Translate

Wednesday, October 31, 2012

Tazara saccos kujenga Hosteli ya kisasa

Na Thompson Mpanji,Mbeya

CHAMA cha kuweka na kukopa cha Tazara Saccos Mkoani Mbeya kinatarajia kujenga hosteli kubwa ya kisasa ili kuachana na dhana ya kuwa tegemezi kutoka kwenye taasisi za kibenki na kuwa mradi huo mkubwa utaweza kusaidia chama kujitegemea chenyewe badala ya kutegemea zaidi kukopa katika benki hizo.



Hatua ya kuwa na ujenzi huo wa hosteli imekuja baada ya uongozi wa Tazara kwa kushirikiana na wanachama kuamua kwa pamoja kuwa na kitega uchumi chao wenyewe ambacho kitasababisha kuacha kukopa katika mabenki kwani hosteli hiyo itakapokuwa imekamilika hakutakuwa na sababu ya kukimbilia tena katika mabenki badala yake watatumia kitega uchumi chao kukuza mtaji wa chama.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama hicho wa kumi na tisa toka kuanzishwa kwake, Mwenyekiti wa Tazara Saccos Mkoani Mbeya Ambrose Shayo amesema kwamba kuanzia wameona kuwa mradi pekee ambao wanaweza kuanza nao ni hosteli kutokana na vyuo vingi kuanzishwa Mkoani hapa na ongozeko la wananchi kuwa kubwa.


Shayo amesema kuwa mradi huo utagarimu kiasi cha shilingi bilioni. 2 na kuwa fedha hizo zitapatikana kwa kila mwanachama kuchangia hisa zake ambazo ni shilingi 3,0000 ambazo watatoa kwa kila mwezi na kwamba mbali ya hisa za wachama pia chama kama kitakuwa kinanunua hisa za mil.8 kila ujenzi huo unatarajio kukamilika ndani ya miaka mitano ijayo sababu uwanja upo tayari ni kuanza tu mchakato wa kutafuta fedha mapema kutoka taasisi zingine kwa kutumia njia mbali mbali.

Aidha Mwenyekiti huyo amesema mwisho wa utekelezaji wa mpango huo ni kuweza kuwekeza na kuanza kujitegemea wenyewe badala ya kutegemea mabenki zaidi ambazo wamekuwa wakitumia kwa muda mrefu.
Mwiisho.

Ajinyonga kwa waya wa simu baada ya kumpiga mkewe

Na Thompson Mpanji,Mbeya

MKAZI wa Iziwa Mkoani Mbeya Mbwiga Mwalungwe(60), amefariki dunia baada ya kujinyonga nyumbani kwake kwa kutumia waya wa simu Oktoba 24 mwaka huu baada ya marehemu kumpiga mkewe.


Inadaiwa marehemu alimpiga mkewe aitwaye Taines Mbwiga(45) Oktoba 23 hali iliyompelekea kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Jijini hapa ambapo alipewa PF3 kwa ajili ya kutibiwa na kulazimu kulazwa hospitalini hapo.

Kutokana na tukio la baada ya mkewe kulazwa hospitalini, Jeshi la Polisi lilianza kufuatilia tukio hilo ndipo marehemu alipogundua kuwa anakabiliwa na mkono wa sheria aliamua kuchukua uamuzi mgumu kwa kuchukua waya wa simu majira ya saa 4 kamili asubuhi Oktoba 24, kisha kujinyonga nyumbani kwake.


Aidha polisi walifika eneo la tukio majira ya saa 6:00 mchana na kuuchukua mwili wa marehemu hadi hospitali ya rufaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kwamba hali ya mwanamke huyo inaendelea vema ambapo ameruhusiwa kutoka hospitalini Oktoba 2 na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali hiyo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi,kuhusiana na tukio hilo Balozi wa mtaa huo Chaina Juma amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba amewaachia jeshi la polisi kufanya uchunguzi ili kupata kiini hasa cha Mwalungwe kujiua kwa kujinyonga na kumuacha mkewe akiendelea kuugua hospitali.


Mwisho.



Mtoto wa miaka nane ajinyonga

MTOTO  mdogo aliyefahamika kwa jina la Calvin Patrick mwenye umri wa miaka nane  mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Iwambi ,Mkazi wa Mtaa wa Ivwanga Kata ya Iwambi Mkoani Mbeya amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya viatu nje ya nyumba yao.
Tukio la kujinyonga kwa mtoto Patrick limetokea majira ya saa 5.00 octobar 27 mwaka huu asubuhi katika mtaa wa Ivwanga wakati wazazi wa mtoto huyo walipokuwa wametoka nyumbani hapo na ndipo mtoto huyo alipochukua jukumu hilo zito na la aina yake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa mtaa huo Chonde Calisto alisema wakati tukio hilo linatokea Baba mzazi wa mtoto huyo Patrick Mwakapalila alikuwa ametoka na kaka mkubwa wa marehemu aitwaye Joshua kuelekea mjini kutafuta mahitaji na kwamba baada ya tukio hilo baba mzazi wa mtoto huyo alipigiwa simu na kutakiwa kurudi haraka nyumbani.

Amesema kuwa baada ya tukio baba mzazi wa mtoto huyo alipigiwa simu ili arudi nyumbani kuona tatizo lililotokea kwa mtoto wake na kwamba baada ya kufika alikuta mwanae huyo mdogo akiwa nje ya nyumba yao akiwa ananing'inia juu akiwa amejinyonga kwa kamba ya viatu"alisema.

Hata hivyo mama mzazi wa mtoto huyo nae hakuwepo nyumbani hapo kwani alikuwa katika shughuli zake za kibiashara ambako anauza duka la mahitaji mbali mbali ya nyumbani eneo la Iwambi ambako jirani na nyumbani.

Chonde amesema mpaka sasa bado hakijafahamika chanzo cha kujinyonga kwa mtoto huyo na polisi walifika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu kwa uchunguzi zaidi ili ndugu waweze kukabidhiwa mara baada ya uchunguzi huo kukamilika .


Mwisho.

serikali haijaridhishwa na ujenzi wa barabara ya kuelekea Chunya

SERIKALI imetishia kuinyang’anya kampuni ya China Communication Construction Limited zabuni ya ujenzi wa barabara ya kutoka Mbeya mjini hadi Lwanjilo wilaya ya Mbeya Vijijini yenye urefu wa kilometa 36 baada ya kutoridhishwa na kasi ya utendaji kazi ya mkandarasi huyo.




Hatua hiyo ya Serikali imetokana na mkandarasi huyo kushindwa kufikia malengo ya ujenzi huo kwa kiwango cha lami katika muda uliopangwa huku akiwa tayari ameshakabidhiwa fedha za awali za mradi huo shilingi bilioni Nane za Tanzania.



Ujenzi huo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 55 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Wahisani wa maendeleo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Mbeya mjini hadi wilayani Chunya yenye urefu wa kilometa 72.



Sehemu ya pili ya ujenzi huo kutoka Lwanjilo hadi Chunya mjini utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 44 kupitia mkandarasi mwingine.



Mkandarasi huyo aliyeanza kazi hiyo Novemba mwaka jana amechukua nafasi ya mkandarasi wa awali kampuni ya Kundan Sing iliyokabidhiwa ujenzi huo mwaka 2010 kabla ua kushindwa kuendelea na kazi kutokana na Serikali kuchelewa kutoa fedha mradi huo.



Hata hivyo tangu alipokabidhiwa kazi hiyo, kasi ya utendaji wake imekuwa ikilalamikiwa na mamlaka husika kwa maelezo kuwa ameshindwa kuifanya kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa.



Akikagua ujenzi huo Oktoba 15, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Greyson Lwenge, amesema Serikali hairidhishwi na kasi ya utendaji kazi ya mkandarasi huyo na kutishia kumnyang’anya zabuni hiyo.



“Nimetembelea ujenzi huu kwa kilometa zote 36 kutoka Mbeya mjini hadi hapa Lwanjilo, ukweli sijaridhishwa na kazi inavyokwenda, mvua zinakaribia kunyesha na hakuna mafanikio yaliyofikiwa kama tulivyotarajiwa.”



“Serikali imeshatangaza kuwa barabara hii ni lazima ikamilike kwa wakati, hivyo kama tutaona mkandarasi huyu anaendelea kusuasua, hatutasita kumnyang’anya kazi na kumtafuta mkandarasi mwingine, tunataka kazi ifanyike hatutaki maneno.” alisema Injinia Lwenge.



Hadi sasa mkandarasi huyo amenza ujenzi wa barabara hiyo katika kijiji cha Lwanjilo katika urefu usiozidi kilometa tano hali inayoitia shaka Serikali kuwa huenda isikamilike kwa wakati katika kipindi cha miezi 36 tangu alipokabidhiwa zabuni hiyo Novemba mwaka jana.



Kutokana na hali hiyo Injinia Lwenge ameiagiza Wakala wa Barabara nchini, TANROADS mkoa wa Mbeya na Mhandisi wa mkoa kuhakikisha mkandarasi huyo anatekeleza kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba uliopo pamoja na kuhakikisha barabara hiyo haifungwi wakati wa mvua ili kuepusha usumbufu kwa wananchi.



Hata hivyo viongozi wa kampuni hiyo ya China Communication Construction Limited hawakuwa tayari kuzungumza na Waandishi wa habari kuhusu hali hiyo huku wakishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kuchelewa kuanza kwa ujenzi huo wakati wakizungumza na Injinia Lwenge.



Awali mmoja kati ya viongozi wa kampuni hiyo ambao pia hawakuwa tayari kutaja majina yao, alijifanya hajui kuzungumza lugha ya Kiingereza na kutumia mkalimani kumjibu Injinia Lwenge kabla ya Naibu Waziri huyo kubaini ujanja huo na kumlazimisha kuzungumza lugha hiyo na hatimaye kufanya hivyo kwa ufasaha mkubwa.



Barabara hiyo ni miongoni mwa barabara zilizomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, CCM, ya mwaka 2010 ambapo Rais Jakaya Kikwete, aliwaahidi wakazi wa vijiji vinavyopitiwa na barabara kuwa atahakikisha inatengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuwaondoakuwa atahakikisha inatengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuwaondolea kero ya usafiri hasa wakati wa mvua.



Ubovu wa barabara hiyo umesababisha wakazi wa kijiji cha Lwanjilo kutozwa kati ya shilingi 8,000 hadi 10,000 kwenda Mbeya mjini umbali wa kilometa 36 wakati nauli ya kutoka Mbeya mjini hadi wilayani Kyela umbali wa zaidi ya kilometa 110 ikiwa ni shilingi 3,000.



Mwisho

Padre Mawasawe-Mkuu wa shirika la waconsolata aliyekufa maji kuzikwa

Jimbo kuu la Dar es Salaam linapokea kwa majonzi na masikitiko makubwa habari za kifo cha Padre Salutaris Luca Massawe, Mkuu wa Shirika la Waconsolata Tanzania, kilichotokea hapo tarehe 25 Oktoba 2012 kwa kuzama baharini, eneo la Msalaba Mtakatifu, mjini Bagamoyo nyakati za Alasiri na mwili wake kupatikana asubuhi tarehe 26 Oktoba 2012.



Kanisa limempoteza kiongozi mahiri na mchapakazi aliyetekeleza kazi zake kwa ufanisi. Kabla ya kuchaguliwa na Wanashirika wenzake hapo tarehe 7 Septemba 2011 kuliongoza Shirika nchini Tanzania, alishiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.


Anakumbukwa sana kutokana na mchango wake wa ushauri katika maboresho ya Taasisi ya Tumaini Media, ambayo iko chini ya Jimbo kuu la Dar es Salaam, inayosimamia TV Tumaini, Radio Tumaini na Gazeti la Tumaini Letu. Alikwisha wahi kufanya utume wake katika Kituo cha Sala cha Waconsolata kilichoko Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.


Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam amesema kwamba, kifo cha Padre Salutaris Lucas Massawe kimeacha pengo kubwa, ambalo halitakuwa rahisi kuweza kuzibika.Waamini wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam wanatarajiwa kufanya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Marehemu Padre Salutaris Massawe tarehe 29 Oktoba 2012 kabla ya kusafirishwa kwenda Jimboni Iringa kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika hapo siku ya Jumanne tarehe 30 Oktoba 2012, kwenye Makao Makuu ya Shirika la Wamissionari wa Consolata nchini Tanzania.

Aliyekuwa Mlezi wa Chadema,Thomas Nyimbo akionesha bango alilobuni wakati akigombea ubunge lililoandikwa "MTU kwanza Chama baadaye"