Na
Thompson Mpanji,Mbeya
SAKATA
la mwanamke mmoja Mkazi wa Mtaa wa Ikuti,Kata ya Iyunga, jijini Mbeya
kutuhumiwa kumuuza mtoto aliyemzaa mwenyewe kwa raia wa kigeni wanaomiliki
kituo kimoja cha watoto yatima cha jijini hapa limezidi kuchukuwa sura mpya
kunaswa na mwandishi wa habari hizi akiwa mafichoni na kuweka mambo hadharani
huku anayedaiwa kuwa msimamizi wa kituo cha Care and Share-Children's home
Anna Kasile akiibukia katika semina ya Makatekista akikiri kumsaidia mwanamke
huyo na amekuwa akizushiwa kuuza watoto.
Aidha
Anna Kasile ambaye anadaiwa kuwa ni mama mkubwa,msimamizi wa kituo aliyedaiwa
kuwa muda wote na wazungu hao amepasua ukweli katika semina ya Mapadre,watawa
wa kike na kiume na makatekista kuhusu kilichotokea.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi,Amina Nganile (29)ambaye anafanyakazi ya kupika
chakula katika mgahawa wa baa moja iliyopo katikati ya Mwanjelwa na Kabwe
(jina tunalihifadhi),jijini hapa alikiri kuingia mkataba wa kutunza mimba na
wazungu waliopelekwa na Mama yake mkubwa (Anna Kasile) baada ya kuuguwa
nusuraya kufa.
Amina
alisema yeye ni mama wa watoto wawili akiwemo Agapto mwenye umri wa miaka
minne na huyo aliyemzaa Novemba,2013 ambaye anatunzwa katika kituo cha care
and share cha Simike kinachosimamiwa na Kasile ambaye ni mama yake Mkubwa.
"Sina
hamu na wanaume kwa sababu aliyenizalisha awali hamtunzi mtoto na huyu
aliyenizalisha anaitwa Amos Mfanyakzi wa stela Farm ni mkazi wa Kyela
hajanitunza wakati wa mimba,niliugua nusura nipoteze maisha na hivyo nilitaka
kuitoa lakini Mama Kasile alinisaidia kunipeleka Hospitali wakanipima Ultra
Sound na kukuta mtoto yupo hai nami nikatibiwa hadi kupona na nikajifunguwa
salama,"amesema.
Ameongeza"nilijifunguwa
mtoto wa kiume mwenye uzito wa kilo tatu na siyo kilo nne na kwamba nilikaa
naye baada ya muda nikawakabidhi mtoto waende kumtunza na mimi nililazwa na
baadaye nikatoka na ninaendelea vizuri na mtoto ninakwenda kumuona."
Alipoulizwa
kuhusu mkataba wa kumtunza mtoto hadi baada ya kufikia umri wa mika 18 ndipo
atamchukuwa alikiri na kusema ni bora aendelee kukaa huko huko kwa sababu
hali yake kiuchumi ni mbaya hata kufikia kudaiwa fedha za mkopo alizokopa
katika shirika la mikopo la Eclof Mbeya baada ya kuuguwa na mdogo wake
kuufilisi mradi wa mkaa aliomuachia.
"Nilikuwa
na stoo ya Mkaa nikiuza kwa madebe na magunia lakini baada ya kuuguwa
nilimkabidhi mdogo wangu aendeshe biashara hiyo lakini ilikufa,kwa hiyo
nililazimika kuuza kila kitu changu na sasa ninaishi kwa rafiki yangu
Nzovwe,hapa nimepata kibarua ninalipwa Sh.2,000 kwa siku sh.1400 pesa ya kula
na Sh.600 pesa ya nauli ya dala dala,hali ni mbaya na ninashindwa kulipa
deni,"amesema.
Hata
hivyo Amina alisema hataki kusikia juu ya wanaume kwa sababu ni wauaji
wanapokutaka kimapenzi wana ahadi lukuki lakini baada ya kujifunguwa
wanakukana hali inayoweza kusababisha kujiuwa ama kufanya jambo lolote baya
kwa hasira baada ya kuchanganyikiwa na anamshukuru Anna Kasile kwa kumnusuru
yeye na mtoto wake.
Anna
kasile akitoa mada inayozungumzia utetezi wa uhai alisema tangu ajiunge na
mikakati hiyo ya kunusuru maisha ya watoto na Prolife amekuwa akikumbana na
mikasa mingi ikiwemo kuhojiwa na watu wa ikulu kuwa anajishughulisha kuuza
watoto anaowaokota jambo ambalo siyo la kweli.
Akizungumzia
suala la Amina amesema baada ya kusikia anataka kutoa mimba kutokana na
kutomjuwa mwanaume aliyempa uja uzito huo alilazimika kumsaiia na kuzungumza
na wazungu akina Kaufmann waliokubali kumtunza na kumuuguza hadi akapona na
kujifunguwa salama na kwamba mtoto yupo hai anaendelea kulelewa katika kituo
chake hadi atakapofikia miaka 18 atamchukuwa.
Amesema
walilazimika kufika kwa Mwanasheria Mwakolo kwa ajili ya kuwekeana mkataba wa
kumtunza mtoto huyo ambapo amedai walilazimika kutoa sh.100,000 kama ada
baada ya kuomba kupunguziwa kutoka Sh.150,000.
Wakili
Mwakolo hakuweza kupatikana licha ya kumuomba miadi ya kuonana naye kupitia
simu yake ya kiganjani baada ya kuomba ufafanuzi wa sheria iliyotumika katika
makubaliano ya mkataba wa kutunza mimba sanjari na kufika ofisini kwake
januari,29 na 30,2013 bila mafanikio ya kuonana naye.
Ofisa
wa Idara ya ustawi wa jamii Mkoa wa Mbeya,Tobias Mwalwego akizungumza na
KIONGOZI amethibitisha kupokea mkataba wa makubaliano kutoka kwa wasamaria
wema waliolalamikia suala hilo na kwamba kwa kifupi hawakifahamu kituo hicho.
"Leo(januari,30)
asubuhi tulikuwa tunajadili mkataba huo ni kitu cha kushangaza wala hakipo
katika sheria na taratibu za kuasili mtoto,na ukiangalia kipengere cha nne
cha masharti hayo(Kwamba baada ya mtoto kufikisha umri wa miaka 18 MAMA MZAZI
ataruhusiwa kumchukuwa mtoto wake) hakiingii akilini kwa sababu atakosa haki
za msingi za malezi na mapenzi ya mama,wakati Mama yake yupo,"amesema.
Aidha
Ofisa huyo amesema hana uhakika kama kituo cha Care and Share-children's home
kama kimesajiliwa kisheria kwa sababu katika idara ya ustawi wa jamii Mkoa wa
Mbeya haikitambui wala shughuli zao licha ya mtu aliyefika ofisini kwake
kujitambulisha kwa jina la Melvin Kauffman kama Ofisa utawala wa kituo hicho
kilicho chini ya Shirika la Harmony International (januari,30,2013).
"Leo
amekuja mgeni mmoja akiwa na familia yake akajitambulisha kuwa ni Melvin
Kauffman kuwa ni Ofisa utawala wa kituo cha Care and Share kilichopo Simike
na kwamba alikuwa anaomba idhini ya kumchukuwa mtoto mmoja yupo Hospitali ya
Rufaa Mbeya kitengo cha uzazi Meta kwa ajili ya kumlea na kwamba anawatunza
watoto kama hao watatu ambao wanaonekana wakubwa lakini huyo mtoto anayedaiwa
kuchukuliwa baada ya mkataba hayupo katika orodha ya watoto aliowaonesha
katika picha na maandishi,"amesema Mwalwego.
Amesema
kuwa amemjibu Melvin kuwa kabla ya kumchukuwa huyo mtoto aliyekuwa Hospitali atalazimikia
kufika katika kituo chake ikiwemo na kufuatilia suala la mkataba wa Amina
Nganile na baadaye kujiridhisha kama kituo hicho kimesajiliwa kisheria na
taratibu za kuwachukuwa na kuwatunza watoto hao kama zimefuatwa.
Kamanda
wa polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani ameahidi kulifuatilia suala hilo na
kujuwa ukweli na undani wake ili kama kuna tatizo liweze kushughulikiwa na
endapo kuna makosa ya kisheria, sheria iweze kuchukuwa mkondo wake.
Mwisho.