Translate

Tuesday, July 31, 2012

Sakata la mgomo wa walimu,RC Njombe amtimua Afisa wa Halamshauri ya Njombe kwa kuhamasisha mgomo wa walimu,aagiza apangiwe kufundisha shule ya msingi


Na Thompson Mpanji,Njombe

WAKATI sakata la mgomo wa walimu likiendelea kwa nchi nzima kuanzia leo(julai,31),Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Capt.Mstaafu Aseri Msangi amemshusha cheo mmoja wa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kuanzia leo kutokana na madai ya kuhamasisha mgomo wa walimu.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewasihi walimu wote kurejea katika maeneo yao ya kazi na kuendelea kufundisha kwani serikali imeshatangaza kuwa mgomo huo ni batili kutokana na  suala hilo kuendelea kushughulikiwa mahakani.

Akitoa tamko hilo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa kwanza wa mwaka  wa wanahisa wa Benki ya wananchi Njombe,Capt.Msangi amemuagiza  Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Njombe,Robert Nehatta kumshusha cheo hadi kuwa mwalimu wa kawaida wa shule ya msingi Mwenyekiti wa Chama cha walimu Tanzania(CWT),mkoani Njombe,Godfray Hambo kutokana na madai ya kuhamasisha mgomo aliodai unashughulikiwa kisheria.

Capt.Msangi amesema haiwezekani Hambo kuisaliti serikali  kwa kuendelea kuhamasisha walimu  kufanya mgomo ilhali naye ni kiongozi wa serikali jambo aliloagiza kuchukuliwa hatua za awali za kumshusha cheo na kwenda kufundisha katika shuel ya sekondari ama ya msingi wakati taratibu nyingine za kinidhamu ikiwemo na sheria  za utumishi wa umma zikifuatiwa.

Mkuu wa Mkoa amesema Mwenyekiti huyo wa CWT Njombe hakupaswa kushika wadhifa huo kutokana na nafasi yake  ya Ofisa elimu takwimu na vifaa wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ambapo alitakiwa  kuhamasisha walimu kufundisha badala ya kuweka kalamu chini.

Amesema endapo walimu wataendelea kugoma na hivyo kusababisha  wanafunzi kukosa masomo ni sawa na kuendeleza adui mmojawapo mbaya wa  ujinga  kwa taifa,donda alilodai  halitapona maumivu wala kufutika kovu lake kwa vizazi   wanavyovijenga na kuviandaa leo.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa wa Njombe amewashukuru walimu wote ambao kwa aslimi kubwa hawajagoma na wanaendelea na kazi na kwamba kwa Njombe mjini ni walimu wasiopungua 24 waliogoma ambapo kwa wilaya ya Makete amepokea taarifa ya shule moja wa sekondari ambayo walimu wake wamegoma ingawa hakuweza kuitaja jina na kama binafsi ama ya serikali.

No comments:

Post a Comment