Translate

Tuesday, January 15, 2013

wazazi wahoji ukimya wa serikali kuchangishwa sh.24,500 kuandikisha mtoto darasa la kwanza shule ya msingi Muungano Mbeya na kuchangishwa ndoo,majembe,mafyekeo,madawati na rim Sekondari za kata vinakwenda wapi ?

Na Thompson Mpanji,Mbeya
 
BAADHI ya wazazi jijini Mbeya wamehoji ukimya wa serikali katika kuhusu malalamiko yao ya utozwaji wa fedha za madawati na michango mingine  katika zoezi zima la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa mwaka 2013 katika shule mbalimbali zikiwemo za msingi na Kata.

Aidha wazazi hao wamehoji  vinakopotelea baadhi ya vifaa vinavyoagizwa na wakuu wa shule za sekondari za kata kwa kila mwanafunzi kupeleka majembe,Madawati,fyekeo,ndoo na bunda la karatasi(Rim) kwani imekuwa ni kero kubwa.

"Kila mwaka walimu wanaagiza wanafunzi wanaofika kuanza kidato cha kwanza katika sekondari za kata kwenda na vifaa hivyo,hayo majembe ukienda kuangalia stoo zao hakuna wanayapeleka wapi,wanaagiza ndoo mpya lakini hata bustani ya kumwagilia hawana,alisema Mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Johnson Mwambepo,mkazi wa Forest.

Mzazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Richard mngoni mkazi wa Kata ya Ruanda alihoji fedha wanayotozwa kiasi cha Sh.24,500 kwa ajili ya kumwandikisha mtoto darasa la kwanza katika shule ya msingi Muungano,jijini Mbeya.

Alisema yeye(Richard) yupo kitandani kwa muda wa mwezi mmoja sasa akiwa anasumbuliwa na homa lakini ameshangazwa kupelekewa taarifa na mke wake aliyempeleka mtoto kuandikisha darasa la kwanza katika shule hiyo iliyopo maeneo ya Stereo kuwa zinahitajika fedha hizo ilhali  hajafanyakazi ya kuingiza fedha kutokana na kuuguwa.

Wakati wazazi hao wakilalamikia hali hiyo serikali ya mtaa  wa Ilomba,jijini Mbeya nayo imelalamikiwa kwa kuwatoza Sh.12,500 mchango wa kuandikisha jina  la kuingia darasa la kwanza mwaka 2013.
 
 
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wazazi (majina yamehifadhiwa)walisema kuwa wameshangazwa  viongozi wa serikali ya mtaa kuandikisha majina ya watoto kwa kutoza sh.12,500 na kwamba mzazi asiyekuwa na kiasi hicho mtoto wake hawezi kupokelewa.
 
Walisema wameambiwa kuwa mzazi ambaye hataweza kutoa fedha hiyo mtoto wake hawezi kusoma shuleni hapo na endapo atakubaliwa basi atatakiwa kukaa chini kwenye vumbi hatoruhusiwa kukalia dawati jambo ambalo wamedai ni unyanyasaji.
 
Mmoja wa wajumbe wa serikali ya mtaa wa Ilomba,Edwin Kamweli alisema hizo ni mbinu chafu za baadhi ya wanasiasa kutaka kuzorotesha maendeleo ya mtaa wa Ilomba kwani mkutano wa hadhara ulikaa na kukubaliana wanannchi wote kutoa mchango huo kwa ajili ya kuboresha mazingira ya shule.
 
"Huu mfumo wa vyama vingi utaturudisha nyuma tukiendekeza maneno bila vitendo…kuna watu wavivu wanatumia fursa ya demokrasia kuturudisha nyuma na sisi tunasema hatuwezi kukubali na haiwasaiidii tunasonga mbele…vikao na mikutano ikiitishwa wanasema wapo bize tuikipitisha maazimio wanasema tunawaonea,"alisema.
 
Kamwela alisema kiasi hicho cha sh.12,500 kilipitishwa na wananchi waliohudhuria mkutano mmoja wa hadhara ikiwa na lengo la kuboresha mazingira ya shule na wanafunzi ili waweze kusoma bila kubanana.
 
Alisema mgawanyo wa fedha hiyo ni Sh.10,000 kwa ajili ya dawati litakalochangiwa na wanafunzi watatu watakaolitumia ambapo kila mmoja atachangia kiasi hicho na kukamilisha gharama ya ununuzi wa dawati moja kwa Sh.30,000.
 
Mwalimu huyo mstaafu aliendelea kufafanua kuwa katika shule hizo mbili za Kagera na Ruanda Nzwovwe kuna mlinzi anayelipwa na hivyo kila mzazi wamekubaliana achangie Sh.1,500 ambapo mchango wa maji ni Sh.1,000.
 
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilomba,Erasto Mwakapoma alifafanua kuwa uandikishwaji ni bure lakini michango hiyo ilitokana na wananchi wenyewe baada ya kukaa katika mkutano wa hadhara wa mtaa wa Ilomba Novemba,30,2012 ambapo yeye alikaribishwa na kwamba wanaochangia ni wananchi wote na siyo wazazi wanaowaandikisha watoto shule pekee.
 
Mwakapoma alisema shule ya msingi Kagera na Ruanda Nzovwe zinatarajia kuandikisha watoto zaidi ya 200 ingawa lengo lilikuwa watoto 130,lakini hawatoweza kukataa kuwaaandiskisha watoto waliofikia umri wa kwenda shule hivyo kunahitajika madawati ya ziada.

Hata hivyo baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya walisema endapo kila mwaka  wanafunzi wanaenda na madawati mapya ama kulipia gharama ya madawati kusengeendelea kuwepo kwa tatizo la madawati na vifaa  vingine kutokana na michango inayotolewa wakati wa uandikishwaji wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment