Translate

Saturday, March 15, 2014

Wanawake ni wadau wakuu wa maendeleo endelevu!



Wanawake ni wadau wakuu wa maendeleo endelevu!


Kardinali Osca Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa anasema, Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2014 inalenga kutambua uwezo wa wanawake katika mchakato wa maendeleo endelevu sanjari na kutafuta suluhu ya ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani. Wanawake sehemu mbali mbali za dunia wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia mustakabali wa maendeleo ya familia na jamii zinazowazunguka.

Wanawake wakiwezeshwa wanaweza kuchangia katika maendeleo endelevu ya Jumuiya ya Kimataifa. Caritas Internationalis kwa kushirikiana na Mfuko wa Fidel Gotz, katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, watatoa jumla ya Euro elfu kumi kwa makundi mawili: Kundi la kwanza ni lile linalotekeleza miradi inayofadhiliwa na Caritas Internationali na sehemu ya pili, Mashirika mengine ya misaada yanayojipambanua kwa kuwajengea uwezo wanawake uwezo kiuchumi. Tuzo hii itatolewa hapo tarehe 16 Oktoba 2014 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani.




Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: TAMKO



 Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: TAMKO

Tamko “matumaini na furaha ya watanzania kwa ujio wa Rasimu ya katiba iliyosheheni utu na misingi ya kujali maslahi ya wote”

Mkutano wa kitaifa wa wajumbe wa kamati za majimbo za Haki na Amani za Kanisa Katoliki Tanzania pamoja na Wanataaluma Wakristo wa Tanzania (CPT), walikutana kwenye Kituo cha kiroho cha Mbagala, Jijini Dar es Salaam, tarehe 5 – 6 Februari, 2014.

Wakitafakari juu ya mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wajibu wa Kanisa Katoliki katika Utume wake wa Kinabii wa kulinda na kujenga haki na amani nchini mwetu, walimshukuru Mungu kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya uwenyekiti wa Jaji Joseph Sinde Warioba, kufanikiwa kuwasilisha rasmi Rasimu Na. 2 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 30 Desemba, 2013 na kuashiria mwanzo wa hatua ifuatayo ya kuunda Bunge Maalumu la Katiba.

Baada ya kuipitia Rasimu hiyo kwa kuongozwa na uchambuzi makini uliowasilishwa na Sekretarieti ya Tume ya Haki na Amani wajumbe wameridhia kwamba :



Kwa hakika Rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni ya watu na sio ya wanasiasa au vyama vya siasa wala asasi za kidini. Kwa sababu hiyo tunatoa mwaliko kwa kila raia wa Tanzania kufurahia ushiriki wake kufikia Rasimu Na. 2 yenye mambo bora yatakayokuwa nguzo ya umoja wa nchi yetu katika Katiba Mpya.

Maadili yaliyomo katika Rasimu Na. 2 ni muhimu kabisa kwa taifa letu.
Wananchi na viongozi wote sharti wajali maslahi kwa wote na wasimamie haki na wajibu wa kila mtu.

Madhumuni ya msingi ya Katiba ni ustawi wa kila Mtanzania, haki za kiuchumi, usalama, kusikilizwa kabla ya kuhukumiwa na haki kwa wote pasipo ubaguzi kwa madhumuni ya kulinda amani.

Katiba yetu lazima isiruhusu wachache wenye nguvu za kisiasa, kiuchumi na kiutawala kutumia vibaya uwezo wao na kusababisha utengano kitabaka katika jamii huku wakijinufaisha kwa kutumia rasilimali za nchi zilizo za wote. Pawepo na udhibiti thabiti wa mienendo ya namna hiyo na uwajibishaji makini kwa wabadhilifu wa mali ya umma.

Katiba ni chombo hai kwa ajili ya kuhudumia jamii na sio jamii kuhudumia Katiba. Kwa sababu hiyo yatupasa kuthubutu kubuni njia mbadala ili kukuza kipato cha raia wa kawaida na kuboresha huduma za jamii kwa kuwa na mipango endelevu ya kiuchumi.

Pendekezo la Muundo wa Muungano wa serikali tatu sio jambo kuu kuliko mengine yote katika Rasimu hii. Muundo wa serikali mbili haukutatua matatizo msingi bali ulilimbikiza kero zilizosababisha Zanzibar kujiundia katiba yake mpya ya mwaka 2010 bila kushauriana na Tanzania Bara (Tanganyika). Pendekezo la serikali tatu lililowekewa mazingira tekelezi yakitoa mwanya wa kuboresha muundo huo kwa njia wazi, shirikishi na za kidemokrasi lina tija kubwa ya kuturudishia hali ya kuwa wamoja.

Mihimili mikuu mitatu; Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Bunge la Jamhuri ya Muungano na Mahakama ya Jamhuri ya Muungano ni taasisi mpya kabisa kwa mujibu wa Rasimu Na. 2 zitakazoongoza, kuratibu na kuwajibisha kila kiungo cha Jamhuri ya Muungano zikiwemo serikali za Nchi Washirika.

Haki ya mtu ya kuishi lazima ilindwe na Katiba kuanzia pale mimba ya binadamu inapo tungwa katika mama na katika hatua zake zote za kumhudumia mama mjamzito.

Kumtambua Mungu na kumtaja katika Katiba yetu kunamaanisha kukiri kwetu Uwepo Wake aliye Muumba wetu na vitu vyote ambavyo mwanadamu anavitegemea kwa uhai wake. Mungu anakuwa rejelea yetu katika kuheshimiana kiutu. Ni chimbuko la utu wa binadamu. Kwa kuwa katika Wimbo wetu wa Taifa tunamwomba Mungu baraka zake ili tufanikiwe na tuishi kwa amani, ni hekima na busara kumkiri katika Sheria Mama – Katiba.


Tunapoelekea kwenye Bunge Maalum la Katiba tunataka mambo yafuatayo ya msingi kabisa yatambuliwe na kufahamika kwa wote:
Watanganyika na Wazanzibar tuwe na nia madhubuti ya kuwa wamoja.

Haki za binadamu za kisiasa, kiuchumi na kijamii zipatikane na kufurahiwa na wote. Umasikini na ufinyu wa bajeti ya serikali ni visingizio tu vya mamlaka kutokutoa haki kwa wote.

Yatupasa kukiri mapungufu yetu katika serikali zetu na itikadi za kisiasa kusudi kwa moyo wa unyenyekevu na mkunjufu tuanze safari mpya katika mwanga mpya wa maridhiano. Pamoja na kukiri kasoro za wakati uliopita tujivunie maendeleo tuliyofanya katika kila nyanja za maisha wakati tukiboresha mifumo na miundo ya utawala.

Ulimwenguni hakuna katiba yoyote kamilifu. Yatupasa tuanze na Rasimu iliyopendekezwa na tuendelee kuiboresha pale itakapobidi.

Tunawasihi wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuweka kando itikadi za vyama vyao kama walivyofanya Wanatume wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika kuandaa Rasimu Na. 2. Bunge Maalum la Katiba lilenge kufanikisha mchakato mwema wa Katiba Mpya itakayoandaa njia na mifumo mipya ambayo kwayo tutahakikishiwa kuwepo kwa taratibu wajibishi na wajibikaji ili kuendeleza ustawi wa jamii na muundo wa Muungano utakaokuwa wazi na tayari wakati wote kuboreshwa kwa manufaa ya Watanzania wote.

