Translate

Tuesday, January 15, 2013

Watoto wana haki ya kuonja upendo kutoka kwa mama na baba zao!

Watoto wana haki ya kuonja upendo kutoka kwa mama na baba zao!



Askofu mkuu Jean Laffitte, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Familia, ametuma ujumbe wa matashi mema na mshikamano wa dhati kwa watu wote watakaoshiriki katika maandamano dhidi ya kupinga sheria ya ndoa za watu wa jinsia moja, mjini Paris, Ufaransa, jumapili, tarehe 13 Januari 2013, kwa kusema kwamba, watoto wana haki ya kupata upendo kutoka kwa baba na mama zao.

Askofu mkuu Laffitte katika mahojiano kwa njia ya simu na Shirika la Habari la Zenit, ameshutumu muswada wa sheria ya ndoa za watu wa jinsia moja kwa kusema kwamba, watu wenye mapenzi mema wana haki ya kupinga sheria ambazo zinakwenda kinyume cha mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu.

Katika kampeni yake kuwania nafasi ya Urais nchini Ufaransa, Rais Francois Hollande aliahidi kwamba, ikiwa kama angeshinda uchaguzi mkuu nchini Ufaransa, angetunga sheria inayoruhusu ndoa za watu wa jinsia moja. Muswada huu wa sheria unaanza kujadiliwa nap engine, ukapita na kuanza kutumika kama sheria, baada ya kupitishwa, mwishoni mwa Mwezi Juni, 2013.

Askofu mkuu Jean Laffitte anawapongeza na kuwashukuru watu wote waliosimama kidete kupinga mmong’onyoko wa maadili; kwa kusimamia mafao ya wengi, kwani kwa asili ndoa ni kati ya bwana na bibi na wala si kinyume chake. Hii ndiyo taasisi ya kweli ambamo motto anaweza kuonja upendo wa kweli kutoka kwa baba na mama yake!

Maelfu ya watu wajimwaga barabarani kutetea msingi bora wa ndoa na familia!

Maelfu ya watu wajimwaga barabarani kutetea msingi bora wa ndoa na familia!



Takribani watu millioni moja kutoka sehemu mbali mbali za Ufaransa, Jumapili, tarehe 13 Januari 2013 walifanya maandamano makubwa kupinga muswada wa sheria unaotaka kuruhusu watu wa jinsia moja kuoana kama Bwana na Bibi na hivyo pia kuruhusia kuasi watoto. Umati huu wa watu ulikusanyika kama kielelezo cha Jamii inayothamini na kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, inayojengeka katika uhusiano wa dhati na unaowajibisha kati ya Bwana na Bibi.

Watu wanasema wanaunga mkono ndoa asilia inayoundwa kati ya Bwana na Bibi, ndiyo maana wamejitokeza kwa wingi kupinga vitendo vinavyokiuka utu na heshima ya binadamu kwa kisingizio cha uhuru na haki sawa. Haya ni maandamano yaliyowashirikisha watu kutoka dini na madhehebu mbali mbali, wote wakiwa na lengo la kusimama kidete kutetea misingi bora ya ndoa na familia, dhidi ya mmong'onyoko wa maadili na utu wema, unaoendelea kujitokeza kwa mwamvuli wa uhuru na haki msingi za binadamu.

Wananchi wa Ufaransa wanabainisha kwamba, Serikali inapaswa kuwa makini katika masuala yanayogusa: Ndoa na Familia; Haki Msingi za Watoto pamoja na kujenga utamaduni wa upatanisho wa kitaifa, ili wananchi waweze kuendelea kuishi kwa amani na utulivu.

Sheria ya nchi isikumbatie utamaduni wa kifo kwa kisingizio cha kuokoa maisha ya Mamamjamzito!

Sheria ya nchi isikumbatie utamaduni wa kifo kwa kisingizio cha kuokoa maisha ya Mamamjamzito!



Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linabainisha kwamba, maisha ya Mama na Mtoto ambaye yuko bado tumboni ni matakatifu na yanapaswa kutunzwa na kuheshimiwa kikatiba na kamwe, sheria za nchi zisikumbatie utamaduni wa kifo, kwa kisingizio cha kuokoa maisha ya Mama mjamzito peke yake. Katiba ya Ireland inakaza utoaji mimba kwa hiyari, lakini inaruhusu mimba hiyo itolewe ikiwa kama maisha ya Mamamjamzito yako hatarini.

Kuna matukio kadhaa ambayo yameendelea kutokea nchini Ireland kiasi cha kuwafanya Maaskofu Katoliki kuibua tena mjadala wa sheria ambayo itaheshimu zawadi ya maisha ya Mama na Mtoto ambaye bado yuko tumboni, kwani hii ni sehemu ya haki msingi wa binadamu. Askofu Christopher Jones, Mwenyekiti wa Tume ya Ndoa na Familia, Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland anasema kwamba, utoaji wa mimba ni mauaji ambayo kamwe hayawezi kuhalalishwa kisheria na ni kinyume cha maadili na utu wema.

Kutokana na kushamiri kwa utamaduni wa kifo, baadhi ya wahudumu wa sekta ya afya wamejikuta wakishinikizwa kutoa mimba kwa kisingizio cha kutaka kuokoa maisha ya Mamamjamzito. Madaktari wanapaswa kutambua kwamba, wao ni wadau wakuu wa maisha, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuokoa maisha ya mama na mtoto ambaye bado yuko tumboni mwa mama yake, kwani maisha ya watu hawa ni matakatifu, yanapaswa kuheshimiwa na kulindwa kikatiba.

Majadiliano yote haya hayana budi kutoa kipaumbele cha pekee kwa wanawake, kwa kuwaelewa, kuwahurumia na kuwaheshimu katika shida na mahangaiko yao ya ndani. Hakuna sababu za msingi zinazoweza kupelekea watu kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo. Wananchi wa Ireland wanataka sasa Serikali iitishe kura ya maoni ili kutengua sheria inayoruhusu utoaji mimba kwa kisingizio cha kutaka kuokoa maisha ya mamamjamzito. Inasikitisha kuona kwamba, kuna zaidi ya wanawake elfu nne kutoka Ireland wanaojihusisha na suala la utoaji mimba nje ya nchi yao.



UJUMBE WA BABA MTAKATIFU KWA SIKU YA 99 YA WAKIMBIZI NA WAHAMIAJI DUNIANI KWA MWAKA 2013

UJUMBE WA BABA MTAKATIFU KWA SIKU YA 99 YA WAKIMBIZI NA WAHAMIAJI DUNIANI KWA MWAKA 2013



Uhamiaji: hija ya imani na matumaini: ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, katika maadhimisho ya Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi, inayodhimishwa na Mama Kanisa tarehe 13 Januari 2013. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba, Mama Kanisa anatembea na binadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani: wakati wa raha, matumaini na shida. RealAudioMP3

Kwa hakika, Kanisa ni mdau mkubwa wa maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, mwanadamu ni mdau mkubwa na mlengwa wa utume wa Kanisa. Hali hii inajionesha kwa namna ya pekee, kwa uwapo na pale anapotangaza, adhimisha, tekeleza matendo ya huruma anapania kumhudumia mtu mzima. Hivi ndivyo inavyojitokeza hata huduma kwa mamillioni ya watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na sababu mbali mbali.

