Translate

Monday, August 30, 2010

Thompson Mpanji


7 comments:

  1. Na Thompson Mpanji,Mbeya

    RAIS wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania(TUCTA),Omari Ayub, amewataka wafanyakazi nchini kuhudhuria katika mikutano mbalimbali ya kampeni ya viongozi wa vyama vya siasa na kuwapima kutokana na hoja zao badala ya kujiingiza moja kwa moja katika masuala ya siasa jambo ambalo linaweza kuchangia uvunjifu wa amani.

    Kauli hiyo imetolewa na Rais huyo mwishoni mwa wiki,wakati akifunga mafunzo ya sheria za kazi kwa wajumbe 38 kutoka taasisi za serikali,mashirika yasiyo ya kiserikali,binafsi na dini kutoka Tanzania bara na visiwani yaliyofanyika katika chuo cha wafanyakazi Ottu,mkoani Mbeya.

    Ayub alisema kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi kuwa Tucta itampa kura kiongozi anayehitaji kura za wafanyakazi na aliyekataa hawatampa ni ya mtu binafsi na siyo tamko la shirikisho.

    "Hakuna kiongozi anayekataa kura za wafanyakazi na tucta haijatoa tamko lolote kwani bado tunaendelea na mchakato wa kudai maslahi yetu na ninawaomba wafanyakazi washiriki katika mikutano ya kampeni na wawapime viongozi wa siasa kwa sera zao,sijamsikia kiongozi anayesema hazitaki kura za wafanyakazi,"alisema.

    Kuhusu suala la rushwa Rais huyo alisema kuwa nyongeza ya mishahara iliyotolewa na serikali kwa wafanyakazi siyo rushwa bali ni sehemu ya utekelezaji wa mazungumzo yaliyoanza mapema na bado yanaendelea kutokana na kiwango hicho kutokidhi matakwa yao.

    Hata hivyo Ayub amewataka wanachama na viongozi wa vyama vya wafanyakazi na Tucta kwa ujumla kutojihusisha na kujiingiza katika masuala ya kisiasa na kwamba hawawezi kufungamana na chama chochote zaidi ya kufuatilia mchakato mzima wa kampeni na kumchagua kiongozi bora,mcha mungu,mwenye uzalendo wa kweli na nchi yake.

    Mwisho.

    ReplyDelete
  2. Na Thompson Mpanji,Mbeya



    BAADHI ya wananchi na wadau wa masuala ya kisiasa mkoani Mbeya wamepinga vikali matokeo ya utafiti uliotelewa Taasisi ya utafiti ya Synovet na mpango wa utafiti na elimu ya Demokrasia (Redet) kuwa ni usanii wa kisiasa unaolenga kuwaadaa watanzania kupokea matokeo ya uongo kama walivyozoea.



    Aidha katika kipindi cha kujadili mada kinachoandaliwa na kurushwa na kituo cha radio cha Mbeya Fm,jijini hapa hakuna mwananchi aliyejitokeza kudai kuhojiwa na Synovet ama Redet ingawa tafiti hizo zinadaiwa kufanywa katika baadhi ya mikoa ukiwemo wa Mbeya.



    Katika kipindi cha jambo Tanzania kinachoandaliwa na kurushwa na shirika la utangazaji la taifa,TBC,Meneja Mkazi wa Taasisi hiyo Hurio alisema kwa mujibu wa taratibu za utafiti za kimataifa ,kunatakiwa na sampuli 110 za kada zote lakini wao wamefanikiwa kufikia kada 3000 .



    Vyombo mbalimbali vya habari nchini vimesikika kuripoti taarifa za utafiti wa Synovet kuelekea katika uchaguzi mkuu kuwa endapo uchaguzi ungefanyika muda huu katika nafasi ya Mgombea urais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania,Jakaya Kikwete angepanda asilimia 61 ya kura Tanzania kupitia CCM, Dk.Willbroad Slaa asilimia 16 na Prof.Ibrahimu Lipumba wa Cuf asilimia 5 na ambao hawaelewi ni asilimia 13.



