Translate

Monday, January 13, 2014

Wawili wasakwa kwa mauaji Kyela na Momba,Mbeya

Na Thompson Mpanji,Mbeya

WATU wawili wanasakwa na Jeshi la polisi kwa udi na uvumba  ili waweze kupandishwa kwa pilato baada ya kutuhumiwa kufanya mauaji katika matukio mawili tofauti Wilaya ya Kyela na Momba,mkoani Mbeya.

Katika tukio la kwanza Bicco Mwakibibi (28),Mkazi wa kijiji cha Lema,Kata ya Ngana,Tarafa ya Tembela,Wilaya ya Kyela,mkoani Mbeya  aliuawa  kwa kupigwa na silaha za jadi,mawe na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake  na kundi la wananchi.

Imeelezwa kuwa tukio hilo limetokea Januari,12,2014 majira ya saa 11.00 alfajiri  baada marehemu na mwenzake  ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja kuvunja kibanda cha biashara  na kuiba  ambapo wananchi walijichukulia sheria mkononi na kwamba mwenzake alikimbia baada ya tukio hilo.

Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya,Kamishana msaidizi mwandamizi,Ahmed Msangi amethibitisha tukio hilo  na kwamba juhudi za kumtafuta kijana aliyekimbia zinaendelea  na ameionya jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi.

Katika tukio la pili, kijana Bonny Silumbe,Mkazi wa Kijiji cha Kapele,Tarafa ya Ndalambo,Wilaya ya Momba,mkoani Mbeya anatafutwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumuuwa kaka yake Adamu Silumbe(27) baada ya kumchoma kisu mgongoni na kufariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya wilaya ya Mbozi.

Kamanda Msangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo  januari,12,2014 majira ya saa 3.30 usiku  na ameonya wananchi kuacha tabia ya kujichukulia  sheria mkononi.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment