Translate

Wednesday, November 14, 2012

Askofu Chengulaamwalika waziri mulugo kuchangisha zaidi ya Sh.mil.100 ujenzi wa kijiji cha watoto yatima cha Kambarage Mbeya

Na Thompson Mpanji,Mbeya
 
MLEZI Mkuu wa Chama cha vijana,wanawake wa kikristo Tanzania(YWCA),Tawi la Mbeya,Askofu Evaristo Chengula wa kanisa Katoliki Jimbo la Mbeya ametoa wito kwa watanzania wote wenye mapenzi mema bila kujali itikadi za kisiasa,dini,kabila wala rangi kuchangia Kijiji cha watoto yatima wanaoishi katika mazingira hatarishi na wenye mtindio wa ubongo cha Kambarage  ili kuweza kukamilisha ujenzi huo.
 
Askofu Chengula ambaye ndiye msimamizi mkuu wa YWCA amemualika Naibu  Waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi,Philipo Mulugo (MP)  kuendesha harambee ya ujenzi wa Kijiji cha watoto yatima cha Kambarage novemba, 24 mwaka huu.
 
Naibu waziri Mulugo anatarajia kuwa mgeni rasmi katika changizo hilo litakaloambatana na  maandhimisho ya miaka 20 ya YWCA,Tawi la Mbeya hafla inayotarajia kufanyika katika ukumbi wa Mkapa,jijini Mbeya.
 
Askofu Chengula ataungana na walezi na wasimamizi wenzake wa chama hicho ambao ni Askofu wa kanisa la Anglikana,nyanda za juu kusini, John Mwela,Askofu wa kanisa la Moravian jimbo la kusini magharaibi,Alinikisa Cheyo,Askofu wa Jimbo la Moravian jimbo la kusini, Lusekelo Mwakafwila na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Konde,Dkt.Islael Mwakyolile.
 
Akizungumza kwa niaba ya Askofu Chengula,Katibu wa YWCA Tawi la Mbeya,Bi.Tabitha Bughali alisema   watarajia mgeni rasmi,Naibu Waziri Mulugo atafanikisha kuchangisha Sh.Mil.100 ili kuendeleza ujenzi huo kwa awamu ulioanza tangu mwaka 2009 ambapo zaidi ya sh.Bil.2 zinahitajika kukamilisha ujenzi huo.
 
Katibu huyo alisema awali Mwenyekiti wa IPP Media, Reginald Mengi  alichangia  zaidi ya Sh.Mil.25 kusaidia ujenzi huo na baadhi ya wadau wengine waliochangia ni pamoja na mmiliki wa shule za Clementine foundation Marry Camm ambaye anatarajiwa kuwasili katika shughuli hizo,Prof.Mwansoko,Mbunge wa viti maalum Mh.Hilda Ngoye,Prof.Mark Mwandosya na wadau wengi.
 
Amewataja wageni watakaohudhuria katika changizo hilo ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Abbas Kandoro,Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Mbeya,wabunge,wakurugenzi wa halmashauri,wakurugenzi wa mahoteli ambapo baadhi ya wadau tayari wameshaanza kutoa michango yao kama Wakili Mbise,,Makasini Hotel,Mwenyekiti wa umoja wa wamiliki wa hoteli Mahenge,Penge Hoteli,Wakili Mshokolwa na wakili Msigwa.
 
Bi.Bughali alisema shughuli hiyo itaendeshwa na kamati ya maandalizi inayoongozwa na Jaji Upendo Msuya ambaye ndiye Mwenyekiti wa kamati ya hiyo na kwamba wafanyabiashara,taasisi za serikali na binafsi na watu mbalimbali wenye mapenzi mema wanatarajia kushiriki katika harambee hiyo na ametoa wito kwa watanzania wote kujitokeza kuiunga mkono YWCA katika harakati za kuwasaidia watoto yatima.
 
Mwisho.

No comments:

Post a Comment