Translate

Sunday, October 2, 2011

matukio ya nondo Mbeya,wauzaji na wamiliki wa bucha za nyama ya ng'ombe wadai mauzo yameshuka kutokana na walaji kuona kinyaa na kuichukia nyama,wasema wanaambulia kuuza maini na figo zisizotundikwa katika nondo

Na Thompson Mpanji,Mbeya

WAKATI matukio ya upigaji wa nondo yakiendelea kushika kasi jijini Mbeya,baadhi ya  wamiliki na wauza Bucha za  nyama ya Ng’ombe,jijini Mbeya wameelezea masikitiko yao ya kushuka kwa  mauzo ya nyama hiyo kutokana na walaji walio wengi  kuona kinyaa  na kuichukia nyama baada ya kuibuka kwa wimbi la uhalifu wa upigaji wa nondo unaohusishwa na imani za kishirikina kuwa zinatumika kuvuta wateja baada ya kutundikia nyama hizo katika maduka hayo.

Kama methali isemayo kufa kufaana ndivyo ilivyotokea kwa biashara hiyo ambapo kwa sasa wafanyabishara wa samaki, maharage,mboga za majani na nyinginezo nyota yao imenga’ra   kutokana na  wateja walio wengi  kuonekana wakikimbilia bidhaa hizo badala ya kitoweo maarufu cha  fileti,steki,mchanganyiko na mbavu.

Wakizungumza na mwamdishi wa habari hizi,  kwa nyakati tofauti,baadhi ya wauzaji na wamiliki wa mabucha  katika maeneo ya Soweto,Mabatini,Mwenjelwa,Mafiati na Sokomatola wamesema mauzo ya nyama hiyo yameporomoka kwa kasi  tangu kuibuka kwa  wimbi la upigaji wa nondo katika kipindi cha miezi kadhaa sasa.

Mmoja wa wauzaji wa Bucha eneo la Sokomatola aliyejimbaulisha kwa jina la Hussein  alisema kuwa nyama nyingi inalala kutokana na wateja kutoonekana  na kwamba wale wanaofika katika mabucha wananua  nyama aina ya figo au  maini ambazo hazitundikwi katika nondo.

Wakati huo huo,baadhi ya wakazi wa Kata ya Mabatini wamelalamikia Operesheni iliyofanywa na Jeshi la polisi kuwa imewaletea usumbufu mkubwa na kuwatia hasara baadhi ya wafanyabiashara kutokana na kikosi cha askari Polisi  kuvamia maeneo  hayo na kuwapiga marufuku wananchi kutembea kuanzia majira ya saa 1.30 usiku.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mianzini,Kata ya Mabatini,Bibi.Elizabeth Mwambungu alisema operesheni iliyoendeshwa jana haikuwa ya kiistaarabu bali walitumia nguvu zaidi  kutokana na watu kupata usumbufu mkubwa wa kukamatwa na kupigwa ovyo jambo lililowafanya wajione kama wakimbizi ndani ya nchi yao.

Bibi.Mwambungu alisema kuwa  hawakuona umuhimu wa Jeshi hilo kufanya doria majira ya saa moja usiku huku muda wa watu kupigwa nondo unaonesha ni kuanzia saa 4 za usiku na kuendelea na kwamba wameshangazwa polisi kuanza doria baada ya kupigwa na kuuawa kwa askari mwenzao  huku  taarifa za upigwaji wa nondo zikifichwa na kudai kuwa  watu wanajeruhiwa ama kuuawa na vitu vyenye ncha kali.

Mwenyekiti huyo alisema uongozi wa mtaa wa mianzini umepanga kuitisha mkutano wa hadhara  siku ya Alhamis saa 8 mchana  kuzungumzia masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao kufuatia kuibuka kwa vitendo vya upigaji wa nondo katika Kata ya Mbalizi Road ambapo imedaiwa  zaidi ya watu  9 wamejeruhiwa akiwepo mtu mmoja kuuawa.

Mchungaji Wiliam Mwamalanga akizungumza na gazeti hili alisema Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya,Advocate Nyombi anapaswa kukubaliana na matokeo ya kuwa uhalifu wa upigaji wa nondo upo mkoani Mbeya na kwamba kilicho mbele yake ni kuweka mikakati kwa kushirikiana na wananchi kupambana na uhalifu huo kwa kutumia mbinu zilizotumika na Makamanda wenzake wa Mkoa wa Mbeya  waliopita  akitolea mfano Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema na Alhaji Suleiman Kova waliofanikiwa kuzima kabisa kadhia hiyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kikao cha dharula cha Kata ya Mbalizi Road kilichoitishwajana  kufuatia matukio ya upigaji wa nondo katika eneo hilo usiku wa kuamkia  jana, imedaiwa kuwa mtu mmoja ameuawa na wengine saba  kujeruhiwa katika  Kata hiyo   wakiwepo wengine wawili  kutoka Kata ya Forest,zote za jijini hapa.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment