Translate

Tuesday, December 11, 2012

mizengwe yatawala uchaguzi mdogo Jimbo la Songwe,wilayani Chunya


Na Thompson Mpanji,Chunya
 
ULE usemi usemao mfa maji haishi kutapatapa na dalili za mvua ni mawingu umeanza kuonekana mapema katika jimbo la Songwe wilayani Chunya, ambapo kunatarajiwa kufanyika uchaguzi mdogo wa Mwenyekiti wa Kijiji cha saza na vitongoji viwili kutokana na wananchi kumtuhumu Mbunge wa Jimbo hilo Philipo Mulugo kuagiza kuhakikisha Chama cha Mapinduzi (CCM) kinashinda kwa gharama yeyote na kwa aina yeyote alimradi Jimbo hilo lisiingie dosari ya kushikwa na vyama vya upinzani hali ambayo inaelezwa na wachambuzi wa kisiasa kuwa ndiyo kwisha kisiasa.
 
Ujumbe mmoja kutoka kwa kada wa Chama cha mapinduzi (CCM) uliofanikiwa kunaswa na gazeti hili unasema kuwa,"Nilijaribu kuongea na usalama uchaguzi usimamishwe hadi mazungumzo ya mezani yatakapochukuwa nafasi wakaelewa ila wansema kesho (Desemba,10) uchaguzi."
 
Wanaodaiwa kukamatwa na Jeshi la Polisi wilayani Chunya ni pamoja na Diwani viti maalum Kata ya Kanga,Katibu wa Chadema wilaya ya Chunya Bryson Mwansimba,wagombea wawili wa kitongoji cha saza kati ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kata ya kanga John Mponzayo,Katibu mwenezi wa Chadema Kata ya Kanga Suleimani Tanganyika,Katibu Mwenezi Kata,Amosi Tanganyika aliyekuwa anagombea Mwenyekiti wa kitongoji cha Saza kibaoni, wasanii waliofika na gari la matangazo na mpiga picha aliyefahamika kwa jina moja la Chris.
 
Tafsiri hizo kwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa zimekuja kufuatia kukamatwa kwa Viongozi,wanachama,wapenzi na watu wanaofanya kazi na Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA),wilayani Chunya ambao wanadaiwa kukamatwa kwa madai ya kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Saza na vitongoji viwili juzi.
 
Katika kampeni hizo zinazodaiwa kufungwa kwa amani na utulivu Desemba,4 mwaka huu majira ya saa 11 jioni viongozi hao wanadaiwa kukamatwa saa 9 usiku katika nyumba za kulala wageni na wengine majumbani mwao ambapo gari tano za jeshi la polisi aina ya 110 Defender zikiwa na askari zinadaiwa kuonekana kufanya doria mithili ya operesheni ya kusaka majambazi lakini kumbe ilikuwa inafanyakazi kubwa ya kuhakikisha Chama cha mapinduzi kinashinda.
 
"Haikuweza kufahamika mara moja kuwa kwanini kulikuwepo na askari lukuki na gharama za mafuta na posho kwa magari na askari polisi zinatokea wapi ingawa kulikuwepo na tetesi kuwa mamilioni kadhaa yamemwagwa kuhakikisha lengo la kuilinda CCM linatimia,"kilisema moja ya chanzo cha habari kutoka Saza, Chunya.
 
Kutokana na kuibuka kwa sintofahamu hiyo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kitendo kinachoendelea kufanyika Jimbo la Songwe kulazimisha uchaguzi kufanyika Desemba,10,2012 licha ya Chadema kumwandikia barua msimamizi wa uchaguzi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya,Maurice Sapanjo kutokubaliana na kuwepo kwa uchaguzi huo kutokana na kukiukwa kwa sheria za uchaguzi bado inaonesha dhahiri ni shinikizo kutoka kwa Mbunge huyo ambaye anadaiwa kusikika akisema lazima CCM ipite kwa gharama yeyote.
 
"Tulisikia juu juu maneno kuwa zimemwagwa Mil.10 kuhakikisha mafuta kwa ajili ya magari na posho za kutosha kwa watakaoendesha zoezi la kufanikisha ushindi wa kishindo kwa CCM,mimi pia nipo mafichoni kwa sababu ni miongoni mwa watu waliowekwa katika orodha kuwa lazima tukamatwe na kuswekwa mahabusu kwa sababu tunatishia kibarua chake cha ubunge lakini unadhani nini kitafuata kama siyo kuzijaza hasira ndugu,,jamaa na marafiki zetu tunaosaidiana kwa hali na mali,hiki ni kifo cha CCM Jimbo la Songwe," kilisema chanzo kingine.
 
Aliongeza, "Unajuwa mbinu wanazotumia baadhi ya wagombea ubunge za kupita bila kupingwa ni kuwaweka sawa baadhi ya viongozi wa upinzani ili wasisimamishe wagombea na hivyo kuonekana wanapita bila kupingwa jambo ambalo siyo kweli huku wakidai rafu hizo zitadhihirika 2015 itakapokuja kuanguka CCm jimbo Songwe kifo cha mende."
 
Akizungumza na gazeti Katibu Mwenezi wa Chama cha Demokrasi na maendeleo(CHADEMA),wilaya ya Mbeya Lucas Mwampiki hilo alisema walishamwamndikia barua msimamizi wa uchaguzi mdogo wa Kata ya saza,Maurice Sapanjo ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya kutokubaliana kufanyika uchaguzi huo kutokana na madai matano ya ukiukwaji wa sheria za uchaguzi lakini amepuuza.
 
Mwampiki ambaye ni Diwani wa Kata ya Mwakibete aliyataja makosa hayo ni pamoja na 1.kuandikisha watu wanaojuwa kusoma na kuandika 100 huku wote wanajuwa kusoma na kuandika,kutowahusisha viongozi au vyama kujuwa na kukagua vituo vya kupigia kura,3.kutowatambulisha wasimamizi wa vituo kwa wagombea au vyama vyao, kutopokea,kuwapa voapo wala kupokea orodha ya mawakala wa vyama pinzani,5.kutokujibu barua za malalamiko za wagombea au vyama kwa wakati.
 
Katibu huyo alitaja rafu iliyochezwa na CCM katika vituo vya kupigia kura ni kuongeza majina bandia ya wapiga kura ambapo katika kituo cha Saza kati wapiga kura waliojiandikisha walikuwa 96 waliongeza majina bandia 32 na kufanya idadi kufikia 128,kituo cha Bwana mzungu walioandikisha kihalali walikuwa 86,majina bandia 38 na kufanya idadi kuwa wapiga kura 124,kituo cha kibao 99 majina yaliyoongezwa 27 na kuwa jumla ya watu 126,kituo cha bwawani 98 waliongeza majina bandia 47 kwa hiyo watu waliowaongeza ni 144 ambapo ni vituo viwili vya Mwembeni na makambini hawakupata idadi.
 
"Watu walioandikishwa na kuongeza 844 kura zao (CCM)zilikuwa 744,kura za Chadema 100 walivyopanga matokeo yaani huo ndiyo ushindi waliojipangia.wananchi wamechoma moto na kuchana karatasi za kupigia kura baada ya kutoridhika na rafu zinazochezwa,"alisema Katibu.
 
Alisema hiyo ni idadi iliyotengenezwa kwa ajili ya ushindi kwa kuchukuwa katika kura za maoni ndani ya CCM na walichoshangazwa ni kupelekwa magari aina ya defender tano, mbili zilirudi Mbeya mjini na tatu zilirudi chunya,wamelazimisha leo (Desemba,10)ufanyike ni wao,vyombo vya ulizi na usalama vinahusika,kijiji cha saza kina malalamiko ya uuzwaji wa kifusi cha mchanga wa dhahabu kwa Sh.Mil.392,shinikizo ni kwa viongozi wakuu wa serikali na mtoto mmoja wa kigogo kwa gharama yeyote lazima ushindi.
 
