Translate

Tuesday, December 11, 2012

Tanzania ikiwa imebakisha miaka 3 ya utekelezaji wamipango nane ya milenia

Na Thompson Mpanji,Mbeya
 
TANZANIA ipo katika utekelezaji wa millennia ambayo ni matokeo ya mkutano wa kilele wa millennia wa umoja wa mataifa uliofanyika mwezi septemba mwaka 2000 na kutokana na hali hiyo sitegemei kuwa kuna mtanzania asiyejuwa malengo hayo nane.
 
Lakini kwa kukumbushana ningependa kuyarejea tena maleongo hayo yaliyopangwa kutekelezwa katika mataifa 189 ambayo yalikuwa ni makubaliano yanayozitaka nchi zote zilizoendelea na zinazoendelea kufanyakazi kwa pamoja na kuhakikisha umaskini na njaa duniani vinatokomezwa,kuhakikisha elimu sawa kwa watoto wote,usawa wa jinsia na uwezeshwaji kwa wanawake.
 
Malengo mengine ni kupunguza vifo vya watoto wachanga,kuokoa maisha ya akina mama wazazi,kupunguza na kutokomeza ugonjwa wa ukimwi,marali na magonjwa mengine maambukizi,kudumisha usafi na ubora wa mazingira pamoja na kudumisha ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo kwa ujumla malengo ya millennia yanasisitiza zaidi maeneo ya afya,elimu,mazingira na ustawi wa jamii kwa ujumla.
 
Disemba,4,2012 kumefanyika tukio muhimu na la kihistoria kwa taifa la Tanzania kutokana na kuwa miongoni mwa nchi 50 kati ya 189 zilizochaguliwa kujadili,malengo hayo nane ya millennia katika kanda saba ambazo mahali yalipofanyika katikamabano ni kanda ya Ziwa (Mwanza),kanda ya kaskazini (Arusha),Kanda ya kati(Dodoma),kanda ya nyanda za juu (Mbeya),kanda ya kusini(Mtwara),kanda ya magharibi (Shinyanga) na kanda ya mashariki (Morogoro).
 
Katika kutekeleza hili,John kajiba mtafiti kutoka taasisi ya utafiti wa mambo ya uchumi na jamii (ESRF-Economic and Social Research Foundation) anasema taasisi hiyo imeombwa kusimamia majadiliano hayo kwa kushirikiana na Ofisi ya rais tume ya mipango katika kanda hizo saba na hasa katika maeneo ya Serikali za mitaa,Asasi za kiraia,watoto,wazee na wanawake wadogo ambapo kwa kanda ya Mbeya yamefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Paradise,Soweto,jijini Mbeya.
 
Kajiba anasema kwa kuwa imebakia miaka mitatu ili kukamilisha miaka 15 iliyopangwa kufikia malengo ya millennia 2015 hivyo watu na taasisi mbalimbali zimeona ni bora kuanza kujadili na kujiuliza kitatokea nini na nini kifanyike baada ya mwaka 2015 ili kuongeza kasi na kutoa msukumo wa maendeleo duniani.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya ESRF kuna mafanikio na changamoto ambazo zimejitokeza katika utekelezaji wa malebngo ya millennia ambapo kwa upande wa Tanzania imefanya vizuri katika maeneo mengi,licha ya baadhi ya maeneo kuwa na matokeo ambayo hayakuridhisha.
 
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Abbas kandoro ambaye alikuwa mgeni rasmi aliyefungua mkutano huo wa mashauriano katika hotuba yake amesema utekelezaji wa Tanzania unategemea utekelezaji wa kila Mkoa na Wilaya na hivyo ni dhahiri utatofautiana.
 
Ametolea mfano kwenye eneo la Ukimwi,Mkoa wa Mbeya una asilimia 9.2 kwa takwimu za mwaka 2008 wakati kitaifa ni asilimia 5.7,kupunguza umaskini kitaifa imetokea asilimia 39 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 1990 hadi asilimia 33.6 kwa takwimu za mwaka 2007.
 
Kandoro anasema pato la mkazi wa Mbeya ni juu ya dola 1 hadi 1.5 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2010 ambapo katika elimu ya msingi na Sekondari ukiangalia katika uwiano wa Ke na Me wamevuka lengo kama nchi kwa asilimia 101 na 205 na kwa Mkoa wa Mbeya ni asilimia 102 na 88 ambayo kwa ujumla haijavuka lengo.
 
Anasema lazima kukiri kuwa bado kuna changamoto katika kutokomeza umaskini wa kipato,njaa,kuboresha afya ya uzazi na huduma za maji salama pamoja na elimu.
 
Kandoro ametoa maoni kuwa endapo kila mtanzania atajituma katika kutafuta maisha na kuzitumia fursa zinazomzunguka,akaacha kuwa mnung’unikaji wa hali ngumu ya maisha huku amekaa kijiweni,akaacha kumtafuta mchawi kwa kila linalomsibu,akawa mchangiaji katika kuhakikisha hali ya utulivu na amani inadumishwa kwa kuheshimu misingi ya utawala bora,kasi ya kuliendeleza taifa itakuwa kubwa.
 
"Kwa sasa bado tunaongea sana, ‘we are talking a lot,’ninaamini mkusanyiko huu utasaidia sana kufanya tathmini ya pamoja kujuwa tulikotoka,tulipo na tunakokwenda,ninaipongeza serikali kuteuwa Taasisi ya utafiti katika Nyanja za uchumi na jamii (ESRF) ifanye kazi ya kukusanya maoni ya wadau mbalimbali,"anasema.
 
Mkuu wa Mkoa huyo amesema kupitia warsha kutoka katika mikoa yote Tanzania, anao uhakika,ushauri na mapendekeo ya washiriki kuhusu kuamua nini kifanyike kwa siku zijazo baada ya 2015 ni muhimu sana.
 
Kutokana na mpango wa millennia mataifa makubwa yaliyoendelea yalipangiwa kutoa asilimia 7 ya pato lao la ndani kuchangia nchi zinazoendelea ambapo ni asilimia 4 ya nchi za Scandinavia zimeonekana kuongoza katika kuchangia ingawa siyo kwa asilimia zote na hiyo ni mojawapo ya changamoto kubwa iliyozikumba nchi nyingi tegemezi kukwama katika mipango na miradi yao ya maendeleo baada ya kukwama kwa misaada.
 
Dkt.John Mduma mwezeshaji ambaye ni Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam anasema lengo la mashauriano hayo ni kutoa kichocheo cha mjadala wa wadau mbalimbali,kujenga taswira ya kimataifa ya hali ya baadaye kwa mapendekezo madhubuti,kuhakikisha na kusikika sauti za maskini na wasio sikika,kutambua na kuchambua masuala yatakayoathiri maendeleo,kushawishi mchakato ndani ya serikali kuu ioane na taasisi na matokeo yanayotarajiwa.
 
Mwisho.

No comments:

Post a Comment