    Awali Mpango wa utafiti na elimu ya kidemokrasia nao wal ambapo asilimia ulitoa matokeo yake ya uchaguzi katika nafasi hiyo kuwa Kikwete angejinyakulia asilimia 71.2,Dk.Slaa.12.3 na Prof.Lipumba 10.3.



    Kufuatia taarifa hizo wadau na wanaharakati mbalimbali wa masuala ya siasa wakiwemo wananchi walio wengi wamehoji njia iliyotumika kupata takwimu hizo na kuona kuwa taasisi hizo ambazo zipo karibu na serikali iliyopo madarakani zinatumika vibaya kuwaweka watawala waliopo madarakani waendelee kutawala kwa maslahi yao.



    Mwenyekiti wa shirikisho la vyama 10 vya siasa mkoani Mbeya,Godfray Davis,alisema lengo lingine ni kijaribu kuwaadaa wafadhiri nje ya Nchi kuwa hata Asasi zisizo za kiserikali zimefanya utafiti wakati ni kiini macho cha CCM.



    God ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha APPT maendeleo alisema ili kudhihirisha kuwa Taasisi ni za ubabaishaji hazioneshi vigezo vya watu waliowahoji,ukumbi na uthibitisho wa kada walizozihoji.



    “Wewe mwenyewe umesikia katika Radio Mbeya watangazaji waliuliza kama kuna mwanambeya yeyote aliyewahi kuhojiwa na mojawapo wa taasisi hizo za utafiti apige simu kuelezea hakuna hata mmoja hata wanahabari,tafiti kama hizi za kitaifa lazima kada zote zihojiwe kunzia za juu hadi chini,wasemaji wa makundi na taasisi za dini,”alisema God.



    Aliyekuwa mgombea wa Ubunge Jimbo la Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuanguka katika mchakato wa kura za maoni,Eugen Kisonga alisema utafiti huo hauna sababu ya kubezwa kwani ndiyo ukweli halisi kuelekea katika uchaguzi mkuu oktoba,31 kinachotakiwa ni kukubaliana na matokeo hayo labda kujaribu kuweka jitihada ya kuzifikia asilimia hizo jambo alilodai haliwezekani.



    Hata hivyo baadhi ya viongozi wa dini waliohojiwa na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema taasisi hizo zinatumika kwa kufuata msemo wa mtumikie kafiri upate mradi wako kwani ni vigumu kwa wahusika wa Redet na Synovet kumwelezea vibaya Mwajiri wao mkuu.





    Mwisho.

    ReplyDelete
  3. Na Thompson Mpanji,Mbozi.

    WANANCHI wa Kijiji cha Chilulumo,Wilayani Mbozi wameulalamikia uongozi wa serikali ya Kijiji hicho kufanya ubadhilifu na kula fedha za michango ya ujenzi wa sekondari zaidi ya Sh.Mil.4.7 ambapo kila mwananchi alichangia kiasi cha Sh.10,000.

    Madai hayo yametolewa na wananchi kupitia barua ya sept,14 iliyoandikwa na wananchi hao kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi na nakala katika Ofisi ya tume ya haki za binadamu taifa na gazeti hili kupata nakala, ikiwa imeambatanishwa na mkataba uliotiwa saini na viongozi wa Kijiji hicho kukiri kufuja fedha hizo kuahidi tarehe ya kuzilipa ambapo hadi sasa hawajatekeleza ahadi hiyo.

    Mwenyekiti wa Tume ya haki za Binadamu ,Said alisema ameipokea barua hiyo yenye kichwa cha habari Matumizi yasiyo sahihi ya mchango na ujenzi wa shule ya Sekondari ya Chilulumo na kwamba katika hali ya kushangaza ujenzi ulianza bila kuwa na kamati ya ujenzi badala yake uliendeshwa na ofisa mtendaji wa Kata.

    “Jambo la kushangaza ujenzi huo ulikuwa ukisimamiwa na mtendaji wa kata pekee bila kamati na pesa alikuwa akipokea yeye na kutunza nyumbani kwake kwa kushirikiana na mtendaji wa Kijiji na Mwenyekiti wa Kijiji,sisi tulichanga zaidi ya Sh.Mil.4.7 lakini matumizi yake hayaeleweki ,”ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

    Imesema mwananchi anapojaribu kuhoji kuhusu fedha hizo anawekwa mahabusu na kutolea mfano wa mwananchi mmoja aliyetajwa kwa jina la Daniel Julius Sinkala hali ambayo imeendelea kuwatia hofu na kupoteza imani na viongozi wao.

    “Kwa vile pesa hizi zina utata tunaahidi kuzifuatilia na kuzirejesha na kwamba tarehe ya mwisho kurejesha fedha hizo ni 10/10/2010,ilisema sehemu ya barua ya mkataba waliowekeana saini 26/9/2010
    ikiwa na mhuri wa Ofisi ya Kijiji na nakala kusambazwa katika ofisi mbalimbali.

    Mtendaji wa Kata,William alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusina na tuhuma hizo alikanusha na kudai wanaohusika na shughuli hiyo ni Viongozi wa kijiji cha chilulumo ambao ni Mtendaji wa Kijiji hivyo mwandishi anapaswa kuwahoji watu hao.

    William alisema katika Kata ya Chilulumo kuna vijiji tisa ambapo malengo ya makusanyo katika miradi mitatu ambayo ni ujenzi wa sekondari ya Chilulumo,ujenzi wa Hosteli ya Mkulwe na ujenzi wa nyumba ya mwalimu mkuu na kwamba kutokana na shule mpya ya sekondari ya Chilulumo kutopewa fedha kutoka serikalini, yeye kama mtendaji wa Kata aliamua kuchukuwa kiasi cha Sh.Mil.8 zilizochangwa na kuigawia sekondari ya Chilulumo mifuko 120 ya saruji,mafundi sh.mil.1.5,nondo 10 kwa sh.220,000,mbao sh.mil.3,misumari Sh..350,000,mchanga sh.800,000 na mawe sh.420,000.

    Alisema alishaunda kamati ya miradi mitatu na kwamba katika kikao cha maendeleo ya kata (WDC) kilichofanyika aprili,9 mwaka huu wakati wa kusomewa taarifa ya mapato na matumizi kiliridhia kuwa matumizi yalikwenda vizuri na kumbukumbu anazo na kwamba Kijiji cha chilulumo kilichanga kiasi cha Sh.Mil.3.7 ambazo wananchi wanahitaji kujuwa fedha zao.

    Mkuu wa Wilaya ya Mbozi,Gabriel Kimoro akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari alisema baada ya kupokea barua kutoka kwa wananchi alimtuma Ofisa elimu taaluma wa Sekondari wa Wilaya ya Mbozi ambapo alimuwasilishia taarifa ya kulimaliza suala hilo.

    Pamoja na taarifa hiyo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi lakini bado wananchi wa Kijiji cha Chilulumo wamedai suala hilo alijamalizika kwani hadi sasa hawajuwi matumizi ya fedha zao yalivyokwenda hali ambayo imewavunja nguvu ya kuendelea kuchangia maendeleo mbalimbali yatakayojitokeza.

    Mwisho.

    ReplyDelete
  4. Na Thompson Mpanji,Mbeya

    WANANCHI wa Kitongoji cha Igawa,Kijiji cha Chapwa,katika Mji mdogo wa Tunduma,wilayani Mbozi wamesema kuna uwezekano mkubwa wa kukosa maji ya kunywa kutokana na madai ya kuuzwa eneo la hifadhi ya vyanzo vya maji kwa mfanyabishara mmoja kwa kiasi cha zaidi ya Sh.Mil.2.

    Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baadhi ya wananchi wa kitongji hicho wamesema kuwa hifadhi hiyo ya maji imeuzwa mwaka 2009 na Mwenyekiti wa kitongoji hicho,Boytone Simbeye kwa mfanyabishara waliyemtaja kwa jina moja la Toronto na kwamba walibaini kuwa eneo hilo limeshauzwa tangu mwaka 2009 baada ya kuliona trekta likiingia kusawazisha eneo hilo julai,11 mwaka huu na kuanza kujenga msingi wa nyumba.

    Aidha walidai baada ya kumhoji mfanyabiashara huyo alisema ameuziwa na serikali ya eneo hilo hali iliyowafanya waanze mchakato wa kufuatilia haki yao hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi ambaye aliwaelekeza wafike ofisi ya mipango miji ili kuhakikisha kama eneo hilo la hifadhi lenye kisima kinachodaiwa kuwepo tangu miaka ya 1940 kama lipo katiika ramani.

    Mwenyekiti wa tume ya haki ya binadamu taifa,Said Madudu alisema wananchi hao walifika kulalamika katika Ofisi yake na hivyo anaendelea na jitihada za kufuatilia kubaini ukweli ili wananchi waweze kutendewa haki ikiwemo ya kutunza vyanzo vya maji na kupata maji safi yaliyo salama.

    Mfanyabishara anayedaiwa kununua eneo hilo,Manase Mselema maarufu kwa jina la Toronto alipozungumza na jambo leo kwa njia ya simu alisema eneo hilo amelinunua kihalali tangu sept.1994 kwa gharama kubwa ingawa hakuwa tayari kuweka bayana na kwamba halipo karibu na chanzo cha maji kama inavyodaiwa.

    “Ni uzushi kuwa eneo langu lipo katika chanzo cha maji niligawiwa na ofisi ya ardhi kihalali,lipo mbali sana na chanzo na lipo katika eneo walilojenga watu wengine na katika eneo langu watu walishapewa fidia,lakini kutokana na chuki za mtu mmoja walishafikisha majungu hadi kwa maofisa usalama,takukuru na viongozi wakubwa,lakini eneo hili siwezi kuliacha nimetumia gharama kubwa sana”alisema.

    Mwenyekiti wa kitongoji cha Igawa,Simbeye ambaye anadaiwa kujihudhuru kufuatia sakata hilo alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi alisema hawezi kuzungumza juu juu bali atafutwe ili naye aweze kuzungumnza ukweli badala ya kuandika habari za upande mmoja.


    Hata hivyo kuna taarifa kisima hicho na kwamba michoro ilishafanyika ilikuwa bado kupitishwa kwani bado eneo hilo lipo katika utafiti uliofanywa kuanzia mwaka 2008,ni mojawapoo ya eneo lililopimwa na kuna visima viwili na kama mamlaka ya maji ya mdogo yanasubiriwa majibu ya andiko mradi kwa watu walioshinda tenda.

    Mkurugenzi wa mamlaka ya Mji mdogo wa Tunduma (TEO) aliyejitambulisha kwa jina la Aidan Mwasiga alisema hakuna kitu kama hicho na kwamba hawezi kugawa eneo muhimu kama hilo labda kama kuna mtu anatumia jina la Ofisi watafuatilia kujuwa uweli ulivyo,"nipo nje kikazi wasiliana na mtu niliyemwachia ofisi anaitwa Mwaselele ili kujuwa hatua gani zimechukuliwa kufuatia malalamiko hayo ila nakumbuka kama limekwenda kwa mkuu wa wilaya ya Mbozi kwa hatua zaidi.

    Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Gabriel Kimoro akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema suala hilo halijamfikia mezani kwake,”hilo bado halijafika kwangu ila limewahi kufika suala la kutoka katika kijiji hicho hicho kulalamikiwa mamlaka ya mji mdogo wa Tunduma kuuza mashamba nililimaliza kwani lilikuwa ni suala la serikali na siyo Mji mdogo kama walivyodai.”

    Mwisho.

    ReplyDelete
  5. Na Thompson Mpanji,Mbeya

    KLABU ya mchezo wa darts ya Polisi mkoani hapa imesema imejiandaa vyema kuchukua ubingwa katika michuano ya taifa ya mchezo huo yanayotarajia kutimua vumbi Novemba,mwaka huu katika viwanja vya Nuru Park Hoteli,,ambapo Mkoa wa Mbeya utakuwa mwenyeji wa mashindano hayo.

    Katibu wa Klabu hiyo,Adelade Chikoma maarufu kwa jina la mchezo huo AD amesema Mkoa wa Mbeya umepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa kuandaa mashindano hayo hivyo katika kuweka mikakati madhubuti wameandaa hafla fupi ya kukaa na kuzungumza na viongozi wa ngazi ya Mkoa,Wilaya na Jiji ili kuweka mambo sawa.

    Chikoma amesema katika hafla hiyo inayotarajia kufanyika oktoba,16,kuanzia majira ya saa 10.00 jioni katika ukumbi wa klabu hiyo Polisi kati jijini hapa,wamemualika Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya,Advocaty Nyombi kuwa mgeni rasmi pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya,Evance Balama,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Ofisa utamaduni na michezo wa jiji na wageni wengine.

    Amesema lengo la kuwaalika Viongozi hao ni kuwapa taarifa ya heshima waliyopewa kitaifa kuandaa mashindano hayo yaliyopangwa kufanyika Novemba,19 hadi 22 mwaka huu,kuwaelezea mikakati yao sanjari na kupata mawazo tofauti kutoka kwao kwa lengo la kuhakikisha Mbeya Polisi Darts Club inabaki na ushindi wa kishindo na hivyo kuuletea sifa Mkoa wa Mbeya.

    Katibu huyo amesema Klabu hiyo imepata mafanikio makubwa kupitia wachezaji wake ambapo tayari wameshaleta vikombe na medali za fedha na shaba katika mashindano ya kimataifa ya kusini mwa Afrika ambapo katika mashindano ya mwaka 2007 mchezaji wa kimataifa Adelade alijinyakulia medali mbili za fedha ambapo katika mwaka 2009 nchini malawi mchezaji huyo alijinyakulia medali moja ya shaba pamoja na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa kimataifa kwa mwaka huo.

    Mwisho.

    ReplyDelete
  6. Na Thompson Mpanji,Mbeya

    MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Mbeya Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA),Joseph Mbilinyi (Mr.Sugu) mwishoni mwa wiki iliyopita alikonga nyoyo za wapenzi,wanachama na washabiki wake kwa kujinadi kwa mistari kuwa hata Chama cha mapinduzi (CCM) wanamjua kuwa ni sugu na lazima CCM wakae chini (washindwe Mbeya mjini).

    Burudani hiyo ilitokea katika mji mdogo wa Mbalizi ambako ndiko kunadaiwa kuwa kuna kambi kubwa ya Chadema wakati wa kumsubiri mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema,Dk.Willbroad Slaa aalipokuwa akitokea kijiji cha Ilembo,wilaya ya Mbeya vijijini ambapo wananchi walisikika wakipiga kelele ya kumuomba Mr.Sugu awaimbie.

    “Nipo katika mchakato wa siasa ili niende kule kule (bungeni), sijaja na CD hapa nina ilani ya Chadema tu jamani lakini ngoja niwape mistari kavu kavu,” Mimi naitwa sugu na wananiita sugu hata vigogo wa CCM wananijuwa nipo juu, CCM lazima ikae mwaka huu hapa sugu hapa Shitambala (Mgombea Ubunge Mbeya Vijiji Chadema),”aliimba huku wananchi wakijibu na kushangilia.

    Mr.Sugu ambaye ni mwanamuzi wa kizazi kipya ambaye amejizolea wapenzi na mashabiki wengi jijini Mbeya alisema katika awamu hii ya uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba,31 mwaka huu,CCM lazima ing’oke katika majimbo yaliyopo ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya.

    Mwisho.

    ReplyDelete
  7. Na Thompson Mpanji,Mbeya



    KIJANA mdogo aliyeibuka na kuanza kutoa huduma ya tiba kwa kutumia kikombe kama alivyokuwa Babu wa Kijiji cha Samunge,Wilaya ya Loliondo,Mch.Ambilikile Mwasapila ameishukuru serikali kwa kumruhusu kuendelea kutoa huduma kwa jamii lakini mizimu yake imekataa kufanya huduma hiyo nje ya nyumbani kwao kwani dawa hiyo haitafanyakazi.



    Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi,kijana Jafari Werna au Fikiri (17) maarufu ‘Babu mtoto wa mabatini,’alisema baada ya kuitwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Bw.John Mwakipesile ofisini kwake alimweleza kuwa yeye ni kijana mdogo hivyo hapaswi kufanya shughuli ya uganga wa jadi hadi atimize umri wa miaka 18 na zaidi.



    Alisema baada ya kujieleza kuwa shughuli hizo alianza akiwa na umri mdogo kwani alikuwa amerithishwa na Bibi yake hivyo alitakiwa kukata kibali ambacho alilipiwa kiasi cha sh.55,000 baada ya viongozi wake wa mashina (mabalozi) na serikali ya Mtaa wa Mianzini anapoishi kufanya mchango huo.



    “Sasa naendelea kutoa huduma na wakaribisha waje wahitaji kutoka maeneo mbalimbali nje na ndani ya mikoa,nawaambia hasa wagonjwa na wenye shida mbalimbali ziwe za ukimwi na magonjwa sugu wanaoishi ndani ya mkoa wa Mbeya wawahi kwani itafika wakati watapata shida kuniona kabisa,alisema.



    Aliongeza,”madudu yangu yamekataa kuhama hapa na yamesema nikihama hapa hii tiba haitafanyakazi tena, wagonjwa na wahitaji waje watu wanapona na wanarudi kunishukuru,wanakunywa kikombe kimoja leo na kingine kesho basi, wanachangia Sh.200 ya kuni za kuchemshia dawa,na kama wanataka kuniona kwa shida nyingine Sh.1000, viongozi wa shina na mtaa wanaendelea kuboresha huduma na usafi ili kuondokana na magonjwa ya milipuko.”



    Mwandishi wa habari hizi amekuta msululu wa magari yaliyoegeshwa katika maeneo mbalimbali ya mtaa wa mianzini huku maelfu ya wananchi katika foleni wakiwa wameshika kikombe cha plastiki mkononi wangine wakiwa wamebebwa katika machela na ndugu,jamaa na marafiki.



    Akisimulia historia yake Jafari alisema alishindwa kumaliza masomo akiwa kidato cha kwanza mkoani morogoro baada ya kushindwa kusoma na kutokewa na maruwe ruwe na kushindwa kuona katika ubao na hivyo kurudishwa nyumbani kwa Bibi yake mzaa mama yake aliyefariki mwaka 2004 mkoani Mbeya ambapo alikabidhiwa mikoba na Bibi yake na kuanza kufanya shughuli za uganga akiwa na umri mdogo.



    “Baada ya mama kufariki baba alinichukuwa kwenda morogoro na huko nikashindwa kuendelea na masomo kutokana na kutokewa na vitu vya ajabu na kushindwa kuona,nikarudishwa kwa Bibi na baadaye nilipoanza uganga siku moja nilioteshwa kuna dawa ya kuponywa ukimwi na magonjwa sugo Mbozi ingawa mbozi sikujuwi nilichukuliwa na kwenda kuchimba usiku na ndiyo hii ninayotoa tiba,”alisema.



    Baadhi ya wananchi waliofika kupata kikombe kwa kijana Jafari wamemshukuru mungu kwa kuwaletea tabibu huyo ambaye atawasaidia hata watu wasio na uwezo wa kwenda Loliondo.



    Mwisho.

    ReplyDelete