"Nawaonya ccm hatutarudi nyuma kudai haki za wanyonge,haturudi nyuma kupigania haki za watanzania ndiyo wanatuchochea zaidi,ccm waache kutegemea vyombo vya dola na kama kweli wangekuwa wanataka haki mbona katika majukwaa yao hawasemi haki wanang'angaania amani na utulivu ,wajuwe amani na utulivu haviwezi kuja bila kutimiza ama kutekeleza haki,navishauri vyombo vya dola waache kufanyakazi ya CCM waache kufanyakazi kwa mazoea,wasiwe chanzo cha kuvuruga amani,"alisema.
 
Wakati yakiwa yametendeka,Hali ya ulinzi na usalama imezidi kuimarishwa kuliko ilivyo kawaida kuanzia maeneo ya mji mdogo wa Mbalizi kuelekea barabara ya Mkwajuni ndani ya jimbo la Songwe na barabara ya kupitia Isanga Mbeya mjini kuelekea makao makuu ya Wilaya kupitia Makongolosi hadi Sawa ambapo askari wa kikosi cha kutuliza ghasia wametanda wakiwa na silaha za moto,mabomu,virungu huku wakiwa wamevalia rasmi na ngao kwa ajili ya kukabili hali yeyote itakayojitokeza ya uvunjifu wa amani.
 
Kwa mujibu wa mshuhuda wamesema kuwa ulinzi huo umeimarishwa kufuatia kuwepo kwa tetesi kuwa wanachama wa Chadema kutoka Tunduma na Mwanjelwa jijini Mbeya wamepanga kuvamia jimboni Songwe kuhakikisha wanafanya vurugu ili uchaguzi usifanyike.
 
Mmoja wa wanachama wa Chadema kutoka Mkwajuni aliyejitambulisha kwa jina moja la Mambwe,ambaye yupo katika maeneo ya Saza anasema kuwa kila kituo kuna askari wanne wa kikosi cha kutuliza ghasia wakiwa wamevalia sare zao rasmi,ngao,mabomu na virungu huku maofisa usalama wakiwa wametanda kila maeneo na kuongeza kuwa ni uchaguzi unaofanywa na wanaccm pekee.
 
"Hali huku siyo shwari wanafanya uchaguzi wa CCM uliolazimishwa na Msimamizi wa uchaguzi wa Wilaya Sapanjo,amepita kutangaza leo kuwa lazima uchaguzi ufanyike na wanapita kuwalazimisha wanachama kwenda kupiga kura,picha za wagombea wa chadema hakuna zimebaki za wagombea wa CCM,nikwambie mizengwe ilianza tangu Desemba,3 walimwagwa maofisa usalama na kufuatilia kila mkutano wa Chadema,,Polisi waliingia tangu Desemba,8 majira ya saa 10 jioni na vitisho vyao utadhani kuna vita,"alisema Mambwe.
 
Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya chunya,Sapanjo alipopigiwa simu hakuweza kupokea licha ya kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kuhusu madai ya ukiukwaji wa sheria za uchaguzi katika uchaguzi huo mdogo wa Kijiji cha saza na vitongoji vyake viwili hakuweza kujibu.
 
Mbunge wa jimbo la Songwe ambaye pia ni Naibu waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi,Philipo Mulugo alipoulizwa kuhusiana na madai hayo dhidi yake alijibu kwa kuhoji"nani anayelalamika?Mimi ni Mbunge wa eneo husika ni lazima nihakikishe chama changu kinapata ushindi mnono kwa kufanya kampeni zinazofuata taratibu za uchaguzi,sasa hao wanaosema mamilioni wameyaona wapi?."
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,Diwani Athumani amekanusha madai ya jeshi lake kutumika kwa maslahi ya chama chochote zaidi ya kuangalia hali ya ulinzi na usalama na kuchukuwa majukumu yake hasa pale inapoonekana uvunjifu wa amani na utulivu unatokea na usalama wa watu na mali zao upo hatarini.
 
"Ni uzushi,nikukumbushe tu kuwa jukumu la msingi la Polisi ni kuwalinda watu na mali zao.juzi mali ziliharibiwa Saza,watu waliumizwa na uporaji ukafanywa.unadhani ni ipi nafasi ya ya polisi katika mazingira hayo? Naamini kuwa mpenda amani hawezi kuwahofia askari,"alisema kamanda Diwani.
 
Mwisho.
 
 

No comments:

Post a Comment