema kati ya hao waliolazwa chumba cha wagonjwa mahututi ni mmoja tu
aliyetambuliwa kwa jina la Jane
Mligo(19), ambaye ni mwanafunzi wa chuo cha ufundi VETA Mbeya, ambapo mwingine
hakuweza kutambuliwa mara moja.
Aliwataja majeruhi wengine nane ambao wamelazwa katika Wodi
za kawaida hospitalini hapo kuwa ni Jose Kalale (28) ambaye ni dereva wa moja
ya Daladala hizo mbili zilizogongwa zikiwa kituoni, pamoja na Kondakta wake
Elia Ambakisye.
Wengine ni Willy Claud (34), Winnie Ipyana(22), God Sanga
(23), Josia Choga (28), Said Omary (18), pamoja na mtoto mdogo, Nasra Japhary, ambaye hata hivyo
umri wake haukuweza kupatikana mara moja .
Kwa upande wake mmoja wa majeruhi hao waliolazwa hospitalini
hapo katika wodi namba moja, Josiah Choga, akisimulia tukio hilo, alisema yeye
alikuwa akitokea katika Mji wa Mwanjelwa na walipofika eneo la Kalobe Daladala
aliyopanda iliegesha kituoni wakati watu wakishuka na ghafla alisikia kishindo
kikubwa kikitokea kwa nyuma .
“Pale kituoni kulikuwa na Daladala Mbili yakwetu ilikuwa
mbele ghafla nilisikia kishindo kikubwa na nilipojaribu kugeuka nyuma
nilishangaa Daladala tuliyokuwemo ikipigwa na kuanza kubingilika hadi mtaroni”
alisimulia Chonga.
Aliongeza kuwa wakati akiwa wamefunikwa ndani ya Mtaro alishangaa
kundi la watu wakifika na kuanza kuwachomoa toka ndani ya Daladala hilo huku
akishuhudia baadhi ya abiri wakichuruzika damu nyingi mwilini mwao.
Naye Nsubiri Kibopile, ambaye ni mashuhuda wa ajali hiyo,
alisema Roli hilo liliziparamia Daladala hizo baada ya kulikwepa gari
lililokuwa likitokea mbele yake ambalo lilikuwa limebeba shehena ya
vinywaji vya moja ya kampuni ya vinywaji
baridi.
“Huyu bwana wa Roli anaonekana tayari alikuwa ameharibikiwa
na Breki hivyo akawa anashuka nalo na alipofika hapa kituoni aliojikuta
akibanwa na lile fuso lililobeba
Soda hivyo kuamua kutanua na ndipo alipozivaa zile Daladala na
kuzitumbukiza Mtaroni” Alisema Kibopile.
Hata hivyo baadhi ya askari wa kikosi cha usalama barabarani
waliokuwepo katika eneo la tukio waliozungumza na Jambo Leo kwa masharti ya
majina yao kutoandikwa gazetini kwa kuwa wao si wasemaji wa jeshi hilo, walidai
ajali hiyo ilisababishwa na Roli hilo la mizigo baada ya kuharibika mfumo wa
Breki.
“’Unajua hilo Roli lazima lilikuwa ‘limefeli’ ndio maana baada ya kuzigonga zile Daladala
lilienda kusimamia mbali zaidi ya nusu kilomita, hata hivyo tunamshukuru mungu
madhara hayakuwa makubwa kwani lingeweza kuacha njia na kwenda kuvamia nyumba ” alisema mmoja wa askari hao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment