Na Thompson Mpanji,Mbarali
WANAFUNZI wa Kata ya
Mahongole na Mwatenga,wilayani Mbarali wameuomba uongozi wa Halmashauri ya
wilaya hiyo kuchukuwa jitihada za dhati kuwasaidia kuwajengea shule za Sekondari
maeneo ya jirani na makazi yao ili kuepusha
madhara yanayoweza kuwakumba hasa kwa wanafunzi wa kike kutokana na
kutembea umbali mrefu katika
vichaka zaidi ya kilomita 14
hadi kufikia shuleni.
Mwito huo umetolewa na
wanafunzi hao walipokuwa wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Kata hizo ambapo wanafunzi kutoka Kijiji cha Sonyanga
wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya
nane hadi shule ya sekondari ya Kata ya Ruiwa,Ilongo zaidi ya Kilimota 10,Kapyo umbali wa zaidi ya
kilimota 14,Igalako na Mahongole Kilomita zaidi ya tatu,Muwela kilomita zaidi
ya saba na Mwatenga umbali wa kilomita
zaidi ya 10.
Wanafunzi hao walisema,
wamekuwa wakichoka na kushindwa kumsikiliza mwalimu vyema baada ya kutemebea umbali mrefu ,wanafunzi
wa kike wamekuwa wakihofiwa kubakwa vichakani huku wengine wakielelezea hofu
yao ya kuuawa kutokana na kuibuka kwa matukio
ya mauaji ya kushtukiza na kutulia yanayokuwa yakitokea wilayani humo
jambo ambalo wamedai linawakosesha raha
na mori wa kuendelea na masomo.
Ofisa Mtendaji Kata ya Mahongole,Juma Mangula amethibitisha kuwepo kwa matatizo hayo
kutokana na wanafunzi wa Kata ya Mahongole na Mwantenga kutegemea shule ya
Sekondari ya Kata ya Ruiwa ambayo awali ilijengwa wakati wa Kata moja
lakini kwa sasa kuna uhitaji mkubwa wa
shule.
Mangula alisema jitihada
zinafanyika za kujenga mabweni ya wanafunzi wa kike ili kujaribu kupunguza tatizo hilo na ameishukuru radio
five kutembelea maeneo hayo ambayo
amedai hayajawahi kufikiwa na vyombo vya habari na ameviomba vyombo
vingine kuiga mfano wa kituo cha radio five.
Naye Diwani wa Kata ya Mahongole,Brown
Mwakibete ametoa mwito kwa wadau wa
elimu kujitokeza kusaidia tatizo la shule kwani wananchi wamekuwa wakisua sua kutokana na kutumia gharama nyingi na kwa muda
mrefu katika kujenga shule ya Sekondari
ya Ruiwa ambayo kutokana na majengo yake kutokuwa na ubora yameanguka na hivyo kuanza kujenga shule nyingine.
Diwani Mwakibete alisema
wakati wananchi wakiwa bado wanajitolea michango katika shule ya Sekondari ya
Ruiwa ikiwa na vyumba vya madarasa kumi
na mbili,mabweni mawili,maktaba na
maabara ghafla ilibomoka na hivyo
wamechukua hatua ya kujenga shule mpya inayotegemewa na Kata ya Mahongole
na Mwantenga ambayo hadi sasa ina vyumba 14 vya madarasa na nyumba mbili za
walimu na kwamba bado haikidhi uhitaji wa wananchi wa kata hizo mbili
Mwisho