Na Thompson Mpanji,Mbeya
JESHI la polisi limefanikiwa kuzima jaribio la baadhi ya madereva
wa boda boda na daladala kuzuia magari yanayobeba mafuta kusafirisha
kwenda nchi za jirani za Zambia baada ya kuamua kuweka kizuizi cha mawe
katika barabara ya Mbeya/ Tunduma,katika maeneo ya mama John kwa madai
ya kukerwa na adha ya mafuta huku wakiyaona yakipita kuelekea nchi
jirani.
Sakata hilo limedumu kwa takribani masaa mawili tangu saa 1 asubuhi
hadi saa 3 asubuhi baada ya madereva wa daladala na waendesha boda
boda kudaiwa kupandwa na jazba ya kukosa mafuta katika kituo cha Orxy
Mama John na hivyo kuamua kupanga mawe barabarani jambo ambalo inadaiwa
endapo Polisi wasingejitokeza haraka hali ingekuwa tete kutokana na
baadhi yao kuonekana waking'ang'ania makufuli ya malori ya mafuta
waliyofanikiwa kuyazuia na kuwateremsha madereva kwa nguvu.
"Ninakwambia kulikuwa na hatari kubwa kama wasingetokea wale FFU
kwa sababu wengine walitaka kuyapiga kiberiti malori hayo ya mafuta
baada ya kuwalazimisha madereva wa magari hayo kufungua nao wakagoma na
huku madereva wa malori ya mafuta nao walikuwa wamechukia kwa hiyo
tungekuwa tunazungumza kitu kingine,na madereva wengine wa malori
walivyopata taarifa kuwa hali siyo shwari waligeuza na kurudi Uyole
kuegesha Uyole walivyopata lakini walipotokea maaskari
walitawanyika,"alisema mmoja wa wafanyakazi wa kituo hicho cha mafuta
ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Alisema kuwa chanzo cha hasira ya watu hao hawakuamini kama mafuta
waliyokuwa wakiyatoa ya petroli kama yamekwisha na kubakiwa na mafuta ya
dizeli na hivyo kuanza kupiga kelele na kuhamishia hasira zao
barabarani hadi Jeshi la polisi likiongozwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya
ya Mbeya Sylivester Ibrahim kuwaaminisha kwa kumuomba mmiliki wa kituo
hicho kupima na kuhakikisha kweli hakuna mafuta waliamua kuondoka.
Gazeti hili limeshuhudia majira ya saa 4 asubuhi baada ya hali ya
utulivu kurejea malori ya mafuta yalionekana yakipita kasi katika maeneo
ya mama John tofauti na siku nyingine ambapo taarifa kutoka kituo cha
Mafuta cha Uyole yanapoegeshwa magari yanayoelekea Tukuyu kuwa mafuta
yapo ila bei ya mafuta ya petroli kwa lita inadaiwa kufikia Sh.3,000.
Mmoja wa waendesha boda boda ambaye hakutaka kutaja jina lake
alisema wamekerwa sana na kitendo cha kuhangahika na kukosa mafuta kwa
takribani siku nne sasa huku magari ya mafuta yakiwa yanapitishwa
machoni pao kwenda zambia na kwingineko jambo ambalo alidai bado
linawasumbua katika vichwa vyao kuwa serikali inafurahi kero hii
wanayoipata walala hoi wa chini huku familia zao zikiendelea kuteseka na
njaa kwa kukosa kufanyakazi.
Suala hili la ukosefu wa mafuta bado linaonekana ni kitendawili kwa
watanzania na kwamba endapo serikali haitalishughulikia na kulimaliza
haraka iwezekanavyo kuna hatari ya malori yanayosafirisha mafuta kwenda
nchi ya zambia kupitia Mbeya yakafanyiwa hujuma kutokana na kuwepo na
tetesi kuwa hawajaridhika kukosa mafuta ilhali wanayaona yanapita mbele
ya machjo yao.
Hata hivyo Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia Mkuu wa Polisi wa
Wilaya ya Mbeya,Sylivester,Mkuu wa upelelezi wa Wilaya,Ntatiro,ofisa
habari wa Polisi na baadhi ya makachero wakiwa wamesimamia hali ya
usalama katika zoezi la utoaji wa mafuta ya Petroli na mafuta ya taa
katika kituo cha Total Mafiati huku kukiwa na foleni kubwa ya
magari,waendesha boda boda,watu walioshika vidumu vya lita tatu na tano.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment