Translate

Saturday, April 23, 2011

Friday, April 15, 2011

Mashirika ya caritas nchini yametakiwa kutokuwa mzigo majimboni

Na Thompson Mpanji,Mbeya
MASHIRIKA ya caritas nchini yametakiwa kujipanga vizuri katika utendaji wa kazi ,uwazi,uwajibikaji na ushirikishwaji ili yasionekne kuwa mzigo wa majimbo ya kanisa katoliki.
Mwito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shirika la Caritas Mbeya,Bw.Edgar Mangasila ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano mtandao wa mashirika ya Caritas kanda ya kusini (SHICANET)  wa siku moja uliofanyika katika ukumbi wa kituo cha malezi kwa vijana,kanisa katoliki,jimbo la Mbeya jijini hapa.
Bw.Mangasila amesema ili  Mashirika la Caritas yaweze kufanya vizuri katika utoaji wa huduma katika jamii na kuonekana yanafanyakazi vizuri, watendajike wanapaswa kufanyakazi kwa ushirikiano,kujipanga vizuri,kufuata miiko na taratibu za kazi na matumizi ya fedha yanayozingatia uwazi pale taarifa inapohitajika.
“Wafanyakazi wa Caritas mjitahidi msiwe mzigo wa majimbo,fanyeni kazi kwa uwazi na uwajibikaji siyo ibakie dhamira  safi tu bali  kila mtu anapohitaji kujuwa kinachoendelea akione,na hili ndiyo moja ya tatizo zinazofanya caritas nyingi zisipige hatua,kuna mashirika mengi kama Miserior ambayo yanapenda kufanyakazi nasi,hivyo tuzitumie fursa hizi,”alisema.
Ametaja sababu nyingine inayopaswa kuizingatia ni kuboresha mazingira ya watendaji,kutafuta mbinu za kutafuta fedha,mahusiano mema ya wafanyakazi na jimbo pamoja na kutekeleza  kwa muda muafaka shughuli zinazopangwa.
Mratibu wa SHICANET,Bw.Lufunyo Mlyuka amesema mkutano huo ni utaratibu wa mtandao kuwaunganisha wanachama  watendaji wa Caritas kutoka  katika majimbo nane ambayo ni Caritas Mbeya,Njombe,Iringa,Songea,Tunduru Masasi,Mahenge,Mbinga na Sumbawanga lengo likiwa ni waratibu kubadilishana mawazo na uzoefu,kuangalia changamoto,mafanikio  na mpangokazi wa Shicanet ili uweze kuwafikia wakurugenzi wote wa caritas.
Mwisho.

Mlemavu asiyeona Chunya aibuka na kudai kutibu magonjwa sugu na ukimwi

Na Thompson Mpanji,Chunya

IDADI ya wataalamu wa tiba ya kikombe inazidi kuongezeka baada ya ‘Babu’Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapila wa Loliondo, wilayani Chunya Mlemavu wa asiyeona  ameibuka  na kudai kutibu magonjwa yote sugu ukiwemo Ukimwi  ambapo maelfu ya wananchi wanamiminika kupata tiba hiyo inayodaiwa kutibu kwa muda wa siku 43.

Hata hivyo taarifa za uhakika zilizolikia gazeti hili zinasema kuwa  msaidizi wa mlemavu huyo, aliyemsindikiza kwenda kuchimba dawa hiyo anadaiwa kutouona mti huo kwa mara ya pili   baada ya kumtoroka bosi wake na kwenda katika msitu kwa lengo la kuichukua dawa hiyo ili aifanyie biashara.

Wakiongea na mwandishi wa habari hizi baadhi ya wananchi wa Kijiji ch Mbuyuni wamesema wameanza kupata huduma hiyo bure  tangu,aprili,7 mwaka huu  na kwamba kuanzia jana mtaalamu huyo ameanza kutoa tiba ya kikombe kwa familia nzima kuchangia kiasi cha sh.500.

Akisimulia kuibuka kwa mtaalamu huyo mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Mbuyuni,Nico Haule amesema mlemavu huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho amedai kuoteshwa mara kadhaa na babu yake marehemu lakini alikuwa akidharau hadi ilipofikia siku  hiyo alipomuomba kijana mmoja amsindikize kuelekea katika milima ya Iseche,Tarafa ya kwimba,wilayani humo.

Msaidizi wa mtaalamu huyo,kaburi Mwankumbi alisema kuwa  aliombwa na Mahela kumsindikiza katika msitu wa milima ya Iseche na Mkwajuni na baada ya kufika huko alishangaa kumwambia walipokuwa wakielekea syo ulipo mti huo na kuelekeza eneo jingine ambapo kipofu huyo alirudi kinyume nyume na kuukamata mti huo na kumwelekeza auchimbe na kurudi nao nyumbani.

“Tulichemsha mti huo na akanywa yeye na mimi na majirani sita akiwemo mdogo wake wa kike ambaye ni mja mzito siku ya pili watu baada ya kupata taarifa walifika wengi,nami nilipoona anatoa  tiba hiyo bure nikamkimbia ili nikauchimbe mti ule na kuwauzia watu lakini nilishangaa sikuuona kabisa na niliporudi kumwambia (Mahela)alicheka,”alisema Mwankumbi.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mbuyuni,Romwad Mwashiuya amethibitisha kuibuka kwa mkazi huyo wa Mbuyuni  aliyemtaja kwa jina la Simon Patson  Mahela ambaye ni  mlemavu wa macho na anaishi kwa msaada wa kuongozwa.

Mwashiuya alisema,  baada ya uongozi kupata taarifa hiyo walifika nyumbani kwake na kuukuta umati wa watu zaidi ya 1000 wakiendelea kupata tiba hiyo na baada ya kumhoji aliwaelekeza na hatimaye  walichukuwa hatua za awali za kumuongezea vikombe kwani alikuwa akitumia kikombe kimoja kuwanyweshea watu wote,pamoja na kumpatia pipa la kuchemshia dawa sanjari na kuboresha hali ya vyoo.

Ofisa wa Afya,Bw.Nicholaus Likokolo alisema baada ya kufika katika eneo hilo wameshauri huduma za choo ziboreshwe na kwamba ingawa yupo nje kikazi lakini  amepata taarifa kuwa  mganga wa kituo cha Afya Mbuyuni amefika pia na kushauri kuchukuwa sample ya dawa na  kuipeleka kwa mganga mkuu wa wilaya ya chunya  ili  aweze kuifikisha kwa mkemia mkuu kwa uchunguzi zaidi.

Wakati huo huo,Katika mtaa wa mianzini,Kata ya mabatini,jijini Mbeya,babu mtoto jafari fikiri amesikika akiwatangazia wananchi wanaokwenda kunywa kikombe kwake kuwa mtu yeyyote atakayefika kwa nia ya kumjaribu ataona cha mkata kuni.

Taarifa hiyo amekuwa akiitoa mganga huyo kufuatia kuumbuka kwa mzee mmoja ambaye anadaiwa kufika kumjaribu na kuichafua huduma hiyo ambayo imekuwa kimbilio la wananchi walio wengi kutoka wilaya mbali mbali za mkoa wa Mbeya ambao wanashindwa kusafiri kufika katika kijiji cha samunge,wilayani Loliondo kwa mchungaji babu Ambilikile mwasapila.

Hata hivyo kuna taarifa ya kupata madhara  baadhi ya wananchi  waliokunywa  dawa hiyo  na kukiuka masharti ya kunywa pombe,kuvuta sigara,kutokunywa dawa ya aina yeyote  na kutofanya tendo la ndoa kwa muda wa siku nane baada ya kunywa vikombe viwili vya tiba hiyo.

Mwisho.

