Translate

Sunday, February 3, 2013

'Kanumba' aibukia Mbeya,adai baba alimkataa akiwa tumboni Shinyanga



Na  Thompson Mpanji,Mbeya

KIJANA anayedai kuwa ni mdogo wa msanii maarufu wa Bongo Movie  marehemu ‘The Great’Steven Kanumba  aliyejitambulisha kwa jina la Lameck Ngogo(20),Mkazi Sokomatola,jijini Mbeya ameibuka na kudai kuwa marehemu Kanumba ni Kaka yake  aliyezaliwa naye kwa Baba   lakini Mama tofauti.

‘Kanumba’ mdogo huyo ameibuka  asubuhi  ya  Januari,3,2013 katika mkutano wa waandishi wa habari na  viongozi na wanachama wa Chama cha NCCR waliofukuzwa kutoka Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA),jijini Mbeya katika ukumbi wa Baa ya Double J,Sinde.

Ilikuwa kama ‘movie’ baada ya kijana huyo mwenye uso wa upole,tabasamu kama la marehemu Kanumba alipoingia na mwandishi wa habari wa kujitegemea,Samwel Mamba,Mkazi wa wilayani Mbozi  na kutulia kama msikilizaji ama naye Mwanahabari lakini macho ya wanahabari wengi yaligonga na kutuwa katika sura yake  huku wakiwa na maswali mengi ya kujiuliza wakisubiri mkutano huo umalizike mapema na kuanza kumhoji mwandishi Samwel kulikoni kijana huyo.

Mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho Samwel huku akiwa ameshabaini kiu ya wanahabari alianza kwa kusema,”jamani nimewaletea mdogo wake kanumba…,nimemuibua kutoka katika guest ya Eden iliyopo maeneo ya uhindini jijini Mbeya ndiko anakofanyakazi.”

Aliendelea kwa kusema,” mimi sina la kuongea zaidi  ya kumsikiliza yeye asimulie historia yake maana mimi nililala katika nyumba hiyo ya kulala wageni leo(januari,3) na baada ya kumuona nilishtuka sana nilipomwita na kumuuliza alinielezea historia yake iliyonisababisha kumuombea ruhusa kwa wakubwa wake ili nije naye hapa leo nikijuwa tutakutana waandishi katika press conference hii.”

Kijana lameck hauwezi kumsingizia   kwa zile hulka za marehemu Star wa Bongo Movie Steve Kanumba ambapo alianza kusimulia historia  yake kuwa yeye ni mtoto  wa kwanza wa Mama yake Alatwingisya Ngogo na kwamba hilo jina analolitumia  la Ngogo ni la Babu yake mzaa mama yake.

Alisema Mama yake  ni mkazi wa Uwanji,Kata ya Mlondo,Wilaya ya Makete mkoani Njombe na kwamba aliwahi kuchukuliwa na Mama yake Mkubwa aliyemtaja kwa jina moja la Jane(Dada yake) na kuishi naye mkoani Shinyanga miaka 20 iliyopita ambapo  alibahatika kupata  uja uzito wa yeye(Lameck) na kutokana na Mama yake mkubwa kuchukia hali hiyo aliamua kumfukuza na kumrejesha nyumbani uwanji anapoishi hadi leo.

Lameck alisema kuwa Mama yake mkubwa huyo ambaye anaishi hadi leo mkoani Shinyanga hakumuuliza Mama yake kuwa mimba hiyo alipewa na nani zaidi ya kumrudisha nyumbani hadi alipojifungua na kuendelea na maisha hadi alipokuja kuolewa  na kuendelea kuishi  na Mume wake  hadi leo.

“Lakini nilipokuwa nikiendelea kukua na kupata ufahamu watu walikuwa wakiniambia kuwa huyo siyo Baba yangu mzazi licha ya mama kunieleza kuwa ndiyo baba yangu mzazi lakini baada ya kumdadisi sana  aliamua kunieleza kuwa ni kweli baba yangu alinikataa tangu nikiwa tumboni huko Shinyanga ambaye ni Baba yake msanii kanumba kabla hajafa,”alisema.

“Baadaye nililelewa na Bibi yangu anaitwa Nilang’ilwa na niliendelea na masomo na kuishia kidato cha pili katika shule ya Sekondari ya Mlondwe  na hivyo nikaja kwa Mjomba wangu Uyole kumsaidia kuuza viatu vya mitumba na baadaye nikatafuta kazi nikapata   katika nyumba ya kulala wageni ya Eden iliyopo Uhindini  ambako huyu Mwandishi alinikuta na kunihoji baada ya mimi kumuona amebeba mabegi ya camera na kuanza kumsimulia historia yangu hii,”alisema.

Aidha Lameck alisema aprili,mwaka 2011 alitafuta nauli na kwenda kumtafuta Baba yake  na alifikia kwa Mama yake mkubwa Jane  huku akifanyakazi katika Gereji  moja  inayoitwa kwa Remmy Shinyanga ambapo alifika katika nyumba ya baba yake na hakufanikiwa kumpata lakini alipata nambari yake ya simu  na kumpigia akijitambulisha lakini mzee huyo alimkataa katu katu kwa mara ya pili ambapo awali kwa mujibu ya maelezo ya mama yake kuwa aliikataa  mimba.

“Ninajuwa mzee anayo haki ya kukataa kwa sababu hajaniona ama hatujaenda kupima DNA kama kweli mimi ni mwanawe ama hapana,mwezi Disemba nilirudi Mbeya  ambavyo kama nilivyosimulia nilipo sasa  na   baada ya kumweleza mama alinisihi niache kumtafuta baba zaidi niangalie maisha yangu,nimekata tamaa na sasa nahangahika na maisha yangu,”alisema kwa majonzi Lameck.

Alipoulizwa  kuwa baada ya kusikia kifo cha kaka yake Kanumba  alikipokea vipi na kama aliwahi kwenda  katika msiba huo,alitikisa mabega kukataa kutokana na kukata tamaa ya kukataliwa na Baba yake,na hakuwa na nauli ya kwenda huko,lakini ameahidi kuwa ipo siku atakwenda moja kwa moja kwa baba yake akamkatae  ana kwa ana,hivyo anatafuta nauli.

Hata hivyo kijana huyo alisema yeye anakipaji cha kutunga  tamthiliya  na hadithi na kwamba aliwahi kwenda kujiunga katika kikundi kimoja cha kuigiza kilichopo pembeni kidogo mwa Jiji la Mbeya,katika mji mdogo wa Mbalizi kinachoongozwa na mtu aliyefahamika kwa jina la Mzushi lakini alikwama kutokana na kushindwa kulipa hela ya kiingilio Sh.250,000 lakini ndoto yake  amedai iko pale pale  ya kurithi  kipaji cha kaka yake  The Great Kanumba.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment