Translate

Tuesday, July 31, 2012

Sakata la mgomo wa walimu,RC Njombe amtimua Afisa wa Halamshauri ya Njombe kwa kuhamasisha mgomo wa walimu,aagiza apangiwe kufundisha shule ya msingi


Na Thompson Mpanji,Njombe

WAKATI sakata la mgomo wa walimu likiendelea kwa nchi nzima kuanzia leo(julai,31),Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Capt.Mstaafu Aseri Msangi amemshusha cheo mmoja wa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kuanzia leo kutokana na madai ya kuhamasisha mgomo wa walimu.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewasihi walimu wote kurejea katika maeneo yao ya kazi na kuendelea kufundisha kwani serikali imeshatangaza kuwa mgomo huo ni batili kutokana na  suala hilo kuendelea kushughulikiwa mahakani.

Akitoa tamko hilo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa kwanza wa mwaka  wa wanahisa wa Benki ya wananchi Njombe,Capt.Msangi amemuagiza  Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Njombe,Robert Nehatta kumshusha cheo hadi kuwa mwalimu wa kawaida wa shule ya msingi Mwenyekiti wa Chama cha walimu Tanzania(CWT),mkoani Njombe,Godfray Hambo kutokana na madai ya kuhamasisha mgomo aliodai unashughulikiwa kisheria.

Capt.Msangi amesema haiwezekani Hambo kuisaliti serikali  kwa kuendelea kuhamasisha walimu  kufanya mgomo ilhali naye ni kiongozi wa serikali jambo aliloagiza kuchukuliwa hatua za awali za kumshusha cheo na kwenda kufundisha katika shuel ya sekondari ama ya msingi wakati taratibu nyingine za kinidhamu ikiwemo na sheria  za utumishi wa umma zikifuatiwa.

Mkuu wa Mkoa amesema Mwenyekiti huyo wa CWT Njombe hakupaswa kushika wadhifa huo kutokana na nafasi yake  ya Ofisa elimu takwimu na vifaa wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ambapo alitakiwa  kuhamasisha walimu kufundisha badala ya kuweka kalamu chini.

Amesema endapo walimu wataendelea kugoma na hivyo kusababisha  wanafunzi kukosa masomo ni sawa na kuendeleza adui mmojawapo mbaya wa  ujinga  kwa taifa,donda alilodai  halitapona maumivu wala kufutika kovu lake kwa vizazi   wanavyovijenga na kuviandaa leo.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa wa Njombe amewashukuru walimu wote ambao kwa aslimi kubwa hawajagoma na wanaendelea na kazi na kwamba kwa Njombe mjini ni walimu wasiopungua 24 waliogoma ambapo kwa wilaya ya Makete amepokea taarifa ya shule moja wa sekondari ambayo walimu wake wamegoma ingawa hakuweza kuitaja jina na kama binafsi ama ya serikali.

BENKI YA NJOCOBA YAWAKOPESHA WANANCHI ZAIDI YA SH.BIL.3,WASIOREJESHA MIKOPO WAPANDISHWA KIZIMBANI WATATU

Na Thompson Mpanji,Njombe

BENKI ya wananchi wa Mkoa wa Njombe(NJOCOBA) imefanikiwa kutoa mikopo ya  zaidi ya Sh.Bil.3.6 hadi kufikia disemba ,mwaka 2011 kwa wananchama wake ikiwa ni mkakati wa  kuboresha hali za maisha ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya.

Aidha Njocoba imefanikiwa kuingiza mapato ya Sh.Mil.554 ambapo faida kwa mwaka  ilifikia Sh.Mil.10 ingawa imeelezwa kuwa benki hiyo ilipata hasara  ya Sh.Mil.289 iliyotokana na gharama kubwa za uanzishwaji wa benki ambazo Benki kuu (BOT) iliamuru kuhesabika kama matumizi ya awali kabla ya benki kufunguliwa.

Akitoa  taarifa fupi  tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Kapt.mstaafu Aseri Msangi,Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo,Bi. Twilumba  Ulaya amesema tangu kufunguliwa rasmi kwa benki hiyo septemba,13,2010 ilianza na zaidi ya sh.Mil.15.8 imekuwa na maendeleo mazuri kwa wananchi kuhamasika kujiunga   hadi kufikia  wateja 5,099  kwa kufungua akaunti mbalimbali.

Amesema benki  hiyo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2011 imefikisha amana ya zaidi ya Sh.Bil.1.8 katika akaunti  za akiba,biashara,muda maalum katika akaunti za makundi maalum,binafsi,makampuni,taasisi,watoto na wanafunzi na ushirika.

Mwenyekiti huyo amesema katika kipindi cha mwaka 2011 zaidi ya hisa 55,000 zenye thamani ya Sh.Mil.55 zilinunuliwa  na hivyo hisa za benki zilifikia 442,000 zenye thamani ya sh.Mil.442 ambapo mtaji uliopo hadi kufikia juni ,2012 umefikia zaidi ya Sh.Mil.290 kiasi ambacho ni chini ya mtaji  unaotakiwa na ununuzi wa hisa wa Sh.Mil.500 na hivyo  kuwaomba wanachama kuongeza ununuzi wa hisa.

Bi.Twilumba amesema urejeshaji wa mikopo  siyo mzuri  kwani kwa kipindi hicho mikopo ambayo ni mibaya na hailipiki  vizuri ni zaidi ya Sh.Mil.267 sawa na asilimia 18 ya mikopo yote na kwamba tayari  kesi tatu za madai  zenye thamani ya zaidi ya Sh.Mil.72.4 hadi kufikia juni,30,2012 zimeshafunguliwa  katika mahakama  ya wilaya ya Njombe.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Kapt.Msangi ametoa wito kwa wakazi wa Njombe kujiunga kwa wingi katika benki yao na kwamba yeye atakuwa mwanahisa  na ataendelea kuhamasisha wakazi wa Njombe wanaoishi Dar es salam na mikoa mingine ikiwemo na halamshauri zote za Wilaya ya njombe kujiunga na benki hiyo.

Hata hivyo Kapt.Msangi ameuomba uongozi wa Benki ya Njocoba na Bodi yake  kuweka mikakati na taadhari kwa baadhi ya wanahisa wasije wakahodhi benki kwa kununua hisa zote na hivyo wanachama kujikuta  hawana chao na kumilikiwa na mtu mmoja hali ambayo itaondoa dhana nzima ya neno Benki ya wananchi.

Mwisho.