Translate

Wednesday, October 31, 2012

serikali haijaridhishwa na ujenzi wa barabara ya kuelekea Chunya

SERIKALI imetishia kuinyang’anya kampuni ya China Communication Construction Limited zabuni ya ujenzi wa barabara ya kutoka Mbeya mjini hadi Lwanjilo wilaya ya Mbeya Vijijini yenye urefu wa kilometa 36 baada ya kutoridhishwa na kasi ya utendaji kazi ya mkandarasi huyo.




Hatua hiyo ya Serikali imetokana na mkandarasi huyo kushindwa kufikia malengo ya ujenzi huo kwa kiwango cha lami katika muda uliopangwa huku akiwa tayari ameshakabidhiwa fedha za awali za mradi huo shilingi bilioni Nane za Tanzania.



Ujenzi huo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 55 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Wahisani wa maendeleo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Mbeya mjini hadi wilayani Chunya yenye urefu wa kilometa 72.



Sehemu ya pili ya ujenzi huo kutoka Lwanjilo hadi Chunya mjini utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 44 kupitia mkandarasi mwingine.



Mkandarasi huyo aliyeanza kazi hiyo Novemba mwaka jana amechukua nafasi ya mkandarasi wa awali kampuni ya Kundan Sing iliyokabidhiwa ujenzi huo mwaka 2010 kabla ua kushindwa kuendelea na kazi kutokana na Serikali kuchelewa kutoa fedha mradi huo.



Hata hivyo tangu alipokabidhiwa kazi hiyo, kasi ya utendaji wake imekuwa ikilalamikiwa na mamlaka husika kwa maelezo kuwa ameshindwa kuifanya kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa.



Akikagua ujenzi huo Oktoba 15, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Greyson Lwenge, amesema Serikali hairidhishwi na kasi ya utendaji kazi ya mkandarasi huyo na kutishia kumnyang’anya zabuni hiyo.



“Nimetembelea ujenzi huu kwa kilometa zote 36 kutoka Mbeya mjini hadi hapa Lwanjilo, ukweli sijaridhishwa na kazi inavyokwenda, mvua zinakaribia kunyesha na hakuna mafanikio yaliyofikiwa kama tulivyotarajiwa.”



“Serikali imeshatangaza kuwa barabara hii ni lazima ikamilike kwa wakati, hivyo kama tutaona mkandarasi huyu anaendelea kusuasua, hatutasita kumnyang’anya kazi na kumtafuta mkandarasi mwingine, tunataka kazi ifanyike hatutaki maneno.” alisema Injinia Lwenge.



Hadi sasa mkandarasi huyo amenza ujenzi wa barabara hiyo katika kijiji cha Lwanjilo katika urefu usiozidi kilometa tano hali inayoitia shaka Serikali kuwa huenda isikamilike kwa wakati katika kipindi cha miezi 36 tangu alipokabidhiwa zabuni hiyo Novemba mwaka jana.



Kutokana na hali hiyo Injinia Lwenge ameiagiza Wakala wa Barabara nchini, TANROADS mkoa wa Mbeya na Mhandisi wa mkoa kuhakikisha mkandarasi huyo anatekeleza kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba uliopo pamoja na kuhakikisha barabara hiyo haifungwi wakati wa mvua ili kuepusha usumbufu kwa wananchi.



Hata hivyo viongozi wa kampuni hiyo ya China Communication Construction Limited hawakuwa tayari kuzungumza na Waandishi wa habari kuhusu hali hiyo huku wakishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kuchelewa kuanza kwa ujenzi huo wakati wakizungumza na Injinia Lwenge.



Awali mmoja kati ya viongozi wa kampuni hiyo ambao pia hawakuwa tayari kutaja majina yao, alijifanya hajui kuzungumza lugha ya Kiingereza na kutumia mkalimani kumjibu Injinia Lwenge kabla ya Naibu Waziri huyo kubaini ujanja huo na kumlazimisha kuzungumza lugha hiyo na hatimaye kufanya hivyo kwa ufasaha mkubwa.



Barabara hiyo ni miongoni mwa barabara zilizomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, CCM, ya mwaka 2010 ambapo Rais Jakaya Kikwete, aliwaahidi wakazi wa vijiji vinavyopitiwa na barabara kuwa atahakikisha inatengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuwaondoakuwa atahakikisha inatengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuwaondolea kero ya usafiri hasa wakati wa mvua.



Ubovu wa barabara hiyo umesababisha wakazi wa kijiji cha Lwanjilo kutozwa kati ya shilingi 8,000 hadi 10,000 kwenda Mbeya mjini umbali wa kilometa 36 wakati nauli ya kutoka Mbeya mjini hadi wilayani Kyela umbali wa zaidi ya kilometa 110 ikiwa ni shilingi 3,000.



Mwisho

No comments:

Post a Comment