Na Thompson Mpanji,Mbeya
MWANAMKE mmoja Mkazi wa Mtaa wa Ikuti,Kata ya Iyunga, jijini Mbeya amedaiwa kumuuza mtoto aliyemzaa mwenyewe kwa wazungu wanaomiliki kituo kimoja cha watoto yatima cha jijini hapa ambao hadi sasa haieleweki walipo pamoja na kichanga chake kiume kinachodaiwa kuzaliwa kikiwa na uzito wa kilogramu nne.
Tukio hilo ambalo limewasikitisha wananchi walio wengine linadaiwa kutokea mwanzoni mwa Novemba,2012 ambapo makubaliano yanadaiwa kufanyika mwezi,oktoba,2012 katika maeneo ya Ikuti mbele ya mashahidi likiwepo kampuni moja la mwanasheria wa kujitegemea la jijini Mbeya.
Mwenyekiti wa mtaa wa Ikuti,Kata ya Iyunga,Immanuel Mwasote amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kumtaja mwanamke huyo kuwa ni Amina Nganile ambaye alikuwa akiishi katika mtaa huo na alikuwa mjazito na wenzake kuthibitisha alijifungua salama lakini baada ya siku mbili alionekana bila mtoto jambo lililowashtusha wengi na kumfikisha ofisini kwake kwa kesi mbili.
Mwasote amesema Amina alifikishwa ofisini kwake na wanakikundi wenzake wa kikundi cha Tumaini kwa madai ya kushindwa kurejesha deni la mkopo katika shirika la Eclof sanjari na kumhoji alikompeleka mtoto ambapo alijibu yupo ustawi wa jamii akiendelea kulelewa .
“Kutokana
na majibu hayo tuliingiwa wasiwasi na ndipo tukampeleka katika kituo
cha polisi Iyunga kwa mahojiano na baadaye walimwachilia,kwa hiyo tuliwaachia polisi waendelee na uchunguzi na baadaye amehama mtaa wangu sijuwi alipokwenda,”amesema.
Akizungumza na Mwandishi wa gazeti hili Msimamizi wa kikundi Tumaini ,Winfrida Nzunda amesema mwenzao huyo alipokuwa mjamzito walikuwa wakija wazungu na gari ambalo nambari zake hawakuzishika na kumchukuwa kumpeleka kuhudhuria kliniki katika Hospitali ya Ifisi na kumrudisha hadi alipojifungua na kulazwa siku moja na kutoka bila mtoto.
Winfrida amesema baada ya kumhoji alielezea kuwa baada ya kujifungua hakuiona sura ya mtoto wake baada ya kuchukuliwa na wazungu hao ambao walikuwa wanawake wawili na wanaume watatu zaidi ya kumfahamisha kuwa amejifungua mtoto wa kiume mwenye uzito wa kilo nne na kwamba hadi leo haelewi alipo mtoto wake na wazungu hajawaona tena.
“Lakini baada ya kumbana sana alituambia kuwa Mama yake huyo aliyemtaja kwa jina la Mama Kasile anayesimamia kituo cha kulelea watoto cha For Care & Share-Children’s Home kilichopo Simike jijini Mbeya ndiye aliyemshawishi kuwekeana mkataba na wazungu hao kumhudumia hadi atakapojifunguwa baada ya kutomjuwa mwanaume aliyempa mimba na ndipo watamchukuwa mtoto kumlea hadi baada ya miaka 18 watamrejesha kwake,”amesema.
Msimamizi huyo wa kikundi amesema kuwa baada ya kumbana zaidi aliwaeleza kuwa mkataba wa kumhudumia ulimalizika baada ya kujifungua na hivyo wazungu hao walimchukuwa mtoto huyo na kwamba alipotoka Hospitali alikwenda kwa Mama Kasile ambako alihudumiwa kwa siku nne na baadaye kufukuzwa kwa madai akajitegemee.
Amesema mwanamke huyo amethibitisha kuwa amedhurumiwa fedha na Mama huyo kwani ana imani amepewa fedha nyingi na kwamba katika hatua ya kushangaza akifika kumwangalia mtoto anaoneshwa wale waliokotwa na kupewa muda wa dakika mbili aondoke jambo ambalo linathibitisha kuwa mtoto wake ameshatoroshwa kwenda mashariki ya mbali.
Hata hivyo Winfrida amesema kuwa baada ya tukio hilo mwanamke huyo amehama hapo mtaa wa Ikuti na haileweki anapoishi maeneo ya Nzovwe na wanaendelea kumsaka kutokana na kushindwa kurejesha deni la zaidi ya Sh.370,000 katika shirika la mikopo la Eclof na hivyo wanahofia kufikishwa mahakamni kutokana na deni la mwenzao huyo.
Meneja wa shirika la mikopo midogo la Eclof tawi la Mbeya,Magdalena Lekaaya amethibitisha kukopeshwa Amina Nganile mkopo wa Sh.400,000 na kutakiwa kurejesha Sh.79,000 kila mwisho wa mwenzi pamoja na wanakikundi wenzake lakini baadaye hakuonekana hadi wanakikundi walipomkamata.
