Translate

Saturday, October 27, 2012

Kardinali Pengo atamka vurugu za Tanzania asema "Kamwe msitumie kinzani, vurugu na misigano ya kidini kujinufaisha kiuchumi, kisiasa, kijamii na kidini"

 Na Thompson Mpanji

MAASKOFU waliopo katika Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya inayoendelea mjini Vatican wamesema, kati ya mambo yanayoendelea kukwamisha mchakato wa majadiliano ya kidini ni pamoja na misimamo mikali ya kiimani.



Wamesema vyanzo hivyo vinasababisha watu kutoheshimu sheria za nchi kwa kutaka kujichukulia sheria mikononi mwao pamoja na malumbano ya kidini yanayolenga kuvunja misingi ya amani na mshikamano kati ya watu wa mataifa kwa malengo binafsi,kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini.



Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar alisema , choko choko, machafuko na uharibifu wa mali kwa misingi ya kidini, zimeendelea kujionesha kwa namna ya pekee nchini Nigeria na Tanzania



Alisema hii ni kutokana na sababu kwamba, watu wanashindwa kuelewa kwamba, kimsingi hakuna dini inayoshabikia mapigano wala machafuko ndani ya Jamii.



Kardinali Pengo alisema, kuna watu ambao wanapenda kutumia tofauti za kidini kama njia ya kujijenga kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini, kiasi hata cha kuhatarisha amani, usalama, utulivu na mshikamano wa kitaifa.



Alisema hali hiyo inatokana na watu kugubikwa na ubinafsi, uchu wa mali na kupenda mno madaraka ambapo hawataki kusikia ukweli mkamilifu kuhusu masuala ya kidini, kwao jambo la msingi ni kufaidika na migogoro na kinzani za kidini.



Kardinali Pengo ametoa wito kwa Waamini wa Dini ya Kiislam na Kikristo kuendeleza moyo wa majadiliano ya kidini, kwa kuheshimiana, kuthaminiana na kujadiliana masuala muhimu ya kidini kwa ajili ya mafao ya wengi na kamwe tofauti zao za kidini zisiwe ni chanzo cha kinzani, vurugu, umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia na uharibifu wa mali ya watu.



Hata hivyo ameishauri Serikali na vyombo vya dola kutekeleze wajibu wake kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unashika mkondo wake.



Amewaonya wanasiasa wanaotumia tofauti za kidini kama njia ya kujitafutia umaarufu, ili hatimaye, kujijenga kiuchumi, kisiasa na kijamii, kuacha mara moja kwani wanaweza kusababisha maafa makubwa kwa Jamii,"Kamwe hasiwepo mtu anayetumia dini kama ngao yao katika medani mbali mbali za maisha."



Aidha Kardinali Pengo amewaomba watanzania na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba, tofauti za kidini na kiimani zimekuwepo nchini humo miaka nenda rudi, lakini watu wakaheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana na anajiuliza, kumetokea nini hata leo hii dini iwe ni chanzo cha kinzani, vurugu na machafuko nchini Tanzania?.



Amefafanua kuwa wote wanaotaka kuchochea vurugu, vita na kinzani kwamba, amani ikitoweka, hakuna mtu atakayesamilika kwani matunda ya kuvunjika kwa misingi ya haki kamwe hayawezi kudumu hivyo ni jukumu la kila mtu kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani na kamwe tofauti za kidini zisiwe ni chanzo cha kinzani, vurugu na umwagaji damu.



Mwisho.





No comments:

Post a Comment