Translate

Sunday, October 2, 2011

wanafunzi wa kike mbarali wahofiwa kubakwa

Na Thompson Mpanji,Mbarali

WANAFUNZI wa Kata ya Mahongole na Mwatenga,wilayani Mbarali wameuomba uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuchukuwa jitihada za dhati kuwasaidia kuwajengea shule za Sekondari maeneo ya jirani  na makazi yao  ili kuepusha  madhara yanayoweza kuwakumba hasa kwa wanafunzi wa kike kutokana na kutembea  umbali mrefu katika vichaka   zaidi ya  kilomita 14  hadi kufikia shuleni.

Mwito huo umetolewa na wanafunzi hao walipokuwa wakizungumza na gazeti hili  kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Kata  hizo ambapo wanafunzi kutoka Kijiji cha Sonyanga  wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya nane hadi shule ya sekondari ya Kata ya Ruiwa,Ilongo  zaidi ya Kilimota 10,Kapyo umbali wa zaidi ya kilimota 14,Igalako na Mahongole Kilomita zaidi ya tatu,Muwela kilomita zaidi ya  saba na Mwatenga umbali wa kilomita zaidi ya 10.

Wanafunzi hao walisema, wamekuwa wakichoka na kushindwa kumsikiliza mwalimu  vyema baada ya kutemebea umbali mrefu ,wanafunzi wa kike wamekuwa wakihofiwa kubakwa vichakani huku wengine wakielelezea hofu yao ya kuuawa kutokana na  kuibuka kwa   matukio ya mauaji  ya kushtukiza  na kutulia yanayokuwa yakitokea wilayani humo jambo  ambalo wamedai linawakosesha raha na mori wa kuendelea na masomo.

Ofisa Mtendaji  Kata ya Mahongole,Juma Mangula  amethibitisha kuwepo kwa matatizo hayo kutokana na wanafunzi wa Kata ya Mahongole na Mwantenga kutegemea shule ya Sekondari ya Kata ya Ruiwa ambayo awali ilijengwa wakati wa Kata moja lakini  kwa sasa kuna uhitaji mkubwa wa shule.

Mangula alisema jitihada zinafanyika za kujenga mabweni ya wanafunzi wa kike ili kujaribu  kupunguza tatizo hilo na ameishukuru radio five kutembelea maeneo hayo ambayo  amedai hayajawahi kufikiwa na vyombo vya habari na ameviomba vyombo vingine kuiga mfano wa kituo cha radio five.

 Naye Diwani wa Kata ya Mahongole,Brown Mwakibete ametoa mwito kwa wadau  wa elimu kujitokeza kusaidia tatizo la shule kwani wananchi wamekuwa wakisua sua  kutokana na kutumia gharama nyingi na kwa muda mrefu katika kujenga  shule ya Sekondari ya Ruiwa ambayo kutokana na majengo yake kutokuwa na  ubora yameanguka na hivyo  kuanza kujenga shule nyingine.

Diwani Mwakibete alisema wakati wananchi wakiwa bado wanajitolea michango katika shule ya Sekondari ya Ruiwa  ikiwa na vyumba vya madarasa kumi na mbili,mabweni mawili,maktaba  na maabara ghafla ilibomoka na hivyo  wamechukua hatua ya kujenga shule mpya inayotegemewa na Kata ya Mahongole  na Mwantenga ambayo hadi sasa  ina vyumba 14 vya madarasa na nyumba mbili za walimu na kwamba bado haikidhi uhitaji wa wananchi wa kata hizo mbili

Mwisho

matukio ya nondo Mbeya,wauzaji na wamiliki wa bucha za nyama ya ng'ombe wadai mauzo yameshuka kutokana na walaji kuona kinyaa na kuichukia nyama,wasema wanaambulia kuuza maini na figo zisizotundikwa katika nondo

