Translate

Sunday, October 2, 2011

wanafunzi wa kike mbarali wahofiwa kubakwa

Na Thompson Mpanji,Mbarali

WANAFUNZI wa Kata ya Mahongole na Mwatenga,wilayani Mbarali wameuomba uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuchukuwa jitihada za dhati kuwasaidia kuwajengea shule za Sekondari maeneo ya jirani  na makazi yao  ili kuepusha  madhara yanayoweza kuwakumba hasa kwa wanafunzi wa kike kutokana na kutembea  umbali mrefu katika vichaka   zaidi ya  kilomita 14  hadi kufikia shuleni.

Mwito huo umetolewa na wanafunzi hao walipokuwa wakizungumza na gazeti hili  kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Kata  hizo ambapo wanafunzi kutoka Kijiji cha Sonyanga  wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya nane hadi shule ya sekondari ya Kata ya Ruiwa,Ilongo  zaidi ya Kilimota 10,Kapyo umbali wa zaidi ya kilimota 14,Igalako na Mahongole Kilomita zaidi ya tatu,Muwela kilomita zaidi ya  saba na Mwatenga umbali wa kilomita zaidi ya 10.

Wanafunzi hao walisema, wamekuwa wakichoka na kushindwa kumsikiliza mwalimu  vyema baada ya kutemebea umbali mrefu ,wanafunzi wa kike wamekuwa wakihofiwa kubakwa vichakani huku wengine wakielelezea hofu yao ya kuuawa kutokana na  kuibuka kwa   matukio ya mauaji  ya kushtukiza  na kutulia yanayokuwa yakitokea wilayani humo jambo  ambalo wamedai linawakosesha raha na mori wa kuendelea na masomo.

Ofisa Mtendaji  Kata ya Mahongole,Juma Mangula  amethibitisha kuwepo kwa matatizo hayo kutokana na wanafunzi wa Kata ya Mahongole na Mwantenga kutegemea shule ya Sekondari ya Kata ya Ruiwa ambayo awali ilijengwa wakati wa Kata moja lakini  kwa sasa kuna uhitaji mkubwa wa shule.

Mangula alisema jitihada zinafanyika za kujenga mabweni ya wanafunzi wa kike ili kujaribu  kupunguza tatizo hilo na ameishukuru radio five kutembelea maeneo hayo ambayo  amedai hayajawahi kufikiwa na vyombo vya habari na ameviomba vyombo vingine kuiga mfano wa kituo cha radio five.

 Naye Diwani wa Kata ya Mahongole,Brown Mwakibete ametoa mwito kwa wadau  wa elimu kujitokeza kusaidia tatizo la shule kwani wananchi wamekuwa wakisua sua  kutokana na kutumia gharama nyingi na kwa muda mrefu katika kujenga  shule ya Sekondari ya Ruiwa ambayo kutokana na majengo yake kutokuwa na  ubora yameanguka na hivyo  kuanza kujenga shule nyingine.

Diwani Mwakibete alisema wakati wananchi wakiwa bado wanajitolea michango katika shule ya Sekondari ya Ruiwa  ikiwa na vyumba vya madarasa kumi na mbili,mabweni mawili,maktaba  na maabara ghafla ilibomoka na hivyo  wamechukua hatua ya kujenga shule mpya inayotegemewa na Kata ya Mahongole  na Mwantenga ambayo hadi sasa  ina vyumba 14 vya madarasa na nyumba mbili za walimu na kwamba bado haikidhi uhitaji wa wananchi wa kata hizo mbili

Mwisho

No comments:

Post a Comment