Katiba Mpya ya Tanzania itakuwa na fursa ya “FURAHA MPYA SHIRIKISHI” kwa Watanzania wengi. Rasimu na. 2 ni hatua njema katika tukio muhimu la kihistoria nchini tanzania. Tunatarajia bunge maalum lisimkane Mungu na lisikashifu mapendekezo ya serikali tatu.


Tunawaalika wananchi wote wa Tanzania kwa dhamira moja, kuliombea na kulisaidia Bunge Maalum la Katiba, liweze kufanya kazi yake kwa ustadi na kujali maslahi ya Taifa na wananchi wote wa Tanzania.



Askofu Mkuu Paulo Ruzoka
MWENYEKITI
Tume ya Haki na Amani - TEC

Maoni ya tume ya haki na amani Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuhusu rasimu ya Katiba Mpya




 Maoni ya tume ya haki na amani Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuhusu rasimu ya Katiba Mpya

Yafuatayo ni maoni ya jumla ya rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyotolewa na Tume ya Haki na Amani Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Chama cha Wanataaluma Wakristo Tanzania, CPT.
A: Utangulizi
Rasimu Na. 2 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitolewa na kuwasilishwa rasmi kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 30 Desemba, 2013. Inawezekana kwamba, hadi sasa, si wote tumepata fursa ya kuipitia angalau mara moja Rasimu hiyo. Nia ya andiko hili ni kutoa maoni ya jumla juu yake. Maoni haya yameandaliwa na Sekretariati ya Tume ya Haki na Amani ya TEC kwa kuzingatia tafakari na uchambuzi makini uliofanywa na Christian Professionals of Tanzania (CPT).
B: Tuliyohimiza, Kuonya na Kutahadharisha Mwanzoni na Juu ya Rasimu Na. 1
Katika mapendekezo yetu ya mwanzo kabisa na yale juu ya Rasimu Na. 1, tulihimiza, kusisitiza, na wakati mwingine kuonya na kutahadharisha kiunyenyekevu lakini kwa makini na ufasaha wa maelezo, mambo muhimi yafuatayo, kati ya mengine:


Misingi thabiti na halali ya Katiba Mpya sharti iwe ni watu/utu, uhuru, haki, ukweli/uwazi na mshikamano vinavyojenga hali ya amani na maendeleo yao/yake: Wananchi kuwa na haki na uwezo zaidi wa kushiriki katika mambo ya maendeleo, uchumi na ya utawala wa nchi yao kihalisia moja kwa moja na kwa njia za uwakilishi.
Umuhimu wa masharti ya kikatiba juu ya maadili mema, uwajibikaji, uwajibishwaji na miiko ya viongozi na watumishi wa umma vikiendana na chombo (Tume) au maelekezo na masharti muafaka ya utekelezaji wake kwa mujibu wa sheria inayozingatia masharti ya Katiba Mpya.
Umuhimu wa umoja wa Taifa letu na uzalendo katika uongozi na utumishi wa umma kwa lengo la kutumikia vyema wananchi na nchi (vizazi vya sasa na vijavyo) kwa ujumla: Sera, malengo, mipango na sheria za Jamhuri ya Muungano na za Nchi Washirika kutakiwa na Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano kuzingatia maslahi ya nchi na wananchi walio wengi na hasa wale walio katika hali hatarishi ya umaskini uliokithiri na jumuiya/makundi yenye vipato vya chini na kufuata katika utekelezaji wake maelekezo na masharti ya Katiba hiyo ya Jamhuri ya Muungano.
Umuhimu wa haki za binadamu zilizopanuliwa na kuboreshwa kwa kuzingatia maadili mema na bila kukiuka sheria ya kimaumbile, ambazo yapasa zitekelezeke pasipo mikwara ya kisheria inayokinzana na nia na madhumuni msingi ya Katiba na inayoacha mianya ya dola/uongozi kukwepa uwajibikaji na uwajibishaji; umuhimu wa kuimarisha haki ya mtu kuishi tangu kutungwa mimba, masharti ya kufuata na kuendesha mambo ya kiimani/kidini pasipo kutumia njia hasi dhidi ya imani/dini za wengine; nk.
Umuhimu wa Katiba Mpya kukomesha tatizo la Katiba na sheria kutoa kwa viongozi na watumishi wakuu Serikalini mamlaka yasiyo na misingi, vigezo, taratibu wala mipaka ungozi na muafaka ya kufuata katika utekelezaji wake au kutunga sheria/kanuni za kuelekeza na kuongoza utekelezaji huo.
Katiba Mpya kudhibiti mamlaka na madaraka (yasiyo na vigezo, taratibu wala kikomo katika utekelezaji wake isipokuwa busara na hekima kama sio hurka) ya Rais: Kwamba katika kutekeleza madaraka hasa ya kuteua na kuwajibisha kinidhamu viongozi wa juu Serikalini na katika utumishi wa umma, hatua za awali zichukuliwe na kukamilishwa na vyombo wakilishi na shirikishi vya umma vilivyoundwa na vinavyofanya kazi kwa mujibu wa ama Katiba Mpya au sheria inayotimiza maelekezo na masharti ya Katiba hiyo – likiwemo Bunge. Kazi ya Rais iwe ni kurasimisha yaliyofanywa na vyombo hivyo husika kwa misingi bora kimaadili.
Kwamba Idara ya Mahakama iwe na haki ya kuwasilisha makadirio yake ya mapato na matumizi ya mwaka moja kwa moja Bungeni kama Mhimili unaojisimamia ili kuimarisha uhuru wake, hadhi yake na utawala wa kisheria nchini; na utaratibu wa kuteua majaji na viongozi katika Mhimili huu ufuate mapendekezo kwenye kifungu cha 6 hapo juu.
Kwamba na maeneo mengine ya utumishi wa umma kama Bunge, ulinzi na usalama, polisi, utawala, maadili na uwajibikaji wa uongozi na watumishi wa umma, usimamizi na uhakiki/udhibiti wa fedha za umma na mambo ya vyama vya siasa yawekewe utaratibu wa kifetha na kuteua viongozi na watumishi waandamizi wake unaofanana na ule unaotajwa kwenye kifungu cha 7 hapo juu.
Tangu mwanzo, suala la Muungano tulilichukulia msimamo wenye mambo ya kimsingi matatu :

Muungano wetu una mizizi mirefu ya kihistoria - kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni -ikiwemo miaka hamsini (50) ya Jamhuri ya Muungano pamoja na magumu na changamoto zake kubwa na ndogo.
Umuhimu wa kuzingatia ukweli kwamba wananchi wengi wa Bara na Zanzibar-Pemba ni maskini au wa kipato duni kisichokidhi mahitaji. Hivyo, wanachohitaji ni maendeleo kutokana na rasilmali ya sehemu hizi mbili, nyingi zikiwa Bara: Muungano sharti ulenge kuleta maendeleo yao na Taifa, si kuwapa wachache (watumishi wao) madaraka na uhondo wa uhuru; sharti uwe ni wa manufaa kubwa kwa maendeleo ya Wananchi wote wa enzi hizi na wa nyakati na vizazi vijavyo.
(i) Muungano wa aina ya serikali mbili umeghubikwa na matatizo mengi ambayo hayajawahi kujadiliwa na kutatuliwa kwa njia halisi na muafaka za kidemokrasia: Lakini hiyo si sababu ya kutamani kurudi nyuma bali ni sababu ya kupiga moyo konde na kutafuta suluhu inayoimarisha, siyo inayoyumbisha, Muungano katika misingi yake ya ‘umoja ni nguvu utengano ni udhaifu’;

