LICHA
ya kuwa na utajiri mkubwa wa madini ya Dhahabu katika Wilaya ya Chunya Mkoani
Mbeya, bado wananchi na wakazi wa wilaya hiyo wanaendelea kuteseka kwa ukosefu
wa maji safi na
salama.
Tatizo la maji limeshindwa kupatiwa
ufumbuzi katika Wilaya hiyo kwa muda mrefu sasa ambapo wadau mbali mbali
wameshauri Serikali kufanya kama ilivyofanya Mkoani Shinyanga kuchukua maji
Ziwa Victoria
kilomita zaidi ya 700.
Wamesema Wilaya ya Chunya ina Ziwa Rukwa
ambalo lingeweza kusaidia kujenga mradi wa maji na kuwaondolea adha wananchi wa
Chunya ziwa ambalo liko umbali usiozidi kilomita 50 hivyo kupunguza gharama kama zilizotokea Mkoani Shinyanga.
Ushauri huo ulitolewa jana na Katibu
Mwenezi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Lukasi Mwampiki,
alipokuwa akihutubia wananchi wa Kijiji cha Saza Wilayani Chunya katika ziara
ya kuimarishja chama inayoendelea Wilayani humo.
Alisema katika kijiji cha Saza ambacho kwa
miaka hamsini tangu uhuru hawajawahi kupata huduma za maji safi na salama licha ya
kuwepo kwa mgodi mkubwa wa madini ya dhahabu inayochimbwa na wawekezaji wa nje.
Alisema kukosekana kwa Maji katika Wilaya
hiyo ni aibu kubwa na inaonesha dhahiri Mwekezaji kutowajali wananchi ambapo
pia hawanufaiki na uchimbaji huo ambao umeshindwa kuwatatulia tatizo sugu la
maji linalowakabili wananchi hao kwa muda mrefu.
Mwampiki alisema Serikali inaweza ikatumia
njia rahisi kama ilivyofanyika Mkoani
Shinyanga ambako tatizo la maji limetatutiliwa kwa kuchukuliwa maji katika Ziwa
Viktoria lililo umbali wa zaidi ya Kilomita 700 ili hali ziwa Rukwa likiwa
jirani kabisa na Wakazi wa Chunya ambao wanaweza kusahau kabisa shida ya maji.
Alisema maji ya Ziwa Rukwa yakichukuliwa
yataondoa gharama na adha wanayoipata Wananchi kwa kusafiri umbali mrefu
kutafuta maji huku wakishindwa kufanya shughuli zingine za maendeleo hususani
wanafunzi ambao hushindwa kuhudhuria masomo ambapo bado maji yanayopatikana
kutofaa kwa matumizi ya binadamu.
Aliongeza kuwa wananchi walitakiwa
kushirikishwa kabla ya mwekezaji hajaanza uchimbaji wa madini ili apewe
vipaumbele vitakavyo wanufaisha moja kwa moja likiwemo tatizo sugu la maji
ambalo alitakiwa alitatue kabla ya kazi yoyote.
Aidha katika hatua nyingine Mwampiki
aliwashauri wananchi wa Kijiji cha Saza kuwahoji Madiwani wao kuhusu hati chafu
zinazotolewa na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali(CAG) kwa Halmashauri na wao
kuziangali tu na kukosesha sifa Halmashauri kwa matumizi mabaya ya fedha za
wananchi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment