Translate

Tuesday, January 15, 2013

Wanasiasa msitatute umaarufu kwa rasilimali ya Tanzania kwani ni mali ya watanzania wote!

Wanasiasa msitatute umaarufu kwa rasilimali ya Tanzania kwani ni mali ya watanzania wote!



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kutumia suala la raslimali za taifa, ikiwamo gesi asilia kujifatufia umaarufu wa kisiasa na kuwapotosha wananchi. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa ni jambo la hatari na lisilo na tija kwa wanasiasa kujaribu kuigawa nchi vipande vipande kwa sababu ya kujitafutia umaarufu kwa kutumia raslimali za taifa.

Rais Kikwete ameyasema hayo, Januari 15, 2013 wakati alipokutana na Balozi wa Uingereza nchini ambaye anamaliza muda wake, Mheshimiwa Dianne Corner ambaye alifika Ikulu, Dar Es Salaam kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi katika Tanzania. Rais Kikwete na Balozi Corner wamezungumzia masuala mbali yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Uingereza, masuala ya ukanda wa Afrika Mashariki na masuala ya kimataifa.

Kuhusu ugunduzi wa gesi asilia uliofanywa na Kampuni BG ya Uingereza katika eneo la Msimbati kwenye Bahari ya Hindi, walikubaliana kuwa hilo ni jambo jema na lenye kuleta matumaini kwa Tanzania hasa wakati itakapoanza kuvunwa katika miaka michache ijayo. Kuhusu siasa zilizoanza kujitokeza kufuatia ugunduzi huo mkubwa wa gesi asilia, Rais Kikwete amesema kuwa ni tabia ya hatari kwa wanasiasa kutumia gesi asilia hiyo ama raslimali nyingine kujijengea umaarufu wao ambao umeporomoka.

“Unawezaje kuwa na nchi moja na taifa moja wakati kila mmoja anadai raslimali kutoka kwenye eneo moja ibakie na kunufaisha watu wa eneo hilo tu. Huwezi kuwa na nchi moja na yenye umoja wakati kuna nchi ya gesi asilia kule Mtwara, kuna nchi ya kahawa kule Kilimanjaro, kuna nchi ya chai na ndizi kule Bukoba,” amesema Rais Kikwete na kuongeza: “Kwa sababu kama gesi asilia inatakiwa kubakia na kunufaisha watu wa Mtwara tu, basi wenye haki zaidi ya kudai jambo hili siyo watu wa Mtwara bali ni watu wa Msimbati ambako ndiko ilipogunduliwa kesi ambako ni maili 60 kutoka Mtwara, kilomita 200 kutoka Newala.”

Ameongeza: “Unajua nchi yetu inao baadhi ya wanasiasa wenye uchu wa umaarufu na ambao wanatumia jambo hili jema kwa manufaa yao binafsi bila kujali umoja na jadi ya taifa letu la raslimali zetu kutumika kuiendeleza nchi nzima.” Kuhusu uhusiano kati ya Tanzania na Uingereza, Rais Kikwete amemshukuru Balozi Corner kwa kazi nzuri ya kuimarisha uhusiano huo. “Umeufikisha uhusiano wetu kwenye hatua ya juu kabisa na tunakushukuru kwa jambo hili.” Mheshimiwa Corner ambaye amekuwa Balozi wa Uingereza nchini Tanzania kwa miaka minne amehamishiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Katiba Mpya ya Tanzania izingatie: haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu na uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo!

Katiba Mpya ya Tanzania izingatie: haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu na uhai wa binadamu dhidi ya utamaduni wa kifo!



Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki Musoma, Tanzania anasema kwamba, kwa miaka kadhaa, watanzania wameonesha hitaji la kuwa na Katiba Mpya, itakayokidhi mahitaji ya watanzania kwa sasa. Hitaji hili linadai mabadiliko ya kina miongoni mwa viongozi wa Serikali, viongozi wa vyama vya kisiasa, viongozi wa kidini na wananchi kwa ujumla wao. Kanisa Katoliki limeendelea kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha Wakatoliki kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya ya Tanzania. RealAudioMP3
Mambo ya kuzingatia kwanza kabisa ni kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu na uhuru wa watu unaheshimiwa, sanjari na uhuru wa kidini, ambao ni mhimili wa haki msingi za binadamu. Kwa vile Katiba ya nchi ni Sheria Mama, kamwe isibebe wala kukumbatia udini unaoweza kuwa ni shinikizo kutoka kwa makundi ya kidini nchini Tanzania.
Sharia, Mahakama ya Kadhi na Mahakimu wa Makahaka ya Kadhi ni mambo ambayo hayapaswi kuingizwa kwenye Katiba ya Tanzania, kwani Tanzania kimsingi ni nchi ambayo haina dini na wala Serikali yake haina dini, lakini watu wake wa dini na imani zao zinazopaswa kuheshimiwa na kulindwa Kikatiba. Shinikizo kutoka katika makundi ya kidini linaweza kuvuruga misingi ya haki, amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa. Imani zisipingane na haki msingi za binadamu. Kama kuna kundi linalotaka uwapo wa Mahakama ya Kadhi, basi ijitegemee na wala isiwe ni sehemu ya shughuli za Serikali.
Kanisa Katoliki lina Mahakama yake, lakini hiki ni chombo huru kinachojitegemea na hakihitaji ridhaa ya ya Serikali ili kutekeleza majukumu yake. Katiba Mpya itetee na kulinda maisha ya mtu tangu pale anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika, kamwe Katiba isikumbatie utamaduni wa kifo. Kuna haja pia ya kufuta adhabu ya kifo!

Mchango wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya

Mchango wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya



Askofu Severine Niwemugizi, Makamu Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, mwishoni wa juma, amewasilisha mapendekezo ya Baraza la Maaskofu Katoliki katika mchakato wa kutoa maoni ya Katiba Mpya ya Tanzania, wakati huu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba inapoendelea kupokea maoini kutoka kwa Makundi. Anasema, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linapinga Mahakama ya Kadhi kuanzishwa na kugharimiwa na Serikali na kwamba, hili ni suala ya waamini wa dini ya Kiislam, wanapaswa wao wenyewe kuianzisha na kuigharimia kwa fedha za waamini wenyewe. Mambo ya kidini si vyema yakaingizwa katika masuala na gharama za Serikali.
Mantiki inayoongoza ukweli huu ni kwamba, dini imekuwepo kabla hata ya Serikali, kumbe, dini inaweza kuongoza mambo yake bila ya kuhitaji ridhaa ya Serikali. Pili, waamini wasiokuwa wa dini ya Kiislam hawaifahamu kwa undani misingi ya Mahakama ya Kadhi, kwani Kadhi ni Mtawala ana Hakimu. Sifa ya kuwa Kadhi ni lazima uwe mwamini wa dini ya Kiislam. Canada ni mfano bora wa kuigwa katika kuendesha Mahakama ya Kadhi.
Akizungumzia kuhusu Tanzania kuwa na uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican, Askofu Niwemugizi alifafanua kwamba, tangu Mwaka 1929 katika Mkataba wa Laterano, Vatican ilijitenga na Italia na hivyo kuwa ni nchi huru inayojitegemea kwa mambo yake na kwamba, inatambulikana hivyo hata katika Jumuiya ya Kimataifa na wala si Shirika au Jumuiya ya Kidini. Ikiwa Tanzania inataka kuvunja uhusiano wake wa Kidipolomasia na Vatican iko huru na ni sawa na kuvunja uhusiano na nchi kama Iran.
Askofu Niwemugizi, ambaye kitaaluma ni Jaalim wa Sheria za Kanisa, anafafanua kwamba, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limeweka bayana ukweli huu, kutokana na uvumi unaoendelea kuzagaa nchini Tanzania kwamba, Serikali inaoongozwa na kuendeshwa kwa mfumo wa Kanisa Katoliki na shinikizo kutoka kwa Waamini wa dini ya Kiislam kwamba, sasa umefika wakati kwa Tanzania kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislam, OIC. Lakini, ikumbukwe kwamba, lengo la OIC ni kueneza Uislam na kufuta Ukristo katika nchi wanachama. Kumbe, OIC haipaswi kuingizwa katika Katiba, kwa vile Tanzania ina uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican.
Kwa uapnde wake Amri mkuu wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini Tanzania, ameitaka Tume ya Marekebisho ya Katiba kutofanyia mzaha suala la Mahakama ya Kadhi na kupendekeza kwamba, suala hili linapaswa kutambulika Kikatiba na kugharimiwa na Serikali. Mahakama ya Kadhi itaongozwa na wasomi wa Sheria za dini ya Kiislam ambao watatoa hukumu kwa masuala ya ndoa, mirathi na talaka.
Anasema, ikiwa kama suala hili litaachiwa mikononi mwa Waislam wenyewe wanaweza kujikuta wakitumia Sharia, kinyume cha Sheria za Nchi. Waamini wa dini ya Kiislam wanataka Ijumaa, iwe ni Siku ya Mapumziko Kitaifa kwa Waislam wote na wanafunzi waruhusiwe kwenda misikitini inapofika saa sita mchana.

Wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican wanahimizwa kutolea ushuhuda ujumbe wa Injili katika medani mbali mbali za maisha!

Wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama mjini Vatican wanahimizwa kutolea ushuhuda ujumbe wa Injili katika medani mbali mbali za maisha!



Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumatatu, tarehe 14 Januari 2013 amekutana na kuzungumza na wanajenzi wa vikosi vya ulinzi na usalama vinavyotekeleza majukumu yao mjini Vatican, kama sehemu ya utamaduni wa kutakiana kheri na matashi mema kwa Mwaka Mpya wa 2013.

Amewashukuru kwa utekelezaji wa majukumu ya ulinzi na usalama mjini Vatican yanayozingatia sadaka na weledi wa kazi, kwa maelfu ya watu wanaofika mjini Vatican kumtembelea Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Makaburi ya Mitume na Mapapa waliotanguliwa mbele ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko, lakini kwa namna ya pekee Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili.

Utekelezaji wa majukumu haya unajionesha hata wakati wa hija zake za kichungaji ndani na nje ya mji wa Roma, mambo yanayomsukuma Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuonesha kweli moyo wa shukrani kutokana na utayari wao katika huduma, makini na watu ambao wana sifa. Hii ni heshima kama sehemu ya utambulisho wao kama wafanyakazi wa serikali na Wanajumuiya wa Kanisa na ni kielelezo cha uhusiano mwema kati ya Vatican na Serikali ya Italia.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, magumu na sadaka kubwa wanayoitoa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku, bila kusahau changamoto na hatari wanazoweza kukutana nazo, kiwe ni kielelezo cha imani yao ya Kikristo, tunu msingi ya maisha ya kiroho ambayo wao wameirithi kutoka kwa wazazi wao na sasa wanaalikwa kuwarithisha pia watoto wao.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani iwe ni fursa kwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama kutangaza kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, Ujumbe wa Injili ya Kristo uweze kupenya katika dhamiri, maisha ya kawaida kwa kushuhudia nguvu ya upendo wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, katika ujumbe wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2013, amebainisha aina mbali mbali za kazi za kulinda na kudumisha amani, jambo linaloonesha wito wa mwanadamu katika kulinda amani, kwani hamu ya kuishi katika amani ni kielelezo cha tamaa ya kutaka kupata utimilifu wa maisha na furaha ya kweli.

Baba Mtakatifu anawatakia wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama utaratibu na utulivu; mambo yanayojenga maisha yenye amani na utulivu na kielelezo cha ustaarabu wa kweli. Anawaweka wote chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, ili aweze kuwaombea kwa Mwanaye Mpendwa: maendeleo, amani, utulivu na kuwalinda dhidi ya hatari zote za maisha: kiroho na kimwili.

Askofu Desiderius Rwoma ateuliwa kuwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Bukoba, Jimbo la Singida sasa liko wazi!

Askofu Desiderius Rwoma ateuliwa kuwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Bukoba, Jimbo la Singida sasa liko wazi!



Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amekubali ombi la Askofu Nestori Timanywa wa Jimbo Katoliki Bukoba, kung'atuka kutoka madarakani na badala yake amemchagua Askofu Desiderius M. Rwoma wa Jimbo Katoliki Singida, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania.

Kwa sasa Jimbo Katoliki Singida, liko wazi. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amemteua Askofu Desiderius Rwoma kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Singida.

Askofu Rwoma, alizaliwa kunako tarehe 8 Mei 1947, Jimboni Bukoba. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi akapadrishwa kunako tarehe 28 Julai 1974. Kwa miaka mingi alikuwa ni Gombera wa Seminari Ndogo ya Rubya na Makamu Askofu jimbo Katoliki Bukoba.

Tarehe 19 Aprili 1999 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, kufuatia kifo cha Askofu Bernard Mabula. Akawekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam hapo tarehe 11 Julai 1999, Kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Katoliki Singida.

Wabunge wa Kenya wajiongezea marupurupu kibao kabla ya kuvunjwa kwa Bunge!

Wabunge wa Kenya wajiongezea marupurupu kibao kabla ya kuvunjwa kwa Bunge!



Kabla ya wananchi wa Kenya hawajarejea tena kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 4 Machi, 2013, Wabunge wa Kenya wameamua kujiongezea marupurupu zaidi, yatakayoigharimu Serikali ya Kenya kiasi cha shilingi billioni mbili, watakapokuwa wanahitimisha shughuli zao Bungeni. Katika muswada huo wa sheria, wabunge wanataka wapewe hati za kusafiria zenye hadhi ya kibalozi, usalama wao pamoja na kupewa mazishi ya kitaifa.

Wananchi wengi wa Kenya wanauangalia muswada huu kwa jicho la makengeza, wakati wanasubiri kama utapishiwa na Rais Mwai Kibaki ili uweze kuwa ni sheria. Katika muswada huo, Rais wa Kenya baada ya kumaliza utumishi wake, atakabidhiwa kitita cha jumla ya shilingi za Kenya millioni 12.6. Baadhi ya wananchi wa Kenya waliohojiwa wanasema kwamba, katika muswada huu Wabunge wameshindwa kuonesha uzalendo kwa nchi yao na badala yake wamejizamisha katika uchu wa mali na heshima, ingawa baadhi yao wanaendelea kushutumiwa kwamba ni mafisadi, wala rushwa na wazembe.

Waziri mkuu wa Kenya, Raila Odinga anasema, Wabunge wanapaswa kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa wananchi waliowapigia kura badala ya kujiingiza katika tamaa ya kupenda fedha mno, inayoweza kuhatarisha amani, usalama na ustawi wa nchi. Hata baada ya kung'atuka madarakani bado wabunge wanataka wapewe ulinzi? Baadhi ya wananchi wanaendelea kuhoji! Wamesahau kwamba, kuna watu wasiokuwa na hatia nchini Kenya wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na ukosefu wa ulinzi na usalama! Lakini wao, jambo hili wanalifumbia macho na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa masilahi yao binafsi.

Mapinduzi ya Zanzibar 1964 yalipania kungo'a ukandamizaji, unyonyaji na ubaguzi

Mapinduzi ya Zanzibar 1964 yalipania kungo'a ukandamizaji, unyonyaji na ubaguzi



Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amesema kuwa moja ya faida kubwa na nyingi za Mapinduzi ya Zanzibar ni kufunguliwa kwa namna kubwa sana kwa nafasi na fursa za elimu kwa watoto wa Wazanzibari Wazawa. Sababu kubwa ya Chama cha Afro- Shiraz Party kufanya Mapinduzi ya mwaka 1964 ilikuwa ni kuondoa ukandamizaji, unyonyaji na ubaguzi waliokuwa wanafanyiwa Zanzibari Wazawa katika kupata huduma ikiwepo elimu.

Akizungumza, Jumamosi, Januari 12, 2013, wakati anazindua Shule ya Sekondari ya Mlimani-Matemwe, Mkoa wa Kaskazini, kwenye pwani ya kaskazini ya Kisiwa cha Unguja, Rais Kikwete amesema kuwa inashangaza sana kuwa baadhi ya watu wanaweza kuendelea kuyabeza Mapinduzi ya Zanzibar wakati yameleta faida kubwa na nyingi kwa wananchi na wanazijua. “Sote tunatambua sababu kubwa ya Chama cha ASP kufanya Mapinduzi ya mwaka 1964 ilikuwa ni kuondosha ukandamizaji, unyonyaji na ubaguzi waliokuwa wanafanyiwa Wazanzibari wazawa katika kupata huduma muhimu ikiwepo elimu. Idadi ya skuli ilikuwa ndogo sana na kwa makusudi wazawa wenzetu chache ndio walibahati kupata elimu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Baada ya Mapinduzi, skuli nyingi zilijengwa na vijana wengi zaidi wanapata elimu. Kazi hiyo inaendelea kama tunavyoshuhudia leo.” Rais Kikwete aliongeza: “Zanzibar na Pemba zilikuwa na shule tatu tu za sekondari za Serikali kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964 – moja ilikuwa Pemba ikiitwa Saidi Abdallah Secondary School na mbili zilikuwa Zanzibar, basi. Zilizobakia zilikuwa shule za sekondari za dini. Leo tu, tunafungua kwa mpigo shule 21 za sekondari mpya. Moja hii ambayo ni moja ya shule 13 ambazo ujenzi wake umekamilika. Nyingine nane zikiwa zinajengwa ikiwa ni pamoja na chuo kipya cha ualimu cha Benjamin William Mkapa.”