(ii) Dhana ya ‘Serkali tatu’ tangu mwanzo ilionekana haifai kwa sababu ya gharama, udogo wa mmoja wa nchi Washirika, na sababu hii ya pili, pia, ilifanya dhana ya ‘Serikali moja’ isitumike kwa hofu ya nchi hiyo ndogo kumezwa; na
(iii) CPT na Kanisa zima (kupitia TEC) mwanzoni tulipendekeza dhana ya ‘Serikali moja’ kwa njia ya mchakato endelevu wa mjadala na maafikiano juu ya mambo muhimu ya Muungano usio na kikomo cha muda bali wenye nia thabiti na lengo mahsusi la umoja kwa misingi muafaka ya kidemokrasia. Hivyo, muundo wa Serikali mbili ungeendelea kurekebishwa huku, pia, mambo ya Muungano yakiendelea kuongezwa au kuboreshwa kwa nia na misingi hiyo. Ingawa kwenye mapendekezo yetu (CPT-TEC) juu ya Rasimu Na. 1 tulitoa mawazo yetu juu ya muundo uliopendekezwa na Tume ya Kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuliendelea kuonya na kusisitiza juu ya athari mbaya za muundo huo kwa mustakabali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Umuhimu wa Serikali kuwa ya kisekula (kutokuwa na dini teule) au kuruhusu masuala ya kidini katika utawala wa nchi (Jamhuri ya Muungano na Nchi Washirika); kutoruhusu mahusiano na nchi nyingine au taasisi kama OIC yanayoilazimu nchi au Serikali yetu kuvunja kanuni msingi hii ya usekula.


C: Ulinganisho kati ya Tuliyohimiza, kuonya na kutahadharisha na Maudhui ya Rasimu Na. 2
Kwa kiwango kikubwa, mambo yaliyotajwa katika vipengele Na. 1 – 8 na 10 yamezingatiwa katika kuandaa Rasimu Na. 2, ingawa bado mtu angependa uboreshaji wa hapa na pale. Lakini tunajua kuwa si kila tulilolipendekeza na hata kwa msisitizo lingechukuliwa au kuwekwa kwa namna inayokithi matazamio na mapenzi yetu; kwani pia yalikuwepo mapendekezo ya makundi na jumuiya nyingine ambazo mawazo na mapendekezo yao ama yalikuwa yanafanana au yanatofautiana, au hata kukinzana, na yale ya kwetu.

Tukipitia kila kipengele na kulinganisha tuliyopendekeza juu ya Rasimu Na. 1 na yaliyomo katika Rasimu Na. 2 tutaona mara moja yaliyochukuliwa kwa namna moja au nyingine hapa na pale na yaliyoachwa kabisa. Hapo, tujiulize ni yepi kati ya yale yaliyoachwa kabisa yatupasa tuendelee kuyasisitiza na ni yepi tuyaache kwa awamu hii ya mchakato wa kuunda Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mifano michache, kati ya masuala ambayo bado yanaibua maswali ndani ya Wakatoliki na watu wengine wenye mwelelekeo wa mawazo unaofanana na wa Kanisa Katoliki, ni kama ifuatavyo:
kulinda haki ya uhai tangu kutungwa mimba kwa mtu;
kutajwa kwa “Mungu” angalau katika Utangulizi;
suala la mahusiano ya kimataifa kuwa ni sehemu ya mambo ya nchi za nje na hivyo kuwa la Muungano na kupunguza uwezekano wa Nchi Washirika kuwa na mahusiano yanayoweza kuimarisha utengano badala ya umoja hasa katika nyanja za kidini;
kukosa kanuni mahsusi ya kijumla ya kukomesha kikatiba tatizo la sheria na kanuni nyingi zinazotoa madaraka yasiyo na mipaka na wajibu usio na masharti fasaha na wazi ya taratibu, misingi, vigezo au adidu rejea na hatua za kinidhamu za kuchukuliwa dhidi ya wasiowajibika na wasiowajibisha ipasavyo kwa mujibu wa Katiba na/au sheria za nchi na, hivyo, kuacha mianya ya kukwepa uwajibikaji na uwajibishaji wa viongozi, watumishi, mamlaka na vyombo vya umma.
Kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jaji Joseph S. Warioba, wakati akiwasilisha Rasimu Na.2, suala lililoendelea kuitesa Tume hiyo hadi mwisho ni lile la Muungano. Sisi pia na wengine wengi nchini lilitutesa na litaendelea kuibua hisia za mashaka: Picha inayotoka ni kwamba moyo wa Watanzania wanaodaiwa na Tume kuwa pia ni wengi kipindi hiki ni wa kuwa na muungano dhaifu wa aina ya Shirikisho si ya kuimarisa na kuendeleza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa nchi huru mbili, Tanganyika na Zanzibar, zilizojivua utaifa wa kila mojawapo ili kuunda Taifa kubwa zaidi na lenye umoja, na hivyo, nguvu zaidi kuliko kila mojawapo ingebaki katika hali yake ya awali ya utengano.


Huu, kama tulivyoonya na kutahadharisha awali, ni moyo wa kuelekea kwenye kutengana si kuungana zaidi. Hapa, yatupasa Watanzania wote tujiulize maswali yafuatayo na tuyatafakari kwa makini:
Je, Rasimu Na. 2 imejaribu vipi kupunguza kasi ya kuporomoka kwa umoja wa kitaifa unaotegemezwa kwenye misingi haba saba (7) iliyobaki?
Na je, yale yaliyopendekezwa yakipita vema kwenye mchakato wa ridhaa ya Wananchi wa Tanzania na kukubaliwa, mustakabali wa Muungano utasimama na kuhakikishwa kwa misingi hiyo?
Au, je, kama baadaye Nchi Mshirika mojawapo ikitafuta uhuru zaidi kama si kujitoa kabisa katika Muungano, ile misingi iliyobaki au itakayorekebishwa kukidhi ukiukwaji uliofanywa dhidi ya Katiba ya sasa, itaweza kuhimili udidimiaji wa moyo wa kuuthamini umoja na kujenga hali na mazingira ya uongozi na wananchi kuona hatari na hasara za utengano?
Je, tuko tayari kuona umoja wetu unasambaratika kama ilivyotokea na inavyotishia kwingineko Barani Afrika [Sudan, Ethiopia, DRC, Libya) na hata nje ya Afrika (USSR,Yugoslavia, Czechoslavia, Muungano wa Kifalme wa Uingereza (UKoGB) ambako Scotland na North Ireland zinatishia kujitenga na kuwa nchi huru kabisa, nk.]? Tutajiepushaje hali ya kujikuta tunakabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu ya tabia na mazoea hatarishi ya kutotumia njia adili za kuendesha masuala muhimu na nyeti ya kitaifa likiwemo la Muungano?

Sababu zinazotolewa za kuendeleza utengano zina asili gani, ya matakwa ya uhuru na maendeleo ya kweli ya wanyonge au ya wenye (uchu na/au) malengo ya madaraka, maslahi binafsi na ya kitabaka yanayokuzwa na kufanywa maslahi ya kitaifa na ya umma?
Je, katika Awamu hii ya IV ya utawala ndani ya Muungano, Muungano una mtetezi katika Dola kati ya wale waliokula viapo kuulinda na kuutetea na, kama wapo, inakuwaje hatujawahi kuwaona au kuwasikia wakijitokeza kidhati na kwa hoja makini -

kuutetea kwa hoja makini ya kudhihirisha faida zake ambazo yapasa ziimarishwe, kulindwa na kuendelezwa kwa manufaa na maslahi zaidi ya kizazi kilichopo na vijavyo?
kuhusu athari za kudhoofika na/au kuvunjika kwake kwa umma wa Watanzania wa kizazi hiki na vizazi vijavyo?
Zinzoelezea jitihada na hatua thabiti na za dhati za kushughulikia mambo na masuala ya Muungano kwa njia za kidemokrasia zilizo adili na makini, shirikishi na wakilishi kwa ngazi za Wananchi na za Serikali?

Tume ya Jaji Warioba imeshindwa kujibu hoja yetu (CPT) ya kubainisha kiyakinifu faida na athari za Muungano ambazo watu waliohojiwa walizitoa licha ya kuorodhesha, pasipo ulinganifu na faida, kero zilizoelezewa (na wawakilishi? wa) pande mbili (Nchi Washirika) za Muungano.
D: Yaliyo Bora na ya Kuhofia Kimaadili na kwa Mustakabali wa Umoja wa Kitaifa Katika Rasimu N. 2
Ya Kuhofia Kimaadili na kwa Mustakabali wa Umoja wa Kitaifa
Kuna mambo matatu muhimu ya kutafakari pamoja kwa njia ya kujiuliza maswali hasa baada ya kuyasikia na kuyasoma yaliyotolewa taarifa na yaliyopendekezwa na Tume ya Kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Tume ya Jaji Warioba). Nayo ni kama ifuatavyo:-
Jambo la kwanza na kuu kati ya mengineyo yanayotia wasiwasi kimaadili na ya kuhofia kwa mustakabali wa umoja wa Taifa letu ni kwamba Tume ya Jaji Warioba imelazimika kupendekeza mfumo/muundo wa Muungano wa serikali tatu badala ya mwendelezo wa serikali mbili kwa sababu hasa ya kuzingatia hali halisi ya sasa ndani ya Muungano: Kwamba mojawapo ya Nchi Washirika (Zanzibar) iliishafanya mabadiliko ya Katiba yake kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vile kwamba haiwezekani hata kufikiria kuendeleza mfumo wa sasa wa Muungano wa serikali mbili ambao vilevile umenung’unikiwa kwa muda mrefu kutokana na kinachoitwa “kero” nyingi za mfumo huo wa serikali mbili. Maana yake ni kwamba tunalazimika kufumua muundo wa sasa pasipo Nchi Washirika kwa pamoja na kwa njia muafaka kujiandaa na kukubaliana kwanza juu ya hatua hiyo kwa sababu mojawapo wa Nchi Washirika imeishajichukulia madaraka tayari ya kuufitinisha na kuubatilisha kwa kufanya mabadiko kadhaa makubwa katika Katiba yake kinyume cha masharti ya Katiba kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyouweka muundo huo.


Hofu na wasiwasi unaojitokeza kihalali kabisa ni kama bado kuna moyo thabiti wa kuendeleza Muungano! Je, kilichotokea kinaashiria kwa upande wa uongozi wa Nchi Washirika zote mbili utamaduni wa dhamira na maadili ya umoja au ya ulegevu na udhaifu wa moyo unaoleteleza utengano? Uongozi wa Muungano unathamini na uko makini kwa kiwango gani kuhusu masuala muhimu na nyeti ya kitaifa?
Jambo la pili la kuhofia kimaadili na kwa mustakabali wa umoja wa Taifa letu linatokana na hilo la kwanza: Nalo ni kama Muungano wa aina ya Shirikisho unaopendekezwa umewekewa misingi ya kutosha katika Rasimu Na. 2 ya Katiba ya Jamhri ya Muungano ya kuhakikisha kwamba kilichojiri kwa muundo wa sasa hakitajirudia chini ya mfumo huo unaopendekezwa? Katika hali ya udhaifu wa dhamira na maadili ya umoja wa kitaifa kwa uongozi, kitakachozuia utovu kwa Nchi Washirika au mojawapo kudiriki kwenda njia yake machoni pa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ni nini? Rasimu ya Katiba Na.2 inajibu vipi swali hili na jibu hilo linatosheleza kuondoa wasiwasi huo na hofu hiyo?

Jambo la tatu na la mwisho kwa mada hii ni la Watanzania kujiuliza kama Katiba ya sasa au ile inayopendekezwa na Tume katika Rasimu N. 2 na hata ya aina nyingine yoyote ile tunayoweza kuibuka nayo mwishoni mwa mchakato wa sasa wa kuunda Katiba Mpya inaweza kujibu na kukidhi mahitaji, matakwa na matumaini yetu yote ya kikatiba? Je, tunaweza kufikia hatua ya kusema kwa pamoja kama Wananchi na Taifa bila kuwa na ngawanyiko wowote kwamba sasa tunayo Rasimu ya Katiba aina ya mfano bora kuliko zote na ambayo ni muafaka kwa kila mmoja wetu katika Nchi Washirika? Je, kuna nchi yoyote duniani ambayo ina katiba kama hiyo?

Je, mjadala juu ya ni kipi kilicho bora kwa wananchi na nchi leo na baadaye kikatiba unaweza kufikia kikoma au ukamilifu au kusitishwa na nguvu yoyote ya kimaumbile? Je, hofu na wasi wasi wetu wa sasa kimaadili na kwa mustakabali wa umoja wa Taifa letu iwe ni sababu ya kutopokea kwa moyo mkunjufu kile kinachoweza kunusuru dhamira na maadili ya umoja katika hali iliyobadilika kihalisia?

Mlolongo huu wa maswali unadai sehemu ya majibu na ni hiyo tunayogeukia hapo chini. Lakini nia si kujibu kila mojawapo ya hayo maswali, kwani mengi yanaonyesha mwelelekeo wa kutohitaji jibu mahsusi. Nia ni kuona kama Rasimu Na. 2 ina maudhui ya mambo bora yanayoweza kuendeleza umoja, kuimarisha mahusiano, mshikamano na kuleta maendeleo kwa wananchi ndani ya Shirikisho la Nchi Washirika.

Kama yapo, swali ni kama yanaweza kuboreshwa na hivyo kutuwezesha kama Taifa, katika kipindi hiki kigumu cha majaribu, kuvuka au kuyakabili magumu hayo kijasiri na hivyo kuendelea kukomaa zaidi kitaifa kutokana na mchakato endelevu wa tafakari, mjadala na maamuzi muafaka ya kidemokrasia kila inapowezekana au kuonekana ni bora kufanya hivyo kwa ajili ya maendeleo na amani ya wananchi na nchi yetu.

Kuna busara kubwa na unabii katika usemi : ”Yaliyopita si ndwele; tugange yajayo!” Tusije tukajitia hatiani kwa kosa la ‘kuifanya migumu mioyo yetu’ na hivyo kushindwa kuzing’amua tunu zilizowasilishwa mbele yetu katika Rasimu Na. 2 pamoja na changamoto zake Rasimu hiyo.
Basi tuangalie kama Rasimu Na. 2 imetuwekea misingi bora ya kuweza kuganga yajayo.

