Translate

Sunday, November 4, 2012

Vyombo vya habari vyanyooshewa kidole,ni kutokana na kutangaza vyuo feki,VETA yasema matangazo yasirushwe hadi wahakikishe wamethibitisha cheti kama kweli chuuo kina usajiri,ikibi wakaangalie na majengo,asema Grace College imesajiriwa rasmi na inajulikana kitaifa

Na Thompson Mpanji,Mbeya




VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuhoji uhalali wa vyuo sanjari na kupata uthibitisho wa vyeti vya usajili kutoka Chuo cha ufundi stadi (VETA),kwa wahusika wanaohitaji kufanya matangazo ya biashara katika Radio,magazeti na Luninga ili kuwasaidia wazazi na wananfunzi wasiweze kupotea na kuingia hasara ya ada na gharama nyinginezo katika vyuo visivyosajiriwa.



Mkurugenzi wa VETA kanda ya nyanda za juu kusini,Justin Rutta ametoa wito huo wakati wa mahafali ya tisa ya wahitimu wa kozi za uhazili,utalii na masuala ya Hoteli na programu ya Kompyuta katika chuo cha kanisa la Neema cha Grace College kilichopo Forest Maghorofani,jijini Mbeya.



Rutta alisema vyombo vya habari kama jicho la jamii vinapaswa kuwasaidia wazazi na wanafunzi wanaohitaji kupata elimu bora inayotambulika kitaifa hasa katika wakati huu ambapo wajanja wengi wameibuka na kuanzisha vyuo visivyo na hadhi,visivyosajiliwa lakini kutokana na ujanja ujanja vimekuwa vikitumia gharama kubwa kujitangaza katika vyombo vya habari vikubwa vinavyotambulika kwa lengo la kuwalubuni wananchi.



"Media ndiyo mhimili unaotoa taswira kwa jamii kuhusu kipi kizuri na kipi kibaya kwa hiyo pamoja na kuhitaji matangazo nawaombeni msirushe matangazo ya vyuo hadi wawaonyeshe cheti cha usajili,kwa sababu vinginevyo media ndiyo itaonekana inashirikiana na mataperi kuipotosha jamii na waulizeni wanapotoka na ikibidi nendeni mkaangalie na majengo yao,"alisema.



Alifafanua kuwa hivi karibuni Veta ilivifunga vyuo vyote ambavyo havikuwa na vigezo vya kutoa elimu na kwamba katika mchakato wa sasa wa kupita kuvikagua na kuvipatia usajiri upya Chuo cha Grace College ni miongoni mwa vyuo vilivyosajiriwa na kutambulika kitaifafa baada ya Veta kukipitisha.



"Wazazi na vijana kuweni macho na vyuo vinavyoanzishwa kitaperi katika maghofu ya nyumba na voichochoro vya kutisha,na matokeo yake mzazi anagharamia ada na gharama nyingine lakini mtoto akihitimu cheti chake chenye mapambo mazuri hakitambuliki kitaifa,chuo hakijasajiriwa na hivyo inakuwa ni hasara kwa mzazi na mtoto anapoteza mwelekeo wake wa baadaye,"alisema Rutta.



Hata hivyo Mkurugenzi huyo aliwataka wahitimu hao kwenda kuwa kielelezo cha chuo cha Grace kuwa ni kisima cha elimu bora,wanafunzi wanaofuata maadili mema,uchapakazi,upendo,ubunifu sanjari na ushirikiano katika maeneo ya kazi watakayofanikiwa kuajiriwa huku akiwataka watakaokosa nafasi wasikate tamaa na badala yake waende kujiajiri na kuondokana na utegemezi.



Awali Mkuu wa chuo cha Grace College,Sinana Otaigo Daniel alisema licha ya chuo hicho kumilikiwa na kanisa la Neema lakini kinapokea wanafunzi wa imani zote,bila ubaguzi na kwamba wanatoa pia elimu ya stadi za maisha,malezi bora, sanjari na kozi ya lugha ya kiingereza na kifaransa, na maosmo ya sekondari kwa miaka miwili na ada zao ni nafuu huku wanafunzi wa kike wakikaa katika Hosteli iliyomo ndani ya uzio wa chuo.



Mkuu huyo alisema kutokana na uhataji wa mahali salama kwa malazi na patulivu kwa kusomea hasa kwa wananfunzi wa kike,mikakati imewekwa ya kuongeza majengo mengine kwa hosteli inayotarajia kulaza wanafunzi zaidi ya 70 huku jitihada nyingine za kujenga mabweni ya wanafunzi wa kiume zikiendelea kwa kushirikiana na wazazi,kanisa na wafadhiri mbalimbali.



Ametoa wito kwa wazazi,wadau wa elimu,wafadhiri na watanzania wote wenye mapenzi mema kujitokeza kukichangia chuo hicho ili kiweze kujenga mabweni ya kutosha na hivyo wanafunzi kuweza kusoma kwa usalama bila bughudha za kidunia na hatimaye kupata viongozi bora wa baadaye na wataalamu wa taifa.



Mwisho.

Friday, November 2, 2012

Abood lauwa Kondakta na kujeruhi 25,ni baada ya kufika Mbeya,ni la Dar Tunduma,mochwari wachanganya maiti

Na Thompson Mpanji,Mbeya

MTU mmoja amefariki dunia na wengine 25 kujeruhiwa baada ya Basi la abiria la kampuni ya Abood lililokuwa likitokea Dar es salaam kuelekea Tunduma, kugongana na lori la mizigo lililokuwa likielelekea Dar es salaama katika maeneo ya Sae kwa Mbilinyi jijini Mbeya.
 
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo linalodaiwa kutokea jana majira kati yasaa moja na mbili usiku walimtaja  kwa jina moja mtu  aliyefariki dunia papo hapo  kuwa ni mmoja wa makondakta wa basi aliyefahamika kwa jina la  white na wengine kujeruhiwa vibaya baada ya lori  lenye konteiner lenye  nambari za usajili T.616 ATQ kutaka kuikwepa basi dogo la abiria maarufu daladala iliyogeuza ghafla  maarufu kusinga katika eneo la Mbilinyi,Sae na kujikuta likivaana na  Basi lenye nambari za usajili T545 AZE lililokuwa likielekea Tunduma.
 
Mashuhuda hao walisema  baada ya dereva wa lori kulikwepa daladala na   alikutana na  basi la Abood  na hivyo  kufanya jitihada za kulikwepa na kujikuta basi hilo likiingia katika  upande wa konteiner la lori.
 
Kamanda wa polisi Diwani Athuman amethibitisha kutokea kwa ajili hiyo na kwamba uchunguzi unaendelea kujuwa chanzo cha ajali.
 
Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Rufaa Mbeya,Thomas  akizungumza kwa njia ya simu alisema walipokea wagonjwa 25 ambapo hadi kufikia leo asubuhi wamebakia na wagonjwa wanne na kwamba  taarifa ya jana jioni inaonesha walipokea maiti mbili lakini inakinzana na  taarifa ya chumba cha kuhifadhia maiti ambayo inaonesha wamepokea maiti moja iliyotokana na ajali ambapo marehemu alitambulika kwa jina la Charles almaarufu white,kabila mpale mkazi wa Kilimanjaro na tayari imechukuliwa na ndugu zake na kusafirishwa.
 
Mwisho.

wananchi Mbeya wafunga barabara kwa masaa sita ,ni kutokana na kugongwa watu zaidi ya 30 wakiwemo watoto wawili wa chekechea


Na Thompson Mpanji,Mbeya

MATUKIO ya ajali yameendelea kuundama Mkoa wa Mbeya  baada ya wananchi  wa Kijiji cha Imezu  kata ya Inyala  wilaya ya Mbeya Vijijini  leo kulazimika kufunga bara bara ya  Mbeya  Dar es Salaam kwa takribani saa sita baada ya kutokea ajali iliyoua watoto  wawili wa chekechea  wanaokadiriwa kuwa na umri wa miaka mitano mpaka sita.

Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani  Mkoa wa Mbeya (RTO) Butusyo Mwambelo amewataja Watoto hao kuwa ni ,Timotheo  Omary (5) na Thadeo Braiston  Malila (5)  ambapo kati ya watoto hao mmoja tayari mazishi yake yamefanyika  na mwili wa mtoto mwingine utasafilishwa  kwenda kijiji cha uwanji Matamba Wilayani Makete.

Amesema kuwa tukio hilo  limetokea  majira ya saa 1.15 asubuhi baada ya watoto hao kugongwa na gari aina ya  yenye namba  za usajili T 798 BVY  tela  T698  BVA lilokuwa kiendeshwa na  Dominick  Mwakalundwa (34) mabibo dar e s salaam lililokuwa likitokea Mbeya  kwenda Mkoani Iringa liligonga watoto  hao waliokuwa pembeni ya bara bara wakitoka shule na kwamba aliokolewa na askari Polisi baada ya wananchi kutaka kumshambulia..

Wakizungumza na  Radio five na matukio  katika eneo la ajali hiyo Wananchi hao,  wamesema kuwa waliamua kuchukua  uamuzi huo  baada ya kuchoshwa na ahadi za serikali kupitia wakala wa bara bara  za kuweka matuta  katika eneo hilo la la shule  ili kuepusha ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara .

Bw.Michael Mashamba mkazi wa kijiji cha Imezu amesema kuwa baada ta tukio hilo kutokea wananchi walijaa eneo la ajali  na kuanza kufunga  bara bara kwa kutumia magogo na mawe  ili kuzuia magari yasipite eneo hilo kwa lengo la kushinikiza serikali kuweka matuta ili kuzuia ajali kutokana na madai ya kufariki watu zaidi ya 30 kwa ajili katika maeneo hayo.

 Hata hivyo baada ya tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Dkt. Norman  Sigalla  aliwaomba wananchi  kufungua bara bara wakati serikali  kwa kushirikiana na wakala wa bara bara (TAN ROADS) ikiwa inaweka utaratibu  wa kuweka matuta hayo haraka iwezekanavyo.

Aidha Sigalla ameliagiza jeshi la polisi  Mkoani hapa kuwachukulia hatua  kali madereva watakoendesha  magari kwa mwendo kasi  na kwamba watozwe faini na adhabu kali ambayo itawafanya wawe na nidhamu  na askari wasiwe marafiki wa madereva.
Mwisho

Wednesday, October 31, 2012

Tazara saccos kujenga Hosteli ya kisasa

Na Thompson Mpanji,Mbeya

CHAMA cha kuweka na kukopa cha Tazara Saccos Mkoani Mbeya kinatarajia kujenga hosteli kubwa ya kisasa ili kuachana na dhana ya kuwa tegemezi kutoka kwenye taasisi za kibenki na kuwa mradi huo mkubwa utaweza kusaidia chama kujitegemea chenyewe badala ya kutegemea zaidi kukopa katika benki hizo.



Hatua ya kuwa na ujenzi huo wa hosteli imekuja baada ya uongozi wa Tazara kwa kushirikiana na wanachama kuamua kwa pamoja kuwa na kitega uchumi chao wenyewe ambacho kitasababisha kuacha kukopa katika mabenki kwani hosteli hiyo itakapokuwa imekamilika hakutakuwa na sababu ya kukimbilia tena katika mabenki badala yake watatumia kitega uchumi chao kukuza mtaji wa chama.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama hicho wa kumi na tisa toka kuanzishwa kwake, Mwenyekiti wa Tazara Saccos Mkoani Mbeya Ambrose Shayo amesema kwamba kuanzia wameona kuwa mradi pekee ambao wanaweza kuanza nao ni hosteli kutokana na vyuo vingi kuanzishwa Mkoani hapa na ongozeko la wananchi kuwa kubwa.


Shayo amesema kuwa mradi huo utagarimu kiasi cha shilingi bilioni. 2 na kuwa fedha hizo zitapatikana kwa kila mwanachama kuchangia hisa zake ambazo ni shilingi 3,0000 ambazo watatoa kwa kila mwezi na kwamba mbali ya hisa za wachama pia chama kama kitakuwa kinanunua hisa za mil.8 kila ujenzi huo unatarajio kukamilika ndani ya miaka mitano ijayo sababu uwanja upo tayari ni kuanza tu mchakato wa kutafuta fedha mapema kutoka taasisi zingine kwa kutumia njia mbali mbali.

Aidha Mwenyekiti huyo amesema mwisho wa utekelezaji wa mpango huo ni kuweza kuwekeza na kuanza kujitegemea wenyewe badala ya kutegemea mabenki zaidi ambazo wamekuwa wakitumia kwa muda mrefu.
Mwiisho.

Ajinyonga kwa waya wa simu baada ya kumpiga mkewe

Na Thompson Mpanji,Mbeya

MKAZI wa Iziwa Mkoani Mbeya Mbwiga Mwalungwe(60), amefariki dunia baada ya kujinyonga nyumbani kwake kwa kutumia waya wa simu Oktoba 24 mwaka huu baada ya marehemu kumpiga mkewe.


Inadaiwa marehemu alimpiga mkewe aitwaye Taines Mbwiga(45) Oktoba 23 hali iliyompelekea kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Jijini hapa ambapo alipewa PF3 kwa ajili ya kutibiwa na kulazimu kulazwa hospitalini hapo.

Kutokana na tukio la baada ya mkewe kulazwa hospitalini, Jeshi la Polisi lilianza kufuatilia tukio hilo ndipo marehemu alipogundua kuwa anakabiliwa na mkono wa sheria aliamua kuchukua uamuzi mgumu kwa kuchukua waya wa simu majira ya saa 4 kamili asubuhi Oktoba 24, kisha kujinyonga nyumbani kwake.


Aidha polisi walifika eneo la tukio majira ya saa 6:00 mchana na kuuchukua mwili wa marehemu hadi hospitali ya rufaa kwa ajili ya uchunguzi zaidi na kwamba hali ya mwanamke huyo inaendelea vema ambapo ameruhusiwa kutoka hospitalini Oktoba 2 na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali hiyo.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi,kuhusiana na tukio hilo Balozi wa mtaa huo Chaina Juma amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba amewaachia jeshi la polisi kufanya uchunguzi ili kupata kiini hasa cha Mwalungwe kujiua kwa kujinyonga na kumuacha mkewe akiendelea kuugua hospitali.


Mwisho.



Mtoto wa miaka nane ajinyonga

MTOTO  mdogo aliyefahamika kwa jina la Calvin Patrick mwenye umri wa miaka nane  mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Iwambi ,Mkazi wa Mtaa wa Ivwanga Kata ya Iwambi Mkoani Mbeya amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia kamba ya viatu nje ya nyumba yao.
Tukio la kujinyonga kwa mtoto Patrick limetokea majira ya saa 5.00 octobar 27 mwaka huu asubuhi katika mtaa wa Ivwanga wakati wazazi wa mtoto huyo walipokuwa wametoka nyumbani hapo na ndipo mtoto huyo alipochukua jukumu hilo zito na la aina yake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwenyekiti wa mtaa huo Chonde Calisto alisema wakati tukio hilo linatokea Baba mzazi wa mtoto huyo Patrick Mwakapalila alikuwa ametoka na kaka mkubwa wa marehemu aitwaye Joshua kuelekea mjini kutafuta mahitaji na kwamba baada ya tukio hilo baba mzazi wa mtoto huyo alipigiwa simu na kutakiwa kurudi haraka nyumbani.

Amesema kuwa baada ya tukio baba mzazi wa mtoto huyo alipigiwa simu ili arudi nyumbani kuona tatizo lililotokea kwa mtoto wake na kwamba baada ya kufika alikuta mwanae huyo mdogo akiwa nje ya nyumba yao akiwa ananing'inia juu akiwa amejinyonga kwa kamba ya viatu"alisema.

Hata hivyo mama mzazi wa mtoto huyo nae hakuwepo nyumbani hapo kwani alikuwa katika shughuli zake za kibiashara ambako anauza duka la mahitaji mbali mbali ya nyumbani eneo la Iwambi ambako jirani na nyumbani.

Chonde amesema mpaka sasa bado hakijafahamika chanzo cha kujinyonga kwa mtoto huyo na polisi walifika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu kwa uchunguzi zaidi ili ndugu waweze kukabidhiwa mara baada ya uchunguzi huo kukamilika .


Mwisho.

serikali haijaridhishwa na ujenzi wa barabara ya kuelekea Chunya

SERIKALI imetishia kuinyang’anya kampuni ya China Communication Construction Limited zabuni ya ujenzi wa barabara ya kutoka Mbeya mjini hadi Lwanjilo wilaya ya Mbeya Vijijini yenye urefu wa kilometa 36 baada ya kutoridhishwa na kasi ya utendaji kazi ya mkandarasi huyo.




