Na Thompson Mpanji,Mbeya
MTANDAO wa jinsia Tanzania(TGNP) kwa kushirikiana na wanaharakati na wadau mbalimbali wanatarajia kushiriki Tamasha mapema septemba,3,2013 ambapo litatoa nafasi na fursa kwa wanaharakati zaidi ya 5,000 kushiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Tukio hili la siku nne,linajumuisha uchambuzi,utafiti,uanaharakati,kujenga uwezo,sanaa vyote vikiwa na matokeo dhahiri ili kutoa ama kuonesha ushuhuda wa yale yanayojiri miongoni mwetu.
Malengo ya tamasha la jinsia 2013 ni kusherehekea miaka ishirini ya harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi inayochangia upatikanaji wa haki za wanawake,usawa wa kijinsia na haki za kijamii.
Kuongeza uelewa wa muktadha uliopo kimataifa,wa mfumo dume na uliberali mamboleo,madhara yake kwa wanawake walioko pembezoni na jamii zao,mapambano yao dhidi ya mifumo chanya na mingine kandamizi,na mikakati mbadala kwa ajili ya ukuaji na maendelo endelevu yenye usawa na haki.
Aidha kuendeleza uelewa wa nadharia na vitendo kwenye ukombozi wa wanawake kimapinduzi,ikiwa ni pamoja na kutunza kumbukumbu za mapambano halisi dhidi ya mfumo dume na uliberali mamboleo,na jinsi ya kuimarisha ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika ngazi zote.
Tunasema hongera TGNP,wadau na wanaharakati wengine kuazimisha Tamasha hilo ambalo ninaamini litawapatia mwelekeo wenu katika harakati hizi za kumkomboa binadamu na hasa mwanamke.
Ninaweza kusema kuwa Tamasha hilo litasaidia kufanya ufuatiliaji na tathmini kuhusu mlikotoka,mlipo na mnapoelekea katika harakati hizi ngumu ambazo kwa wakati mwingine zinahatarisha maisha na hivyo kuhitaji moyo wa kujitolea na kujituma zaidi kutoka ndani ya sakafu ya moyo,ndani ya mishipa na damu kwa ujumla.
Tunaamni kuwa tamasha hilo pia litawaweka pamoja na kupanga mikakati na mipango kazi itakayotekelezeka katika ngazi zote kwa ajili ya ujenzi wa harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi nchini Tanzania,Afrika na dunia kwa ujumla.
Tamasha hili litasaidia kuimarisha utambuzi,mitandao,ujenzi wa nguvu za pamoja na miungano ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi kama misingi ya kuelekea tapo la ukombozi wa wanawake kimapinduzi wa Afrika.
Tunaambiwa kuwa katika Tamasha hilo kutakuwa na Mada mbalimbali kama vile jinsia Demokrasia na maendeleo,miaka 20 ya harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi,haki na usawa wa kijinsia,tuko wapi na tunakwenda wapi,Mapambano ya haki ya ardhi na uchumi,rudisha rasilimali kwa wananchi,mapambano ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi kwa ajili ya Demokrasia kwenye vyombo vya kiserikali na visivyo vya kiserikali.
Mada nyingine ni pamoja na mabadiliko ya katiba au mapinduzi,Mapambano ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi na ujenzi wa tapo miaka ishirini ijayo sanjari na ujenzi wa umoja wa Afrika kwa mtazamo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi.
Kabla ya kuendelea tuangalie hili Shirika la TGNP linatoka wapi na linafanya nini katika jamii,ni miongoni mwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya jitihada mbalimbali katika kuhakikisha tatizo hili linakomeshwa kabisa na kutoweka katika jamii ya kitanzania na dunia kwa ujumla.
Ni shirika la kiraia na kiuharakati,linalotetea mabadiliko ya kijamii kwa mtazamo wa kifeministi ambayo yanalenga kwenye usawa wa jinsia,ukombozi wa wanawake,haki za kijamii,kufikia na kumiliki rasilimali kwa wanawake,vijana na makundi mengine yaliyoko pembezoni.
Dhana ya TGNP ni kujenga tapo la mabadiliko katika jamii,ambalo litachangia kuwepo kwa jamii yenye mabadiliko ambayo inatambua na kuthamini masuala ya jinsia,demokrasia,haki za binadamu na haki za kijamii.
Kwa mujibu wa Ofisa uhusiano wa TGNP Kenny Ngomuo anasema septemba,3,2013 ni Tamasha la jinsia ambalo huandaliwa na mtandao wa jinsia Tanzania(TGNP) wakishirikiana na mtandao wa mashirika watetezi wa haki za binadamu na usawa wa jinsia (FemAct),pamoja na washirika wao wengine kama mitandao ya jinsia ngazi ya kati ( IGNs),zilizopo katika ngazi za wilaya,makundi mbalimbali ya kijamii ambayo ni sehemu ya semina za jinsia na maendeleo (GDSS) za TGNP, na vikundi vingine ambavyo vimetambuliwa katika utafiti kuhusu harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi (TFMB).
Ngomuo ansaema Tamasha la jinsia ni nafasi ya wazi kwa ajili ya watu binafsi,mashirika na mitandao,walio katika mapambano yanayofanana,kubadilishana uzoefu,taarifa,kujengeana uwezo,kusherehekea mafanikio na kutathmini changamoto zilizo mbele yao,kujenga na kuimarisha mitandao,na kupanga kwa pamoja mikakati kwa ajili ya kuleta mabadiliki ya kijamii kwa mtazamo wa kifeministi,kujengeana uwezo ili kuchangia katika mijadala ya wazi kuhusu maendeleo ya jamii na binafsi.
Ofisa huyo anasema Lengo kuu la tamasha ni kuwaleta pamoja wanawake/wanaharakati wa kifeministi na wengineo,ambao wanawamini kwenye usawa wa jinsia na ukombozi wa wanawake ,kutoka Nyanja zote za maisha ,kutoka vijiji na wilaya za Tanzania,na sehemu mbalimbali duniani,kwa lengo la uanaharakati na ushirikishanaji wa taarifa kwa masuala mahsusi.
Anasema taswira ya TGNP inafanya jitihada za kuwezesha ukuaji wa vuguvugu la ukombozi wa mwanamke kimapinduzi lenye misingi yake katika jamii hivyo kupelekea kufanyakazi moja kwa moja na wanaharakati katika makundi ya kijamii,wanamtandao na makundi ya muungano katika ngazi mbalimbali.
Ngomuo anasema mkazo mkubwa unawekwa katika kukuza uwezo wa hayo makundi na mitandao ili yaweze kufanya uchambuzi wa kijinsia na ujenzi wa nguvu ya pamoja katika kutekeleza mipango yenye kuleta mabadiliko ndani ya jamii zao na kujenga mahusiano na wengine katika ngazi ya jamii ya taifa,kikanda na kimataifa.
Anafafanua zaidi kuwa dhima ya TGNP ni kuwa chachu katika ujenzi wa harakati za vuguvugu la ukombozi wa mwanamke kimapinduzi unaolenga kubomoa mfumo dume na mifumo mingine kandamizi ikiwepo ukoloni mamboleo,ubeberu na ubepari ngazi zote,kutetea,kushawishi na kushinikiza uwepo wa usawa wa jinsia,ukombozi wa mwanamke kimapinduzi,haki ya kijamii.
Aidha Ngomuo anabainisha Dira yao ni kuwepo kwa jamii ya Tanzania inayoheshimu usawa wa jinsia na haki ya kijamii,kusimamia haki za jamii.
Hata hivyo anahitimisha kwa kuelezea mafanikio kwa miaka 20 tangu TGNP ianzishwe ni kuwa imefanikiwa kushawishi sera za umma kuingiza masuala ya harakati za vuguvugu la ukombozi wa mwanamke kimapinduzi,ikiwepo kuingiza masuala ya usawa wa kijinsia na haki za kijamii kwenye mifumo na taasisi ikiwemo na kukuza hamasa na uelewa wa wanachama,washiriki na serikali,kila lakheri TGNP na wadau wengine katika Tamasha hilo ambalo litaongeza kasi,ari na nguvu ya kufanyakazi zaidi!!.
tmpanji@yahoo.com
www.mpanjimwanamai.blogspot.com
0765 813180
No comments:
Post a Comment