Yaliyo Bora Kimaadili na kwa Umoja wa Taifa
Yapo mambo kati ya maudhui ya Rasimu Na. 2 ambayo ni mazuri na muhimu kiasi kwamba yapasa tuyachukulie kama mambo msingi yanayobeba na yanaweza kudumisha na kuendeleza utamaduni, maadili na dhamira au moyo wa umoja wa nchi yetu Tanzania katika hali halisi ya sasa. K`wayo, katika mazingira ya umoja wa aina ya shirikisho, kuna uwezekano kwa Nchi Washirika (viongozi na wananchi wake) -
kuendeleza kidemokrasia mahusiano ya karibu kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni na kwa kutambua mema ya kushirikiana kwa namna hiyo zaidi na zaidi na magumu ya kufanya kinyume chake;
kutambua umuhimu wa kuheshimiana na kushirikiana kimshikamano kwa misingi iliyo bora na iliyowekwa kikatiba kwa maridhiano muafaka; na
kutambua na kuthamini vema tunu na rasilmali za kila Nchi Mshirika zinazoweza kutumika kwa manufaa zaidi kwa wananchi kwa kuongeza, kuimarisha na kuendeleza zaidi misingi ya mshikamano na umoja kisiasa, kiuchumi na/au kiutamaduni.

Kwa ajili ya hayo, ni muhimu tutambue mambo manne ya msingi zaidi kijamii kwa umoja wa Nchi Washirika katika aina yoyote ya muungano au mashikirikiano: Mambo hayo hudhihirika katika kiwango cha juu cha kufanana na kuzingatiwa katika nyanja nne (4) za maisha ya siku hadi siku. Na hayo mambo, pamoja na nyanja hizo, ni kama ifuatavyo:
(a) Utamaduni (lugha, maadili, mila na desturi na historia ya pamoja ya mahusiano/ushirikiano wenye manufaa kwa Nchi/Wananchi Wahusika);
(b) Mifumo ya kisheria (Katiba, sheria na kanuni msingi);
(c) Miundo ya dola (wizara, idara, taasisi na asasi zake kuu na za kijamii); na, kubwa kuliko yote
(d) Moyo wa kuthamini umoja na ushirikiano kwa misingi thabiti na muafaka ya ‘toa na pokea’ (toa chako anachohitaji mwenzako ili nawe upokee chake unachohitaji kwake), uhuru, haki, ukweli na mshikamano kwa misingi ya kuheshimiana na kustahimiliana.
Mambo haya na nyanja hizi nne kati ya nyingine tukizitafakari na kuzijadili kwa makini tutagundua siri ya udumifu wa umoja, ushirikiano na mshikamano wa dhati wa madola, taasisi za kikanda na za kimataifa na hata kila dola na kila nchi iliyo na sifa au historia inayoashiria uwepo wa mambo hayo. Nyanja hizi zinawezesha mazungumzo na mjadala endelevu wa kuelekeza nchi ndogo au kubwa, moja au mbili na hata zaidi kwenye namna moja ya umoja au ushirikiano kutoka viwango vya chini hadi vya kileleni. Kwa uhakika, misingi hii hii inaendelea kusaidia dunia kujenga hali mpya ya mahusiano na ushirikiano wa kikanda na wa kimataifa pasipo wakati wote utumiaji wa mabavu, mauaji na maangamizi ya kivita.

Kwa kuzingatia maelezo hayo, tuangalie kwa kifupi, mambo yaliyo bora katika Rasimu Na. 2 yanayoweza kuwa ni nguzo za kuegemezea umoja na ushirikiano endelevu chini ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nayo ni kama ifuatavyo:
(1)Yale yote yaliyo kwenye Sura ya Kwanza hadi Sura ya Nne; yaani:
Jina, Mipaka, Alama, Lugha na Tunu za Taifa; Mamlaka ya Wananchi, Utii na Hifadhi ya Katiba;
Malengo Muhimu, Misingi ya Mwelekeo wa Shughuli za Serikali na Sera za Kitaifa;
Maadili na Miiko ya Uongozi na Utumishi wa Umma; na
Haki za Binadamu, Wajibu wa Raia na Mamlaka za Nchi (na Mipaka ya Haki za Binadamu).

Kati ya hayo, yale yaliyo katika Sura ya Kwana, Sura ya Pili na Sura ya Nne ni baadhi ya mambo sita (6) ambayo hayawezi kufanyiwa mabadiliko -
“hadi mabadiliko hayo yaungwe mkono na theruthi mbili ya wananchi wa Jamhuri ya Muungano kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano kwa Kura ya Maoni itakayoendeshwa na kusimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria za nchi”.
Masharti kuhusu Uraia wa Jamhuri ya Muungano yanafanya jambo hilo muhimu liwe na hadhi ya kikatiba, ambapo hadi sasa halikuwa la kikatiba bali la sheria ya kawaida iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Masharti kuhusu Serikali ya Jamhuri ya Muungano - Serikali, Rais, Makamu wa Rais na Baraza la Mawaziri pamoja na Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali hiyo - licha ya kuwa lina magumu na changamoto kadhaa za ‘’Shirikisho’’, lina uzuri wa kuendeleza dhana na siasa ya umoja na mshikamano wa kitaifa ndani ya Jamhuri ya Muungano-Shirikisho wa (Nchi Washirika) Tanzania.
Bunge la Jamhuri ya Muungano ni jambo kubwa lingine la kutilia maanani kama chombo kimojawapo cha kusaidia kuendeleza mjadala, mahusiano, sheria, kanuni na taratibu rasmi za umoja wa kitaifa katika hali iliyobadilika kikatiba kwenye muundo wa dola la Taifa na kupungua kwa mambo ya Muungano au umoja wa kitaifa.

Mahakama (ya Juu na ya Rufani) ya Jamhuri ya Muungano itakuwa chombo muhimu sana cha kujenga msingi mpya na kuimarisha misingi iliyodhoofishwa ya kisiasa, kiutamaduni na hata ya kiuchumi ya Jamhuri ya Muungano-Shirikisho. Masharti husika ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya sasa yanaunda Mahakama ya Jamhuri isiyo na madaraka juu ya raia na dola ya kuamua mashauri na kuwajibisha bali ya kushauri na kusuruhisha tu. Hata hivyo, hayajawahi kutekelezwa hadi leo. Masharti ya Katiba tarajiwa kwa Mujibu wa Rasimu Na. 2, yanaifanya “Mahakama ya Juu [kuwa] ni ngazi ya mwisho ya rufani katika Jamhuri ya Muungano ...”. Aidha, inatoa kwa Mahakama ya Juu hiyo madaraka ya–

(a) pekee na ya awali ya kusikiliza na kuamua mashauri yanayohusu matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhyri ya Muungano;
(b) kusikiliza na kuamua mashauri yatakayowasilishwa na wananchi, Serikali za Nchi Washirika kuhusu tafsiri au utekelezaji wa Katiba hii;
(c)usikiliza na kuamua migogoro baina ya Nchi Washirika na Serikali ya Jamhuri ya Muungano;
(d)kusikiliza na kuamua rufani kutoka Mahakama ya Rufani [ya Jamhuri ya Muungano];
(e)kutoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali za Nchi Washirika, pale itakapoombwa; na
(f)kusikiliza na kuamua shauri lolote litakalowasilishwa mbele yake kwa mujibu wa Katiba hii au sheria nyingine yoyote itakayoipa Mahakama hiyo mamlaka.
Vile vile “Mahakama ya Rufani pamoja na mahakama za Nchi Washirka, isipokuwa Mahakama ya Juu, zitalazimika kufuata maamuzi ya Mahakama ya Juu”.
Pamoja na hayo, Ibara ya 167(1) inaipa Mahakama ya Rufani mamlaka ya-
kusikiliza na kuamua kila rufani inayowasilishwa mbele ya Mahakama ya Rufani kutokana na hukumu au uamuzi wowote wa Mahakama Kuu za Nchi Washirika au Mahakama yoyote ya chini iliyopewa mamlaka maalumu ya kusikiliza mashauri ambayo kwa kawaida husikilizwa na Mahakama Kuu;
kufanya mapitio ya maamuzi ya Mahakama Kuu za Nchi Washirika au mahakama yoyote ya chini iliyopewa mamlaka kusikiliza mashauri ambayo kwa kawaida husikiliwa na Mahakama Kuu.

