Wabunge wa Kenya wajiongezea marupurupu kibao kabla ya kuvunjwa kwa Bunge!
Wananchi wengi wa Kenya wanauangalia muswada huu kwa jicho la makengeza, wakati wanasubiri kama utapishiwa na Rais Mwai Kibaki ili uweze kuwa ni sheria. Katika muswada huo, Rais wa Kenya baada ya kumaliza utumishi wake, atakabidhiwa kitita cha jumla ya shilingi za Kenya millioni 12.6. Baadhi ya wananchi wa Kenya waliohojiwa wanasema kwamba, katika muswada huu Wabunge wameshindwa kuonesha uzalendo kwa nchi yao na badala yake wamejizamisha katika uchu wa mali na heshima, ingawa baadhi yao wanaendelea kushutumiwa kwamba ni mafisadi, wala rushwa na wazembe.
Waziri mkuu wa Kenya, Raila Odinga anasema, Wabunge wanapaswa kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa wananchi waliowapigia kura badala ya kujiingiza katika tamaa ya kupenda fedha mno, inayoweza kuhatarisha amani, usalama na ustawi wa nchi. Hata baada ya kung'atuka madarakani bado wabunge wanataka wapewe ulinzi? Baadhi ya wananchi wanaendelea kuhoji! Wamesahau kwamba, kuna watu wasiokuwa na hatia nchini Kenya wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na ukosefu wa ulinzi na usalama! Lakini wao, jambo hili wanalifumbia macho na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa masilahi yao binafsi.
No comments:
Post a Comment