Na Thompson Mpanji,Mbeya

WAKATI matukio ya upigaji wa nondo yakiendelea kushika kasi jijini Mbeya,baadhi ya  wamiliki na wauza Bucha za  nyama ya Ng’ombe,jijini Mbeya wameelezea masikitiko yao ya kushuka kwa  mauzo ya nyama hiyo kutokana na walaji walio wengi  kuona kinyaa  na kuichukia nyama baada ya kuibuka kwa wimbi la uhalifu wa upigaji wa nondo unaohusishwa na imani za kishirikina kuwa zinatumika kuvuta wateja baada ya kutundikia nyama hizo katika maduka hayo.

Kama methali isemayo kufa kufaana ndivyo ilivyotokea kwa biashara hiyo ambapo kwa sasa wafanyabishara wa samaki, maharage,mboga za majani na nyinginezo nyota yao imenga’ra   kutokana na  wateja walio wengi  kuonekana wakikimbilia bidhaa hizo badala ya kitoweo maarufu cha  fileti,steki,mchanganyiko na mbavu.

Wakizungumza na mwamdishi wa habari hizi,  kwa nyakati tofauti,baadhi ya wauzaji na wamiliki wa mabucha  katika maeneo ya Soweto,Mabatini,Mwenjelwa,Mafiati na Sokomatola wamesema mauzo ya nyama hiyo yameporomoka kwa kasi  tangu kuibuka kwa  wimbi la upigaji wa nondo katika kipindi cha miezi kadhaa sasa.

Mmoja wa wauzaji wa Bucha eneo la Sokomatola aliyejimbaulisha kwa jina la Hussein  alisema kuwa nyama nyingi inalala kutokana na wateja kutoonekana  na kwamba wale wanaofika katika mabucha wananua  nyama aina ya figo au  maini ambazo hazitundikwi katika nondo.

Wakati huo huo,baadhi ya wakazi wa Kata ya Mabatini wamelalamikia Operesheni iliyofanywa na Jeshi la polisi kuwa imewaletea usumbufu mkubwa na kuwatia hasara baadhi ya wafanyabiashara kutokana na kikosi cha askari Polisi  kuvamia maeneo  hayo na kuwapiga marufuku wananchi kutembea kuanzia majira ya saa 1.30 usiku.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mianzini,Kata ya Mabatini,Bibi.Elizabeth Mwambungu alisema operesheni iliyoendeshwa jana haikuwa ya kiistaarabu bali walitumia nguvu zaidi  kutokana na watu kupata usumbufu mkubwa wa kukamatwa na kupigwa ovyo jambo lililowafanya wajione kama wakimbizi ndani ya nchi yao.

Bibi.Mwambungu alisema kuwa  hawakuona umuhimu wa Jeshi hilo kufanya doria majira ya saa moja usiku huku muda wa watu kupigwa nondo unaonesha ni kuanzia saa 4 za usiku na kuendelea na kwamba wameshangazwa polisi kuanza doria baada ya kupigwa na kuuawa kwa askari mwenzao  huku  taarifa za upigwaji wa nondo zikifichwa na kudai kuwa  watu wanajeruhiwa ama kuuawa na vitu vyenye ncha kali.

Mwenyekiti huyo alisema uongozi wa mtaa wa mianzini umepanga kuitisha mkutano wa hadhara  siku ya Alhamis saa 8 mchana  kuzungumzia masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao kufuatia kuibuka kwa vitendo vya upigaji wa nondo katika Kata ya Mbalizi Road ambapo imedaiwa  zaidi ya watu  9 wamejeruhiwa akiwepo mtu mmoja kuuawa.

Mchungaji Wiliam Mwamalanga akizungumza na gazeti hili alisema Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya,Advocate Nyombi anapaswa kukubaliana na matokeo ya kuwa uhalifu wa upigaji wa nondo upo mkoani Mbeya na kwamba kilicho mbele yake ni kuweka mikakati kwa kushirikiana na wananchi kupambana na uhalifu huo kwa kutumia mbinu zilizotumika na Makamanda wenzake wa Mkoa wa Mbeya  waliopita  akitolea mfano Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema na Alhaji Suleiman Kova waliofanikiwa kuzima kabisa kadhia hiyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kikao cha dharula cha Kata ya Mbalizi Road kilichoitishwajana  kufuatia matukio ya upigaji wa nondo katika eneo hilo usiku wa kuamkia  jana, imedaiwa kuwa mtu mmoja ameuawa na wengine saba  kujeruhiwa katika  Kata hiyo   wakiwepo wengine wawili  kutoka Kata ya Forest,zote za jijini hapa.

Mwisho.

Sunday, August 14, 2011

chadema yamtumia salama Mstahiki Meya wa Mbeya

Na Thompson Mpanji,Mbeya




CHAMA cha Demokrasia na maendeleo kimemtaka Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi,Wilaya ya Mbeya mjini,Athanas Kapunga akisubiri Mahakamani ili waweze kuyatolea ushahidi madai yao kwake ya kuweka mikakati ya kukihujuma chama hicho.



Aidha Chadema imesema wataendelea kumshtakia kwa wananchi kuhusu hujuma anazoendelea kuzifanya yeye kama kiongozi wa chama kuwahujumu wananchi na hivyo kurudisha maendeleo ya Jiji la Mbeya nyuma kutokana na kuwarubuni Madiwani wa Chadema kuhamia CCM.



Hayo yamesemwa jana na Jacob Kalua Mratibu wa Operesheni Twanga kote kote, iliyohitimishwa jana katika Kata ya Iganzo,jijini Mbeya wakati akizungumza na gazeti hili.



Kalua alisema madai ya Kapunga kutishia nyau hayajaanza leo,na kwamba kitendo cha kutoa vitisho hivyo kunawaongezea kasi ya kuendelea kusema kwa waannchi yale anayoyafanya na kwamba wamemtaka atangulie mahakamani kudaifidia hizo na watamkuta na kuyaweka yote bayana.

“Kapunga hasiwashe moto ambao atashindwa kuuzima kuita vyombo vya habari asidhani tunatishika, kwa sababu tunayoyasema tunayo ushahidi nayo,tutamweka hadhrani huko mahakamni na vyombo vya habari vitayaandika,”alisema.



Kampunga ambaye pia Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya ameelezea dhamria yake ya kukifikisha chama hicho mahakamani kudai fidia kutokana na kile alichoelezwa kumtukana sanjari na kumtuhumu kuwanunua madiwani hasa Diwani wa Kata ya Nzovwe kupitia Chadema Ezron Mwakalobo aliyehamia CCM.



Wakati huo huo Chadema imeombwa kuwa makini na wapambe wa Chama hicho ambao wanakipaka matope Chama hicho kwa kauli chafu ambazo zinapelekea baadhi ya wananchi kukiita chama cha kihuni.



Hayo yamesemwa na mmoja wa wananchi wa Kata ya Iganzo wakati wa hitimisho la mkutano wa operesheni twanga kote kote na kudai kuwa wapambe ndiyo wanaochafua sifa ya chama ambacho kinaonekana dhahiri kina lengo la kumkomboa mtanzania.



Mwisho.

Friday, July 29, 2011

walimu Mbeya nusura wachapane makonde kwa kudai posho

Na Thompson Mpanji,Mbeya

OFISI ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imewataka walimu kuilinda heshima ya taaluma yao pindi wanapokuwa katika makundi mbalimbali ya kijamii na mikutano sanjari na kujenga uaminifu katika vyombo vya fedha badala ya kugushi nyaraka za mishahara kwa lengo la kujikupatia mikopo kwa njia ya rahisi ya udanganyifu.

Ushauri huo umetolewa na mweka hazina wa Halmshauri ya Wilaya ya Mbeya,Bw.Chamba Bigambo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Bibi.Juliana Malange wakati wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Chama cha akiba na mikopo cha Mbeya Teacher,s Saccos uliofanyika jana jijini hapa.


Bw.Bigambo aliyasema hayo kufuatia vuta nikuvute na baadhi ya walimu ambao ni wanachama wa Saccos hiyo kudai posho ya kikao huku wakihoji uhalali wa wanachama wengine kulipwa na wengine kukosa.

Mvutano huo ulitokea mara baada ya kufunguliwa kwa mkutano ambapo baadhi ya kundi lililoonekana kuandaa ajenda hiyo ya siri kunyoosha mkono na kudai hawapo tayari kuendelea na mkutano hadi suala lao la kulipwa posho liwe limetatuliwa.


Mwenyekiti wa Mbeya Teachers Saccos,Bibi.Anna Mwakalukwa aliurejesha mkutano huo katika hali ya kawaida baada ya viongozi mbalimbali akiwemo Ofisa Ushirika kutoka Wizara ya kilimo,Chakula na Ushirika na Ofisa Ushirika wa Wilaya kuwasomea vifungu vya sheria,kanuni na taratibu ambapo yeye alitoa ufafanuzi kuwa katika mkutano mkuu wa 12 uliofanyika mwaka 2010 katika ajenda nambari 9 kuhusu hisa za mwanachama, walikubaliana kila mwanachama awe na hisa 10 ambapo hisa moja ni sh.10,000 na kwamba mwanachama asiyefikisha idadi hiyo ya hisa siyo mwanachama kamili .


Bibi.Mwakalukwa alisema kuwa kutokana na ajenda hiyo mkutano mkuu huo wa 12 ulipitisha azimio kuwa mwanachama ambaye hajafikia hisa 10 hatohusika na posho zitakazotolewa kuanzia katika mkutano mkuu wa 13 jambo ambalo limetekelewa na kwamba endapo kutakuwa na hoja ya kutenguliwa kwa azimio hilo basi lijadiliwe mwishoni.


Hata hivyo Mgeni rasmi huyo aliposimama alielezea masikitiko yake kuhusu mvutano huo ambao haukuwa na mantiki yeyote kutokana na walalamikaji kutofuata maandishi yaliyokuwemo katika muhtasari wa mkutano uliopita na kwamba endapo walikuwa na hoja za msingi basi ni vema wangetumia busara kuandika na kupitisha mbele kwa mwenyekiti kuliko kuanzisha malumbano yasiyo na msingi kwa wanataaluma hao ambao ni mfano wa kuigwa kwa jamii,.

Bw.Bigambo aliwafunda walimu hao kujiheshimu na kujenga nidhamu mbele ya mgeni rasmi katika mikusanyiko yeyote na mahali penginepo badala ya kuonesha utovu wa nidhamu jambo ambalo amedai halikumfurahisha hata kidogo.


Naye Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Mbeya,Lucas Busigazi amewashauri walimu waache tabia ya kughushi hati za mishahara kama Bibi.Mwakalukwa alivyodai katika taarifa yake na kwamba ni vema walimu wakawa na nidhamu katika kukopa na kurejesha kwa wakati badala ya kutanguliza tama ambazo zinaweza kuja kuwagharimu katika vyombo vya sheria pindi wakibainika.


Mwisho.

Thursday, July 21, 2011

Na Thompson Mpanji,Mbeya

CHAMA cha akiba na mikopo cha walimu Mbeya Teacher’s Saccos,jijini

Mbeya kimefanikiwa kutoa mkopo wa zaidi ya Sh.Bil.1.1 kwa wanachama

wake zaidi ya 1,148 wakiwemo wanaume 539 na wanawake 609 hadi kufikia

Disemba,2010.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,Ofisini kwake,Mwenyekiti wa Chama

hicho,Bibi,Anna Mwakalukwa alisema kuwa Chama hicho kilianzishwa mwaka

1995 na kusajiliwa mwaka 1997 kikiwa na wanachama 100 wakiwemo wanaume

54 na wanawake 46 wakiwa na akiba ya Sh.45,000 bila kuwa na hisa wala

amana.


Bibi.Mwakalukwa alisema kuwa kutokana na mwamko wa wanachama Mbeya

Teacher’s Saccos imefikia akiba ya Sh.Mil.408.8,hisa Sh.Mil.54.1 na

amana Sh.275,000 na amewataka wanachama kujenga utamaduni wa kujiwekea

amana badala ya kukimbilia mikopo.


Aidha Mwenyekiti huyo alisema takwimu za idadi ya wanachama

zinathibitisha ukweli usiopingika kuwa akina mama ni nguzo na mfano wa

kuigwa katika kutambua umuhimnu wa kujiwekea akiba ili kumtokomeza

adui umaskini.


Hata hivyo Mwenyekiti huyo amewataka wanachama wa Mbeya Teacher’s

Saccos kujitokeza kwa wingi katika mkutano mkuu wa 13 unaotarajiwa

kufanyika julai,22 mwaka huu katika ukumbi wa Nuru Park (Royal

Zambezi),uliopo Soweto,jijini Mbeya.



Mwisho.

Saturday, April 23, 2011

Friday, April 15, 2011

Mashirika ya caritas nchini yametakiwa kutokuwa mzigo majimboni

Na Thompson Mpanji,Mbeya
MASHIRIKA ya caritas nchini yametakiwa kujipanga vizuri katika utendaji wa kazi ,uwazi,uwajibikaji na ushirikishwaji ili yasionekne kuwa mzigo wa majimbo ya kanisa katoliki.
Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shirika la Caritas Mbeya,Bw.Edgar Mangasila ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano mtandao wa mashirika ya Caritas kanda ya kusini (SHICANET)  wa siku moja uliofanyika katika ukumbi wa kituo cha malezi kwa vijana,kanisa katoliki,jimbo la Mbeya jijini hapa.
Bw.Mangasila amesema ili  Mashirika la Caritas yaweze kufanya vizuri katika utoaji wa huduma katika jamii na kuonekana yanafanyakazi vizuri, watendajike wanapaswa kufanyakazi kwa ushirikiano,kujipanga vizuri,kufuata miiko na taratibu za kazi na matumizi ya fedha yanayozingatia uwazi pale taarifa inapohitajika.
“Wafanyakazi wa Caritas mjitahidi msiwe mzigo wa majimbo,fanyeni kazi kwa uwazi na uwajibikaji siyo ibakie dhamira  safi tu bali  kila mtu anapohitaji kujuwa kinachoendelea akione,na hili ndiyo moja ya tatizo zinazofanya caritas nyingi zisipige hatua,kuna mashirika mengi kama Miserior ambayo yanapenda kufanyakazi nasi,hivyo tuzitumie fursa hizi,”alisema.
Ametaja sababu nyingine inayopaswa kuizingatia ni kuboresha mazingira ya watendaji,kutafuta mbinu za kutafuta fedha,mahusiano mema ya wafanyakazi na jimbo pamoja na kutekeleza  kwa muda muafaka shughuli zinazopangwa.
Mratibu wa SHICANET,Bw.Lufunyo Mlyuka amesema mkutano huo ni utaratibu wa mtandao kuwaunganisha wanachama  watendaji wa Caritas kutoka  katika majimbo nane ambayo ni Caritas Mbeya,Njombe,Iringa,Songea,Tunduru Masasi,Mahenge,Mbinga na Sumbawanga lengo likiwa ni waratibu kubadilishana mawazo na uzoefu,kuangalia changamoto,mafanikio  na mpangokazi wa Shicanet ili uweze kuwafikia wakurugenzi wote wa caritas.
Mwisho.

Mlemavu asiyeona Chunya aibuka na kudai kutibu magonjwa sugu na ukimwi

Na Thompson Mpanji,Chunya

IDADI ya wataalamu wa tiba ya kikombe inazidi kuongezeka baada ya ‘Babu’Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapila wa Loliondo, wilayani Chunya Mlemavu wa asiyeona  ameibuka  na kudai kutibu magonjwa yote sugu ukiwemo Ukimwi  ambapo maelfu ya wananchi wanamiminika kupata tiba hiyo inayodaiwa kutibu kwa muda wa siku 43.

Hata hivyo taarifa za uhakika zilizolikia gazeti hili zinasema kuwa  msaidizi wa mlemavu huyo, aliyemsindikiza kwenda kuchimba dawa hiyo anadaiwa kutouona mti huo kwa mara ya pili   baada ya kumtoroka bosi wake na kwenda katika msitu kwa lengo la kuichukua dawa hiyo ili aifanyie biashara.

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi baadhi ya wananchi wa Kijiji ch Mbuyuni wamesema wameanza kupata huduma hiyo bure  tangu,aprili,7 mwaka huu  na kwamba kuanzia jana mtaalamu huyo ameanza kutoa tiba ya kikombe kwa familia nzima kuchangia kiasi cha sh.500.

Akisimulia kuibuka kwa mtaalamu huyo mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Mbuyuni,Nico Haule amesema mlemavu huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho amedai kuoteshwa mara kadhaa na babu yake marehemu lakini alikuwa akidharau hadi ilipofikia siku  hiyo alipomuomba kijana mmoja amsindikize kuelekea katika milima ya Iseche,Tarafa ya kwimba,wilayani humo.

Msaidizi wa mtaalamu huyo,kaburi Mwankumbi alisema kuwa  aliombwa na Mahela kumsindikiza katika msitu wa milima ya Iseche na Mkwajuni na baada ya kufika huko alishangaa kumwambia walipokuwa wakielekea syo ulipo mti huo na kuelekeza eneo jingine ambapo kipofu huyo alirudi kinyume nyume na kuukamata mti huo na kumwelekeza auchimbe na kurudi nao nyumbani.

“Tulichemsha mti huo na akanywa yeye na mimi na majirani sita akiwemo mdogo wake wa kike ambaye ni mja mzito siku ya pili watu baada ya kupata taarifa walifika wengi,nami nilipoona anatoa  tiba hiyo bure nikamkimbia ili nikauchimbe mti ule na kuwauzia watu lakini nilishangaa sikuuona kabisa na niliporudi kumwambia (Mahela)alicheka,”alisema Mwankumbi.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mbuyuni,Romwad Mwashiuya amethibitisha kuibuka kwa mkazi huyo wa Mbuyuni  aliyemtaja kwa jina la Simon Patson  Mahela ambaye ni  mlemavu wa macho na anaishi kwa msaada wa kuongozwa.

Mwashiuya alisema,  baada ya uongozi kupata taarifa hiyo walifika nyumbani kwake na kuukuta umati wa watu zaidi ya 1000 wakiendelea kupata tiba hiyo na baada ya kumhoji aliwaelekeza na hatimaye  walichukuwa hatua za awali za kumuongezea vikombe kwani alikuwa akitumia kikombe kimoja kuwanyweshea watu wote,pamoja na kumpatia pipa la kuchemshia dawa sanjari na kuboresha hali ya vyoo.

Ofisa wa Afya,Bw.Nicholaus Likokolo alisema baada ya kufika katika eneo hilo wameshauri huduma za choo ziboreshwe na kwamba ingawa yupo nje kikazi lakini  amepata taarifa kuwa  mganga wa kituo cha Afya Mbuyuni amefika pia na kushauri kuchukuwa sample ya dawa na  kuipeleka kwa mganga mkuu wa wilaya ya chunya  ili  aweze kuifikisha kwa mkemia mkuu kwa uchunguzi zaidi.

Wakati huo huo,Katika mtaa wa mianzini,Kata ya mabatini,jijini Mbeya,babu mtoto jafari fikiri amesikika akiwatangazia wananchi wanaokwenda kunywa kikombe kwake kuwa mtu yeyyote atakayefika kwa nia ya kumjaribu ataona cha mkata kuni.

Taarifa hiyo amekuwa akiitoa mganga huyo kufuatia kuumbuka kwa mzee mmoja ambaye anadaiwa kufika kumjaribu na kuichafua huduma hiyo ambayo imekuwa kimbilio la wananchi walio wengi kutoka wilaya mbali mbali za mkoa wa Mbeya ambao wanashindwa kusafiri kufika katika kijiji cha samunge,wilayani Loliondo kwa mchungaji babu Ambilikile mwasapila.

Hata hivyo kuna taarifa ya kupata madhara  baadhi ya wananchi  waliokunywa  dawa hiyo  na kukiuka masharti ya kunywa pombe,kuvuta sigara,kutokunywa dawa ya aina yeyote  na kutofanya tendo la ndoa kwa muda wa siku nane baada ya kunywa vikombe viwili vya tiba hiyo.

Mwisho.

Kibaka aliyeiba Sh.10,000 yang'angania mkononi,apooza miguu na mkono

Na Thompson Mpanji,Mbozi

KIJANA mmoja mpiga debe wa magari yanayofanya safari zake Kamsamba-Mlowo wilayani Mbozi amekumbwa na mkasa wa aina yake baada ya  kudaiwa kuiba fedha  ambayo baadaye ilikutwa imenasa katika mkono wake wa kulia na miguu yote miwili kupooza huku akiwa amelazwa katika zahanati moja wilayani humo.

Tukio hilo la aina yake limetokea ,aprili,10 majira ya mchana baada ya kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Jacob Jengela kuokota fedha Sh.10,000 inayodaiwa kudondoshwa na  muhudumu wa kituo cha kuuza  mafuta kinachomilikiwa na mfanyabiashara aliyetajwa kwa jina moja la Chaula kilichopo maeneo ya Mlowo wilayani humo na kuikanyaga kwa mguu baada ya kuiona na baadaye kuificha mkononi ambapo mhudumu huyo baada ya kushtuka alipiga kelele ya kuibiwa na kijana huyo aliamua kutimua mbio lakini mbio zake ziliishia sakafuni baada ya kudondoka ghafla na kupooza.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa baada ya kijana huyo kuanguka chini huku akiwa anajizoa zoa na kuonekana anashindwa kunyanyuka wananchi wenye hasira kali walimvamia na kutaka kumchoma moto lakini askari polisi wa kituo kidogo cha Polisi cha mlowo walifanikiwa kumuokoa na kumkimbiza katika zahanati iliyotajwa kwa jina la Tumaini kwa ajili ya  uchunguzi na matibabu zaidi.

Aidha  inadaiwa kuwa chanzo cha kuanguka na kupooza miguu yote miwili na mkono wa kulia ulionasa noti hiyo  ya sh.10,000 iliyoendelea kung'ang'ania  ikiwa imenasa mkononi huku akiwa amelazwa  katika zahanati hiyo  hadi kipindi hiki kinaporuka hewani ni kutokana na imani inayohusishwa na masuala ya kishirikana kuwa fedha hiyo ilikuwa imetegwa.

Hata hivyo kipindi hiki baada ya kusasiliana na mmiliki wa kituo hicho aliyetajwa kwa jina moja la Chaula amesema anadhani kijana huyo alikuwa na matatizo ya maradhi ya muda mrefu kwani baada ya yeye kupokea taarifa hiyo alimuuliza mhuhudu ambaye alidai hakumbuki kama alidondosha fedha hiyo.

Mwisho.