Jambo la Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano

Umuhimu wa jambo hili kwa kuendeleza umoja wa kitaifa katika hali iliyobadilika ni mkubwa na wa kimsingi kabisa. Kwa mujibu wa Ibara ya 1 ya Rasimu Na. 2, licha ya kwamba kinachopendekezwa ni Muungano wenye muundo wa Serikali Tatu, bado umoja wa kitaifa kikatiba utabaki kama hayo yote yaliyoelezwa tayari na yanayofuata hapa chini yanavyoashiria. Tukianza na hiyo Ibara ya 1:
(1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo limetokana na Muungano wa nch mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.
Aidha, chini ya Ibara ya 71 kuhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano,
(2) Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu na:
(a) atakuwa taswira ya Jamhuri ya Muungano na watu wake;
(b) atakuwa alama ya umoja, uhuru wa nchi na mamlaka yake; na
(c) atakuwa na dhamana ya kukuza na kuhifadhi umoja wa kitaifa.
Ibara ya 235(1) inatamka kuwa «jukumu la ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano ni la kila rai». Hata hivyo, Ibara ya 236 inaweka masharti kuhusu vyombo vya Ulini na Usalama wa Taifa:
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania;
Jeshila Polisi la Jamhuri ya Muungano; na
Idara ya Usalama wa Taifa.

Chini ya Ibara ndogo ya 236(4) na (5):
Mtu hataruhusiwa kuanzisha taasisi, kampuni, jumuiya au shirika linalohusiana na ulinzi na usalama wa Taifa au ushirika wa kijeshi, isipokuwa kama inavyoruhusiwa na Katiba hii au sheria za nchi.
Vyombo vya ulinzi na usalama wa Taifa vitakuwa chini ya mamlaka ya Rais.
Haya si mambo ya kubeza au kuchukuliwa kivyepesi bali kuyaona kuwa ni baadhi ya misingi ya umoja wa Taifa letu kusimamia na kusonga mbele katika hali mpya kikatiba, kisiasa na kiuchumi.
Jambo lingine bora ambalo ni kubwa na la msingi kimaadili na kwa mustakabali wa umoja wa Taifa ni masharti yanayohusu Tume (Huru), Mabaraza na Kamati mbalimbali zilizoundwa kikatiba kwa ajili ya maeneo na sehemu zote muhimu za utumishi wa umma. Hivi ni vyombo vyenye dhima ya kuweka kwa mujibu wa sheria misingi ya taratibu za uwazi, na iliyo shirikishi na wakilishi katika uteuzi wa viongozi wa juu na watumishi waandamizi wa umma na masuala husika ya kimaslahi na ya kinidhamu. Kwavyo, tatizo la Mhimili mmoja wapo (Serikali/Urais) wa Mihimili mitatu ya Dola kuwa na madaraka yasiyo na mipaka, misingi, vigezo na taratibu muafaka na wazi linaweza kudhibitiwa kwa kiwango kikubwa.

Tume hizo muhimu kwa majina ni kama ifuatavyo:
Tume Huru ya Uchaguzi ya (Jamhuri ya) Muungano;
Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali;
Tume ya Utumishi wa Bunge;
Tume ya Utumishi wa Mahakama;
Tume [Huru] ya Maadili na Uongozi na Uwajibikaji;
Tume [Huru] ya Haki za Binadamu;
Tume ya Utumishi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania;
Tume ya Utumishi wa Jeshi la Polisi.

Kamati za Muungano ni kama ifuatavyo:-
Kamati ya Uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi;
Kamati Maalimu ya Uteuzi [wa Viongozi na Watumishi Waandamizi wa Umma];
Kamati Maalimu ya Uteuzi wa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu;
Kamati ya Utekelezaji wa Katiba katika Muda wa Mpito.

Kuna Baraza moja la Muungano lililopendekezwa, nalo ni:
Baraza la Ulinzi na Usalama la Taifa.
Rasimu imependekeza miaka minne (4) ya Kipindi cha Mpito. Mauthui ya Ibara husika ni mazuri na kwa kiwango kikubwa yanakidhi mapendekezo yetu na bila shaka na ya watu na asasi nyinginezo zilizowasilisha maoni kwa Tume ya Jaji Warioba. Kamati maalumu ya kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano inayopendekezwa, pia, itashughulikia mapendekezo ya sheria muafaka mbalimbali zinazolengwa na Katiba Mpya hiyo pamoja na urekebishaji wa sheria nyingine zitakazoathiriwa na Katiba hiyo.


Kipindi hiki muhimu kitatoa fursa ya kwanza kwa Wananchi na viongozi wao kujipanga upya baada ya Katiba Mpya kupitishwa kulingana na masharti ya Katiba hiyo. Kitakuwa ni kipindi cha kuendelea kujadiliana, kutafautiana bila kuzozana na kukubaliana kwa misingi ya kidemokrasia na katika hali ya amani na utuluvu. Hii itatokea kama tutafanikiwa kukabili vema changamoto za mchakato kabla na wakati wa kuijadili na kuipitisha Katiba Mpya tarajiwa katika hatua za awali mbili zilizobaki, ya Baraza la Kutunga Katiba na Kura ya Maoni. Hivyo, pia, utakuwa ni wakati muafaka wa kutahini moyo wetu wa umoja na ukomavu wetu wa kisiasa kama Taifa.
TUOMBE MUNGU!

F: Hitimisho
Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 2013 ilitegemewa kuibua mjadala wenye msisimko wa aina yake; kwani umechangiwa mawazo, maoni na hata mapendekezo maalumu yaliyotolewa kwa mdomo, kwa maandishi na kwa njia nyingi mbalimbali zilizokaribishwa na Tume ya Jaji Warioba. Jambo moja la wazi tangu Rasimu Na. 1 kutangazwa ni la Wananchi kugawanyika katika makundi makuu manne.

Jambo hilo ni lile la muundo wa Jamhuri ya Muungano: Baadhi, wanapendelea muundo wa sasa wa Serikali mbili uendelee; baadhi, ule wa Serikali moja (mara moja, katika muda mfupi au, kimchakato, baada ya muda usiotabilika sasa), baadhi, ule wa Serikali tatu, kama Rasimu inavyopendekeza, na baadhi, Muungano wa mkataba. Haijulikani hatima ya mjadala huu kipindi hiki itakuwa nini au vipi: Je tutaibuka na Katiba Mpya au tutarejea kwenye Katiba tata ya sasa? Itakumbukwa kuwa tulijiuliza swali hili tangu mwanzo wa mchakato wa kushughulikia suala la Katiba Mpya chini ya Sheria husika na ya Tume ya Jaji Warioba; na bado linatukabili!
Lakini hali hii isitutishe wala kutupa wasiwasi kwani inaashiria jinsi watu walivyoamka kisiasa na kwamba kweli wanataka mabadiliko. Hata hivyo, mabadiliko hayo wanayotaka kwa dhati hayaashiriwi hasa na mawazo kuhusu muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Kwa kuichambua Rasimu kwa makini tumeona kwamba yako mambo yaliyo muhimu na ya msingi zaidi kimaadili na kwa maendeleo na mustakabali wa Taifa letu katika hali ya umoja kuliko inavyoonekana kijuujuu.

Cha kuhofia ni kama katika Nchi Washirika kuna moyo wa dhati wa umoja, hasa kwenye ngazi ya viongoi wa kisiasa, wa kuyathamini hayo yaliyo muhimu na ya msingi zaidi na kukubali ‘tugange yajayo’. Kuwania madaraka na umaarufu wa kisiasa, na hivyo, kuweka mkazo katika mambo ya kimuundo na kuhofia mabadiliko ya kimsingi katika mgawanyo wa madaraka ya kiutawala kunaweza kuteka mjadala na mchakato mzima. Hivyo, tusipokuwa makini, tunaweza kuingizwa au kujikuta tumesukumizwa kwenye bwawa la tope la malumbano na hoja zisizo na tija wala maslahi halisi kwa umma wa Wananchi pande zote mbili za Muungano.
Je, CPT na Mama Kanisa Katoloki chini ya TEC kwa ujumla wetu tuko tayari kusimama, kuungana na wengine wenye mapenzi mema na kutetea yote yaliyo bora, kushauri namna ya kushughulikia yanayotia hofu kwa njia adili na kuhadharisha umma, kukemea na kuonya, panapolazimu, kiadilifu? Wanaotaka kujenga nguvu ya hoja na sio hoja ya nguvu, tuwasikilize na tujadiliane pamoja kihoja.

Wale watakaoendekeza hoja ya nguvu, ya kulazimisha kimabavu, tuwakemee na kuwaonya ipasavyo kihoja vivile na kwa unyenyekevu wa moyo. Nyakati hizi ni za demokrasia, uwazi, kujenga mshikamano kwa ridhaa ya wenye mamlaka na Wananchi katika Nchi Washirika zote mbili kwa busara, hekima, unyenyekevu na ustahimilivu wa moyo mpana.
Kwa vyovyote vile na kama alivyoasa Mwadhama Policarp Kardinali Pengo kwenye mkutano wa Hija wa WAWATA majuzi, yatupasa tusali na kuomba Mungu atuepushe na janga linaloweza kutokea kutokana na kutengana kwa shari na chuki kwa kinachoitwa “kero za Muungano za muda mrefu”.

Tusisahau tahadhari na maonyo ya Hayati Baba wa Taifa, Julius K. Nyerere anayebezwa na kudhihakiwa na maadui wa umoja wa Jamhuri ya Muungano kwa maneno makali na mengi ya uzushi na ya kashfa. Aliyosema ni ya kinabii: dhambi ya kubaguana kwa misingi ya Utanganyika na/au Uzanzibari inaweza kuzaa balaa la wananchi na uongozi baguzi kubaguana ndani kwa ndani ya Nchi Washirika au Nchi Mshirika itakayoitenda dhambi hiyo kwa hasara na madhara kwa wote, Wananchi na Nchi Washirika. Hivyo, hata kama mtenda dhambi hiyo ni mojawapo ya hizo Nchi Washirika, madhara yake yataathiri vibaya Nchi Washirika zote mbili kutokana na jinsi zilivyo kijamii!

Sunday, March 2, 2014

Mtambo wa kuhakiki na kusimamia mawasiliano ya simu wazinduliwa Tanzania




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, Alhamisi, Februari 27, 2014, amezindua Mtambo wa Kuhakiki na Kusimamia Mawasiliano ya Simu (Telecommunications Traffic Monitoring System –TTMS) katika sherehe fupi lakini ya kufana iliyofanyika Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mjini Dar Es Salaam.

Mtambo huo unalenga kuhakiki na kusimamia mawasiliano ya simu zinazoingia nchini kutoka nje ya nchi kwa kubaini jinsi matumizi ya simu yanavyofanyika, kubaini bei zinazotozwa na faida inayopatikana pamoja na kuihakikishia Serikali mapato yake stahiki.

TCRA imeupata mtambo huo wenye gharama ya dola za Marekani milioni 25 bila kuununua moja kwa moja. Mtambo huo umenunuliwa na kufungwa na Kampuni ya SGS ya Uswisi ikishirikiana na Kampuni ya JVG ya hapa nchini. Kampuni hiyo itausimamia na kuuendesha mtambo huo kwa miaka mitano chini ya utaratibu wa “Jenga, Endesha na Hamisha – Build, Operate and Transfer”kipindi ambako itaweza kurudisha gharama zake kabla ya kuukabidhi kwa TCRA.

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma amemwambia Rais Kikwete katika sherehe hizo kuwa ufungaji wa mtambo huo hautaongeza bei ya mawasiliano kwa watumiaji wa simu. Badala yake, amesema Profesa Nkoma, Serikali itanufaika kwa kupata kiasi cha dola za Marekani milioni moja kwa mwezi ikiwa ni gawio lake kutokana na faida itakayotokana na mtambo huo mpya.

Tayari TCRA imekwishakabidhi kwa Serikali dola milioni moja za mwezi uliopita na katika sherehe ya leo, Profesa Nkoma ameikabidhi Hazina mfano wa hundi yenye thamani ya sh 1,684, 357. 283 (sawa na dola milioni moja) kwa mwezi wa Februari. Amesema kuwa fedha yake tayari imewekwa kwenye Akaunti ya Mfuko wa Hazina.

Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Rais Kikwete ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya mawasiliano katika miaka tisa iliyopita na jinsi gharama za mawasiliano zilivyopungua katika kipindi hicho kutokana na hatua mbali mbali zilizochukuliwa na serikali na hasa ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa. Amesema kuwa matumizi ya simu yameongezeka kutoka laini za simu milioni 3.6 mwaka 2005 hadi kufikia laini milioni 28 mwishoni mwa mwezi uliopita wakati watumiaji wa Internet wameongezeka kutoka milioni 4.9 mwaka 2011 hadi kufikia milioni tisa wa sasa.

Kuhusu gharama za simu, Rais amesema kuwa gharama hizo zimepungua kwa asilimia 57 kati ya mwaka 2009 na 2013 kwa upande wa simu wakati punguzo hilo kwa upande wa internet ni asilimia 75.

Makumi ya wanafunzi wa shule ya sekondari ya Yobe waua- Nigeri

a



Msemaji wa Tume maalum ya kijeshi katika mji wa Yobe, Kaskazini mwa Nigeria , amethibitisha uwepo wa shambulio la kighaidi, lililoua wanafunzi 29 wa Shule ya Sekondari ya Buni Yadi, Yobe, Kaskazini mwa Nigeria, usiku wa manane, Jumatatu kuamkia Jumanne, wakati wanafunzi hao wakiwa wamelala katika mabweni yao.


Msemaji wa Tume ya Kijeshi katika eneo hilo, Lazaro Eli , Jumanne alithibitisha habari hizo, bila ya kutaja idadi ya majeruhi, kwamba watu wasiojulikana, wanaodhaniwa kuwa wana kikundi wa Boko Haram,walifungulia risasi za moto kwa hosteli ya wanafunzi ya Yobe. saa nane za usiku kuamkia Jumanne.

Boko Haram wanatuhumiwa pia Septemba mwaka jana, katika mkoa huo, kufanya shambulio la kighaidi lililo ua wanafunzi 40 katika Chuo cha Kilimo cha Gujba .
Pia , mapema mwezi Julai mwaka jana , Boko Haram, walifanya mashambulizi kwa wanafunzi wa Sekondari ya Serikali , Mumoda , na kuua zaidi ya 40 ya wanafunzi.


Kw aajili ya kukabiliana na mashambulizi hayo, serikali ya Rais Jonathan imepeleka kikosi kingine cha maaskari kuongoeza nguvu ya lindo na msako wa kuwakamata waharifu .

