Translate

Friday, April 18, 2014

Taarifa ya RPC Mbeya Ahmed msangi,Aprili,18,2014

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ahmed Z. Msangi anatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana kwa ukaribu zaidi na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati za wahalifu na uhalifu katika maeneo mbalimbali pale waonapo viashiria ambavyo si vya kawaida au pindi tukio linapojitokeza ikiwa ni kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno, mazungumzo ya simu au kwa kufika moja kwa moja kituo cha Polisi Kilipo Karibu na maeneo yao.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawahakikishia Wananchi/Wakazi wa Mkoa wa Mbeya na Wageni wote hali ya Amani na Utulivu katika Kipindi hiki cha kusherehekea Sikukuu ya Pasaka. Kila Mwananchi aone anawajibu wa kufuata na kutii sheria zilizowekwa bila kushurutishwa. Pia rai kwa wananchi kuacha muangalizi/waangalizi nyumbani wanapotoka kwenda katika Ibada za Mkesha na Sherehe kwa jumla kwa ajili ya ulinzi na usalama wa mali zao.

Kwa watumiaji wa Vyombo vya Moto wafuate na kuzingatia Sheria na Alama za Usalama Barabarani ili kuepuka ajali. Halikadhalika watembea kwa miguu kuwa makini na matumizi ya barabara ikiwa ni pamoja na kuvuka katika maeneo yenye vivuko [zebra crossing].

Aidha Kamanda wa Polisi anawataka wazazi/walezi kuwa makini na watoto wadogo kwa kutowaacha wakatembea bila uangalizi wa kutosha. Wamiliki wa kumbi za Starehe kuzingatia taratibu za uendeshaji wa Biashara zao ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya pia anatoa shukrani kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Mbeya kwa ushirikiano mkubwa wanaoonyesha kwa Jeshi la Polisi na kwa wananchi kwa njia ya kuhabarisha umma.

Nitumie nafasi hii kuwatakia Sikukuu njema ya Pasaka, kwa kuungana na Wakristu Dunia kote kusherehekea kufufuka kwa Yesu Kristo.

Mwisho