Kibaka aliyeiba Sh.10,000 yang'angania mkononi,apooza miguu na mkono

Na Thompson Mpanji,Mbozi

KIJANA mmoja mpiga debe wa magari yanayofanya safari zake Kamsamba-Mlowo wilayani Mbozi amekumbwa na mkasa wa aina yake baada ya  kudaiwa kuiba fedha  ambayo baadaye ilikutwa imenasa katika mkono wake wa kulia na miguu yote miwili kupooza huku akiwa amelazwa katika zahanati moja wilayani humo.

Tukio hilo la aina yake limetokea ,aprili,10 majira ya mchana baada ya kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Jacob Jengela kuokota fedha Sh.10,000 inayodaiwa kudondoshwa na  muhudumu wa kituo cha kuuza  mafuta kinachomilikiwa na mfanyabiashara aliyetajwa kwa jina moja la Chaula kilichopo maeneo ya Mlowo wilayani humo na kuikanyaga kwa mguu baada ya kuiona na baadaye kuificha mkononi ambapo mhudumu huyo baada ya kushtuka alipiga kelele ya kuibiwa na kijana huyo aliamua kutimua mbio lakini mbio zake ziliishia sakafuni baada ya kudondoka ghafla na kupooza.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema kuwa baada ya kijana huyo kuanguka chini huku akiwa anajizoa zoa na kuonekana anashindwa kunyanyuka wananchi wenye hasira kali walimvamia na kutaka kumchoma moto lakini askari polisi wa kituo kidogo cha Polisi cha mlowo walifanikiwa kumuokoa na kumkimbiza katika zahanati iliyotajwa kwa jina la Tumaini kwa ajili ya  uchunguzi na matibabu zaidi.

Aidha  inadaiwa kuwa chanzo cha kuanguka na kupooza miguu yote miwili na mkono wa kulia ulionasa noti hiyo  ya sh.10,000 iliyoendelea kung'ang'ania  ikiwa imenasa mkononi huku akiwa amelazwa  katika zahanati hiyo  hadi kipindi hiki kinaporuka hewani ni kutokana na imani inayohusishwa na masuala ya kishirikana kuwa fedha hiyo ilikuwa imetegwa.

Hata hivyo kipindi hiki baada ya kusasiliana na mmiliki wa kituo hicho aliyetajwa kwa jina moja la Chaula amesema anadhani kijana huyo alikuwa na matatizo ya maradhi ya muda mrefu kwani baada ya yeye kupokea taarifa hiyo alimuuliza mhuhudu ambaye alidai hakumbuki kama alidondosha fedha hiyo.

Mwisho.

Monday, August 30, 2010

watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi wamezishukia Asasi zinazowahudumia kwa kwa madai ya kutowapatia huduma stahili,wadai ARV's basi

Na Thompson Mpanji,Mbeya

WAGONJWA wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya ukimwi wamezilalamikia Asasi zinazoshughulika na masuala ya ukimwi,watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu jijini Mbeya kwa kutowapatia lishe na huduma nyingine muhimu kama wanavyopangiwa na madaktari.

Madai hayo yametolewa na wagonjwa kutoka katika Kata mbalimbali jijini hapa walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti kufuatia kuwepo kwa tetesi za kutelekezwa kwa wagonjwa hao.

Walisema kuwa wameshangazwa na ukimya uliopo katika asasi wanazohudumiwa tofauti na ilivyokuwa awali kwani walikuwa wakipatiwa huduma zote kufuatana na maelekezo ya madaktari wanaowahudumia na kwamba maisha yao yapo hatarini kutokana na madawa wanayoyatumia kwa ajili ya kurefusha maisha yanawamaliza nguvu kutokana na kuyanywa bila kupata lishe.

Walisema tangu walipopima afya zao na kugundulika kuwa wanaishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi walikuwa wakiandikiwa na madaktari kupata lishe bora kama samaki,matunda,mayai na maziwa pamoja na fedha ya nauli lakini tangu mwezi januari,2010 hadi sasa hakuna huduma yeyote waliyoipata zaidi ya kupigwa kalenda na wahusika katika Asasi wanazohudumiwa.

“Wanasema hawana fedha sasa wanawezaje kuja majumbani tulipo na kutupatia elimu kila kata kama hawajaletewa fedha na wafadhili kama wanavyotuambia,ni uongo hawa wanakula fedha kupitia migongo yetu,ni bora hata madawa haya tusiyatumie kwa sababu yanahitaji kula,”alilalamika mmoja wa wagonjwa ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.

Mmoja wa viongozi wa asasi ambayo hakupenda kutaja jina lake alisema tayari asasi zilishatiliana saini katika mkataba wa kukubaliana kuwapatia fedha lakini hadi sasa wamelipwa awamu moja ambayo ilitakiwa waipate tangu mwaka 2009 lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida wamelipwa kuanzia mwenzi mei,juni, na agosti,2010.

“Afadhari tusingesaini mkataba na sheria inasema ukivunja mkataba utashtakiwa sasa leo tuwashtaki wamarekani kwa kukiuka mkataba?,mama mmoja alikuja juzi huku analia njaa hata nauli hakuwa nayo huku ameandikiwa na daktari apewe lishe na sisi hatuna yeye ni mgonjwa wa BMI lakini hata mfukoni hatuna cha kumpa,”alisema.

Alisema kuwa kutokanma na hali hiyo hali imekuwa ngumu na watu wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi hawaamini kama tatizo siyo lako kutokana na ahadi walizowahi kuwapatia kuwa wafadhiri walikubali kuwatumia hatua iliyofikia hata wahudumu na wafanyakazi wa Asasi hiyo kufukuzwa na matusi juu wanapowatembelea wagonjwa majumbani.

Mwenyekiti wa mtandao wa Mbeya HIV aids Padre Johnathan Mwashilindi, akizungumza na mwandishi wa habari hizi amekiri kuwepo kwa tatizo hilo kwa mara ya kwanza tangu waanze kusaidiwa na serikali ya Marekani kupitia wasimamizi wao Water reed na hasa kwa upande wa wagonjwa wa huduma za majumbani katika asasi zote 22 zilizopo katika mtandao huo.
Amezitaja asasi ambazo zimekumbwa na adha hiyo na mahali zilipo katika mabano ni pamoja na Caritas Mbeya,Anglikan,Shidepha+,Ok Tree,Seta,IRTF,Kihumbe na TPDF Mbalizi (jijini Mbeya),Hospitali ya misheni ya Mbozi,ABC Tunduma na Shidepha+ Mbozi (Mbozi),Hosana (Ileje),CSDO na Fedea (Chunya),Shidepha+Mbarali,TAG na SKIMMVU (Mbarali),LCCB na Igogwe Hospitali (Rungwe) na Usaka,Mango Tree na John Hus (Kyela)

Padre Mwashilindi alisema kuwa walifikia hatua ya kulazimika kukopa fedha kwa ajili ya kuondoa aza waliyokuwa wanakabiliana nayo watoto ya kufukuzwa mashuleni kutokana na kukosa ada na kuwapatia vifaa muhimu vya shule ambapo fedha zilizotumwa hivi karibuni zinatumika kwa ajili kurejesha madeni waliyokopa.
Alisema asasi nyingi zimeshindwa kukopa kutokana na kushindwa kulipia riba kwa sababu mikopo mingi ina masharti ya kulipa riba na wao hawafanyi biashara bali wanatoa huduma

Hata hivyo Padre huyo alisema baada ya kuwasiliana na wasimamizi wa Mradi huo unaosimamiwa na Shirika la Water Reed kutoka nchini Marekani wamesema kuwa tatizo kubwa ni kuchelewa kupitishwa kwa bajeti ya Wizara ya afya nchini Marekani.

Mwisho.

Thompson Mpanji