Wanamgambo wa Boko Haram wanadai kufanya mashambulio hayo kwa kutaka eneo la Kaskazini , litawaliwe kwa sharia kali za Kiislamu, na hawataki elimu toka mataifa ya Magharibi . Na hivyo Mikoa ya Kaskazini Borno na Adamawa inayo kaliwa na Waislamu wengi zaidi imeathiriwa kwa kiwango kikubwa.

Kwa ajili ya kudhibiti utendaji wa kikundi hicho, serikali, imeliweka eneo chini ya utawala wa kidharura tangu Mei mwaka 2013 baada ya kutokea mashambulio mfululizo. Pamoja na uwepo wa utawala huo wa kidharura , bado watu wanaendelea kuuawa katika mashambulizi tofauti tofauti katika eneo hilo la Kaskazini mwa Nigeria.

Waraka kuhusu Elimu Katoliki wazinduliwa mjini Vatican




Majiundo ya majadiliano ya kitamaduni katika shule za Kikatoliki: ili kuishi kwa pamoja utamaduni wa upendo. Ni hati iliyowasilishwa kwa waandishi wa habari mjini Vatican na Viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, chini ya uongozi wa Kardinali Zenon Grocholewski

Ni hati ambayo imepitishwa na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 28 Oktoba 2013, kama kumbu kumbu ya miaka 48 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha hati kuhusu elimu inayojulikana kama "Gravissimum Educationis". Hii ni hati muhimu sana kuwahi kutolewa baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Kardinali Grocholewski anasema, mwaka 2015, Kanisa litafanya Jubilee ya Miaka 50 tangu hati juu ya Elimu ilipochapishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa vatican. Kanisa Katoliki limekuwa ni mdau mkubwa katika sekta ya elimu kwani kuna zaidi ya vijana billioni moja wanaopata elimu kutoka katika: shule na taasisi za elimu zinazosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki. Kuna waalimu na wafanyakazi millioni 58 ambao wameajiriwa kwenye shule na taasisi hizi.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2008 hadi mwaka 2011 kumekuwepo na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaosoma katika shule na taasisi za Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Idadi hii imepungua Barani Ulaya, lakini imeongezeka Barani Afrika, Asia na Oceania. Idadi ya wanafunzi wanaosoma kwenye shule na taasisi za Kanisa katika nchi changa ingeweza kuongezeka, lakini kuna mambo kadhaa ambayo bado yanakwamisha jitihada hizi.

Baadhi ya sababu hizi ni vita, kinzani na majanga asilia. Kuna uhaba mkubwa wa waalimu duniani na kwamba, kuna upungufu wa waalimu millioni 1.7, ili kufikia lengo la kuwa na waalimu wenye sifa na ubora unaotakiwa na UNICEF. Hali hii ni mbaya zaidi Barani Afrika, kwani takwimu zinaonesha kwamba, kuna mwalimu mmoja kwa wanafunzi mia moja!

Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki limeendelea kusaidia kutoa utambulisho wa shule na taasisi zinazoendeshwa na kumilikiwa na Kanisa Katoliki. Kanisa linatambua kwamba, shule na taasisi hizi ni mahali pa ushuhuda wa imani unaowashirikisha, waamini walei pamoja na watawa ambao kwa kiasi kikubwa wanatekeleza utume wao kwenye sekta ya elimu.

Hati hii mpya anasema Kardinali Zenon Grocholewski inagusa kwa karibu zaidi changamoto mbali mbali za mwingiliano wa kitamaduni unaojitokeza kutokana na utandawazi na maendeleo sayansi na teknolojia. Walengwa wakuu wa hati hii ni wazazi na walezi we nye dhamana ya malezi na majiundo kwa watoto wao; waalimu, majaalimu na wafanyakazi ambao kwa pamoja wanaunda Jumuiya ya walezi.

Hati hii ni msaada mkubwa kwa Tume za Mabaraza ya Maaskofu kuhusu elimu pamoja na wadau mbali mbali wanaojihusisha na sekta ya elimu. Hii ni nyenzo ya majadiliano ya kitamaduni inataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu; uhuru wa kidini kwa kuzingatia utambulisho wa Kanisa Katoliki. Neno msingi ni majadiliano!

Lengo ni kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kitamaduni katika sekta ya elimu, ili kujenga na kuimarisha utamaduni wa upendo, dhamana inayotekelezwa na Kanisa katoliki katika sekta ya elimu na kama sehemu ya utangazaji wa Injili ya Furaha.

Askofu mkuu Angelo Vincenzo Zani, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la elimu anasema, tema ya majadiliano ni sehemu ya mchakato wa utume unaofanywa na Mama Kanisa katika sekta ya elimu. Hii ni changamoto iliyotolewa na Makardinali kunako Mwaka 2008 kwa kuhamasisha Kanisa kushirikiana na wadau mbali mbali katika sekta ya elimu, ili kuchangia maboresho ya elimu duniani. Kunako mwaka 2008, wawakilishi kutoka dini na madhehebu mbali mbali walichangia kuhusu umuhimu wa elimu katika mwingiliano wa tamaduni.

Baraza likaanza kazi yake kwa baraka na utashi wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2011 muswada wa hati hii, ukapitishwa na wajumbe wa Baraza la Kipapa la elimu. Mang'amuzi ya majadiliano ya kitamaduni ni jambo ambalo limeonesha mafanikio makubwa sehemu mbali mbali za dunia.

Kunako Mwaka 2015 Kanisa litaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulipochapisha Waraka kuhusu elimu. Mwaka huu pia Kanisa litaadhimisha Jubilee ya Miaka 25 tangu Katiba kuhusu elimu ilipochapishwa na kufanya rejea kuhusu vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki.

Uchunguzi unafanywa kuhusu uhakika wa miili ya Mapadre waliotekwa nyara DRC!




Hadi sasa hakuna habari za uhakika kuhusu mahali walipo Mapadre watatu wa Shirika la Assumption waliotekwa nyara kunako Mwezi Oktoba, 2012 nchini DRC. Habari zisizothibitishwa bado zinabainisha kwamba, kuna kaburi la pamoja ambalo limegunduliwa likiwa na masalia ya mwili wa Padre Jean Pierre Ndulani ambaye kwa miaka kadhaa alikuwa anatekeleza utume wake nchini Scotland na mwaka 2012 akarejea nchini kwao na hapo akakumbana na mkasa wa kutekwa nyara na watu wasiojulikana hadi leo hii.

Akizungumza na Shirika la Habari za Kimissionari, FIDES, Askofu Melchisedech Sikuli Paluku wa Jimbo Katoliki Butembo-Ben, mahali ambako Wamissionari watatu waliotekwa nyara walikuwa wanafanya shughuli zao za kichungaji anasema, kuna haja kwa watu kuvuta subira kwani kuna makuburi mawili yaliyopatikana yakiwa na miili kadhaa, lakini haijafahamika ikiwa kama kuna miili pia ya Mapadre waliotekwa nyara. Viongozi wa Kanisa wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubainisha ukweli wa mambo.

Wamissionari waliotekwa nyara ni Padre Jean Pierre Ndulani, Padre Anselme Wasikundi pamoja na Padre Edmond Bamutute, walitekwa nyara hapo tarehe 21 Oktoba 2012 walipokuwa katika Parokia ya Notre Dame des Pauvres, Kilometa 70 kutoka Makao makuu ya Jimbo Katoliki la Butembo Beni, lililoko nchini DRC.