Uzinduzi wa shule hiyo yenye majengo na huduma za kisasa ikiwa ni pamoja na maabara za masomo ya fikizia, kemia, biolojia na kompyuta ni sehemu ya Sherehe za Miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambayo sherehe zake zimefanyika leo kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Zanzibar, na kuhudhuriwa na Rais kikwete. Shule hiyo iliyogharimu kiasi cha Sh. Bilioni 1.8 mpaka sasa ni moja ya shule 19 za sekondari zinazojengwa Tanzania Visiwani chini ya Mradi wa Uimarishaji wa Elimu ya Lazima (ZABEIP) miaka mitano unaogharimiwa kwa pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Dunia.

Serikali ya Mapinduzi (SMZ) inatoa dola za Marekani milioni sita na Benki ya Dunia dola za Marekani milioni 42 ikiwa ni mkopo wenye masharti nafuu na mradi wenyewe ulioanza kutekelezwa Julai 2008 unafikia mwisho wake Juni mwaka huu, 2013. Chini ya mradi huo, zinajengwa shule 10 za sekondari (kidato cha kwanza hadi cha sita) katika kila wilaya za Tanzania Visiwani, zinajengwa shule tisa za sekondari (kidato cha kwanza hadi cha nne) – tano Unguja na nne kisiwani Pemba, kinajengwa chuo kipya cha ualimu cha William Benjamin Mkapa Kisiwani Pemba na shule sita zinafanyiwa matengenezo makubwa.

Mradi huo pia ni matokeo ya mazungumzo kati ya Rais Kikwete na uongozi wa Benki ya Dunia wakati alipofanya ziara yake ya kwanza Marekani mwaka 2006 baada ya kuwa amekuwa Rais wa Tanzania ambako aliushawishi uongozi wa Benki hiyo kukubali kutoa fedha za kugharimia mradi huo mkubwa zaidi kuliko mwingine wowote kufanywa na Serikali katika historia ya Zanzibar. Aidha, kutekelezwa kwa mradi huo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambayo iliiagiza Serikali ya Mapinduzi kujenga shule za kisasa za sekondari 21 katika wilaya zote za Unguja na Pemba.

Chini ya Mradi wa ZABEIP, tayari shule za sekondari 13 zimekamilika kujengwa na ujenzi wa shule sita zilizobakia pamoja na Chuo cha Ualimu cha Benjamin William Mkapa Kisiwani Pemba unaendelea. Na ili kufikisha idadi ya shule 21 za sekondari kama inavyoelekeza Ilani ya CCM, ujenzi wa shule nyingine mbili zilizosalia unaendelea katika eneo la Mkanyageni Kisiwani Pemba na Kiblateni Kisiwani Unguja kwa gharama ya pamoja ya Serikali ya Mapinduzi na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo (BADEA).

Shule ya Mlimani-Matemwe yenye huduma kamili za elimu na ambayo ni sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne, ilianza kupokea wanafunzi Septemba mwaka jana kwa vidato vya kwanza na tatu. Wanafunzi 231 ndiyo walianzisha shule hiyo ya kutwa na yenye hadhi ya wilaya ikiwa na wavulana 145 na wasichana 86. Shule hiyo ina walimu tisa wakiwemo wawili wa kujitolea kutoka Nigeria. Sherehe hizo za uzinduzi wa shule hiyo zilizohudhuriwa na viongozi wa SMZ akiwamo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Balozi Seif Idi imehudhuriwa na mamia ya wakazi wa eneo la Mlimani-Matemwe.