Na Thompson Mpanji,Mbeya
WAKATI Serikali na baadhi ya mashirilka na watu mbalimbali
wakikesha na kukuna vichwa wakitafuta tiba ya maambukizi ya virusi vya
ukimwi,hali imekuwa tofauti kwa baadhi ya watanzania wasio na mapenzi
mema kwa watu wanaopata maradhi hayo baada ya kuanza kuchakachua dawa na
vyakula vya asili zinazodaiwa kuwasadia kwa asilimia kubwa kuwapatia
nafuu wagonjwa wenye maambukizi.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni serikali kupitia mamlaka husika
iliingia mzozo na hata kufikia kuzuia baadhi ya dawa zinazotolewa na
shirika moja nchini kutokana na madai ya kutengeneza dawa feki za ARVs
jambo ambalo lilileta sintofahamu na hata wahusika kuamua kutolea
ufafanuzi wa sakata hilo ambalo lilidaiwa kuingiliana na masuala ya
kisiasa na maslahi binafasi ya watu.
Wataalamu wa tiba asili nao wameanza kupaza sauti zao kupitia
vyombo vya habari kuiomba serikali na mamlaka husika kuingilia kati na
kuwadhibiti maharamia hao wa tiba na vyakula asili ambazo zimekuwa
zikiwasaidia watanzania walio wengi wenye maradhi sugu na maambukizi ya
virusi vya ukimwi kwa gharama nafuu na hatimaye kurudisha matumiani ya
kuendelea kuishi na familia zao, sanjari na kufanyakazi.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wajasiliamali wanaotengeneza
`vyakula na tiba za asili kupitia matunda ya Ubuyu na Mlonge, Racher
Alfan Mwasajone almaarufu Mama Peter,Mkazi wa Dodoma mtaa wa Makulu ya
Njedengwa alisema wameingiliwa na maharamia wa madawa na kuanza
kutengeneza bidhaa feki ambazo zimeanza kuonekana kutowasaidia tena na
kuondoa matumaini kwa watu waliokumbwa na maradhi sugu ikiwemo Ukimwi.
Mjasiliamali huyo ambaye alihudhuria maonyesho ya wajasiliamali
jijini Mbeya hivi karibuni alisema uchakachuaji huo unafanyika hasa
katika mafuta ya ubuyu na mlonge na sasa wameingia katika unga wa ubuyu
na mlonge kwa kuchanganya na unga mwingi wa mahindi ama muhogo ambapo
kwa upande wa mlonge wanachanganya na majani ambayo hayaeleweki jambo
ambalo linapunguza nguvu ya viini lishe vinavyokwenda kusaidia kinga ya
mwili na kutibu maradhi mengine zaidi ya 40.
Racher alisema watu hao wasio na chembe ya huruma wamekuwa
wakichanganya mafuta ya alizeti ama mafuta ya karanga katika mafuta ya
mlonge na ubuyu na kuuza kwa bei ya chini huku wahitaji wakiyanunua
kutokana na unafuu wa bei baada ya kupata ushuhuda ama historia ya kazi
yake lakini matokeo yake hawapati aueni aidha kutokana na kutokana na
ukosefu wa viini lishe katika bidhaa hizo feki ama vitu
vinavyochanganywa kuwa sumu na kuuwa viini lishe.
Amefafanua kuwa ili kubaini mafuta ya ubuyu ama mlonge yaliyo safi
ni vema kuangalia wepesi wa mafuta wakati wa kuinamisha chupa iliyokuwa
na mafuta chini juu ambapo kwa unga wa ubuyu utajulikana kuwa ni halisi
kwa kupata radha halisia ya ubuyu ambapo kwa majani ya mlonge hayana
ukali na unga wake unanukia harufu nzuri ya kipekee inayomshawishi
mtumiaji kunywa ama kulamba.
Hata hivyo Racher ametoa wito kwa serikali kupitia mamlaka husika
kufuatilia kwa kina uhalifu huo na kuudhibiti kwani unaweza kuleta
madhara makubwa kwa watumiaji wanaohitaji kupata tiba na hatimaye
kuendelea kupoteza nguvukazi ya taifa kwa uzembe,makosa na tamaa ya watu
wachache wasio na mapenzi mema na watanzania wenzao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment