Na Thompson Mpanji,Mbeya
BAADHI ya wazazi jijini hapa wamelalamikia hatua ya serikali ya
mtaa wa Ilomba,jijini Mbeya kuwatoza Sh.12,500 mchango wa kuandikisha
jina la kuingia darasa la kwanza mwaka 2013.
Hatua hiyo inadaiwa kwenda kinyume na maagizo ya Waziri wa
nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI),Kassim majaliwa kuwa kuandikisha
darasa la kwanza ni bure na hakuna michango yeyote iliyoruhusiwa
kisheria.
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wazazi (majina
yamehifadhiwa)walisema kuwa wameshangazwa viongozi wa serikali ya mtaa
kuandikisha majina ya watoto kwa kutoza sh.12,500 na kwamba mzazi
asiyekuwa na kiasi hicho mtoto wake hawezi kupokelewa.
Walisema wameambiwa kuwa mzazi ambaye hataweza kutoa fedha hiyo
mtoto wake hawezi kusoma shuleni hapo na endapo atakubaliwa basi
atatakiwa kukaa chini kwenye vumbi hatoruhusiwa kukalia dawati jambo
ambalo wamedai ni unyanyasaji.
"Wametuambia eti kama hatutowi basi watoto wetu watakuwa wakisoma
huku wakiwa wamekaa kwenye vumbi darasani na wenzao waliolipa watakaa
katika madawati…ndiyo maana watoto wetu wanarudi wamechafuka ovyo kila
siku kumbe ni sababu ya kuwanyanyapaa,"alisema.
Mmoja wa wajumbe wa serikali ya mtaa wa Ilomba,Mwl.Edwin Kamweli
alisema hizo ni mbinu chafu za baadhi ya wanasiasa kutaka kuzorotesha
maendeleo ya mtaa wa Ilomba kwani mkutano wa hadhara ulikaa na
kukubaliana wanannchi wote kutoa mchango huo kwa ajili ya kuboresha
mazingira ya shule.
"Huu mfumo wa vyama vingi utaturudisha nyuma tukiendekeza maneno
bila vitendo…kuna watu wavivu wanatumia fursa ya demokrasia kuturudisha
nyuma na sisi tunasema hatuwezi kukubali na haiwasaiidii tunasonga
mbele…vikao na mikutano ikiitishwa wanasema wapo bize tuikipitisha
maazimio wanasema tunawaonea,"alisema.
Mwl.Kamwela alisema kiasi hicho cha sh.12,500 kilipitishwa na
wananchi waliohudhuria mkutano mmoja wa hadhara ikiwa na lengo la
kuboresha mazingira ya shule na wanafunzi ili waweze kusoma bila
kubanana.
Alisema mgawanyo wa fedha hiyo ni Sh.10,000 kwa ajili ya dawati
litakalochangiwa na wanafunzi watatu watakaolitumia ambapo kila mmoja
atachangia kiasi hicho na kukamilisha gharama ya ununuzi wa dawati moja
kwa Sh.30,000.
Mwalimu huyo mstaafu aliendelea kufafanua kuwa katika shule hizo
mbili za Kagera na Ruanda Nzwovwe kuna mlinzi anayelipwa na hivyo kila
mzazi wamekubaliana achangie Sh.1,500 ambapo mchango wa maji ni
Sh.1,000.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilomba,Erasto Mwakapoma alifafanua kuwa
uandikishwaji ni bure lakini michango hiyo ilitokana na wananchi wenyewe
baada ya kukaa katika mkutano wa hadhara wa mtaa wa Ilomba
Novemba,30,2012 ambapo yeye alikaribishwa na kwamba wanaochangia ni
wananchi wote na siyo wazazi wanaowaandikisha watoto shule pekee.
Mwakapoma alisema shule ya smingi Kagera na Ruanda Nzovwe
zinatarajia kuandikisha watoto zaidi ya 200 ingawa lengo lilikuwa watoto
130,lakini hawatoweza kukataa kuwaaandiskisha watoto waliofikia umri wa
kwenda shule hivyo kunahitajika madawati ya ziada.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment