Translate

Monday, February 11, 2013

Papa Benedikto XVI atangaza kujuuzuru kutoka katika madaraka ya kuliongoza Kanisa Katoliki



Papa Benedikto XVI atangaza kujuuzuru kutoka katika madaraka ya kuliongoza Kanisa Katoliki 

http://sw.radiovaticana.va/global_images/x.gif



Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita katika maadhimisho ya Mkutano wa Makardinali Jumatatu, tarehe 11 Februari 2013, ametangaza rasmi kwamba, kuanzia tarehe 28 Februari 2013 saa 2:00 Usiku atang'atuka kutoka madarakani na viongozi wenye dhamana ya kuitisha mkutano wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro, watapaswa kufanya hivyo.

Baba Mtakatifu anasema, baada ya kuchunguza dhamiri yake mbele ya Mwenyezi Mungu pamoja na umri wake, anatambua kwamba, hana tena nguvu ya kutekeleza majukumu yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huu ni utume ambao unapaswa kutekelezwa kwa maneno na matendo; sala na mateso.

Ulimwengu huu unakabiliwa na mabadiliko makubwa katika imani, jambo ambalo linahitaji kwa kiasi kikubwa maisha ya imani, ili kuweza kuliongoza Kanisa na kutangaza Injili ya Kristo. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema kwa unyenyekevu kwamba, katika miezi ya hivi karibuni, ametambua kwamba, hawezi tena kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Kwa utashi na uhuru kamili anatamka wazi kwamba, dhamana ya kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, aliyokabidhiwa na Makardinali kunako tarehe 19 Aprili 2005 itafikia ukomo wake hapo tarehe 28 februari 2013 saa 2:00 Usiku. Baba Mtakatifu anawashukuru wote kwa upendo na kazi walizoshirikiana kwa pamoja katika kutekeleza majukumu yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anaomba radhi kwa mapungufu yake ya kibinadamu.

Kwa sasa analikabidhi Kanisa kwa Yesu Kristo mchungaji mkuu. Anamwomba Bikira Maria kuwasaidia Makardinali katika mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro. Anasema, ataendelea kulitumikia Kanisa katika maisha ya Sala.

No comments:

Post a Comment