Tatizo la wakimbizi ni jambo linaloyahusisha mamillioni ya watu kutoka katika medani mbali mbali za maisha na nui kati ya changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kitaifa na Kimataifa kutokana na ukweli kwamba, kila mkimbizi ana haki zake msingi ambazo zinapaswa kuheshimiwa na kulindwa katika mazingira yote.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anasema, kutokana na sababu hizi msingi ndiyo maana ameamua kwamba, Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji kwa Mwaka 2013 yaongozwe na kauli mbiu ”Uhamiaji: hija ya imani na matumaini. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Jubilee ya miaka hamsini tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulipozinduliwa; Miaka sitini tangu Waraka juu ya Wahamiaji ulipochapishwa na wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kuadhimisha Mwaka wa Imani katika mwamko wa Uinjilishaji Mpya.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, imani na matumaini ni chanda na pete katika hija ya maisha ya wahamiaji na wakimbizi na kwamba, hizi ni tunu ambazo haziwezi kamwe kutenganishwa, kwani katika mahangaiko yao ugenini mara nyingi Wahamiaji na Wageni wanatumaini kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma kamwe hataweza kuwaacha kamwe watoto wake wanaomkimbilia kwa imani na matumaini licha ya ukweli kwamba, wanalazimika kutoka katika mazingira na nchi yao, lakini iko siku wataweza kurudi tena.

Katika sekta ya Wakimbizi na Wahamiaji, Mama Kanisa anaonesha upendo wa Kimama, kwa kuguswa kwa namna ya pekee, kutokana na umaskini na mahangaiko ya watu hawa. Ndiyo maana daima amekuwa mstari wa mbele kubainisha mikakati ya kichungaji, ili kukidhi mahitaji ya watu hawa pamoja na kuwasaidia wadau mbali mbali wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutoa huduma kwa Wahamiaji na Wakimbizi.

Kanisa linaendelea kujitahidi kuhakikisha kwamba, Wahamiaji, Wakimbizi na wale wanaotafuta hifadhi ya kisiasa wanashirikishwa katika maisha ya kijamii na kitamaduni ya wenyeji wao, bila kusahau mwelekeo wa kidini ambayo ni haki msingi ya kibinadamu. Huu ndio msingi mahususi wa Kanisa linapotekeleza utume wake. Kwa Wakristo, mwingiliano huu unahitaji pia kukoleza moyo wa majadiliano ya Kiekumene, ili kuweza kuzihudumia Jumuiya Mpya na kwa upande wa Kanisa Katoliki, hii ni changamoto ya kuwashirikisha na kuwaingiza katika miundo ya shughuli za kichungaji kwa kuheshimu Mapokeo ya madhehebu yao. Huduma za kichungaji zinakwenda sanjari na mikakati ya maendeleo inayomlenga mtu mzima: kiroho na kimwili; ni fursa pia ya kukutana na Yesu anayewaimarishia matumaini yao.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita anasema kwamba, Kanisa na Mashirika yake ya misaada linalenga kuwajengea uwezo Wakimbizi na Wahamiaji ili waweze kushiriki na kuwajibika kikamilifu katika maendeleo yao kwa kuchangia pia katika ustawi, hali wakifurahia haki na dhamana ya Jamii husika. Wakimbizi na Wahamiaji ni watu wenye imani na matumaini, wanapania kupata fursa nzuri zaidi za maisha. Hawa si watu wanaotamani kuboresha tu hali yao ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Mara nyingi ni kundi ambalo linaleta hofu na wasi wasi, hasa ikiwa kama ni watu ambao wamekumbana na madhulumu pamoja na vita kama chanzo kikuu cha kuwafanya kuzikimbia nchi zao, bado wanaendelea kubaki na makovu katika maisha yao. Lakini yote haya si kikwazo kwa Wahamiaji kujenga msingi wa maisha mapya yanayosimikwa katika matumaini na ujasiri.

Ni matumaini ya watu hawa kwamba, watapokelewa, watasaidiwa na kuonjeshwa mshikamano jambo ambalo lina manufaa lakini linabeba dhamana nzito. Licha ya magumu wanayokumbana nayo, ni watu wanaoweza kuendelea kuchangia taaluma, urithi wao wa kijamii na kitamaduni, ushuhuda wa imani yao ambao unaweza kuwa kweli ni chachu kwa Makanisa ya Zamani, kiasi cha kutoa mwaliko wa kuweza kukutana na Kristo na hatimaye, kulifahamu Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema, kila taifa linayo haki ya kuwa na sera zinazoratibu wahamiaji; kwa kuzingatia mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Ikumbukwe kwamba, kila mtu anayo haki ya kuhama kutoka sehemu moja hadi nyingine kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, ili kutekeleza ndoto na uwezo wake; lakini ieleweke kwamba, ni haki msingi kwa kila mtu kuishi katika nchi yake mwenyewe, jambo hili linawezekana pale tu mambo yanayopelekea watu kuzikimbia nchi zao yamedhibitiwa kikamilifu.

Wahamiaji na wakimbizi wengi ni matokeo ya myumbo wa uchumi kimataifa, ukosefu wa mahitaji msingi, majanga asilia, vita pamoja na kinzani za kijamii. Badala ya kundi hili kuonekana kana kwamba, ni mahujaji wa imani na matumaini, wanajikuta wakishinikizwa na hali halisi ya kuchukua maamuzi magumu ya kuzikimbia nchi zao na matokeo yake, wanajikuta wameathirika zaidi na wala si wahusika wakuu kwa maamuzi ya kutaka kuzihama nchi zao.

Baadhi ya watu hawa wamefanikiwa kuboresha maisha yao, kiasi cha kushirikishwa kikamilifu katika maisha ya Jamii inayowazunguka, lakini bado kuna kundi kubwa linalodhulumiwa na kunyanyasika, kiasi kwamba, linanyimwa hata haki zake msingi au linajikuta likijihusisha na vitendo ambavyo vina madhara makubwa kwa Jamii inayowapokea. Mchakato wa kuwashirikisha Wahamiaji na Wakimbizi unagusa haki zao msingi, majukumu, utu na heshima yao. Ni wajibu wa wageni hawa kuthamini na kujali tunu msingi zinazotolewa na Jamii inayowahifadhi.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kuna haja pia ya kuwaangalia Wahamiaji haramu, jambo linalopelekea uwepo wa biashara haramu ya binadamu na wahanga wakubwa hapa ni wanawake na watoto. Vitendo hivi vya jinai havina budi kulaaniwa na wahusika wafikishwe kwenye mkondo wa sheria na kwamba, sheria za nchi zitumike kudhibiti wimbi la Wahamiaji haramu, ili kuwakatisha tamaa watu wengine wenye mawazo kama haya, ili wasijikute wanatumbukia katika biashara haramu ya binadamu.

Jambo hili linawezekana kwa kuwa na mbinu mkakati ya maendeleo endelevu kwa nchi husika; kudhibiti biashara haramu ya binadamu, kuwa ni mikakati itakayowawezesha watu kupata vibali halali ya kuingia katika nchi husika na kwamba, kila mtu anapaswa kuangaliwa katika undani wake hasa pale vibali vya hifadhi ya kisiasa vinavyopkuwa vinashughulikiwa. Sera bora ziende sanjari na elimu sahihi ili kuwawezesha watu kuunda dhamiri nyofu. Kuna haja pia ya kudumisha ushirikiano kati ya Serikali, Kanisa na Taasisi mbali mbali zinazojitoa mhanga kwa ajili ya kukuza na kudumisha maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kwa Kanisa, jukumu hili ni kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo.

Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee, Wakimbizi na Wahamiaji kutumia siku hii kuamsha tena imani na matumaini yao kwa Kristo ambaye anatembea nao katika mahangaiko yao ya kila siku. Anawahimiza kujibidisha kukutana naye katika matendo ya huruma wanayopatiwa katika hija ya maisha yao kama wahamiaji. Anawaalika kufurahi kwani iko siku wataweza kuvuka vikwazo na magumu haya, kwa kuendelea kuamini katika mang’amuzi, uwazi na kupokelewa kwao mambo ambayo wanayaonja kutoka kwa watu mbali mbali. Maisha ni safari ndefu, yenye mabonde na milima, lakini ina mwanga wa matumaini, ambao ni Yesu Kristo, lakini ili kuuona Mwanga huu kuna haja ya kukutana na Mashahidi wa Mwanga.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi Duniani inayoadhimishwa tarehe 13 Januari 2013 kwa kuongozwa na kauli mbiu ”Uhamiaji: hija ya imani na matumaini” chini ya ulinzi wa Bikira Maria, kielelezo cha matumaini na faraja; nyota ambayo kwa njia ya uwepo wake wa kimama, yuko karibu katika kila hatua ya maisha ya mwanadamu. Anawapatia wote baraka zake za kitume.



Mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri Yohane Paulo II kuwa mtakatifu wazidi kupamba moto!

Mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri Yohane Paulo II kuwa mtakatifu wazidi kupamba moto!



Kardinali Giovanni Battista Re, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makleri, hivi karibuni ameonesha matumaini makubwa kwamba, mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kuwa Mtakatifu unaendelea kwa kasi nzuri, pengine akatangazwa kuwa Mtakatifu, katika kipindi cha miaka michache ijayo!
Kardinali Re ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa kuzindua kitabu kilichoandikwa na mtaalam wa masuala ya Vatican Mimmo Muol, kuhusiana na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, aliyekuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro lakini pia Mshahiri.
Matumaini ya Kardinali Re yanatokana na ukweli kwamba, kuna miujiza ambayo imekwisha pokelewa kama kielelezo cha utakatifu wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, hatua kubwa katika kutangazwa kuwa na Mama Kanisa kuwa Mtakatifu. Miujiza hii inaendelea kufanyiwa kazi na wataalam wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu. Miujiza inayohusu uponyaji inapembuliwa na madaktari bingwa wapatao saba, wenye dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanapata ukweli wote kuhusu muujiza unaozungumzwa.
Kwa vile hii ni kazi nyeti, madaktari hawa wanaifanya kazi hii kwa umakini mkubwa ili kuona ikiwa kama ugonjwa huu umepona kutona na tiba au ni kwa njia ya neema na Baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya maombi ya Mwenheri husika. Madaktari hao wanapokubaliana kwamba, uponyaji huu uko nje ya maelezo ya kawaida, basi hapo, Kanisa linaweza kutamka kwamba, huu ni muujiza.

wazazi wahoji ukimya wa serikali kuchangishwa sh.24,500 kuandikisha mtoto darasa la kwanza shule ya msingi Muungano Mbeya na kuchangishwa ndoo,majembe,mafyekeo,madawati na rim Sekondari za kata vinakwenda wapi ?

Na Thompson Mpanji,Mbeya
 
BAADHI ya wazazi jijini Mbeya wamehoji ukimya wa serikali katika kuhusu malalamiko yao ya utozwaji wa fedha za madawati na michango mingine  katika zoezi zima la uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa mwaka 2013 katika shule mbalimbali zikiwemo za msingi na Kata.

Aidha wazazi hao wamehoji  vinakopotelea baadhi ya vifaa vinavyoagizwa na wakuu wa shule za sekondari za kata kwa kila mwanafunzi kupeleka majembe,Madawati,fyekeo,ndoo na bunda la karatasi(Rim) kwani imekuwa ni kero kubwa.

"Kila mwaka walimu wanaagiza wanafunzi wanaofika kuanza kidato cha kwanza katika sekondari za kata kwenda na vifaa hivyo,hayo majembe ukienda kuangalia stoo zao hakuna wanayapeleka wapi,wanaagiza ndoo mpya lakini hata bustani ya kumwagilia hawana,alisema Mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Johnson Mwambepo,mkazi wa Forest.

Mzazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Richard mngoni mkazi wa Kata ya Ruanda alihoji fedha wanayotozwa kiasi cha Sh.24,500 kwa ajili ya kumwandikisha mtoto darasa la kwanza katika shule ya msingi Muungano,jijini Mbeya.

Alisema yeye(Richard) yupo kitandani kwa muda wa mwezi mmoja sasa akiwa anasumbuliwa na homa lakini ameshangazwa kupelekewa taarifa na mke wake aliyempeleka mtoto kuandikisha darasa la kwanza katika shule hiyo iliyopo maeneo ya Stereo kuwa zinahitajika fedha hizo ilhali  hajafanyakazi ya kuingiza fedha kutokana na kuuguwa.

Wakati wazazi hao wakilalamikia hali hiyo serikali ya mtaa  wa Ilomba,jijini Mbeya nayo imelalamikiwa kwa kuwatoza Sh.12,500 mchango wa kuandikisha jina  la kuingia darasa la kwanza mwaka 2013.
 
 
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wazazi (majina yamehifadhiwa)walisema kuwa wameshangazwa  viongozi wa serikali ya mtaa kuandikisha majina ya watoto kwa kutoza sh.12,500 na kwamba mzazi asiyekuwa na kiasi hicho mtoto wake hawezi kupokelewa.
 
Walisema wameambiwa kuwa mzazi ambaye hataweza kutoa fedha hiyo mtoto wake hawezi kusoma shuleni hapo na endapo atakubaliwa basi atatakiwa kukaa chini kwenye vumbi hatoruhusiwa kukalia dawati jambo ambalo wamedai ni unyanyasaji.
 
Mmoja wa wajumbe wa serikali ya mtaa wa Ilomba,Edwin Kamweli alisema hizo ni mbinu chafu za baadhi ya wanasiasa kutaka kuzorotesha maendeleo ya mtaa wa Ilomba kwani mkutano wa hadhara ulikaa na kukubaliana wanannchi wote kutoa mchango huo kwa ajili ya kuboresha mazingira ya shule.
 
"Huu mfumo wa vyama vingi utaturudisha nyuma tukiendekeza maneno bila vitendo…kuna watu wavivu wanatumia fursa ya demokrasia kuturudisha nyuma na sisi tunasema hatuwezi kukubali na haiwasaiidii tunasonga mbele…vikao na mikutano ikiitishwa wanasema wapo bize tuikipitisha maazimio wanasema tunawaonea,"alisema.
 
Kamwela alisema kiasi hicho cha sh.12,500 kilipitishwa na wananchi waliohudhuria mkutano mmoja wa hadhara ikiwa na lengo la kuboresha mazingira ya shule na wanafunzi ili waweze kusoma bila kubanana.
 
Alisema mgawanyo wa fedha hiyo ni Sh.10,000 kwa ajili ya dawati litakalochangiwa na wanafunzi watatu watakaolitumia ambapo kila mmoja atachangia kiasi hicho na kukamilisha gharama ya ununuzi wa dawati moja kwa Sh.30,000.
 
Mwalimu huyo mstaafu aliendelea kufafanua kuwa katika shule hizo mbili za Kagera na Ruanda Nzwovwe kuna mlinzi anayelipwa na hivyo kila mzazi wamekubaliana achangie Sh.1,500 ambapo mchango wa maji ni Sh.1,000.
 
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilomba,Erasto Mwakapoma alifafanua kuwa uandikishwaji ni bure lakini michango hiyo ilitokana na wananchi wenyewe baada ya kukaa katika mkutano wa hadhara wa mtaa wa Ilomba Novemba,30,2012 ambapo yeye alikaribishwa na kwamba wanaochangia ni wananchi wote na siyo wazazi wanaowaandikisha watoto shule pekee.
 
Mwakapoma alisema shule ya msingi Kagera na Ruanda Nzovwe zinatarajia kuandikisha watoto zaidi ya 200 ingawa lengo lilikuwa watoto 130,lakini hawatoweza kukataa kuwaaandiskisha watoto waliofikia umri wa kwenda shule hivyo kunahitajika madawati ya ziada.

Hata hivyo baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya walisema endapo kila mwaka  wanafunzi wanaenda na madawati mapya ama kulipia gharama ya madawati kusengeendelea kuwepo kwa tatizo la madawati na vifaa  vingine kutokana na michango inayotolewa wakati wa uandikishwaji wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza.

Mwisho.

Monday, December 24, 2012

watoto waandikishwa kwa malipo Mbeya

Na Thompson Mpanji,Mbeya
 
BAADHI ya wazazi jijini hapa wamelalamikia hatua ya serikali ya mtaa wa Ilomba,jijini Mbeya kuwatoza Sh.12,500 mchango wa kuandikisha jina  la kuingia darasa la kwanza mwaka 2013.
 
Hatua hiyo inadaiwa kwenda kinyume na maagizo ya Waziri wa nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI),Kassim majaliwa kuwa kuandikisha darasa la kwanza ni bure na hakuna michango yeyote iliyoruhusiwa kisheria.
 
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wazazi (majina yamehifadhiwa)walisema kuwa wameshangazwa  viongozi wa serikali ya mtaa kuandikisha majina ya watoto kwa kutoza sh.12,500 na kwamba mzazi asiyekuwa na kiasi hicho mtoto wake hawezi kupokelewa.
 
Walisema wameambiwa kuwa mzazi ambaye hataweza kutoa fedha hiyo mtoto wake hawezi kusoma shuleni hapo na endapo atakubaliwa basi atatakiwa kukaa chini kwenye vumbi hatoruhusiwa kukalia dawati jambo ambalo wamedai ni unyanyasaji.
 
"Wametuambia eti kama hatutowi basi watoto wetu watakuwa wakisoma huku wakiwa wamekaa kwenye vumbi darasani na wenzao waliolipa watakaa katika madawati…ndiyo maana watoto wetu wanarudi wamechafuka ovyo kila siku kumbe ni sababu ya kuwanyanyapaa,"alisema.
 
Mmoja wa wajumbe wa serikali ya mtaa wa Ilomba,Mwl.Edwin Kamweli alisema hizo ni mbinu chafu za baadhi ya wanasiasa kutaka kuzorotesha maendeleo ya mtaa wa Ilomba kwani mkutano wa hadhara ulikaa na kukubaliana wanannchi wote kutoa mchango huo kwa ajili ya kuboresha mazingira ya shule.
 
"Huu mfumo wa vyama vingi utaturudisha nyuma tukiendekeza maneno bila vitendo…kuna watu wavivu wanatumia fursa ya demokrasia kuturudisha nyuma na sisi tunasema hatuwezi kukubali na haiwasaiidii tunasonga mbele…vikao na mikutano ikiitishwa wanasema wapo bize tuikipitisha maazimio wanasema tunawaonea,"alisema.
 
Mwl.Kamwela alisema kiasi hicho cha sh.12,500 kilipitishwa na wananchi waliohudhuria mkutano mmoja wa hadhara ikiwa na lengo la kuboresha mazingira ya shule na wanafunzi ili waweze kusoma bila kubanana.
 
Alisema mgawanyo wa fedha hiyo ni Sh.10,000 kwa ajili ya dawati litakalochangiwa na wanafunzi watatu watakaolitumia ambapo kila mmoja atachangia kiasi hicho na kukamilisha gharama ya ununuzi wa dawati moja kwa Sh.30,000.
 
Mwalimu huyo mstaafu aliendelea kufafanua kuwa katika shule hizo mbili za Kagera na Ruanda Nzwovwe kuna mlinzi anayelipwa na hivyo kila mzazi wamekubaliana achangie Sh.1,500 ambapo mchango wa maji ni Sh.1,000.
 
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilomba,Erasto Mwakapoma alifafanua kuwa uandikishwaji ni bure lakini michango hiyo ilitokana na wananchi wenyewe baada ya kukaa katika mkutano wa hadhara wa mtaa wa Ilomba Novemba,30,2012 ambapo yeye alikaribishwa na kwamba wanaochangia ni wananchi wote na siyo wazazi wanaowaandikisha watoto shule pekee.
 
Mwakapoma alisema shule ya smingi Kagera na Ruanda Nzovwe zinatarajia kuandikisha watoto zaidi ya 200 ingawa lengo lilikuwa watoto 130,lakini hawatoweza kukataa kuwaaandiskisha watoto waliofikia umri wa kwenda shule hivyo kunahitajika madawati ya ziada.
 
Mwisho.