Amesema baada ya kumhoji na kumtania kwanini ameshindwa kurejesha mkopo ilhali ameshamuuza mtoto alikiri na kudai hajapewa hata senti moja na kwamba hana uwezo wa kulipa deni wamfikishe kokote na hivyo kumuona kama amechanganyikiwa na kumwagiza aende kutafuta hela hiyo chini ya udhamini wa wanakikundi wenzake lakini hajaonekana.
Baadhi ya ndugu,jamaa na marafiki wa Amina kutoka katika kijiji cha Isongole Umalila,wilaya ya Mbeya vijijini wakizungumza na gazeti hili wamesikitishwa na kulaani vikali tukio hilo na kjuiomba serikali iweze kuchukuwa mkondo wake.
Gazeti hili linayo nakala ya mkataba wa makubaliano ya kumuuza mtoto huyo baada ya ‘wazungu’ hao kutunza mimba ya mwanamke huyo aliyetajwa kwa jina la Amina Paulo Nganile na mtoto atayezaliwa hadi afikie umri wa miaka 18.
Nakala ya mkataba huo una masharti sita yaliyoainishwa katika kutimiza makubaliano yaliyofanywa
Oktoba,5,2012 kati ya kituo cha kulea watoto maarufu “Watunzaji’ Care
& Share-Children’s home wa S.L.P. 573,Mbeya-Tanzania,East Afrika
Phone No.0252502749 na Amina Paulo Nganile anayeishi karibu na Itende
JKT,eneo la Nzovwe,Mbeya ambaye kwa upande mwingine anaitwa MAMA MZAZI.
Sehemu
ya makubaliano hayo yameandikwa kama ifuatavyo:” kwamba watunzaji ni
wenye kumiliki kituo cha kulelea watoto wadogo chini ya umri wa miaka
18,kwamba kwa hiari yao watunzaji na kwa hiari ya MAMA MZAZI ambaye ni mjamzito wamekubaliana kuwa MAMA MZAZI atatunzwa na kituo hicho yeye mwenyewe na kusaidia gharama za kujifungua mtoto.
“Kwamba baada ya mtoto kuzaliwa ‘watunzaji’ wataendelea kumtunza mtoto
atakayezaliwa mpaka atakapofikia umri wa miaka 18,kwamba baada ya mtoto
kufikisha umri wa miaka 18 ‘mama mzazi ‘ataruhusiwa kumchukuwa mtoto wake,kwamba matunzo kwa mama mzazi yatakoma mara baada ya kujifungua.”
Sharti la sita limesema,” kwamba MAMA MZAZI hamjuwi aliyempa mimba na hivyo hana uwezo wa kutunza mimba na mtoto atayezaliwa hivyo anakubali kuwa mtoto atayezaliwa atunzwe na ‘watunzaji ‘hadi atakapofikia umri wa miaka 18.”
Aidha sehemu ya mkataba huo imesema makubaliano hayo yametiwa sahihi na wahusika wote mbele ya mwanasheria ambaye ni Melvin
Kauffman wa For care & share-children’s home na ‘Mama Mzazi’ Amina
Paulo Nganile na shahidi aliyeandikwa kwa jina la Anna Kasile mwenye
nambari ya simu 0754 615021 mbele ya Wakili kutoka kampuni ya Mwakolo
and Co.Advocates,P.O.BOX 2908,Mbeya-0754052231 ikiwa imewekwa na mhuri
wa kampuni hiyo ya mwanasheria wa kujitegemea.
Jitihada za kumtafuta ‘mama mzazi’ ambaye ni mama wa kichanga cha kiume kilichozaliwa na uzito wa kilo nne zinaendelea ili kupata ukweli wa tukio hili ambapo anayedaiwa mama mkubwa aliyemshawishi kumuuza mtoto huyo alipopigiwa simu na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo alijibu kwa jazba kuwa hasipotezewe muda
Anna Kasile ambaye anadaiwa kuwa ni mama mkubwa,msimamizi wa kituo aliyekuwa muda wote na 'wazungu' hao alimwambia mwandishi wa habari hizi kuwa amuulize vizuri Amina sababu ya yote hayo na ikiwezekana amtafute aende naye kituoni hapo.
Kasile amesema amehojiwa na watu wengi ikiwemo
waandishi wa habari na polisi kwa hiyo amechoka kujieleza, hawezi
kupoteza muda kwa ajili ya masuala ya kipuuzia na hatimaye alikata simu
na alipopigiwa zaidi ya mara nne alikata simu licha ya kutumiwa ujumbe
mfupi wa maandishi kufafanua tuhuma dhidi yake kuwa amekuwa na kawaida
ya kuwauza watoto anaowaokota wametupwa na kuwalea hakujibu.
Jitihada za kuwasiliana na Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya,Diwani Athumani,a Kampuni ya Wakili Mwakolo(Mwakolo and Co. Advocates) na Ofisi ya ustawi wa jamii Mkoa wa Mbeya kujuwa utaratibu wa kuasili watoto na mkataba wa makubaliano zinaendelea.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment