Translate

Thursday, January 31, 2013

Mwanamke anayedaiwa kumuuza mtoto aibuka mafichoni aweka mambo hadharani ni baada ya kumnasa anapoishi na mgahawani,Mama mkubwa anayedaiwa kuwa msimamizi wa kituo cha yatima naye aibukia katika semina ya kiroho atoa ufafanuzi

Na Thompson Mpanji,Mbeya
SAKATA la mwanamke mmoja Mkazi wa Mtaa wa Ikuti,Kata ya Iyunga, jijini Mbeya kutuhumiwa kumuuza mtoto aliyemzaa mwenyewe kwa raia wa kigeni wanaomiliki kituo kimoja cha watoto yatima cha jijini hapa limezidi kuchukuwa sura mpya kunaswa na mwandishi wa habari hizi akiwa mafichoni na kuweka mambo hadharani huku anayedaiwa kuwa msimamizi wa kituo cha Care and Share-Children's home Anna Kasile akiibukia katika semina ya Makatekista akikiri kumsaidia mwanamke huyo na amekuwa akizushiwa kuuza watoto.
Aidha Anna Kasile ambaye anadaiwa kuwa ni mama mkubwa,msimamizi wa kituo aliyedaiwa kuwa muda wote na wazungu hao amepasua ukweli katika semina ya Mapadre,watawa wa kike na kiume na makatekista kuhusu kilichotokea.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi,Amina Nganile (29)ambaye anafanyakazi ya kupika chakula katika mgahawa wa baa moja iliyopo katikati ya Mwanjelwa na Kabwe (jina tunalihifadhi),jijini hapa alikiri kuingia mkataba wa kutunza mimba na wazungu waliopelekwa na Mama yake mkubwa (Anna Kasile) baada ya kuuguwa nusuraya kufa.
Amina alisema yeye ni mama wa watoto wawili akiwemo Agapto mwenye umri wa miaka minne na huyo aliyemzaa Novemba,2013 ambaye anatunzwa katika kituo cha care and share cha Simike kinachosimamiwa na Kasile ambaye ni mama yake Mkubwa.
"Sina hamu na wanaume kwa sababu aliyenizalisha awali hamtunzi mtoto na huyu aliyenizalisha anaitwa Amos Mfanyakzi wa stela Farm ni mkazi wa Kyela hajanitunza wakati wa mimba,niliugua nusura nipoteze maisha na hivyo nilitaka kuitoa lakini Mama Kasile alinisaidia kunipeleka Hospitali wakanipima Ultra Sound na kukuta mtoto yupo hai nami nikatibiwa hadi kupona na nikajifunguwa salama,"amesema.
Ameongeza"nilijifunguwa mtoto wa kiume mwenye uzito wa kilo tatu na siyo kilo nne na kwamba nilikaa naye baada ya muda nikawakabidhi mtoto waende kumtunza na mimi nililazwa na baadaye nikatoka na ninaendelea vizuri na mtoto ninakwenda kumuona."
Alipoulizwa kuhusu mkataba wa kumtunza mtoto hadi baada ya kufikia umri wa mika 18 ndipo atamchukuwa alikiri na kusema ni bora aendelee kukaa huko huko kwa sababu hali yake kiuchumi ni mbaya hata kufikia kudaiwa fedha za mkopo alizokopa katika shirika la mikopo la Eclof Mbeya baada ya kuuguwa na mdogo wake kuufilisi mradi wa mkaa aliomuachia.
"Nilikuwa na stoo ya Mkaa nikiuza kwa madebe na magunia lakini baada ya kuuguwa nilimkabidhi mdogo wangu aendeshe biashara hiyo lakini ilikufa,kwa hiyo nililazimika kuuza kila kitu changu na sasa ninaishi kwa rafiki yangu Nzovwe,hapa nimepata kibarua ninalipwa Sh.2,000 kwa siku sh.1400 pesa ya kula na Sh.600 pesa ya nauli ya dala dala,hali ni mbaya na ninashindwa kulipa deni,"amesema.
Hata hivyo Amina alisema hataki kusikia juu ya wanaume kwa sababu ni wauaji wanapokutaka kimapenzi wana ahadi lukuki lakini baada ya kujifunguwa wanakukana hali inayoweza kusababisha kujiuwa ama kufanya jambo lolote baya kwa hasira baada ya kuchanganyikiwa na anamshukuru Anna Kasile kwa kumnusuru yeye na mtoto wake.
Anna kasile akitoa mada inayozungumzia utetezi wa uhai alisema tangu ajiunge na mikakati hiyo ya kunusuru maisha ya watoto na Prolife amekuwa akikumbana na mikasa mingi ikiwemo kuhojiwa na watu wa ikulu kuwa anajishughulisha kuuza watoto anaowaokota jambo ambalo siyo la kweli.
Akizungumzia suala la Amina amesema baada ya kusikia anataka kutoa mimba kutokana na kutomjuwa mwanaume aliyempa uja uzito huo alilazimika kumsaiia na kuzungumza na wazungu akina Kaufmann waliokubali kumtunza na kumuuguza hadi akapona na kujifunguwa salama na kwamba mtoto yupo hai anaendelea kulelewa katika kituo chake hadi atakapofikia miaka 18 atamchukuwa.
Amesema walilazimika kufika kwa Mwanasheria Mwakolo kwa ajili ya kuwekeana mkataba wa kumtunza mtoto huyo ambapo amedai walilazimika kutoa sh.100,000 kama ada baada ya kuomba kupunguziwa kutoka Sh.150,000.
Wakili Mwakolo hakuweza kupatikana licha ya kumuomba miadi ya kuonana naye kupitia simu yake ya kiganjani baada ya kuomba ufafanuzi wa sheria iliyotumika katika makubaliano ya mkataba wa kutunza mimba sanjari na kufika ofisini kwake januari,29 na 30,2013 bila mafanikio ya kuonana naye.
Ofisa wa Idara ya ustawi wa jamii Mkoa wa Mbeya,Tobias Mwalwego akizungumza na KIONGOZI amethibitisha kupokea mkataba wa makubaliano kutoka kwa wasamaria wema waliolalamikia suala hilo na kwamba kwa kifupi hawakifahamu kituo hicho.
"Leo(januari,30) asubuhi tulikuwa tunajadili mkataba huo ni kitu cha kushangaza wala hakipo katika sheria na taratibu za kuasili mtoto,na ukiangalia kipengere cha nne cha masharti hayo(Kwamba baada ya mtoto kufikisha umri wa miaka 18 MAMA MZAZI ataruhusiwa kumchukuwa mtoto wake) hakiingii akilini kwa sababu atakosa haki za msingi za malezi na mapenzi ya mama,wakati Mama yake yupo,"amesema.
Aidha Ofisa huyo amesema hana uhakika kama kituo cha Care and Share-children's home kama kimesajiliwa kisheria kwa sababu katika idara ya ustawi wa jamii Mkoa wa Mbeya haikitambui wala shughuli zao licha ya mtu aliyefika ofisini kwake kujitambulisha kwa jina la Melvin Kauffman kama Ofisa utawala wa kituo hicho kilicho chini ya Shirika la Harmony International (januari,30,2013).
"Leo amekuja mgeni mmoja akiwa na familia yake akajitambulisha kuwa ni Melvin Kauffman kuwa ni Ofisa utawala wa kituo cha Care and Share kilichopo Simike na kwamba alikuwa anaomba idhini ya kumchukuwa mtoto mmoja yupo Hospitali ya Rufaa Mbeya kitengo cha uzazi Meta kwa ajili ya kumlea na kwamba anawatunza watoto kama hao watatu ambao wanaonekana wakubwa lakini huyo mtoto anayedaiwa kuchukuliwa baada ya mkataba hayupo katika orodha ya watoto aliowaonesha katika picha na maandishi,"amesema Mwalwego.
Amesema kuwa amemjibu Melvin kuwa kabla ya kumchukuwa huyo mtoto aliyekuwa Hospitali atalazimikia kufika katika kituo chake ikiwemo na kufuatilia suala la mkataba wa Amina Nganile na baadaye kujiridhisha kama kituo hicho kimesajiliwa kisheria na taratibu za kuwachukuwa na kuwatunza watoto hao kama zimefuatwa.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani ameahidi kulifuatilia suala hilo na kujuwa ukweli na undani wake ili kama kuna tatizo liweze kushughulikiwa na endapo kuna makosa ya kisheria, sheria iweze kuchukuwa mkondo wake.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment