Translate

Saturday, October 27, 2012

Mujata yaiasa jamii kushirikiana na Polisi

Na Thompson Mpanji,Mbeya




CHAMA cha Muungano wa Jamii Tanzania (MUJATA) kimewataka wanajamii wote kwa ujumla kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kukomesha maovu yanayotokea kwenye jamii mbali mbali nchini.



Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Mujata kanda,Shayo Soja katika kongamano la Chama hicho ambalo limehusisha viongozi mbalimbali na wajumbe kutoka mikoa mbalimbali ya nyanda za juu kusini ikiwepo Iringa,Njombe,Ruvuma,Katavi pamoja na Mbeya.



Akizindua kongamano hilo katika ukumbi wa Royal College of Tanzania tawi la Mbeya,kamanda wa polisi mkoani hapa Diwani Athuman amesema jeshi la polisi lipo kwa ajili ya kushirikiana na Mujata ili kuhakikisha kuwa maovu yote yanayotendeka katika jamii yanakomeshwa.



Diwani amewaomba Mujata kutoa ushirikiaano wa hali na mali kwa jeshi ili kuweza kutokomeza kabisa kila aina ya uovu na amewashukuru kwa kutoa taarifa kwa jeshi la polisi katika vitendo vya ukatili vilivyowahi kujitokeza hapo awali kwa kuzika watu wakiwa hai.



Alisema vitendo vya ukatili,unyanyasaji wa kijinsia pamoja na maovu yatendekayo kwenye jamii yatakomeshwa endapo jamii haitakuwa tayari kufumbia macho vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa polisi.



Wakati huo huo,Chama hicho kimefanya uchaguzi wa kuteuwa viongozi katika nafasi mbalimbali za Chama ikiwa ni pamoja na kumpata Mwenyekiti wa pamoja na makamu wake.



Uchaguzi huo ambao umesimamiwa na kamati ya uchaguzi ya Mujata ambapo Mwenyekiti aliyechaguliwa ni Soja pamoja na makamu wake Christina Joel hao wote kwa pamoja wamekishukuru chama kwa kuwaamini kwa mara nyingine.



Mwisho.

Kardinali Pengo atamka vurugu za Tanzania asema "Kamwe msitumie kinzani, vurugu na misigano ya kidini kujinufaisha kiuchumi, kisiasa, kijamii na kidini"

 Na Thompson Mpanji

MAASKOFU waliopo katika Sinodi ya Maaskofu juu ya Uinjilishaji Mpya inayoendelea mjini Vatican wamesema, kati ya mambo yanayoendelea kukwamisha mchakato wa majadiliano ya kidini ni pamoja na misimamo mikali ya kiimani.



Wamesema vyanzo hivyo vinasababisha watu kutoheshimu sheria za nchi kwa kutaka kujichukulia sheria mikononi mwao pamoja na malumbano ya kidini yanayolenga kuvunja misingi ya amani na mshikamano kati ya watu wa mataifa kwa malengo binafsi,kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini.



Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar alisema , choko choko, machafuko na uharibifu wa mali kwa misingi ya kidini, zimeendelea kujionesha kwa namna ya pekee nchini Nigeria na Tanzania



Alisema hii ni kutokana na sababu kwamba, watu wanashindwa kuelewa kwamba, kimsingi hakuna dini inayoshabikia mapigano wala machafuko ndani ya Jamii.



Kardinali Pengo alisema, kuna watu ambao wanapenda kutumia tofauti za kidini kama njia ya kujijenga kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini, kiasi hata cha kuhatarisha amani, usalama, utulivu na mshikamano wa kitaifa.



Alisema hali hiyo inatokana na watu kugubikwa na ubinafsi, uchu wa mali na kupenda mno madaraka ambapo hawataki kusikia ukweli mkamilifu kuhusu masuala ya kidini, kwao jambo la msingi ni kufaidika na migogoro na kinzani za kidini.



Kardinali Pengo ametoa wito kwa Waamini wa Dini ya Kiislam na Kikristo kuendeleza moyo wa majadiliano ya kidini, kwa kuheshimiana, kuthaminiana na kujadiliana masuala muhimu ya kidini kwa ajili ya mafao ya wengi na kamwe tofauti zao za kidini zisiwe ni chanzo cha kinzani, vurugu, umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia na uharibifu wa mali ya watu.



Hata hivyo ameishauri Serikali na vyombo vya dola kutekeleze wajibu wake kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unashika mkondo wake.



Amewaonya wanasiasa wanaotumia tofauti za kidini kama njia ya kujitafutia umaarufu, ili hatimaye, kujijenga kiuchumi, kisiasa na kijamii, kuacha mara moja kwani wanaweza kusababisha maafa makubwa kwa Jamii,"Kamwe hasiwepo mtu anayetumia dini kama ngao yao katika medani mbali mbali za maisha."



Aidha Kardinali Pengo amewaomba watanzania na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba, tofauti za kidini na kiimani zimekuwepo nchini humo miaka nenda rudi, lakini watu wakaheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana na anajiuliza, kumetokea nini hata leo hii dini iwe ni chanzo cha kinzani, vurugu na machafuko nchini Tanzania?.



Amefafanua kuwa wote wanaotaka kuchochea vurugu, vita na kinzani kwamba, amani ikitoweka, hakuna mtu atakayesamilika kwani matunda ya kuvunjika kwa misingi ya haki kamwe hayawezi kudumu hivyo ni jukumu la kila mtu kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani na kamwe tofauti za kidini zisiwe ni chanzo cha kinzani, vurugu na umwagaji damu.



Mwisho.





Thomas Nyimbo awashangaa watanzania kumshangaa waziri Mulugo




MWANASIASA mkongwe nchini,Thomas Nyimbo amesema yaliyotokea kwa Naibu Waziri wa Elimu na ufundi stadi,Philipo Mulugo katika mkutano nchini Afrika ya kusini siyo ya kushangaza katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani hiyo ndiyo taswari ya viongozi wetu.



Nyimbo ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Njombe,mwasisi wa TANU na Chama cha Mapinduzi (CCM) na mlezi wa CHADEMA ameyasema hayo leo katika mkutano wake na wanahabari katika Hoteli ya Mount Livingstone,jijini hapa na kuongeza kuwa tukio la Naibu waziri Mulugo kuzungumza mambo ambayo hayaendani na nafasi yake siyo jambo jipya kwake kutokana na nchi inavyoendeshwa.



Alisema hiyo ni taswira tosha kuwa asilimia kubwa ya Viongozi wa nchi wanaoteuliwa hawana sifa ya uongozi bali wanapewa nafasi hizo kama zawadi kutokana na kufanikisha jambo fulani hali itakayoendelea kuwatafuna watanzania kutokana na mfumo na utaratibu huo.



"Hili jambo ni jipya kwa watu wasiojuwa utaratibu na mfumo mzima wa nchi,kwagu mimi siyo jipya...nimeambiwa nilete dereva nami badala yake nampeleka 'Tandiboi' unategemea nini ndiyo manaa nchi haiendi,"alisema.



Aliongeza kwa kusema hakuna sababu ya kumlaumu Mulugo kwa kuonekana kushindwa kuzungumza lugha ya kiingereza vizuri sanjari na kutoijuwa historia ya Tanzania kwa sababu wapo wengine ambao wangeshindwa kabisa hata kuongea na kuishia mabubu.



"Wanamlaumu nini huyo Waziri hii ndiyo hali halisi,afadhari hata yeye aliyejitahidi hata kuzungumza na mmesikia,wapo wengine wanaweza kunyama kwa kushindwa kuzungumza na tusingejuwa,aibu hii tuendelee kubeba,kwa sababu watamlinda,"alisema.



Baadhi ya wananchi wa jimbo la Songwe ambao ndiye Mbunge wao walisema kuwa tukio hilo limepokelewa kwa maoni tofauti kutokana na kushindwa kuamini kile kilichomtokea Mbunge wao Mulugo.



"Tunamsubiri aje atuambie,ni nini kilichomsibu,ndiyo hali halisi ya uwezo wake ama alikumbwa na kitu ambacho hatujakijuwa ni nini...lakini ili ni mojawapo ya nyundo ya kummaliza kisiasa katika uchaguzi mkuu mwaka 2015,"alisema mmoja wa wananchi hao.



Mkazi wa Kijiji cha Mkwajuni wilayani Chunya (jina limehifadhiwa ) alisema yeye ni mwanachama wa CHADEMA lakini amempongeza Naibu waziri kwa kutoa nafasi na matumiani makubwa kwa upinzani kushindwa katika uchaguzi mkuu unaokuja kutokana na kuonesha uwezo wake mdogo wa ufahamu na hivyo kushindwa kuwaletea maendeleo.



"Kama Naibu waziri wa elimu katika wizara nyeti kama hiyo haelewi hata historia ya nchi yake ataifanyia nini Tanzania na hawezi kutusaidia hata wapiga kura wake katika maendeleo kwa sababu uwezo na upeo wake unaonekana ni mdogo,na kibaya zaidi amekuwa akionekana kutumia mabavu na vitisho vingine kuongoza,"alisema.



Alisema kuwa Mulugo alifikia hatua ya kupeleka viti vya walemavu zaidi ya 200 akisema amenunua yeye pamoja na msaada wa wa visima vya maji ya kunywa vilivyofadhiriwa na mfanyabishara maarufu nchini Sabodo akidai alitoa yeye jambo linaloonesha kuwa haijapangi katika kuzungumza.



"Amefikia hatua anawaagiza watendaji wa vijiji na Kata kuwa hataki vyama vya siasa katika jimbo lake,kweli anaelewa maana ya Demokrasia?,na kila anapopita anatoa vitisho hata kwa walimu,nchi haiwezi kuongozwa kwa mtindo wa mabavu akama anavyotaka yeye,alisema.



Mwisho.

Tuesday, July 31, 2012

Sakata la mgomo wa walimu,RC Njombe amtimua Afisa wa Halamshauri ya Njombe kwa kuhamasisha mgomo wa walimu,aagiza apangiwe kufundisha shule ya msingi


Na Thompson Mpanji,Njombe

WAKATI sakata la mgomo wa walimu likiendelea kwa nchi nzima kuanzia leo(julai,31),Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Capt.Mstaafu Aseri Msangi amemshusha cheo mmoja wa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kuanzia leo kutokana na madai ya kuhamasisha mgomo wa walimu.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amewasihi walimu wote kurejea katika maeneo yao ya kazi na kuendelea kufundisha kwani serikali imeshatangaza kuwa mgomo huo ni batili kutokana na  suala hilo kuendelea kushughulikiwa mahakani.

Akitoa tamko hilo wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa kwanza wa mwaka  wa wanahisa wa Benki ya wananchi Njombe,Capt.Msangi amemuagiza  Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Njombe,Robert Nehatta kumshusha cheo hadi kuwa mwalimu wa kawaida wa shule ya msingi Mwenyekiti wa Chama cha walimu Tanzania(CWT),mkoani Njombe,Godfray Hambo kutokana na madai ya kuhamasisha mgomo aliodai unashughulikiwa kisheria.

Capt.Msangi amesema haiwezekani Hambo kuisaliti serikali  kwa kuendelea kuhamasisha walimu  kufanya mgomo ilhali naye ni kiongozi wa serikali jambo aliloagiza kuchukuliwa hatua za awali za kumshusha cheo na kwenda kufundisha katika shuel ya sekondari ama ya msingi wakati taratibu nyingine za kinidhamu ikiwemo na sheria  za utumishi wa umma zikifuatiwa.

Mkuu wa Mkoa amesema Mwenyekiti huyo wa CWT Njombe hakupaswa kushika wadhifa huo kutokana na nafasi yake  ya Ofisa elimu takwimu na vifaa wa Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ambapo alitakiwa  kuhamasisha walimu kufundisha badala ya kuweka kalamu chini.

Amesema endapo walimu wataendelea kugoma na hivyo kusababisha  wanafunzi kukosa masomo ni sawa na kuendeleza adui mmojawapo mbaya wa  ujinga  kwa taifa,donda alilodai  halitapona maumivu wala kufutika kovu lake kwa vizazi   wanavyovijenga na kuviandaa leo.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa wa Njombe amewashukuru walimu wote ambao kwa aslimi kubwa hawajagoma na wanaendelea na kazi na kwamba kwa Njombe mjini ni walimu wasiopungua 24 waliogoma ambapo kwa wilaya ya Makete amepokea taarifa ya shule moja wa sekondari ambayo walimu wake wamegoma ingawa hakuweza kuitaja jina na kama binafsi ama ya serikali.

BENKI YA NJOCOBA YAWAKOPESHA WANANCHI ZAIDI YA SH.BIL.3,WASIOREJESHA MIKOPO WAPANDISHWA KIZIMBANI WATATU

Na Thompson Mpanji,Njombe

BENKI ya wananchi wa Mkoa wa Njombe(NJOCOBA) imefanikiwa kutoa mikopo ya  zaidi ya Sh.Bil.3.6 hadi kufikia disemba ,mwaka 2011 kwa wananchama wake ikiwa ni mkakati wa  kuboresha hali za maisha ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya.

Aidha Njocoba imefanikiwa kuingiza mapato ya Sh.Mil.554 ambapo faida kwa mwaka  ilifikia Sh.Mil.10 ingawa imeelezwa kuwa benki hiyo ilipata hasara  ya Sh.Mil.289 iliyotokana na gharama kubwa za uanzishwaji wa benki ambazo Benki kuu (BOT) iliamuru kuhesabika kama matumizi ya awali kabla ya benki kufunguliwa.

Akitoa  taarifa fupi  tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Kapt.mstaafu Aseri Msangi,Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo,Bi. Twilumba  Ulaya amesema tangu kufunguliwa rasmi kwa benki hiyo septemba,13,2010 ilianza na zaidi ya sh.Mil.15.8 imekuwa na maendeleo mazuri kwa wananchi kuhamasika kujiunga   hadi kufikia  wateja 5,099  kwa kufungua akaunti mbalimbali.

Amesema benki  hiyo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2011 imefikisha amana ya zaidi ya Sh.Bil.1.8 katika akaunti  za akiba,biashara,muda maalum katika akaunti za makundi maalum,binafsi,makampuni,taasisi,watoto na wanafunzi na ushirika.

Mwenyekiti huyo amesema katika kipindi cha mwaka 2011 zaidi ya hisa 55,000 zenye thamani ya Sh.Mil.55 zilinunuliwa  na hivyo hisa za benki zilifikia 442,000 zenye thamani ya sh.Mil.442 ambapo mtaji uliopo hadi kufikia juni ,2012 umefikia zaidi ya Sh.Mil.290 kiasi ambacho ni chini ya mtaji  unaotakiwa na ununuzi wa hisa wa Sh.Mil.500 na hivyo  kuwaomba wanachama kuongeza ununuzi wa hisa.

Bi.Twilumba amesema urejeshaji wa mikopo  siyo mzuri  kwani kwa kipindi hicho mikopo ambayo ni mibaya na hailipiki  vizuri ni zaidi ya Sh.Mil.267 sawa na asilimia 18 ya mikopo yote na kwamba tayari  kesi tatu za madai  zenye thamani ya zaidi ya Sh.Mil.72.4 hadi kufikia juni,30,2012 zimeshafunguliwa  katika mahakama  ya wilaya ya Njombe.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Njombe,Kapt.Msangi ametoa wito kwa wakazi wa Njombe kujiunga kwa wingi katika benki yao na kwamba yeye atakuwa mwanahisa  na ataendelea kuhamasisha wakazi wa Njombe wanaoishi Dar es salam na mikoa mingine ikiwemo na halamshauri zote za Wilaya ya njombe kujiunga na benki hiyo.

Hata hivyo Kapt.Msangi ameuomba uongozi wa Benki ya Njocoba na Bodi yake  kuweka mikakati na taadhari kwa baadhi ya wanahisa wasije wakahodhi benki kwa kununua hisa zote na hivyo wanachama kujikuta  hawana chao na kumilikiwa na mtu mmoja hali ambayo itaondoa dhana nzima ya neno Benki ya wananchi.

Mwisho.

Sunday, October 2, 2011

wanafunzi wa kike mbarali wahofiwa kubakwa

Na Thompson Mpanji,Mbarali

WANAFUNZI wa Kata ya Mahongole na Mwatenga,wilayani Mbarali wameuomba uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuchukuwa jitihada za dhati kuwasaidia kuwajengea shule za Sekondari maeneo ya jirani  na makazi yao  ili kuepusha  madhara yanayoweza kuwakumba hasa kwa wanafunzi wa kike kutokana na kutembea  umbali mrefu katika vichaka   zaidi ya  kilomita 14  hadi kufikia shuleni.

Mwito huo umetolewa na wanafunzi hao walipokuwa wakizungumza na gazeti hili  kwa nyakati tofauti katika vijiji vya Kata  hizo ambapo wanafunzi kutoka Kijiji cha Sonyanga  wanatembea umbali wa kilomita zaidi ya nane hadi shule ya sekondari ya Kata ya Ruiwa,Ilongo  zaidi ya Kilimota 10,Kapyo umbali wa zaidi ya kilimota 14,Igalako na Mahongole Kilomita zaidi ya tatu,Muwela kilomita zaidi ya  saba na Mwatenga umbali wa kilomita zaidi ya 10.

Wanafunzi hao walisema, wamekuwa wakichoka na kushindwa kumsikiliza mwalimu  vyema baada ya kutemebea umbali mrefu ,wanafunzi wa kike wamekuwa wakihofiwa kubakwa vichakani huku wengine wakielelezea hofu yao ya kuuawa kutokana na  kuibuka kwa   matukio ya mauaji  ya kushtukiza  na kutulia yanayokuwa yakitokea wilayani humo jambo  ambalo wamedai linawakosesha raha na mori wa kuendelea na masomo.

Ofisa Mtendaji  Kata ya Mahongole,Juma Mangula  amethibitisha kuwepo kwa matatizo hayo kutokana na wanafunzi wa Kata ya Mahongole na Mwantenga kutegemea shule ya Sekondari ya Kata ya Ruiwa ambayo awali ilijengwa wakati wa Kata moja lakini  kwa sasa kuna uhitaji mkubwa wa shule.

Mangula alisema jitihada zinafanyika za kujenga mabweni ya wanafunzi wa kike ili kujaribu  kupunguza tatizo hilo na ameishukuru radio five kutembelea maeneo hayo ambayo  amedai hayajawahi kufikiwa na vyombo vya habari na ameviomba vyombo vingine kuiga mfano wa kituo cha radio five.

 Naye Diwani wa Kata ya Mahongole,Brown Mwakibete ametoa mwito kwa wadau  wa elimu kujitokeza kusaidia tatizo la shule kwani wananchi wamekuwa wakisua sua  kutokana na kutumia gharama nyingi na kwa muda mrefu katika kujenga  shule ya Sekondari ya Ruiwa ambayo kutokana na majengo yake kutokuwa na  ubora yameanguka na hivyo  kuanza kujenga shule nyingine.

Diwani Mwakibete alisema wakati wananchi wakiwa bado wanajitolea michango katika shule ya Sekondari ya Ruiwa  ikiwa na vyumba vya madarasa kumi na mbili,mabweni mawili,maktaba  na maabara ghafla ilibomoka na hivyo  wamechukua hatua ya kujenga shule mpya inayotegemewa na Kata ya Mahongole  na Mwantenga ambayo hadi sasa  ina vyumba 14 vya madarasa na nyumba mbili za walimu na kwamba bado haikidhi uhitaji wa wananchi wa kata hizo mbili

Mwisho

matukio ya nondo Mbeya,wauzaji na wamiliki wa bucha za nyama ya ng'ombe wadai mauzo yameshuka kutokana na walaji kuona kinyaa na kuichukia nyama,wasema wanaambulia kuuza maini na figo zisizotundikwa katika nondo

Na Thompson Mpanji,Mbeya

WAKATI matukio ya upigaji wa nondo yakiendelea kushika kasi jijini Mbeya,baadhi ya  wamiliki na wauza Bucha za  nyama ya Ng’ombe,jijini Mbeya wameelezea masikitiko yao ya kushuka kwa  mauzo ya nyama hiyo kutokana na walaji walio wengi  kuona kinyaa  na kuichukia nyama baada ya kuibuka kwa wimbi la uhalifu wa upigaji wa nondo unaohusishwa na imani za kishirikina kuwa zinatumika kuvuta wateja baada ya kutundikia nyama hizo katika maduka hayo.

Kama methali isemayo kufa kufaana ndivyo ilivyotokea kwa biashara hiyo ambapo kwa sasa wafanyabishara wa samaki, maharage,mboga za majani na nyinginezo nyota yao imenga’ra   kutokana na  wateja walio wengi  kuonekana wakikimbilia bidhaa hizo badala ya kitoweo maarufu cha  fileti,steki,mchanganyiko na mbavu.

Wakizungumza na mwamdishi wa habari hizi,  kwa nyakati tofauti,baadhi ya wauzaji na wamiliki wa mabucha  katika maeneo ya Soweto,Mabatini,Mwenjelwa,Mafiati na Sokomatola wamesema mauzo ya nyama hiyo yameporomoka kwa kasi  tangu kuibuka kwa  wimbi la upigaji wa nondo katika kipindi cha miezi kadhaa sasa.

Mmoja wa wauzaji wa Bucha eneo la Sokomatola aliyejimbaulisha kwa jina la Hussein  alisema kuwa nyama nyingi inalala kutokana na wateja kutoonekana  na kwamba wale wanaofika katika mabucha wananua  nyama aina ya figo au  maini ambazo hazitundikwi katika nondo.

Wakati huo huo,baadhi ya wakazi wa Kata ya Mabatini wamelalamikia Operesheni iliyofanywa na Jeshi la polisi kuwa imewaletea usumbufu mkubwa na kuwatia hasara baadhi ya wafanyabiashara kutokana na kikosi cha askari Polisi  kuvamia maeneo  hayo na kuwapiga marufuku wananchi kutembea kuanzia majira ya saa 1.30 usiku.

Mwenyekiti wa mtaa wa Mianzini,Kata ya Mabatini,Bibi.Elizabeth Mwambungu alisema operesheni iliyoendeshwa jana haikuwa ya kiistaarabu bali walitumia nguvu zaidi  kutokana na watu kupata usumbufu mkubwa wa kukamatwa na kupigwa ovyo jambo lililowafanya wajione kama wakimbizi ndani ya nchi yao.

Bibi.Mwambungu alisema kuwa  hawakuona umuhimu wa Jeshi hilo kufanya doria majira ya saa moja usiku huku muda wa watu kupigwa nondo unaonesha ni kuanzia saa 4 za usiku na kuendelea na kwamba wameshangazwa polisi kuanza doria baada ya kupigwa na kuuawa kwa askari mwenzao  huku  taarifa za upigwaji wa nondo zikifichwa na kudai kuwa  watu wanajeruhiwa ama kuuawa na vitu vyenye ncha kali.

Mwenyekiti huyo alisema uongozi wa mtaa wa mianzini umepanga kuitisha mkutano wa hadhara  siku ya Alhamis saa 8 mchana  kuzungumzia masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao kufuatia kuibuka kwa vitendo vya upigaji wa nondo katika Kata ya Mbalizi Road ambapo imedaiwa  zaidi ya watu  9 wamejeruhiwa akiwepo mtu mmoja kuuawa.

Mchungaji Wiliam Mwamalanga akizungumza na gazeti hili alisema Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya,Advocate Nyombi anapaswa kukubaliana na matokeo ya kuwa uhalifu wa upigaji wa nondo upo mkoani Mbeya na kwamba kilicho mbele yake ni kuweka mikakati kwa kushirikiana na wananchi kupambana na uhalifu huo kwa kutumia mbinu zilizotumika na Makamanda wenzake wa Mkoa wa Mbeya  waliopita  akitolea mfano Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema na Alhaji Suleiman Kova waliofanikiwa kuzima kabisa kadhia hiyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kikao cha dharula cha Kata ya Mbalizi Road kilichoitishwajana  kufuatia matukio ya upigaji wa nondo katika eneo hilo usiku wa kuamkia  jana, imedaiwa kuwa mtu mmoja ameuawa na wengine saba  kujeruhiwa katika  Kata hiyo   wakiwepo wengine wawili  kutoka Kata ya Forest,zote za jijini hapa.

Mwisho.