Hatua hiyo ya Serikali imetokana na mkandarasi huyo kushindwa kufikia malengo ya ujenzi huo kwa kiwango cha lami katika muda uliopangwa huku akiwa tayari ameshakabidhiwa fedha za awali za mradi huo shilingi bilioni Nane za Tanzania.



Ujenzi huo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 55 zilizotolewa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Wahisani wa maendeleo ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya kutoka Mbeya mjini hadi wilayani Chunya yenye urefu wa kilometa 72.



Sehemu ya pili ya ujenzi huo kutoka Lwanjilo hadi Chunya mjini utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 44 kupitia mkandarasi mwingine.



Mkandarasi huyo aliyeanza kazi hiyo Novemba mwaka jana amechukua nafasi ya mkandarasi wa awali kampuni ya Kundan Sing iliyokabidhiwa ujenzi huo mwaka 2010 kabla ua kushindwa kuendelea na kazi kutokana na Serikali kuchelewa kutoa fedha mradi huo.



Hata hivyo tangu alipokabidhiwa kazi hiyo, kasi ya utendaji wake imekuwa ikilalamikiwa na mamlaka husika kwa maelezo kuwa ameshindwa kuifanya kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa.



Akikagua ujenzi huo Oktoba 15, Naibu Waziri wa Ujenzi, Injinia Greyson Lwenge, amesema Serikali hairidhishwi na kasi ya utendaji kazi ya mkandarasi huyo na kutishia kumnyang’anya zabuni hiyo.



“Nimetembelea ujenzi huu kwa kilometa zote 36 kutoka Mbeya mjini hadi hapa Lwanjilo, ukweli sijaridhishwa na kazi inavyokwenda, mvua zinakaribia kunyesha na hakuna mafanikio yaliyofikiwa kama tulivyotarajiwa.”



“Serikali imeshatangaza kuwa barabara hii ni lazima ikamilike kwa wakati, hivyo kama tutaona mkandarasi huyu anaendelea kusuasua, hatutasita kumnyang’anya kazi na kumtafuta mkandarasi mwingine, tunataka kazi ifanyike hatutaki maneno.” alisema Injinia Lwenge.



Hadi sasa mkandarasi huyo amenza ujenzi wa barabara hiyo katika kijiji cha Lwanjilo katika urefu usiozidi kilometa tano hali inayoitia shaka Serikali kuwa huenda isikamilike kwa wakati katika kipindi cha miezi 36 tangu alipokabidhiwa zabuni hiyo Novemba mwaka jana.



Kutokana na hali hiyo Injinia Lwenge ameiagiza Wakala wa Barabara nchini, TANROADS mkoa wa Mbeya na Mhandisi wa mkoa kuhakikisha mkandarasi huyo anatekeleza kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba uliopo pamoja na kuhakikisha barabara hiyo haifungwi wakati wa mvua ili kuepusha usumbufu kwa wananchi.



Hata hivyo viongozi wa kampuni hiyo ya China Communication Construction Limited hawakuwa tayari kuzungumza na Waandishi wa habari kuhusu hali hiyo huku wakishindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu kuchelewa kuanza kwa ujenzi huo wakati wakizungumza na Injinia Lwenge.



Awali mmoja kati ya viongozi wa kampuni hiyo ambao pia hawakuwa tayari kutaja majina yao, alijifanya hajui kuzungumza lugha ya Kiingereza na kutumia mkalimani kumjibu Injinia Lwenge kabla ya Naibu Waziri huyo kubaini ujanja huo na kumlazimisha kuzungumza lugha hiyo na hatimaye kufanya hivyo kwa ufasaha mkubwa.



Barabara hiyo ni miongoni mwa barabara zilizomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, CCM, ya mwaka 2010 ambapo Rais Jakaya Kikwete, aliwaahidi wakazi wa vijiji vinavyopitiwa na barabara kuwa atahakikisha inatengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuwaondoakuwa atahakikisha inatengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuwaondolea kero ya usafiri hasa wakati wa mvua.



Ubovu wa barabara hiyo umesababisha wakazi wa kijiji cha Lwanjilo kutozwa kati ya shilingi 8,000 hadi 10,000 kwenda Mbeya mjini umbali wa kilometa 36 wakati nauli ya kutoka Mbeya mjini hadi wilayani Kyela umbali wa zaidi ya kilometa 110 ikiwa ni shilingi 3,000.



Mwisho