Tume ya Haki na Amani ya
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania:
TAMKO
Mkutano wa kitaifa wa wajumbe wa kamati za majimbo za Haki na Amani za Kanisa Katoliki Tanzania pamoja na Wanataaluma Wakristo wa Tanzania (CPT), walikutana kwenye Kituo cha kiroho cha Mbagala, Jijini Dar es Salaam, tarehe 5 – 6 Februari, 2014.
Wakitafakari juu ya mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wajibu wa Kanisa Katoliki katika Utume wake wa Kinabii wa kulinda na kujenga haki na amani nchini mwetu, walimshukuru Mungu kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya uwenyekiti wa Jaji Joseph Sinde Warioba, kufanikiwa kuwasilisha rasmi Rasimu Na. 2 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 30 Desemba, 2013 na kuashiria mwanzo wa hatua ifuatayo ya kuunda Bunge Maalumu la Katiba.
Baada ya kuipitia Rasimu hiyo kwa kuongozwa na uchambuzi makini uliowasilishwa na Sekretarieti ya Tume ya Haki na Amani wajumbe wameridhia kwamba :
Kwa hakika Rasimu iliyowasilishwa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni ya watu na sio ya wanasiasa au vyama vya
siasa wala asasi za kidini. Kwa sababu hiyo tunatoa mwaliko kwa kila raia wa Tanzania
kufurahia ushiriki wake kufikia Rasimu Na. 2 yenye mambo bora yatakayokuwa
nguzo ya umoja wa nchi yetu katika Katiba Mpya.
Maadili yaliyomo katika Rasimu Na.
2 ni muhimu kabisa kwa taifa letu.
Wananchi na viongozi wote sharti wajali maslahi kwa wote na wasimamie haki na wajibu wa kila mtu.
Wananchi na viongozi wote sharti wajali maslahi kwa wote na wasimamie haki na wajibu wa kila mtu.
Madhumuni ya msingi ya Katiba ni
ustawi wa kila Mtanzania, haki za kiuchumi, usalama, kusikilizwa kabla ya
kuhukumiwa na haki kwa wote pasipo ubaguzi kwa madhumuni ya kulinda amani.
Katiba yetu lazima isiruhusu
wachache wenye nguvu za kisiasa, kiuchumi na kiutawala kutumia vibaya uwezo wao
na kusababisha utengano kitabaka katika jamii huku wakijinufaisha kwa kutumia
rasilimali za nchi zilizo za wote. Pawepo na udhibiti thabiti wa mienendo ya
namna hiyo na uwajibishaji makini kwa wabadhilifu wa mali ya umma.
Katiba ni chombo hai kwa ajili ya
kuhudumia jamii na sio jamii kuhudumia Katiba. Kwa sababu hiyo yatupasa
kuthubutu kubuni njia mbadala ili kukuza kipato cha raia wa kawaida na kuboresha
huduma za jamii kwa kuwa na mipango endelevu ya kiuchumi.
Pendekezo la Muundo wa Muungano wa
serikali tatu sio jambo kuu kuliko mengine yote katika Rasimu hii. Muundo wa
serikali mbili haukutatua matatizo msingi bali ulilimbikiza kero zilizosababisha
Zanzibar kujiundia katiba yake mpya ya mwaka
2010 bila kushauriana na Tanzania Bara (Tanganyika). Pendekezo la serikali
tatu lililowekewa mazingira tekelezi yakitoa mwanya wa kuboresha muundo huo kwa
njia wazi, shirikishi na za kidemokrasi lina tija kubwa ya kuturudishia hali ya
kuwa wamoja.
Mihimili mikuu mitatu; Serikali ya
Jamhuri ya Muungano, Bunge la Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Jamhuri ya
Muungano ni taasisi mpya kabisa kwa mujibu wa Rasimu Na. 2 zitakazoongoza,
kuratibu na kuwajibisha kila kiungo cha Jamhuri ya Muungano zikiwemo serikali
za Nchi Washirika.
Haki ya mtu ya kuishi lazima
ilindwe na Katiba kuanzia pale mimba ya binadamu inapo tungwa katika mama na
katika hatua zake zote za kumhudumia mama mjamzito.
Kumtambua Mungu na kumtaja katika
Katiba yetu kunamaanisha kukiri kwetu Uwepo Wake aliye Muumba wetu na vitu
vyote ambavyo mwanadamu anavitegemea kwa uhai wake. Mungu anakuwa rejelea yetu
katika kuheshimiana kiutu. Ni chimbuko la utu wa binadamu. Kwa kuwa katika
Wimbo wetu wa Taifa tunamwomba Mungu baraka zake ili tufanikiwe na tuishi kwa
amani, ni hekima na busara kumkiri katika Sheria Mama – Katiba.
Tunapoelekea kwenye Bunge Maalum la Katiba tunataka mambo yafuatayo ya msingi kabisa yatambuliwe na kufahamika kwa wote:
Watanganyika na Wazanzibar tuwe na
nia madhubuti ya kuwa wamoja.
Haki za binadamu za kisiasa,
kiuchumi na kijamii zipatikane na kufurahiwa na wote. Umasikini na ufinyu wa
bajeti ya serikali ni visingizio tu vya mamlaka kutokutoa haki kwa wote.
Yatupasa kukiri mapungufu yetu
katika serikali zetu na itikadi za kisiasa kusudi kwa moyo wa unyenyekevu na
mkunjufu tuanze safari mpya katika mwanga mpya wa maridhiano. Pamoja na kukiri
kasoro za wakati uliopita tujivunie maendeleo tuliyofanya katika kila nyanja za
maisha wakati tukiboresha mifumo na miundo ya utawala.
Ulimwenguni hakuna katiba yoyote
kamilifu. Yatupasa tuanze na Rasimu iliyopendekezwa na tuendelee kuiboresha
pale itakapobidi.
Tunawasihi wajumbe wa Bunge Maalum
la Katiba kuweka kando itikadi za vyama vyao kama
walivyofanya Wanatume wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika kuandaa Rasimu Na.
2. Bunge Maalum la Katiba lilenge kufanikisha mchakato mwema wa Katiba Mpya
itakayoandaa njia na mifumo mipya ambayo kwayo tutahakikishiwa kuwepo kwa
taratibu wajibishi na wajibikaji ili kuendeleza ustawi wa jamii na muundo wa
Muungano utakaokuwa wazi na tayari wakati wote kuboreshwa kwa manufaa ya
Watanzania wote.
Katiba Mpya ya Tanzania itakuwa na fursa ya
“FURAHA MPYA SHIRIKISHI” kwa Watanzania wengi. Rasimu na. 2 ni hatua njema
katika tukio muhimu la kihistoria nchini tanzania. Tunatarajia bunge maalum
lisimkane Mungu na lisikashifu mapendekezo ya serikali tatu.
Tunawaalika wananchi wote wa Tanzania kwa dhamira moja, kuliombea na kulisaidia Bunge Maalum la Katiba, liweze kufanya kazi yake kwa ustadi na kujali maslahi ya Taifa na wananchi wote wa Tanzania.
Askofu Mkuu Paulo Ruzoka
MWENYEKITI
Tume ya Haki na Amani - TEC
No comments:
Post a Comment